JUMAMOSI
WIKI YA 23 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 10:14-22a
Zab/Kit: 116:12-13, 17-18
Injili: Lk 6:43-49
Nukuu
“Kwa
ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu,” 1Kor 10:14
“Kikombe
kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule
tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?” 1Kor 10:16
“Hamwezi
kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani,” 1Kor 10:21
“Kwa
maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana,
katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk
6:43-44
TAFAKARI: “Mhenga au Lihoka katika Imani.”
Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo, Yesu
anaijenga kwa upana taswira ya kuwa Wahenga, yaani, kutambulika kwa matendo
yetu mema. Kama mtu huwa kile alacho, basi kile alicho mtu leo ni tokea la
historia yake. Yesu anasema, tu wahenga kwa sababu, “kwa
kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi
tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk 6:44. Kwa maneno mengine
hawezi kutoa usicho kuwa nacho. Na zaidi ya hayo, kwangu mimi na wewe leo wenye
ufahamu huu, yanipasa kutenda mema na kuwa mwema kila siku. Hiyo ndiyo njia
salama kwa mwili na roho yako katika umilele.
Matokea ya kweli hii ni
kwamba, “mtu mwema katika hazina njema ya
moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake
hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo
wake,” Lk 6:45. Mtu mwema ndiye Mhenga, na mtu mwovu ndiye Lihoka.
Ndugu yangu, ni lipi
ungependa kuwa au kuacha nyuma baada ya maisha yako hapa duniani? Yesu anatupa
uhakika wa kile tutakachokuwa pale tutakapoamua kufuata mafundisho yake. “Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu
na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake,” Lk 6:47. Ni kwa kusikia neno lake na
kulitenda huwa wahenga mara baada ya maisha yetu hapa duniani.
Lihoka, yaani, roho
ovu, katika maana ya ‘evil spirit,’ kwayo hakuna kitu cha kuigwa. Ni roho ya
uharibufu, yaani, ‘destructive spirit,’ isiyo pendezwa na jema au wema. Ni roho
isiyotulia na isiyo na mwelekeo wa kudumu na wa umilele. Ni sawa na “yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu
aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu,
ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa,” Lk 6:49.
Muhenga ikiwa ni mtu
yule mwenye kuacha kitu cha kuigwa, na kielelezo halisi cha wema, “Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba
chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto
uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri,”
Lk 6:48. Ndugu yangu, wewe hu mhenga au
lihoka? Ichunguze nafsi!
Mhenga kamwe haishi kwa
hofu. Muhenga uiishi kweli katika haki. Katika hili, Mtume Paulo anatupa wosia
kuikimbia ibada ya sanamu, 1Kor 10:14. Ibada za sanamu ni kutumaini nguvu
fulani kutoka kitu ambacho hakina uhai na uhasili wa hicho ukitegemeacho. Ibada
ya kisanamu huanza na wewe mwenyewe kwa kujiinua kusiko kweli na kujivika
kinyago-‘mask,’ na kupoteza taswira yako ya kweli.
Ibada ya sanamu hubeba
pia yale tuyatukuzayo katika maisha yasiyosema chochote au kuthibitisha
chochote kuhusu umilele wako, mfano; utajiri wako, umaarufu wako, cheo chako,
na nguvu kimamlaka isiyoweza kukuokoa siku ya mwisho. Katika hili Musa anamsifu
Mungu na kusema kwa furaha baada ya kuvuka
baharí ya Sham, “nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na
mpanda farasi amewatupa baharini,” Kut 15:1. Tumaini letu na Mungu ayafanyaye
yote katika yote ndani yetu. Na “kwa ajili ya hayo, wapenzi
wangu, ikimbieni ibada ya sanamu,” 1Kor 10:14. Wakuabudiwa ni Mungu peke yake.
Kristo akiwa ndiye
kielelezo chetu na kiunganishi chetu kama daraja kuelekea kwa Baba na Ufalme
wake, tunaposhiriki Sakramenti ya Ekaristi, yaani, mwili na damu yake, kamwe
tusivunje ushirika pamoja naye, jirani zetu, na Mungu. Mtume Paulo anatuachia
changamoto hii: “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si
ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa
Kristo?” 1Kor 10:16. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, Kristo
akiwa yote katika yote, yaani, Kanisa nasi tu viungo vyake katika mwili huo
yaani, Kanisa, tu mfano na fumbo hili la Ekaristi Takatifu. Mtume Paulo alisema
fumbo hili kama ifuatavyo, “kwa kuwa mkate
ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu
ya ule mkate mmoja,” 1Kor 10:17. Ndugu yangu, wewe na mimi si chochote bila
Kristo mwenye kuyaratibisha yote na kuyaunganisha katika umoja na utofauti wake
kama Kanisa na Sakrameti ya WOKOVU.
Kweli hii
inapojidhihirisha, yaani, Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu, na Kristo kama mwili, nasi kama viungo vyake,
sadaka tuzitoazo huwa na maana. Kinyume chake, yaani, kufifishwa kwa kweli hii,
sadaka tuzituazo ukosa maana ndani na katika Kristo Yesu, na kumtukuza shetani
aliyependa muda wote sifa pasipo siha. Kwa maana hiyo, “vitu
vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi
ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe
cha mashetani,” 1Kor 10:20. Michanganyo katika maisha ni saratani mbaya sana
kiroho. “Hamwezi
kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani,” 1Kor 10:21. Ni
heri kuwa joto au baridi kiimani kuliko kuwa vuguvugu kiimani.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kila
mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano
wake,” Lk 6:47
Tusali:-Ee Yesu, tujalie Imani thabiti. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario