IJUMAA
WIKI YA 23 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 9:16-19, 22b-27
Zab/Kit: 84:3, 4, 5, 6, 12
Injili: Lk 6:39-42
Nukuu
“Akawaambia
mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?” Lk 6:39
“Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu,
niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti
iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?” Lk 6:42a
“Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho
lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika
jicho la ndugu yako,” Lk 6:42b
“Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia;
maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16
“Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya
mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi,” 1Kor 9:19
“Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote
nipate kuwaokoa watu,” 1Kor 9:22b
TAFAKARI: “Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote
nipate kuwaokoa watu.”
Wapendwa wana wa
Mungu, kukengeuka kwetu
katika Imani kunatokana na unafiki wetu. Kwa ufupi unafiki ni kuujua ukweli
ulivyo lakini kutokana na mazingira au mtazamo wa watu, mhusika anaukwepa
ukweli ule na kuishi kadiri na mazingira yale na mitazamo ya watu wale ili
kuwapendezesha au kuwafurahisha. Mtindo huu wa maisha mgawanyiko ndio anao
uhoji Bwana wetu Yesu Kristo na kusema, “Au,
utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho
ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako
mwenyewe?” Lk 6:42a. Kwa upande mwingine ni kuishi kile usicho na kukubali kuwa
kivuli cha kitu ambacho sicho ulicho.
Ili urudi katika mstari ulioukwepa, yaani Imani ya
kweli, itakupasa kuurudia ukweli kama ulivyo na kwa kufanya hivyo utaweza
kusonga mbele na kuwa nuru na mwanga kwa wengine. Kwa sababu, “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini
kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake,” Lk 6:40. Yanipasa
kuongozwa na dhamiri njema na hai kila wakati, na kutenda kadiri ya dhamiri ile
njema na hai hata kama itanigharimu katika kweli na haki.
Jambo hili la kuishi kile usicho na kukubali kuwa
kivuli cha kitu ambacho sicho ulicho, Yesu Kristo anakemea mtazamo huo kwa
nguvu zake zote na bila kupepesa macho. Wenye tabia kama hizi Yesu Kristo hana
haya kutuambia hivi; “Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako
mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la
ndugu yako,” Lk 6:42b. Yesu amewafananisha watu wa mtindo huu wa unafaiki kwa
nyakati mbalimbali kama vipofu na makaburi yaliyopakwa chokaa. Yesu anahoji
ukakasi huu wa kutokusimama katika kweli, haki, na imani ya kweli akisema,
“Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?” Lk
6:39. Ole kwa waandishi na mafarisayo
kama makaburi yaliyopakwa chokaa na wanafiki tunasoma vizuri habari hii kutoka
mwinjili Mathayo hasa ile sura ya 23 yote.
Ndugu yangu, kama wewe leo una taaluma yoyote ile na
ukashindwa kutoa huduma kadiri ya taaluma yako kwa wale wanaohitaji huduma
hiyo, jua kwamba tendo hilo ni mwelekeo wa ukengeufu wa kile ulichosomea, na
mwisho wa siku tendo hilo litaathiri Imani yako kwa kiwango hicho hicho. Jambo
hili likikutokea huwezi kukwepa tuhuma na lawama za kuwa mnafiki, na huna
tofauti na waandishi na mafarisayo wa nyakati zile za Yesu. Basi kama mimi ni
mwalimu wa dini, mwanasheria, Bwana afya, mwalimu, Mwanasiasa, nk, ni wakati wa
kujichunguza vizuri.
Wapendwa katika Kristo, ukweli huu wa kusimama katika
kweli, kuisema kweli, na kutoyumbishwa katika kweli juu ya Imani ya kweli, inajionyesha
wazi katika somo la kwanza, yaani, waraka ule wa kwanza wa Mtume Paulo kwa
Wakorintho. Leo Makanisa mengi, niseme, "nyumba za sala" kwa maana
halisi, zimebebwa na ajenda kuu mbili: utoaji tu wa shuhuda, na uhubiri wa
msisimko usio wa kina na wenye ishara za zima moto ukilenga mwisho wa nyakati. Ni
nyumba za sala na siyo Kanisa kwa taswira zifuatazo:
1. Utambulika kwa
majina husika ya "waanzilishi" wao, mfano, "Kanisa la Nabii
Edgar." Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, Kanisa ni la
Kristo na sisi wabatizwa ni viungo vyake, "vivyo hivyo na sisi tulio wengi
tu mwili mmoja na Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake," Rum 12:5.
Mtume Paulo anatoa salamu kwa wana Kanisa la Korintho kwa utambulisho huu,
"kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo
Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu
Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu," 1Kor 1:2. Na hapa ndipo kila
mbatizwa anao wajibu wa kuihubiri habari njema ya wokovu. Naye Mtume Paulo anatoa msisitizo wa jambo
hili na kusema, “Maana, ijapokuwa naihubiri
Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16.
Hatufanyi hivyo, yaani, kuihubiri Injili kwa lengo la kujiinua au kujisifu
nafsi zetu, bali twafanya hivyo ili Kristo aongezeke nasi tupungue, Yoh 3:30
2. Hubabe ujumbe wa
sifa binafsi ikiwa ni tangazo mahususi la kuwavutia watu lenye muono wa
"kibiashara," mfano: "kwa mzee wa upako," "chemchemi
ya uzima" "kanisa la ufufuo," Kanisa la wanyakuliwa wa
mwisho," "kanisa la amri kumi za Mungu," nk. Je, twajua kile
tunachowakilisha kwa Kristo na Kanisa lake? Je, twayafanya haya kwa maslahi
yetu binafsi na kumtumia Kristo kama njia ya kupitisha mambo yetu ya siri?
Ndugu yangu, Mtume Paulo anasema, “nikiitenda
kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu,
nimeaminiwa uwakili,” 1Kor 9:17.
3. Mara zote huwa na
sura ya kifamilia. Ikiwa "kanisa" hili lilianzishwa na marafiki
wawili au watatu, kikomo chake ni mfarakano wa kimasilahi, na mwisho hubakia
kifamilia zaidi kwani marafiki hawa hutengana na kila mmoja kujitwalia cheo
atakacho. Mfano, "kanisa la Askofu Edgar," au "Kanisa la
mtumishi wa Mungu Edgar." Je, nafasi hizi nizakujitwalia au kuhesabiwa
haki katika mastahili yake? Na ninayafanya hayo yote ili mwisho wake iwe nini? “Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa
nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo
wangu nilio nao katika Injili,” 1Kor 9:18
4. Nyumba hizi za sala
hazina mwelekeo wa kumkuza mtu kiroho na kumfanya huru kuiishi imani yake
kiutambuzi na kutafakari malengo ya Mungu katika maisha yake. Huwafanya waamini
wake kama "mazuzu fulani hivi na tegemezi" waliobanwa kifikra kama
watumwa. Ukweli wa neno la Mungu badala ya kuwaweka huru huwafanya watumwa.
Huacha kumwabudu Mungu na kuwaabudu viongozi wao, "watumikiwa." Hili
silo lengo la kuihubiri habari Njema ya Wokovu. Habari Njema ni kumfungua mtu
kutoka vifungo vya dhambi na kumweka huru kuyaelekea maisha yale timilifu ya
umilele. Katika hili Mtume Paulo anasema wazi jinsi alivyofanya; “Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote,
nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi,” 1Kor 9:19. Na
aliwapata wengi zaidi katika kweli na haki, na waliojitambua walijua ni nani
wamtumikie, yaani, Mungu wa kweli na hai. “Nimekuwa hali zote kwa watu wote,
ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu,” 1Kor 9:22b
5. Mtazamo wa neno
"sadaka," katika maana halisi hupotea na kuishia katika mali za
ulimwengu huu. Watu wengi huvutwa na viini macho na mazingaumbwe yaliyoandaliwa
kwa ustadi mkubwa. Je, katika hali na mazingira kama haya, Kristo anabaki kuwa
kielelezo cha kweli: Njia, Kweli, na Uzima, Yoh 14:6? Kwa vile twapenda sana
Ishara, hasa zama zetu hizi, mtego huu umewanasa wengi na bado wengi
wanaendelea kunaswa. Ukweli ubaki kuwa huu, “Nami
nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine,” 1Kor
9:23. Zaidi ya hayo ni dhihaka kwa Mungu, na maigizo kwa mwanadamu.
Ndugu yangu, Ishara sio
kigezo cha kwanza cha IMANI. Imani kabla ya yote ni ufunuo ulio wazi na binafsi
wa Mungu mwenyewe kwa watu wake. Imani ni tendo au hatua ya pili ikiwa ni
mwitikio wa UFUNUO huo wa Mungu kwa yule aliyeupokea. Na imani hiyo ndiyo utusukuma
kupiga mbio kuelekea mede ile, yaani utakatifu wako. Licha ya kwamba imani
yaweza kuchukuliwa kama tendo la kijumuiya au jumuiya fulani ya watu fulani,
imani vile vile ubaki kuwa tendo binafsi. Naye Mtume Paulo anasema hivi, “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga
mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo,
ili mpate,” 1Kor 9:24. Na mbio hii ya Imani ulenga mara zote lile lililo jema
na bora zaidi. “Na kila ashindanaye katika
michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji
iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika,” 1Kor 9:25. Na
kisichoharibika ni kile kidumucho milele, nao ni UZIMA WA MILELE.
Ni ukweli usio tia
shaka kwamba tendo hilo la Ufunuo wa Mungu limeonekana wazi kwa Neno kufanyika
mwili "umwilishwaji," kwa Yesu wa Nazaret-kihistori, na sasa
laendelea katika Kanisa Kimasakramenti, na kwa nyakati zijazo kwa Maandalizi ya
"upyaisho"-Kiroho zaidi na kiutakatifuzwa kwa yale yote yaliyoumbwa.
Ndugu yangu, ni jukumu
la kila mbatizwa kuhubiri ujumbe huu muhimu wa habari njema za Ufalme wa Mungu.
Yesu Kristo analifahamu hilo na ndiyo maana habumbaziki na umati wa watu
unaomfuata, na wala kwa miujiza anayoifanya ambayo kwayo wengi wanamfuata. Kwa
kuliona hili Yesu anasema, "twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo
karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hilo nalitokea," Mk 1:38. Na
kwa upande mwingine, nami ninayeihubiri Habari Njema hiyo ya wokovu nisijisahau
kuwa nami nahitaji wokovu huo. “Hata mimi
napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama
apigaye hewa; bali nautesa mwili
wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa
kukataliwa,” 1Kor 9:26-27. Sote twahitaji Neema, Huruma na Upendo wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nami
nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine,” 1Kor
9:23
Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie neema zako ili
tudumu na kuyafanya yale ambayo yatatufikisha hapa ulipo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario