JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-C
Somo:
Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23
Zab/Kit: 88:2-3, 4-5, 6, 7-8
Injili: Lk 9:51-56
Nukuu:
“Lakini wenyeji
hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53
“Wanafunzi wake Yakobo na
Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka
mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54
“Akawageukia,
akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55
“Kwa maana Mwana wa
Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a
“Baada ya hayo Ayubu
akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake,” Ayu 3:1
TAFAKARI:
“Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.”
Wapendwa wana wa Mungu, sehemu hii ya Injili n asomo letu la leo juu ya
habari ile ya Ayubu, inafua ‘kweli ya Mungu’ ambayo hubaki kuwa ‘siri’ katika
maisha yetu ya kila siku. Ni kweli kabisa katika hali na mazingira ambayo
twateseka tu bila sababu ya teso hilo, maisha upoteza maana yake. Hii ndiyo
hali aliyokuwa nayo Ayubu baada ya kupatwa na janga lile la majaribu na kuanza
kulaani, Ayu 3:1. Kulaani kwa kile usichokijua vizuri hakutakufanya kuelewa
fumbo la kile usichokijua vizuri. Kuzama katika fumbo usilolielewa ili upate
maana yake ni kujiuliza swali hili; Je, katika jambo hili, Mungu wataka
kunifundisha nini? Hakuna jaribu lisilo kuwa na mlango wa kutokea, 1Kor 10:13.
Kuupata mlango wa kutokea ni kuachana na laana na laumu.
Yesu Kristo aliye Mungu
na Mwanadamu anaelekea Yerusalemu kwa kile kinachosimuliwa na Mwinjili Luka
kama “siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia.” Je, kupaa bila kupitia
mateso, kifo, na ufufuko? Mwinjili Luka halisemi jambo hili kwa kukosea. La!
Hasha. Kupaa kwa Yesu ni hitimisho linalo elezea Wokovu ikiwa ndiyo lengo
lengwa katika historia nzima ya mwanadamu (Yoh 1:14, Gal 4:4-5). Wokovu huo
unathibishwa kwa Ufufuko wake Kristo Yesu. Ufukuko huo ni alama ya wazi ya
ushinda dhidi ya kifo kilichokuwa adui yetu mkubwa. Na Kifo hicho cha Kristo
Yesu ni alama wazi ya upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu kutuweka huru kutoka
utumwa wa dhambi. Kwa maana nyingine, kupaa kwa Kristo kusingekuwa na maana
kama kusingesema chochote kuhusu wokovu, ufufuko, na kifo. Na kuelekea
Yerusalema katika maana ya “kukaza uso wake kwenda Yerusalemu,” kulimaanisha,
mateso, kifo, wokovu, ufufuko, na kupaa.
Hata pamoja na mpango
huu mahususi uliobeba kilele cha historia mzima ya wokovu wa mwanadamu, jambo
hili kwa ajabu kubwa na mshangao halimgusi mwanadamu. Hii ndiyo kweli ya Mungu
inayobaki kuwa siri katika maisha ya mwanadamu. Na hii ndiyo maana ya maneno
haya; “Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda
Yerusalemu,” Lk 9:53. Mwenye kufikiriwa kuhusu kesho na hatma yake itakuaje
hana habari kabisa na kile anachofanyiwa.
Kwa bahati nzuri au
mbaya siri hii haikufichwa kabisa kwa baadhi ya wateule wa Mungu. Mwanga wa siri hii unafunuliwa kwa wanafunzi
wake Yesu, kama asemavyo mwenyewe kwamba, “Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme
wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia
wasielewe,” Lk 8:10. Kufunuliwa kwa siri hii kuna kuwa bahati mbaya kwa namna
wanafunzi wake Yesu wanavyotafuta suluhu ya mambo hasa katika safari hii ya
kuelekea Yerusalemu alipoyakazia macho yake Yesu. Na mambo yalikuwa hivi;
“Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka
tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye
alivyofanya]?” Lk 9:54. Yesu hakuja kufanya mwendelezo wa sheria ile ya jino
kwa jino, bali kuitakatifuza na kuifanya kamili, Mt 5:17. Na lengo na uwepo
wake Yesu siyo kuukumu ulimwengu bali ulimwengu
uukolewe na yeye, Yoh 3:17.
Ni wazi kabisa kwa kile
walichoshupalia wanafunzi wake Yesu, Yakobo na Yohana cha onyesha kile kilicho ndani
ya mioyo yao na ubinadamu wao. Na hapa ndipo Yesu “Akawageukia, akawakanya.
[Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55. Yesu anawakanya
wao na sisi leo kama Wakristo na Wafuasi wake kwamba mtindo wa jino kwa jino
siyo staha na maadili yetu kama Wakristo. Kufanya hivyo ni kutokujua fumbo zima
la wokovu wetu. Ukweli ni kwamba, “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za
watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza
roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a
Tusali:-Ee
Yesu, tuondolee ile roho ya kukata tamaa na kuwa watu wa visasi. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario