jueves, 29 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 27 YA MWAKA-C



Somo I: Hab 1:2-3; 2:2-4

Zab/Kit: 95:1-2, 6-7, 8-9

Somo II: 2Tim 1:6-8, 13-14

Injili: Lk 17:5-10

Nukuu

“Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa,” Hab 1:2

“Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji,” Hab 2:2

“Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu,” 2Tim 1:6

“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7

“Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu,” 2Tim 1:14

“Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani,” Lk 17:5

“Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6

“Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10

TAFAKARI: “Tuongezee imani Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 27 ya mwaka “C” wa Kanisa. Mama Kanisa kwa namna ya pekee leo anatutaka tutafakari kwa makini kuhusu IMANI. Imani ikiwa ni kuamini pasipo shaka yanayoonekana na yasiyoonekana, Ebr 11:1, Imani thabiti ni suluhu ya mambo mengi tusiyoyajua bado. Imani thabiti utuzamisha kwenye fumbo zima la maisha. Ukweli ni kwamba ingawa twaishi katika ulimwengu huu yapo mambo mengi tusiyoyajua licha ya ufahamu wetu kama wanadamu.

Nabii Habakuki aliyefanya unabii wake katika jamii isiyo amini katika haki na baadaye kuwa chukizo kwa Mungu, anaona anguko kubwa sana mbele yake. Unabii huu unafananishwa na kile alichokiona Yesu kutokea juu ya anguko la Yerusalemu na mwisho wa nyakati, Mt 24. Pamoja na ukweli kwamba Nabii Hakukuki anaona uovu ndani ya jamii yake, na watesi wao, yaani, mataifa yaliyokuwa yanawazunguka, pona yao kama taifa kutoka ovu huo ni kusimama katika imani ya kweli na haki. Kuushinda uovu uliosababishwa kwa kutokutenda haki, Mungu anamjibu na kusema, “Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake,” Hab 2:4.

Hata pamoja na jibu hilo la Mungu, kuelewa ukweli huo na kuukubali kwa wezekana tu kwa Imani. Ni kwa imani tu twaamini ushindi wa mwisho katika uaminifu wetu kwa Mungu. Sehemu hii ya unabii wa Habakuki twaweza utafasiri katika mwelekeo wa fundisho kadiri ya vitabu vile vya hekima. Naye Nabii Isaya katika kweli hii anasema, “Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba,” Isa 33:6. Na katika mwono huo huo na ulio wa juu zaidi, Mtume Paulo katika fundisho lake la kuhesabiwa haki kwa Imani, anasema, “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani,” Rum 1:17; Gal 3:11. Hapa hakuna mkanganyo au kupingana kwa kweli hiyo. Uaminifu kwa Mungu ndiyo upekee huo uokoao, na uaminifu ndio uwezekano wa Imani kwa Mungu.

Mtume Paulo katika mantiki hii anatutaka tuelewe kwamba wokovu siyo tu swala la imani kwa wakati ujao, bali ni tendo la imani halisi, na chanzo cha uaminifu endelevu. Undani na uzito wa fundisho hili la Mtume Paulo ndilo alisemalo kwa Timotheo kwamba, “Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu,” 2Tim 1:13-14

Katika somo letu la Injili, Mitume wanamwomba Yesu awaongezee Imani, Lk 17:6. Kwa upande mwingine twaweza kuona tatizo  ambalo linawakabili wafuasi wake Yesu-Wakristo, ikiwa ni pamoja na wewe na mimi kama wabatizwa. Fundisho la Yesu, yaani, “Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6, tunaweza lihusisha na habari ile ya uponywaji wa kijana yule aliyekuwa na pepo mwenye kumtesa sana, na wanafunzi wake Yesu kushindwa kumtoa, Mk 9:18. Baada ya Yesu kumkemea Baba wa kijana yule kwa kutokuwa na Imani, “Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu,” Mk 9:24.

Ndugu yangu, Imani ya kweli na thabiti hata kama ingekuwa ndogo kiasi gani inatokeo kubwa na la ajabu katika maisha yetu, (Rej Mt 17:20, 21:21). Neno kuhusu mtumwa, Mt 17:7-10, linatupatia fundisho la pekee. Yesu mwenyewe akiichukulia hali ya maisha yake aliyokuwa akiyaishi licha ya ukuu aliokuwa nao-Mungu na Mwanadamu, mtumwa anatufundisha na kutuonyesha fundisho hususi kuhusu habari njema. Mtumwa hawezi jiinua na kujipongeza kwa kazi yake, zaidi ya kufanya na kutimiza wajibu wake. Na hivi ndivyo Mtume Paulo asemavyo, “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16. Hakuna la kujisifia, zaidi ya kutimiza kwa uaminifu kile upaswacho kutimiza.

Fundisho hili ya Yesu katika Injili ya leo linaenda kinyume kabisa na mwono ule wa mafarisayo waliojiongezea mapambio kwa kazi zao na kusahau ukweli kwamba siyo kazi katika kazi ndizo zinazotuhesabia haki, bali ni neema na kwanyo ni zawadi ya Kimungu kwetu. Kamwe hatuwezi jifananisha na vitu au idadi ya yale tuyatendayo, bali roho na upendo ule utusukumao kufanya mambo hayo hata kama ni madogo na macheche sana. Hivyo roho hiyo na upendo huo katika kutenda, na kwa kibali chake Mungu na kwa kadiri ilivyompendeza twahesabiwa haki. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu, kwamba, “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Kuna furaha ya kweli tunapojibandua kutoka vitu na mali, na kutovifanya ndio mwisho wa kila kitu ingawa twavihitaji hapa na pale.

Kwa maana hiyo, wewe na mimi kama Wakristo tusipokuwa na Kristo Yesu katika maisha yetu tuna hasara kubwa sana. Na ukweli ni huu; bila Kristo Yesu huna njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6. Na kama huna hivi, je, uzima wa milele unawezekana kwako? Tunapomwamini Kristo Yesu, Yeye hukaa kati yetu, naye huwa mwanga, kweli, na uzima wenyewe. Ni kweli hapa na pale tutakutana na magumu fulani katika ufuasi wetu kwake. Ila bila Kristo ni vigumu kuyabeba hayo na kuyashinda. Pamoja na udhaifu na uduni wa mwanadamu kama asemavyo Mhaburi, 103:14-15, mtu huyu mara zote na muda wowote anaitwa na Kristo Yesu.

Mtume Paulo licha ya kugundua kwamba Timotheo ameitwa na Kristo Yesu katika kuiishi na kuihubiri Injili, bado kuna mambo hayajakaa sawa. Katika kweli hii anamkumbusha Paulo anamkumbusha Timotheo na sisi pia, “kuichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:6-7. Nguvu na neema hii yapaswa kuonekana kwa Mkristo, na siyo kuwa goigoi.

Mtume Petro katika hili (kutokuwa na woga na hofu) anasema, “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe,” 2Pet 1:10. Mkristo hana sababu ya kumwogopa mtu au kitu chochote kile, kwa sababu, “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo,” 1Yoh 4:18. Jambo la ajabu leo baadhi yetu Wakristo na tuliopewa dhamana na Mama Kanisa tumekuwa goigoi hata kusimama tu katika kweli hofu imetupiga.

Je, Yesu anasema nini kuhusu kumwonea haya mbele za watu katika kweli na haki? Ni vyema tukayakumbuka vizuri maneno haya ya Yesu, Bwana, na Mwokozi wetu. Naye anasema, “Kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu,” Lk 9:26. Neno la Mungu ndilo litupalo nguvu na ujasiri. Na Imani na Upendo na nguvu ya Roho Mtakatifu ndivyo vinavyotuwezesha kuushika ujumbe na mafundisho ya Mungu. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26.

Na Roho huyu Mtakatifu siyo roho mtakavitu, na mwenye kufanya kadiri ya matakwa yako au yangu. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh 16:13. Huyu ndiye Roho Mtakatifu, na siyo roho mtakavitu. Siyo roho mtakavitu kwa sababu ya tabia yake kwamba; moja, ni kuongoza katika kweli yote. Pili, hunena kwa shauri lake mwenyewe. Tatu, huyasikia ayanenayo (kama upendo wa Mungu Baba na Mwana). Na mwisho, upasha habari yake kwetu.

Kijana Tumaini Ndewenga alitoka kijiji kilichoaminika sana kwa uchawi. Akiwa mwaka wa pili Chuo Kikuu Baba yake mzazi alifariki. Kifo cha Baba yake kilihusishwa na Mzee Change hapo kijijini. Mzee huyu akiisha kunywa pombe na kulewa huaza kujisifia kuwa yeye ndiye gwiji la uchawi hapa kijijini.

Akiwa kwenye msiba wa Baba yake, Mzee Change alisikika kilabuni akisema, “na hako katoto kake kasomi nakapa siku 7 nako katamfuata Baba yake huko aliko.” Maneno haya yalisambaa kwa haraka sana kijijini hapo kama moto wa petroli, kwa sababu wasifu wa Mzee Change hakuna asiyeujua. Habari hii ilipomfikia Tumaini alisema, “mwambieni Mzee Change yeye atakufa siku mbili kabla ya hizo saba alizonipa kuisha.”

Kijana Tumaini ambaye hakuwahi kuterereka hata siku moja kuhusu kile alicho amini juu ya uhai kuwa ni mali na zawadi ya Mungu, habari ile haikumshtusha hata kidogo. Hata hivyo Tumaini alitaka kutoa somo kwa wanakijiji wenzake. Somo lenyewe lilikuwa hivi; zikiwa zimebaki siku siku mbili ili neno la Mzee Change kutimia juu ya Tumaini, Mzee Change akiwa kilabuni anapata pombe muda wa saa moja usiku, Tumaini alimchukua jogoo na kumnyonyoa angali mzima na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Mzee Change na kumfunga Jogoo yule kwenye tendego la kitanda.”

Mzee Change kama kawaida yake alirudi nyumbani akiwa kesha lewa na kujilaza kitandani. Ilipofika majira ya saa kumi na moja alfajiri, jogoo yule alianza kuwika na sauti ilisikika ikitoka uvunguni mwa kitanda. Ghafla Mzee Change alishtuka na kutazama uvunguni. Mara alipomwona jogoo asiyekuwa na manyoya alifungasha kila kilicho chake na kukimbia kijiji kile akiamini kifuatacho ni kifo kama alivyosema Tumaini kabla ya siku mbili za mwisho alizotabiri Tumaini kufa yeye atakufa.

Ndugu yangu, simama katika imani ya kweli!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu,” 2Tim 1:14

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tuongezee Imani, ili tuwaze mara zote na kutenda Matakatifu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario