miércoles, 21 de septiembre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 25 YA MWAKA-C


ALHAMISI WIKI YA 25 YA MWAKA-C

Somo: Mhu 1:2-11

Zab/Kit: 90:3-4, 5-6, 12-13, 14, 17bc

Injili: Lk 9:7-9

Nukuu:

“Na Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu,” Lk 9:7

 “Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona,” Lk 9:9

“Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili,” Mhu 1:2

“Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini yajua?” Mhu 1:3

“Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima,” Mhu 1:4

TAFAKARI: “Ubatili.”

Wapenda wana wa Mungu, kadiri ya Mhubiri, anayaona maisha si kitu wala chochote, bali ni ‘ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili,’ Mhu 1:2. Swali la msingi na la kujiuliza ni hili, nitawezaje kuitamani hiyo kesho kama sioni maana ya leo? Kama tumeumbwa ili tuishi milele, na Mungu akaona inafaa tuwepo ulimwenguni hapa, iweje tena niwe na mawazo haya kwamba mtu apata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua?’ Mhu 1:3; 2:22.

Ndugu yangu, ni vyema nikaelewa kwamba vyote vinavyoonekana na visivyoonekana alivyoviumba Mungu kwa asilimia kubwa vinamlenga huyu mwanadamu aliyepewa heshima ya juu kabisa kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni katika hali na mazingira hayo, “Bwana aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18. Pamoja na mahangaiko na sintofahamu za maisha, ulimwenguni hapa pana kusudio la Mungu katika maisha yetu. Hapa ndipo uwanja wa kujua kusudi la kuumbwa kwetu na kujiandaa katika uzima ule wa milele. Duniani hapa ni pahala pa kujiandaa, na siyo mwisho wetu.

Ni kweli kwa wakati twaonekana kupita na dunia kubaki. Hatuna sababu ya kukata tamaa kwanii huo ndio ukweli kama asemavyo Mhubiri kwamba, “Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima,” Mhu 1:4. Hata hivyo kwa muda mfupi tuwapo hapa duniani ni vyema kufahamu vizuri kusudi la kuumbwa kwetu. Na kusudi la kuumbwa kwetu tungali hapa nduniani ni kumjua Mungu, kumpenda Mungu, kumtumikia Mungu, na mwisho kurudi kwake mbinguni.

Ni kweli kabisa hapa na pale tutakatishwa tamaa, ila isiwe sababu ya kutokuona kusudi la Mungu katika upana wa uumbaji wake. Ufanyalo zuri leo, kesho laweza kufutwa kwa hila tu na kutoweka. Ila pamoja na hali hiyo, hatuwezi kufuta wema wa lililo jema mbele ya macho ya Mungu. Kumbe si vyema kuutazama ulimwengu mwono asi. Ukiruhusu hali hii, basi elewa ushajifungia mwenyewe katika gereza fikra zako mwenyewe na kuliruhusu giza litawale maisha yako. Ni kweli isiyotia shaka kwamba, kwa mwona na mtazama wako kama tokeo la mang’amuzi yako, “mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia,” Mhu 1:8. Na hata kama huo ndio ukweli kwa kiasi fulani, jambo hilo linapobaki katika historia yake, huendelea kuwa somo kwa vizazi na vizazi. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu,” Mhu 2:21.

Pamoja na mtizamo huu wa Mhubiri, maisha ni zaidi ya yale tuyafanyayo leo au kuyamiliki. Jambo la maana na muhimu ni kuwa huru nje ya yale tuyafanyayo na kuyamiliki. Tusipojibadua katika haya, maisha hukosa maana na hasa pale yanapotoweka yale tuyafanyayo na kuyamiliki. Ni swala la wakati kwamba itafika mahali hatutaweza kufanya chochote. Ukweli ni kwamba, “yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka,” Mhu 1:9ab

Je, katika hali na mazingira kama hayo ya kutokufanya chochote, utu wetu utatoweka kwa sababu tu wazee? Utajiri na mali tulizonazo tumemilikishwa kwa muda tu na wakati ukifika watamilikishwa wengine, nasi tutaondoka kama tulivyokuja bila chochote kwa sababu,  Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Ndugu yangu, tunapojimilikisha yale ambayo kwa asili siyo yetu, mwisho wa siku huwa ni ubatili na masikitika makubwa.Kwa kuwa (Mtu kama huyo) siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili,” Mhu 2:23.

Ndugu yangu, mtu wa kuyapa maana maisha yako ni wewe mwenyewe. Na kama leo unaishi hapana shaka kwamba leo yako ni tokeo la jana yako, na kesho yako iwe nzuri au mbaya yategemea sana unachofanya leo na sasa. Kumbe ni vyema nikawa na fanya kila mara kama siyo kila siku zoezi la dhamiri. Dhamiri njema kama sauti ya ‘Mtoto mchanga na Mtakatifu ndani yetu,’ ukuzwa kwa kufahamishwa yaliyo mema, mazuri, na yenye kulibeba tumaini la kweli. Huu ni mwaliko kwako na kwangu kuzitafakari njia zetu kila siku.

Na katika kutafakari njia zako yatupasa kuhoji ukaribu wako na Mwana wa Mungu. Herode anaingiwa na hofu baada ya kusikia habari za Yesu kwa sababu alifikiri baada ya kumwangamiza Yohane Mbatizaji kwa kumkata kichwa siku ya sherehe ya kuzaliwa kwake-Herode, angeendelea kuisahaulisha na kuiridhisha dhamiri yake mbaya katika uovu. Herode anataka kumwona Yesu si kwa sababu anataka kuanzisha uhusiano mzuri naye, bali bila shaka kutafuta namna ya kumwangamiza ili asiwe tishio kwake kama alivyokuwa mtangulizi wake, Yohane Mbatizaji.

Hivyo Herode anawajibu wale waliomletea habari juu ya Yesu na kusema, “Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona,” Lk 9:9. Tukitaka kuwa na amani ya kweli ndani yetu lazima tupatanishwe na Kristo. “Huyu manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi,” Mdo 10:43. Na bila kujisalimisha kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwokozi wetu, yote ndani yetu ubaki kuwa ‘ubatili.’

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona,” Lk 9:9
Tusali:-Ee Yesu, tujalie neema ya kuyaona yote kama uyaonavyo Wewe. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario