lunes, 5 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 23 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 23 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 7:25-31
Zab/Kit: 45:11-12, 14, 15, 16, 17
Injili: Lk 6:20-26
Nukuu
Basi, naona hili kuwa jema, kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo,” 1Kor 7:26 

Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke,” 1Kor 7.27

 “Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu,” Lk 6:20

Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka,” Lk 6:21

Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu,” Lk 6:22 

Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo,” Lk 6:23 

TAFAKARI: “Maisha ni kuchagua, na ukishachagua ni kuwajibika ipasavyo.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna lililo rahisi katika maisha. Kila aina ya mtindo wa maisha una changamoto zake. Kuwajibika katika maisha kama ipasavyo ndiko kutakako kuletea nafuu katika maisha hayo. Kwa maneno nyingine unapofanya uzembe fulani na wakujitakia kwa kile ulichochagua kuishi na ndio wito wako, maisha hayo lazima yatakuwiya magumu.

Hali hiyo ya uzembe ikupelekayo katika ugumu wa maisha, ni sawa na kuhesabika kuwa huru kinadharia ila mfungwa kivitendo. Hutoweza kuwa na furaha katika hali na mazingira kama hayo kimaisha. Mtume Paulo anapojitazama mwenyewe na mtindo wa maisha-useja, anaona unafuu wake. Unafuu huo unaonekana kwake kwa sababu kesha ipokea hali hiyo, na kuwajibika ipasavyo. Naye anasema, basi, naona hili kuwa jema, kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo,” 1Kor 7:26. Maisha ni kuwajibika.

Kama swali chokonezi, Mtume Paulo anaenda kwenye uhalisia wa kile akisemacho. Naye anauliza, Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke,” 1Kor 7:27. Mwenzi wako wa ndoa hawezi kuwa mzingo kwako kama ulichagua mwenyewe mfumo huo wa maisha kuwa bila shuruti na ukawa tayari kuwajibika kwa kile ulichochagua. Ikiwa uliingia katika mfumo huo wa maisha kwa vionjo na mbwembwe za wakati, jiandae kwa sintofahamu nyingi katika maisha hayo. Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo,” 1Kor 7:28. Dhiki huja pale unapoishi maisha bila malengo.

Maisha yoyote yale uongozwa na lengo. Hata hivyo, pamoja na mipango mengi mtu aweza kuwa nayo katika maisha, lengo kuu la maisha ni kuishi milele. Maisha ninayoishi leo na sasa yanisukume katika ukamilifu wake, yaani, umilele licha ya udhaifu nilio nao hapa na pale. Maisha ninayoishi yaniandae katika cheo changu halisi, yaani, utakatifu. Bila utakatifu siwezi kuiona mbingu. Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu,” 1Kor 7:29-30.

Maisha niliyochagua na kuwajibika kwayo yasiwe ndiyo mwisho wa kila kitu, bali yawe chachu ya mimi (kama mtawa na mkleri) au wote wawili (katika Sakramenti ya ndoa) kuufikia UTAKATIFU. Hivyo mambo yale ya kujibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija nijiepushe nayo. Niwe na kiasi kwa kila kitu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya kwamba, Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita,” 1Kor 7:31 

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, katika jamii yetu leo wapo watu wengi wanaolia kwa shida mbalimbali na hawana pa kushika. Maisha kwao kila siku afadhali ya jana. Na huu ndio ujumbe wa Yesu kwa wanafunzi wake; Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu,” Lk 6:20.

Hata pamoja na hali hii wapo wanaosheherekea na kutapanya vitu ovyo bila kuwajali wahitaji na wanyonge.Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata,” Lk 6:24Kristo anatuambia wanaotaabika sasa katika ulimwengu huu watacheka na kufurahi milele. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka,” Lk 6:21

Kwa upande wa pili, wote wanaocheka sasa na kuyafumba macho yao kwa kutokuona shida za wenzao hao wataomboleza daima. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia,” Lk 6:25. Je, ndugu yangu kwa nini waandaa maombolezo ya kudumu katika umilele wote unaposhindwa kunyoosha mkono wa heri kwa mwitaji unayeishi naye katika familia yako, jumuiya yako ya kitawa, jumuiya yako ndogo ya Kikristo, ofisi moja ya kazi, kigango chako, na hata parokia yako?

Vile vile katika jamii yetu leo wapo wengi wanaochukiwa bila sababu ya msingi, wanaotengwa kutokana na misimamo yao katika kweli na haki, wanaoshutumiwa na kunenewa uovu kwa sababu tu wanapenda kumuishi Kristo na kuwa pembeni ya kundi ovu linalopendwa na wengi. Hawa Kristo anasema thawabu yao ni kubwa mbinguni.Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo,” Lk 6:22-23.

Kinyume chake ni wale wanaopenda kuonwa wema na kusifiwa hata kama hawajafanya chochote. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo,” Lk 6:26. Hawa taji lao ni unabii wa uongo ambalo halina thamani yoyote mbele ya Mungu. Hawa ndio wale wanaopoteza muda na maisha yao kila siku kuwapendezesha watu na wao wenyewe kutaka kupendezeshwa. Ni sawa na parachuti lililojaa hewa na kuelea juu kabisa angani na mara hufikwa na kikomo linapokutana na ncha ndogo sana ya mwiba. Hewa yote hutoweka na kusinyaa.

Tumsifu Yesu Kristo!

Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu,” Lk 6:22

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie moyo wa huruma na upendo kwa wote tunaoishi nao. Amina


No hay comentarios:

Publicar un comentario