domingo, 4 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 23 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 23 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 5:1-8
Zab/Kit: 5:5-6, 7, 12
Injili: Lk 6:6-11
Nukuu
Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye,” 1Kor 5:1 

Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo,” 1Kor 5:2 

 “Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli,” 1Kor 5:7b-8

Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama,” Lk 6:8 

Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?” Lk 6:9 

 “Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu,” Lk 6:11 

TAFAKARI: Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika.”

Wapendwa wana wa Mungu, kutokuwa na hofu ya Mungu ndani mwa mtu umuondolea aibu na woga wa kutenda yale yasiyo mpendeza Mungu. Mtu wa mtindo huo ujazwa ujasiri kwa yasiyo dhaniwa kufanywa kwa akili ya kawaida. Hali na mazingira haya yanaikuta jumuiya ya Korintho, hasa kwa swala la mahusiano ya kimapenzi katika familia. Hii ni zinaa mbaya sana! Naye Mtume Paulo anasema, Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye,” 1Kor 5:1. Pamoja na hali hiyo mbaya kimaadili, jambo hilo haliwaogofi jumuiya ya Korintho. Badala yake wanajisifia na kujipongeza. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo,” 1Kor 5:2. Jamii inayofurahia uovu anguko lake ni kubwa sana.

Yaliyotokea Korintho nyakati hizo za Mtume Paulo si mageni tuitazamapo jamii yetu leo. Zipo kesi nyingi tu za mahusiano ya kimapenzi kati  ya familia na hata ndugu wa damu. Jambo hili linakuwa baya sana pale hali hiyo inapochukuliwa kama jambo la kawaida licha ya kufanywa kwa usiri mkubwa. Hata hivyo uzito wa jambo hili haupo tu kwa swala la mahusiano ya karibu na ya kimapenzi kwa ndugu wa karibu na wa damu, bali uzito huu upo pale ambapo jamii ufurahia uovu na hata kuubariki kuendelee.

Leo kwa sababu zetu binafsi na maslahi binafsi, tunakosa nguvu ya kimaadili kukemea uovu kwa vile tu mtenda uovu huo yu upande wetu. Ni swahiba wetu, nk. Mwono huu na kiwango hiki cha uelewa ni anguko kubwa la jamii. Na hivi ndivyo asemavyo Mtume Paulo, Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo,” 1Kor 5:3. Jamii inapokosa ule uthabiti wa kusema, kuonya, na kukosoa katika maana ya kujenga, kesho ya jamii hiyo inakabiliwa na giza nene sana. Uhalalishaji wa uovu ni njia na sababu mojawapo ya kuiua dhamiri hai ndani ya mtu. Hali  hii siyo ya kufumbia macho hata kidogo!

Kwa ushauri wake Paulo anasema, lazima  kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu,” 1Kor 5:5. Maana yake ni kwamba, uovu ni uovu tu, hatuwezi kuuhalalisha kwa jambo au namna yoyote lile. Tatizo kubwa hapa ni woga na unafiki wa kusema lililo kweli hasa pale jambo hilo, yaani, uovu linapofanywa au kutendwa na kwenye nguvu na katili, au mamlaka fulani.

Na mara zote swali kubwa hubaki kuwa hili, ‘ni nani atakaye mfunga paka kengele?’ Badala yake wengi kwa unafiki tunabaki kusifia hali hiyo na wakati mwingine kujisifu wenyewe tukifikiri kwamba kwa kufanya hivyo  tutabaki salama. Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima?” 1Kor 5:6. Mambo makubwa na yakushangaza machoni mwa watu leo yalianza kidogo kidogo na watu kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote ile ya kukemea kwa sababu ya hofu, woga, na unafiki.

Salama yetu ipo katika kweli na haki. Na usalama upo pale tutakapo kuwa tayari kuona ukweli wa jambo kama lilivyo, na siyo kama tulivyo. Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu,” 1Kor 5:7. Chachu hiyo ya kuona jambo kama lilivyo ipo ndani ya kila mmoja wetu. Na hii ndiyo dhamiri hai ndani ya mtu. Tusiisaliti dhamiri hii kwa urafiki upofu au kujionea huruma na kutaka watu watuonee huruma. “Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli,” 1Kor 5:7b-8. Kristo kwa Mkristo ndiyo kielelezo halisi ya kupambana na uovu.

Mkristo mwenye kufumbia macho uovu ajue kwamba haishi maisha ya ufufuko. Mkristo mwenye kuishi maisha ya ufufuko uyatafuta yaliyo juu kule Kristo aliko. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi,” Kol 3:1-2. Na mwenye  kuridhia na kuushabikia uovu, hata kama anaishi hana uhai ndani yake.

Kristo anatutaka tuwe na uhai, na tena tuwe nao tele. Kristo Yesu ndiye Njia, kweli, na Uzima wetu, Yoh 14:6. Kristo akiwa ndiye Mchungaji mwema wa kondoo zake, anajitofautisha na mwivi mwenye nia ya kuiba na kuwachinja kondoo. Katika hili Yesu anasema, Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10.10-11. Ni kwa namna hiyo ya uchungaji mwema, na akiwa katika sinagogi akifundisha siku ya sabato, Yesu anakutana na mtu aliyepooza mkono, Lk 6:6. Huyu ni kondoo wake na mwenye kuhitaji uponyaji. Kwa upande wa pili, Mafarisayo walioishikilia sheria ya sabato hasa kutokufanya kazi, wanamtega Yesu waone atakachofanya ili wawe na sababu ya kumtia hatiani, Lk 6:7. Watu hawa hawana nia ya kuutokomeza uovu, bali kuuridhia na kuushabikia uovu kwa manufaa yao binafsi.

Pamoja na hali na mazingira hayo Yesu anasimamia mafundisho sahihi juu ya Upendo wa Mungu, na kuuvunja ukimya ule wa uovu. Na ndivyo alivyo yatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama,” Lk 6:8. Huu ndio ujasiri wa Mkristo hai na mwenye kuiona kweli, kuisema kweli, na kuisimamia kweli. Na baada ya kuiona kweli, kuisema kweli, na kuisimamia kweli, ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?” Lk 6:9. Swali hili la Yesu limebeba mafundisho ya kweli kuhusu huruma na upendo wa Mungu.

Lengo la Yesu hapa ni kuziamsha kama siyo kuzifufua dhamiri zao zilizokuwa zimekufa. Aulizalo Yesu kwa Mafarisayo anakuuliza wewe na mimi pia. Na mwisho katika kuisimamia kweli kisawa sawa, Yesu akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Lk 6:10. Na hili ndilo anguko lao wale wauridhiao na kuushabikia uovu, wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu,” Lk 6:11. Mwisho wa chuki ni aibu!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?” Lk 6:9


Tusali:-Ee Yesu, tufanye vyombo vyako vya haki, kweli, Upendo na Amani. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario