IJUMAA
WIKI YA 24 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 15:12-20
Zab/Kit: 17:1, 6-7, 8, 15
Injili: Lk 8:1-3
Nukuu
“Basi,
ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu
husema kwamba hakuna kiyama ya wafu?” 1Kor
15:12
“tena kama Kristo
hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure,” 1Kor 15:14
“Lakini sasa
Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala,” 1Kor 15:20
“na wanawake
kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni
Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,” Lk 8:2
“na
Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa
wakimhudumia kwa mali zao,” Lk 8:3
TAFAKARI: “Na
kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure.”
Wapendwa wana wa Mungu, katika ulimwengu huu wa vitu na ‘ponda mali
kifo chaja,’ unajaribu kwa namna yoyote ile kuondoa uwepo wa Mungu, na kumwinua
mwanadamu kama hatma ya kila kitu. Kwa nini uwepo wa Mungu ni tatizo katika
ulimwengu huu wa vitu na ponda mali kifo chaja? Uwepo wa Mungu unasema kuhusu
hatma ya mwanadamu ikiwa ni maisha baada ya kifo. Uwepo wa Mungu unasema na
kuzisuta dhamiri zetu kuhusu; kweli, haki, upendo na huruma. Hizi ni tabia na
hali ya Mungu. Binadamu katika ulimwengu wa vitu na starehe zake, ni aheri
aishi bila uwepo wa Mungu kwani unamwogofya kuhusu kiyama na hukumu yake.
Mtume Paulo katika somo letu la leo anauweka bayana mpango mzima wa
historia yetu ya wokovu na kile kitakacho jiri siku ya mwisho. Ukweli ni
kwamba, “ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma
Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini
ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4.4-5. Hivyo Kristo
kama kielelezo chetu ndiye pia hitimisho letu na hakimu yetu.
Mateso na kifo chake
Kristo yanasema zaidi kuhusu ukombozi (wokovu wa mwanadamu), na maisha ya
umilele, yaani, ufufuko baada ya mateso na kifo cha Kristo- mtu yule mwenye
haki. Katika mtazamo huu, mateso hayatenganishwi na ukombozi, na wala ukombozi
hautenganishwi na ufufuko. Kwa maneno mengine, palipo na utukufu palitanguliwa
na msalaba, na palipo na msalaba panatupeleka katika utukufu. Hali na mazingira
haya ya Mateso, Msalaba, Wokovu, Ufufuko, na Utukufu yanasema sana kuhusu Yesu
Kristo. Na mazingira hayo na hali hizo, zinasema sana kuhusu kiyama ya wafu.
Ndugu yangu unayesafiri
nami katika tafakari hii, kupoteza muda wako na nguvu zako kupinga uwepo wa
Mungu na kiyama ya wafu ni sawa na kutwanga maji katika kinu. Kama wabisha nipe
hakikisho la wewe kwamba hauzeeki na hutokufa. Ukweli ni huu ambao wengi
hatupendi kuusikia; “hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala
hakuna afaye kwa nafsi yake,” Rum 14:7. Ni katika uelewa huu kwamba Mtume Paulo
anauliza swali hili, “Basi, ikiwa Kristo
anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba
hakuna kiyama ya wafu?” 1Kor 15:12. Ufufuko
wa Bwana wetu Yesu Kristo wasema sana juu ya upya wa maisha, na hesabu ya
maisha hayo ya upyaisho siku ya mwisho-kiyama.
Wapendwa wana wa Mungu, yapo mambo mengi
naweza kuwa na mashaka nayo, ila hili sina shaka nalo hata kidogo. Ukitazama
wale wote walikuwa na hofu ya Mungu, na kwa namna moja au nyingine walianzisha
mifumo ya maisha na kuwaongoza watu katika imani fulani, waliishi na mwisho wa
siku walikufa. Ukweli huu ni pamoja na Kristo mwenyewe. Kristo alizaliwa kama
Mungu na Mwanadamu katika asili hizo
mbili; na kwa namna ya pekee, aliishi na kuhisi uchungu na mateso kama wanadamu
wengine ingawa hakutenda dhambi, 1Pet 2:21-22, na mwisho alikufa. Lakini jambo
la pekee ni hili, alikaa kaburini siku ya kwanza, ya pili, na ya tatu
alifufuka. Wengine, yaani, waazilishi wa mifumo ya maisha na hofu ya Mungu
kiimani, tangu walipolala hadi leo hawajaamka. Hawa wanasubiri kuamshwa na
Kristo siku ya mwisho.
Hivyo kwa kufufuka kwake Yesu Kristo
kiyama ya wafu ipo. Tunatumaini kwamba nasi siku moja tutafufuliwa kutoka wafu
kwa sababau kielelezo chetu, yaani, Yesu Kristo, kesha yashinda mauti, Ebr 2:9.
Hivyo ni kiroja kufikiri kwamba, “kama
hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka,” 1Kor 15:13. Kweli juu ya Kristo
haituambii hivyo. Kristo kafufuka, na kiyama ipo. Hivyo ndugu yangu, mamlaka
fundishi ya Kanisa yanapata uzito wake kwa sababu Kristo anayetangazwa na
kuhubiriwa kesha fufuka. Ni katika mantiki hiyo kwamba, “kama
Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure,” 1Kor
15:14. Na lingekuwa jambo hili ni la kizushi tu (Ufufuko wa Kristo), basi
lisingeweza kudumu kwa miaka hiyo yote zaidi ya 2000. Mungu bado anafanya kazi
na watu wake kila siku. Ndugu yangu, “Kristo
amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala,” 1Kor 15:20. Na ndani na katika
Kristo wote watahuishwa.
Wapendwa wana wa Mungu,
Injili ya leo inatufundisha jambo la muhimu sana kuhusu maisha yetu ya kiroho
na mali tulizonazo. Jambo la muhimu siyo tu kusikia juu ya kule unakokwenda au
unako tarajia kwenda, bali kujua njia itakayo kufikisha kule unapokwenda ua
tarajia kwenda. Ukweli ni kwamba, waliokwisha kupata neema, baraka, na uponyaji
ni wale tu waliojinyenyekesha kwa Kristo mwanakondoo wa Mungu, na kumtumikia
kwa mali zao. Hawa ni wale walioifahamu njia ya kuwafikisha kule ilipo furaha
yao ya ndani na ya kweli.
Hawa ndio wale “wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo
wabaya na magonjwa wakaponywa; na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa
mali zao,” Lk 8:2a, 3b. Je, ndugu yangu, una uhusiano wa namna gani kati ya
maisha yako ya kiroho na mali ulizokuwa nazo?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini
sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala,” 1Kor 15:20
Tusali:-
Ee Yesu, tuongoze katika njia iliyo sahihi kila siku ya maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario