sábado, 24 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 26 YA MWAKA-C


JUMATATU WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Somo: Ayu 1:6-22

Zab/Kit: 17:1, 2-3, 6-7

Injili: Lk 9:46-50

Nukuu:

“Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao,” Ayu 1:6

 “Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu,” Ayu 1:8

 “Wakaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao,” Lk 9:46

“akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa,” Lk 9:48

TAFAKARI: “Maisha ni Jaribu, yakupasa kulishinda.”

Wapendwa wana wa Mungu, mwelekeo huu wa maisha, “maisha ni jaribu,” huonekana katika hadithi ya Biblia yote. Wakati wote Mungu huijaribu tabia ya watu, imani yao, utii, upendo, ukamilifu na uaminifu wao. Mungu alimjaribu Ibrahimu kwa kumwambia amtoe sadaka mwanae Isaka. Mungu alimjaribu Yakobo alipopaswa kufanya kazi miaka ya ziada ili kumpata Raheli kama mkewe. Na katika somo la leo tunaona Ayubu anajaribiwa na Mungu Imani na utajiri wake.

Adamu na Hawa walishindwa jaribio katika bustani ya Edeni, na Daudi alishindwa majaribu yake kutoka kwa Mungu mara kadhaa. Lakini Maandiko Matakatifu hutupa mifano mingi ya watu walioshinda majaribu makubwa mfano Yusufu, Ruthu, Esta na Daniel. Mungu anajua wazi maisha ya Ayubu na uaminifu wake. Naye Mungu anasema, “hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu,” Ayu 1:8b

Lakini jambo la ajabu katika simulizi hili tunaona mazungumzo Mungu na shetani juu ya Ayubu. Fundisho ni kwamba, Mungu anaweza kuruhusu ovu ila hawezi kuwa sehemu ya uovu ule. Na lengo siyo kupoteza bali kuimarisha kile kinachojaribiwa. Pamoja na ukweli kwamba Mungu alilijua undani wa Ayubu, anamruhusu shetani kuijaribu imani na utajiri wake bila kumdhuru Ayubu. “Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana,” Ayu 1:12. Ayubu anapoteza yote ikiwa ni familia yake, mifungo yake, wahudumu wake, na anabaki yeye mwenyewe, Ayu 1:13-19.

Hata pamoja na hali na mazingira haya ya kupoteza vyote, Ayubu hakumdhihaki Mungu wala kufanya kufuru yoyote ile, Ayu 1:22.  “Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe,” Ayu 1:20-21. Ikiwa dunia na vyote ni mali ya Mungu, Zab 24:1, hatuna sababu ya kulalamika wa kuhuzunika kwa sababu hakuna kilicho chetu zaidi ya kumilikishwa kwa muda mfupi tu.

Hakuna furaha yoyote ile kama kigoto chetu cha maisha na fikra yote tukiiweka kwenye mali. Kujiambatanisha na vitu hupunguza dhamani ya maisha yetu na kupoteza kabisa lengo lile la kuumbwa wetu. Tumeumbwa tuishi milele. Mali na utajiri ulionao ukusaidie kuufikia uzima wa milele na siyo mwenye mwisho wa mali hizo kwani kwayo hazima umilele.

Ndugu yangu, ukweli ni kwamba majaribu hukuza tabia na kuiweka wazi, na maisha yote ni majaribu. Siku zote unajaribiwa. Mungu siku zote anatazama unavyoenenda kwa watu, matatizo, mafanikio, migongano, magonjwa, mambo ya kukatisha tamaa, hata hali ya hewa!

Mungu anaangalia hata matendo rahisi sana kama vile unapofungulia mlango wengine, unapookota kipande cha takataka, unapoonyesha upole kwa karani au mhudumu, unapomsikiliza mfanyakazi wako wanyumbani, nk.

Ndugu, ukweli ni kwamba hatuyajui majaribu yote ambayo Mungu anatupa lakini tunaweza kutabiri baadhi yake, kwa kuzingatia Maandiko Matakatifu. Utajaribiwa kwa mabadiliko makubwa, kucheleweshwa ahadi, matatizo magumu, sala zisizojibiwa, lawama zisizostahili, na hata mikasa isiyo na sababu.

Ndugu, katika maisha yangu nimetambua kuwa Mungu anajaribu imani yangu kupitia matatizo, anajaribu tumaini langu kwa njia ya mali, na anajaribu upendo wangu kwa njia ya watu. Kila mmoja analo jaribu lake. Jaribu la muhimu sana ni jinsi unavyotenda unapoacha kuhisi uwepo wa Mungu katika maisha yako. Wakati mwingine Mungu hujiondoa kwa makusudi, na hatuoni uwepo wake.

Mfalme Hezekia alipatwa na jaribu hili. "Walakini kwa Habari ya wajumbe wa wakuu wa Babeli, waliotumwa kwake kuuliza ajabu iliyofanywa katika nchi, Mungu akamwacha, ili amjaribu, ili kwamba ayajue yote yaliyokuwemo moyoni mwake." 2Nya 32:31. Hezekieli alikuwa amefaidi ushirika wakaribu na Mungu,  lakini kwa wakati wa muhimu sana Mungu alimwacha peke yake ilia mpime tabia yake, adhihirishe udhaifu wake, na amwandae kwa MAJUKUMU ZAIDI. Kumbe lengo la majaribu si kutuangamiza, bali tunaandaliwa kwa mambo makubwa zaidi, na kwa malengo makubwa zaidi ya Mungu.

Ndugu, ukielewa kuwa maisha ni jaribu, unatambua kuwa hakuna kitu kidogo katika maisha yako. Hata tukio dogo sana lina maana kubwa katika kukuza tabia yako. Kila siku ni siku ya muhimu, na kila dakika ni wasaa wa kukua kitabia, kuonyesha upendo, au kumtegemea Mungu. Majaribu mengine hata huyatambui. Lakini yote  haya yana matokeo ya milele.

Habari njema ni kwamba Mungu anakutaka ushinde mtihani huo wa maisha, kwa hiyo haruhusu majaribu unayoyapata kuwa makubwa kuliko neema anayokupatia katika kukabili majaribu hayo." Jaribu haliwapati ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hata waacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili." 1Kor 10:13

Ndugu yangu, kila unaposhinda jaribu, Mungu hutambua na kupanga kukupa tuzo la milele. Mtume Yakobo anasema, "heri mtu astahimikiye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao." Yak 1:12. Na majaribu mengine tuyapatayo katika maisha utufundisha fadhila ya unyenyekevu. Na ukubwa wako mbele ya Mungu haujengwi wala kupimwa kwa mali, sifa, umaarufu au nguvu zako kiushawishi ulizo nazo, bali ukubwa wako huu upimwa kwa kiasi kile cha unyenyekevu ulichonacho mbele zake Mungu.

Bila kufahamu ukweli huu, yaani, ‘kipimo hiki cha unyenyekevu,’ ni rahisi kuipoteza njia na tumaini lake, yaani, uzima ule wa milele. Leo katika somo la Injili tunaona njinsi ambavyo wanafunzi wa Yesu wakibishana njiani kuhusu ‘nani aliyemkubwa kati yao.’ Kutafuta ukubwa na ukuu bila kujua mapaswa na matakwa yake, ni chanzo kikubwa sana cha kwenda kinyume na mpango wa Mungu na watu wake. Jaribu hili la ‘ukubwa na kutaka kuwa wakubwa kiiutawala bila sifa na siha’ ni jaribu kubwa sana kwa walio wengi.

Yesu baada ya kutambua ukweli huu, ‘minyukwano ya ukubwa,’ ndani ya mioyo ya wanafunzi wake, anawapa angalizo ya kile wanachokitamani. Naye Yesu anawaambia wanafunzi wake kwa mfano, “Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa,” Lk 9:48. Udogo anauongelea Yesu ni ule utayari wa kujifunza, kumtegemea Mungu pasipo shaka kama afanyavyo mtoto kwa mzazi wake, kujishusha na kujinyenyekeza hasa tutoapo huduma kwa wengine pasipo kujiinua binafsi zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, ye yote atakaye fanya tendo lolote la upendo, matumaini, na imani hata kama si mmoja katika mtazamo wa kundi unaloishi na jumuiya unayoshirikiana nayo, mtu huyo hayupo kinyume cha matamanio ya Mungu kwetu. Jambo hili Yesu analiweka sawa anapopata taarifa ya wanafunzi wake walipomkataza mtu mmoja kutenda lililojema eti kwa vile tu hakuwa mmoja wao. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu,” Lk 9:50. Kuwa kinyume na mpango wa Mungu ni pamoja na kule kutojisalimisha kwa mtu huyo katika mpango mzima wa wokovu wa Mungu. Ni pale pia tunapojiinua nafsi zetu na kusahau hatma ya maisha yetu. Ni pale pia kwa uhakika tunapojitanguliza mbele zaidi na kusahau usalama wetu upo chini na jemedari wetu Mkuu Yesu Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa,” Lk 9:48b

Tusali:-Ee Yesu, tuimaishe katika majaribu yetu ya kila siku. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario