miércoles, 28 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 26 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Somo: Ayu 42:1-3, 5-6, 12-16

Zab/Kit: 119:66, 71, 75, 91, 125, 130

Injili: Lk 10:17-24

Nukuu:

“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika,” Ayu 42:2

 “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona,” Ayu 42:5

 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19

“Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20

TAFAKARI: “Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, Wanafunzi wa Yesu wale sabini, wanarudi katika utume wao na kustajabia mambo makuu ya Mungu aliowatendea. Uhusiano wetu mzuri na Mungu ni chanzo kikubwa sana cha furaha yetu ya kweli. Lakini Yesu anawaambia wasiwe na furaha tu kwa sababu walimwona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme, bali ndani yao Mungu aweza kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na n’nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19. Huu ndio msingi wa furaha ya kweli kwa wale wote wenye hofu ya Mungu. Mahusiano mazuri na Mungu, hutujengea uwezo mkubwa sana wa kupambana na uovu.

Mara tuyaonapo haya makuu yakifanyika ndani mwetu tusibweteke. Dunia hii tunapoishi pamoja na uzuri wake na mambo yake, siyo mahali petu pa kudumu. Hapa ni mahali tu pa maandalizi ya umilele. Ni jukumu la kila mmoja wetu kupafanya hapa duniani kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi huku tukijua siyo sehemu ya mwisho na ya umilele. Maandalizi mazuri ya hapa duniani ndiyo jibu la uhakika wa maisha hayo ya umilele. Hivyo furaha yetu kwa yote tutakayoyapata hapa duniani itupe taswira halisi ya maisha baada ya haya. Kuhusu ukweli huu Yesu anawaonya wanafunzi wake nasi pia kwa kusema, Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20. Furaha yetu isiwe tu ya leo na kesho, bali furahi hii ipewe kibali na Mungu Baba wa Mbinguni. Tufurahi na Mungu milele mbinguni.

Wapendwa wana wa Mungu, ufahamu wa siri na ukweli huu,  Mungu anautoa kwa wanyenyekevu wake wa moyo. Wanyenyekevu wa moyo hufunuliwa siri za Mungu kwa sababu wapo tayari kusikia, kufanya, na kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Hivyo Yesu anamshukuru Mungu kwa niaba ya wanyenyekevu wote wa Moyo na kusema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21b. Ni uchanga wetu kama watoto tupo tayari kujifunza, kusikiliza, kufanya, na kuishi kadiri ya matakwa ya Mungu.

Mara baada ya kuzama katika fumbo zima la maisha yake, na kugundua furaha na usalama wake upo kwa Mungu, na hasa pale alipojisalimisha kwake, Ayubu anayaona makusudi ya Mungu katika maisha yake. Naye anamwambia Mungu, “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika,” Ayu 42:2. Mungu hujua mipango ya kila mmoja wetu kwa sababu kama Baba utuwazia yaliyo mema siku zote, Yer 29:11. Ayubu anaona udogo wake katika upendo huu wa Mungu ulio wa ajabu.

Ayubu kwa upande mwingine anatukumbusha kuweka lawama mbali mara tupatwapo na majanga katika maisha. Swali la kujiuliza katika hali hiyo ya sintofahamu ni hili; Je, Mungu anataka kunifundisha nini kwa hili lililonitokea? Naye Ayubu anaihoji nafsi yake na kusema, “ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua,” Ayu 42:3. Mungu aliyeonekana kuwa mbali sana, na wa historia, sana anaonekana kuwa karibu na rafiki wa ajabu. Kwa kinywa chake Ayubu anakiri kweli hii na kusema, “nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona,” Ayu 42:5. Kumbe furaha ya kweli ni kujenga urafiki wa karibu na Mungu.

Ukaribu na Mungu ukukumbusha udogo wako, na mapaswa yako katika kweli na haki. Ukaribu wako na Mungu ukuongezea hofu ya Mungu ndani yako, na hivyo kuwa mikono salama zaidi. Na ukaribu wako na Mungu ukunyenyekesha na kuwa tofauti katika, kuona, kuamua, na kutenda. Na ndivyo ilivyokuwa kwa Ayubu anapojitazama na kuchukua hatu. Ni kwa “sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu,” Ayu 42:6. Ukaribu wako na Mungu ukuongoza katika toba ya kweli na majuto. Unyenyekevu ule ukupelekeao kuona tofauti, kuamua tofauti, na kutenda tofauti, ni sawa na kuzaliwa upya na  katika nuru ya kweli, Mungu mwenyewe.

Kuzaliwa upya huku na kuwa katika nuru ya Mungu kunamrudishia hadhi yake Ayubu ikiwa ni pamoja na yale aliyoyapoteza hapo mwanzo, Ayu 42:13-15. Hakika mtu yule amtegemeaye Bwana hatopungukiwa na chochote. Mahangaiko na sintofahamu huwa za muda tu, na unapo simama imara kiimani katika hali na mazingira haya ya sintofahamu, Mungu ubaki kuwa mtetezi wako, mwaminifu kwako, na kukuongoza katika njia salama na kukubariki. “Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu,” Ayu 42:12. Nani kama Mungu?

Ndugu yangu tulio safiri zote katika tafakari hii, furaha ya kweli siyo kwa haya tunayojibovusha nayo leo na sasa, bali pale tunapopewa kibali na Mungu na kutuheshabiwa haki. Ayubu anapata kibali mbele ya Mungu na kuhesabiwa haki kwani Mungu alipendezwa naye.  “Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne,” Ayu 42:16. Mungu upendezwa na kila mmoja wetu tunapokuwa waaminifu katika Sura na Mfano wake, Mwa 1:27, kwa sababu ni kwa jinsi hiyo alikuumba, na kwa namna hiyo ataka uwe.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona,” Ayu 42:5

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie furaha ya ndani kwako na ndani yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario