KUMBUKUMBU
YA BIKIRA MARIA MAMA YETU WA MATESO
Somo: 1Kor 15:1-11
Zab/Kit: 118:1-2, 16ab-17, 28
Injili: Yoh 19:25-27
Nukuu
“Maana
mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi
Kanisa la Mungu,” 1Kor 15:9
“Lakini
kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si
bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni
neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10
“Na penye
msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa
Klopa, na Mariamu Magdalene,” Yoh 19:25
“Basi
Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu,
alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao,” Yoh 19:26
“Kisha
akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule
akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:27
TAFAKARI: “Mama, tazama, mwanao. Mwana
tazama, mama yako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Mama Yetu wa Mateso. Wapendwa
katika Kristo, ukiyatazama maisha yako na jinsi Mungu anavyoendelea kuwa upendo
na huruma kwako, hakika yote ndani yetu ni kwa neema ya Mungu. Hakika, “Bwana,
kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Mungu huyu
aliye Huruma na Neema anajidhihirisha wazi katika historia mbaya aliyokuwa nayo
Sauli wa Tarso.
Leo kwa neema ya Mungu,
Paulo anajulikana kama Mtume. Paulo anatoa ushuhuda wa maisha yake na kusema, “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili
kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu,” 1Kor 15:9. Hata pamoja
na ukweli huo, huruma na neema ya Mungu ni kubwa zaidi ya uovu wako kama
utajisalimisha kwake. “Lakini kwa neema ya
Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali
nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya
Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10. Mungu
yupo tayari kuanza upya nawe endapo tu kama upo tayari. Hizi ni neema za Mungu
zinazotuzunguka kila wakati. Na kwa namna ya pekee mwaka huu wa Kanisa wa
huruma ya Mungu ni wakati wa kutumia fursa hiyo vizuri.
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tunapo mtafakari Mama Bikira Maria kama Mama wa wateso, tafakari hii
inatupeleka moja kwa moja katika tukio lile kubwa la kukombolewa kwetu pale
Golgota-fufu la kichwa, ambapo kadiri ya masimulizi, Bikira Maria na Mtume
Yohana walikuwa chini ya Msalaba Yesu alipotundikwa juu yake. Katika tukio
hili, Bikira Maria anashiriki moja kwa moja mateso ya Mwanaye Mpendwa akiwa na
sitofahamu nyingi moyoni mwake. Bikira Maria kama Mama, bado anakumbukumbu
dhahiri moyoni mwake ambazo leo inakuwa kinyume chake. Naomba nikurudishe nyuma
ili uelewe mambo mazito yaliyokuwa ndani ya moyo wa Mama Maria ambayo leo
katika tukio hili anakosa majibu yake.
Ndugu yangu tunaye
safiri sote katika tafakari hii, katika tukio lile la kupashwa habari Mama
Bikira Maria aliambiwa haya na Malaika Gabrieli; “Tazama, utachukua
mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu,
ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba
yake,” Lk 1:31-32. Bikira Maria alijiuliza haya moyoni mwake akiwa chini ya
Msalaba ule aliye tundikwa mwanaye, ‘haya ndiyo hayo makuu ya mwana wa aliye
juu na Bwana Mungu ndiye ameamua kumpa kiti cha mtindo huu?’ Kama Mama, Bikira
Maria alikuwa na uchungu mkubwa sana! Hili ni jaribu kuwa sana la Imani kwa
Mama Bikira Maria.
Bikira Maria katika
hali hii ya uchungu alitafakari pia aliyoambiwa na Malaika Gabrieli kwamba, “Ataimiliki
nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:33.
Matokeo yake leo anaona Mwanaye Mpendwa kusubishwa kati ya waovu, wezi wawili.
Maswali yake ni haya; Mungu anawezaje kuruhusu hali hii? Na katika hali na
mazingira haya ya fedheha awezaje basi Mtoto wangu kuwa na utawala usio na
mwisho? Hata hivyo, Bikira Maria aliendelea kubaki chini ya Msalaba akiamini
pasipo shaka neno hili la Mwanaye, “NITAFUFUKA!”
Bikira Maria kama
Mwanamke na Mama, ni taswira hai ya Mungu Baba aliye ishi ufu wa mtoto wake.
Mungu katika tukio hili kama Mama amemtaka sadaka kubwa sana. Tukio hili la
Mama Bikira Maria linatufikirisha sadaka ile ya Ibarahimu aliyokuwa tayari
kuitoa kwa Mungu kwa mwanaye Mpendwa Isaka, Mwa 22:1-14. Kutoka na tukio hili,
Bikira Maria anaufunua ufahamu mkubwa na waajabu kuhusu Mungu, kutoka ndani ya
moyo wake kama mama. Bikira Maria ni mtu pekee anayeshirikishwa mateso,
uchungu, mahangaiko ya Mungu katika hali ya kibinadamu katika ushirikishwaji wa
thamani ile ya kukombolewa.
Katika hali hii ya
kushiriki mateso ya Mwanaye Yesu Kristo, Bikira Maria anapewa hadhi ya kuwa
Mama wa wanadamu yote bila kujali leo itikadi zao kiimani. “Basi
Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu,
alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao,” Yoh 19:26. Kwa tendo hili na kifo
chake Bwana wetu Yesu Kristo, sadaka yake Kristo pale Msalabani ni kwa binadamu
wote. Kama Mama katika ushiriki wa mateso haya, alichokitaka Mwanaye ni sawa na
alichokitaka Mama yake kama waswahili wasemavyo, “uchungu wa mwana aujuaye
mzazi wake.” Umama aliopenda Bikira Maria kama Mama ni hali hiyo aliyotupenda
Yesu upeo hata kuyatoa maisha yake kwa ajili yako na yangu. Ni katika mantiki
hii, Bikira Maria anashiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu, na kuzaliwa kwa
ubinadamu mpya kwa imani na kwa umoja na Kristo.
Neno
“Mama, tazama, mwanao,” Yoh 19:26, ni kweli yetu halisi kuhusu wito wetu. Yesu
anaendelea kutuambia kwamba sisi ni wana wa kweli katika mwana. Yesu amekwisha
fanywa ndugu yetu. Na katika kweli hii, sisi kama wafuasi wa Kristo, Mama Maria
ndiye Mama Yetu. Ni wito wetu sasa kumchukua Mama Maria katika mioyo yetu kwa
sababu uhakika huo tunao. Ni katika maana hiyo kwamba, “tangu saa ile
mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:27. Mama Bikira Maria chini
ya Msalaba aliishikilia tumaini ile ya ufufuko wa mwanaye Yesu Kristo pasipo
shaka yoyote ile. Na katika uhimara huu wa imani, alisubiri ufufuko wa mwanaye.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Na tangu saa
ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:27b
Tusali:- Ee
Yesu Mwema, asante kwa uwepo wa Mama yako aliyeyashiriki Mateso yako. Nasi kwa
kupitia Mama yako Mpenzi tushiriki Mateso yako.Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario