JUMAMOSI
WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 4:6-15
Zab/Kit: 145:17-18, 19-20, 21
Injili: Lk 6:1-5
Nukuu
“Basi
baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato?”
Lk 6:2
“Yesu
akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na
njaa, yeye na wale aliokuwa nao?” Lk 6:3
“Akawaambia, Mwana
wa Adamu ndiye Bwana wa sabato,” Lk 6:5
“Maana nadhani ya
kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa
sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu,” 1Kor 4:9
“Sisi
tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo;
sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati
heshima,” 1Kor 4:10
TAFAKARI: “Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo. Mwana wa
Adamu ndiye Bwana wa sabato.”
Wapendwa wana wa Mungu, Kristo ni kielelezo cha
yote yale tuyafanyayo ili tuurithi ufalme wa Mbingini tulioandaliwa na
kuutamani. Kristo ndiye dira na mpango mzima wa Mungu kwa wokovu wetu. Na “hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu
alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini
ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4.4-5. Leo Yesu
anataka Wayahudi, Wewe, na Mimi tuelewe kwamba yale yote tuyafanyayo yaendane na
thamani ya upendo wa Mungu kwetu, na Yeye, yaani, Kristo ndiye msingi wa vyote.
Yesu hapingi kuzishika sheria na kuzihemu,
bali anachokipinga ni tabia ile ya kuzishika sheria hizo pasipo ufahamu wake na
umaana wake. Sheria hizo wazishikazo Mafarisayo na waandishi badala ya
kuwafanya watu wawe karibu na Mungu, zilizidi kuwatenganisha watu na Mungu.
Ndiyo maana Wayahudi walikuwa wepesi sana kuona katazo la sheria na adhabu
yake, kuliko elekezo la sheria katika ukamilifu. “Basi
baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato?”
Lk 6:2. Kwa kuziamsha dhamiri zao zilizolala, Yesu anawaonyesha mkanganyika wa
sheria hizo wanazozishika bila ufahamu na umaana wake. “Yesu
akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na
njaa, yeye na wale aliokuwa nao?” Lk 6:3. Mfano huu ni moja tu ya mapungufu ya
sheria zile walizokuwa wakizishika ambazo kwa uhakika haikuwa torati kama
alivyowaachia Musa, bali tafarisi yake, yaani, Talmud.
Tendo walilofanya wanafunzi wa Yesu,
yaani, ‘siku ya sabato kupita katika mashamba,
na kuvunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao, 1Kor 4:1, tendo
hilo halikuwa tofauti na kile alichofanya Daudi, yaani, kuingia katika nyumba
ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe,
ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao, Lk 6:4. Sheria hizi na hasa tafasiri ile ya torati, Talmud,
zilikuwa na mapungufu makubwa. Ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa ili kukidhi
mahitaji yao binafsi.
Kristo akiwa msingi wa
maisha yetu na sababu ya yale yote tuyafanyayo, tutakuwa huru kweli kweli
tukijua ni nani tunayemtumikia. Hivyo Yesu anawaambia Wayahudi “Mwana wa Adamu
ndiye Bwana wa sabato,” Lk 6:5. Kristo ndiye
mizania ya kweli kuhusu Mungu tunayemwamini na kumwabudu. Kristo ndiye anayejua
siri ya ufalme wa Mungu. Ndugu yangu, Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh
14:6. Akiupigilia msumari wa mwisho, Yesu anasema, “hakuna mtu awezaye kuja
kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44.
Kristo ndiye itimisho, Siku ya Bwana, na Bwana wa siku ya Bwana, yaani, Sabato.
Mtume Paulo na wenzake, walizama ndani
kabisa katika fumbo hili la Kristo, yaani, kielelezo hai na itimisho la yote.
Na ndivyo Paulo anavyowataka jumuiya ile ya Korintho wamuona Kristo kupitia
maisha yao. “Basi
ndugu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu, ili
kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja
wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe,” 1Kor 4:6. Kila
mbatizwa na mfuasi wa Kristo, ni Kristo mwingine pale alipo. Maisha ya Mkristo
lazima yaakisi maisha ya Kristo. Akiyaona maisha yake kama Mtume, Paulo
anasema, “maana nadhani ya kuwa Mungu
ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu
tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu,” 1Kor 4:9.
Ndani na katika Kristo,
Mtume Paulo hayaogopi mateso kwa ajili ya Kristo. Mtume Paulo na wenzake
hawahuzuniki wala kudhihakiwa kwa ajili ya Kristo. Na wala hawaoni aibu kuitwa
wapumbavu kwa ajili ya Kristo. Nasi wafuasi wake Kristo hatuoni haya
kudhihakiwa kwa ajili ya Kristo Yesu. Hivyo Mtume Paulo anaiambia jumuiya ile
ya Wakristo wa Korintho kwamba, “Sisi tu
wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi
tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati
heshima,” 1Kor 4:10. Huu ni mtazama chanya wa Mkristo ambaye Kristo Yesu ni
kielelezo na hitimisho la yote katika maisha yake.
Je, waisikia kiu ya Kristo katika
maisha yako? Kristo Yesu hubaki kuwa kiu yako kama Kristo Yesu ataendelea kuwa
kielelezo na hitimisho la yote katika maisha yako. Katika kweli hii Mtume Paulo
anasema, “hata
saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao,”
1Kor 4:11. Mkristo mwenye mwono huu chanya katika maisha yake amtazamapo
Kristo, mara zote ukabiliana na uovu kwa wema. Na “kisha twataabika tukifanya
kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili,”
1Kor 4:12. Hali na mazingira haya ambapo Kristo huwa kila kitu kwetu, utujengea
furaha ya ndani katika mateso.
Na ndivyo ilivyo
kwamba, “tukisingiziwa twasihi; tumefanywa
kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa,” 1Kor 4:13. Hii ni
furaha tuipatayao katika mateso tuwapo ndani na katika Kristo Yesu. Na mwenye
kuifahamu siri hii huwa baba wa wengi ambaye atawazaa wengi katika Kristo Yesu
kwa njia ya Injili. Mtume Paulo ni mfano halisi aliyeifahamu siri hii. Naye
anasema, “Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu
kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi
niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” 1Kor 4:15. Je, wapenda kuwa
mmoja katika siri hii? Kama jibu ni
NDIYO, basi anza leo kuwa na mwono chanya juu ya Kristo Yesu, na kuwa tayari
kuuvaa unyenyekevu kama Kristo alivyo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa
twastahimili,” 1Kor 4:12b
Tusali:-Ee
Yesu, kwako na kwako tu, tujalie furaha ya kweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario