sábado, 24 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 26 YA MWAKA-C



Somo I: Amo 6:1, 4-7

Zab/Kit: 146:7, 8-9a, 9bc-10

Somo II: 1Tim 6:11-16

Injili: Lk 16:19-31

Nukuu

“Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea,” Amo 6:1

“ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini,” Amo 6:4

 “Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole,” 1Tim 6:11

“Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi,” 1Tim 6:12

 “Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa,” Lk 16:19

“Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake,” Lk 16:20-21

 “Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu,” Lk 16:31

TAFAKARI: “Pambo la dunia: ‘kuvaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.’ Pambo la Roho ni ‘Neema ya Utakaso’”

Wapendwa wana wa Mungu, somo la Injili la tupa kisa cha tajiri na maskini Lazaro. Tajiri anajulikana kwa mwono wake, na maisha yake ya anasa na hilo ndilo pambo lake la dunia. Lazaro anajulikana kwa jina lake, umaskini wake na unyonge wake, na hilo ndilo pambo lake la Roho-pambo la mbinguni. Tajiri huyu anayafunua mapambo ya dunia ambayo ni mengi sana. Mapambo haya huipamba miili yetu na kuonekana nadhifu. Na baadhi ya mapambo haya ya dunia ni pamoja na “ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini,” Amo 6:4. Kula bila kutoka jasho na tena kwa dhuluma.

Pambo la dunia hii ni pamoja na “ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi,” Amo 6:5. Zipo baadhi ya nyimbo zenye kusifia mfumo wa kifisadi na kuwazubaisha watu kwa kuwafaidia kunakotokana na ujinga ambao umesababishwa na mfumo huo huo wa kifisadi.

Pambo la dunia hii ni pamoja na “ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu,” Amo 6:6. Akina Yusufu leo ni kama akina Lazaro, yaani, wale wote wanaotaabika kwa sababu mimi na wewe tumeshindwa kujali na kuwajibika kadiri ya nafasi na uwezo tulikuwa nao. Pamoja na hali ngumu ya maisha na umasikini uliokithiri katika jamii yetu, wapo watu wanaojibovusha kwa maisha ya starehe na anasa ilhali baadhi yetu hawana uhakika wa jioni yao.

Lazaro ambaye ni maskini wa kutupwa na kudharauliwa kwa kiasi kikubwa anayafunika mapambo ya mbinguni. Mapambo ya mbinguni ung’arisha nyoyo zetu na kuzifanya kama theluji. Pambo hili la mbinguni, yaani, pambo la Roho, ni ile Neema ya Utakaso tuipatayo kwa matendo yetu mema.

Kosa kubwa la tajiri huyu ni dhambi ya kutotimiza wajibu. Ndugu yangu, kabla ya kuendelea na tafakari hii nikuombe usali kwanza sala ya “NAKUUNGAMIA.” Dhambi ya kutotimiza wajibu, ni kosa la nne tunalokiri katika sala hii ya “nakuungamia Mungu mwenyezi.” Lazaro tunaambiwa mara zote alikaa kwenye mlango, ikimaanisha kwamba kwa vyovyote vile tajiri huyu alimwona Lazaro katika dhiki yake na ilimpasa tajiri huyu afanye kitu. Kutotimiza wajibu, ni kosa la kutokufanya kitu wakati ulitakiwa kufanya kitu hicho kwa sababu kipo chini ya uwezo wako.

Tajiri huyu anahukumiwa kwa kutokujali na kutokufanya chochote. Kosa hili la kutokuja ndilo linalowapeleka wana wa Israeli utumwani. “Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma,” Amo 6:7. Na hili silo jambo la kushangaza leo kuona mzawa anakuwa mtumwa kwenye nchi yake mwenyewe. Leo siyo jambo la ajabu kuona mgeni akimtumikisha mzawa kwa jeuri na kebehi ya hali ya juu. Huu ndio utumwa ambao leo kama Taifa tunakutana nao kwa sababu ya ubinafsi ya watu wachache.

Ndugu yangu, tazama mazingira unayoishi, Je, akina Lazaro hawapo? Wale Mungu aliotubariki kuwa na Magari binafsi, Je, unapofunguliwa geti hujamwona Lazaro pembeni akisubiri wema na upendo wako? Wale ambao hula vizuri kila siku na asubuhi kumwaga viporo vya wali na vipande ya samaki, Je, huwaoni akina Lazaro wakilichungulia shimo taka kwa masikitiko? Wewe ambaye kila siku huingia ofisini na mkoba wako, Je, humuoni Lazaro kwenye benchi akisubiri wema na huruma yako?

Ukweli ni kwamba, wote tutakufa na kujongea kiti cha ukumu. Tunapoishi hapa duniani, tunaaswa na mzaburi, “usiogope mtu atakapopata utajiri, na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab 49:16-17. Mambo yote yatupayo ufahari ipo siku tutayaacha. Je mbele ya Mungu tutafika na jambo gani kama utambulisho wetu? Bila Utakatifu huwezi kumwona Mungu.

 Ndugu yangu, kituo cha tisa cha njia ile ya Msalaba; Yesu anaanguka mara ya tatu. Njia ya msalaba kwa kutumia misale ya waamini, kuna maneno haya katika kituo hiki cha tisa; “Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee Yesu mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo mbinguni.” Katika kujibovusha huko, hujakutana na akina Lazaro? Hali hii ya kujibovusha ndiyo anayoikemea Nabii Amosi na kusema, “Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea,” Amo 6:1. Leo wapo watu kati yetu licha ya ugumu wa maisha kila kona wanaomba Mungu awape uhai na afya waendelee kuvitumbua walivyovikusanya kwa dhuluma na ufisadi.

Ila tunapojitesa na kuwajali wengine, hakika tutapata tuzo mbinguni. Mateso aliyoyapata Tajiri, alitamani na kuomba taarifa zile ziwafikie ndugu zake ili wasije patwa na mateso yale. Ibrahimu anamjibu, “Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.” Lk 16:29,31. Ndugu yangu, hapa Musa anawakilisha Sheri za Mungu na Amri zake. Manabii hapa ni wale  wahudumu wa neno la Mungu. Kwa maana nyingine tungesema, sisi kama wafuasi wa Kristo tunajua taratibu zitupasazo kuishi, ikiwa ni pamoja na Amri za Mungu.

Na Amri kuu kupita zote ni Amri ya upendo.Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii,” Mt 22:37-40. Pili, tumepewa wachungaji, na wapo muda wote kwa kutuhudumia hasa kiroho. Tunaonywa na kufundishwa kupitia mahubiri yao. Kwa kuyashika haya mawili na kuyaishi, basi tuzo tutalipata. Nje ya hapo tutegemee mateso makali. Je, tufanye nini?

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, salama yako na yangu ni kuyakumbatia mapambo ya mbinguni-pambo la roho. Naye Mtume Paulo anasema, “Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo (mapambo ya dunia); ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole,” 1Tim 6:11. Pambo la mbinguni ni pamoja na ‘kufuata haki.’ Na kutafuta ni kuwasaidia wale wote wanaohitaji masaada wako. Na imani ni tokeo au tunda la haki. Ni dhihaka na kejeri mbele ya Mungu, na maigizo kwa mwanadamu kuihubiri amani bila kuzingatia haki na kutenda haki.

Pambo la mbinguni ambalo ni pambo la roho ni pamoja na ‘kuishi utauwa.’ Kuishi utauwa ni kuzishika amri za Mungu na kuishi maisha ya utakatifu. Ni kufanya malipizi ya dhambi zangu zote nilizotenda. Ni kushiriki ibada Takatifu na kushiriki Sakramenti za Kanisa katika mastahili yake.

Pambo la roho yako ni pamoja na kuishi imani iliyo thabiti. Leo unapokutana na Mkristo mwenzako huwezi kujua kasimama au kachuchumaa katika imani. Tumekuwa na pozi la chura. Huwezi kujua kasimama au kachuchumaa. Ndugu yangu, “Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi,” 1Tim 6:12. Ni kuishi maisha ya ushuhuda wa kweli, na Kristo akiwa ndiye kielelezo cha kila kitu katika maisha yangu.

Pambo la roho ambalo ndilo pambo la mbinguni ni pamoja na kuishi ‘upendo, saburi, na upole.’ Upendo, Saburi, na Upole ni sifa za Mungu na ndivyo alivyo. Upendo, Saburi, na Upole huu wa Mungu umefunuliwa kwetu wazi kwa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, yaani, Yesu Kristo. Huyu ndiye wewe na mimi tunayeagizwa “mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele,” 1Tim 6:13a, 16. Amina!

Ikiwa yapata miezi sita tangu Mzee Thomas Sasambua na familia yake kuhamia kwenye nyumba yao mpya na ya kisasa kutokea mtaani kwao, alimwomba Padre aibariki nyumba hiyo ili kuzipata neema na baraza za Mungu.

Padre pasipo shaka na kwa nafasi aliyokuwa nayo Mzee Thomas kama mwenyekiti wa baraza la wazee parokiani, alikwenda kuibariki nyumba ile. Dada Getruda ambaye ni mfanyakazi wa ndani, alimsaidia Padre kubeba chombo cha maji ya Baraka wakati Mama na Baba wa familia ile wakiwa wanaandaa vitafunwa baada ya zoezi hili.

Wakati zoezi hili likiendelea ndani mle, kwenye kona fulani kulionekana kuwa na kifurushi fulani hivi. Ndipo kwa udadisi Padre alimuuliza Dada Getruda, “na hicho hapo ni nini?” Getruda ambaye alishindwa kujizuia kwa uchungu ule na kuanza kulia, alijibu, “Baba Padre hicho ndicho kitanda changu. Usiku baada ya kumaliza kuosha vyombo na kupiga nyumba deki, hukunjua kirago hicho na kujilaza katika korido hili.” Tendo hili lilimsikitisha sana Padre.

Baada ya zoezi lile la kubariki nyumba, Mzee Thomas Sasambua alimkaribisha Padre kinywaji na chakula. Kwa hali ilivyokuwa, Padre alimjibu na kumwambia, “hongera sana Mzee Thomas kwa nyumba nzuri na ya kisasa. Ila kuna mwana familia yako mmoja bado analala nje. Na mwana familia huyo ni Binti huyu Getruda. Fanya utaratibu naye alale ndani. Asante kwa chakula na kinywaji. Siku Getruda akilala ndani ya nyumba yako nitaarifu nitakuja kula na kunywa. Asante na kwa heri.” Padre aliondoka.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu,” Lk 16:31

Tusali:-Ee Yesu tujalie Neema ya kuyatamani mapambo ya mbingu, pambo la roho-Neema ya Utakaso. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario