JUMAMOSI
WIKI YA 24 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 15:35-37, 42-49
Zab/Kit: 56:10, 11-12, 13, 14
Injili: Lk 8:4-15
Nukuu
“Lakini
labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?” 1Kor 15:35
“Ewe
mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo
uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au
nyingineyo,” 1Kor 15:36-37
“Mpanzi alitoka
kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka
karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila,” Lk 8:5
“Nyingine
zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena
hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie,” Lk 8:8
“Na wale penye
mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana
mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13
“Na
zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa
na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote,” Lk 8:14
“Na
zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao
hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia,” Lk 8:15
TAFAKARI: “Na
zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao
hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.”
Wapendwa wana wa Mungu, Leo
Yesu anatupa mfano wa Mpanzi akitutaka kuujenga uhusiano mzuri na Mungu kupitia
neno lake. Simulizi hili la Mpanzi linasimuliwa na wote watatu-‘fanana,’ (Mt
13:1-9, 18-23; Mk 4:1-20, Lk 8:4-15). Neno la Bwana ni uzima kwetu na neno hilo
hututoa mautini na kuingia uzimani. “Amin,
amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka
yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini
kuingia uzimani,” Yoh 5:24. Maadui wa neno la Mungu wa kwanza ni shetani na hila
zake. Ila shetani wa mtu ni mtu mwenyewe.
Unaporuhusu
hali ya ukavu ndani ya maisha yako ndivyo hivyo hivyo unavyo yapalilia makazi
ya shetani ndani ya nafsi yako. Hawa ndio zile mbegu
“zilizoanguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa
angani wakazila,” Lk 8:5. Ni vyema kila siku ukawa hata na dakika 15 za
kulisoma neno la Mungu na kulifanya lako. Usomapo neno hilo jiulize linasema
nini juu ya maisha yako.
Adui
wa pili kuhusu neno la Mungu ni dhiki na udhia katika maisha yetu. Katika dhiki
za maisha na udhia Yesu anatuambia neno la uzima kwamba Yeye kesha ushinda
ulimwengu hivyo tuwe na imani ndani yake. Naye Yesu anasema, “Tazama, saa yaja, naam,
imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke
yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani
ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda
ulimwengu,” Yoh 16:32-33.
Ndugu yangu bila kushikamana
na Kristo aliyeushinda ulimwengu katika dhiki na udhia hutaweza kuushinda
ulimwengu huu kwa nguvu zako mwenyewe. Kuzitumainia nguvu zako ni kuelekea
kushindwa kabisa. Hawa ni zile mbegu “Nyingine
zilizoanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba,” Lk
8:6
Adui wa tatu wa neno la
Mungu ni shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine.
Leo watu wengi lengo la maisha yao yote huongozwa na tamaa ya kupata vitu.
Msukumo huu wa kutaka zaidi kila siku una misingi yake katika udanganyifu wa
kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa
salama; lakini mawazo hayo yote matatu si ya kweli. Hawa ni kama mbegu
zile “zilizoanguka kati ya miiba, na
miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga,” Lk 8:7. Mali
huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na sababu kubwa ndugu yangu, vitu
havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka vipya, vikubwa, na bora zaidi.
Kuna imani pia kwamba
nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na mali ni vitu viwili
tofauti. Thamani yako haitegemei mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu
maishani mwako si vitu! Imani ya watu wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo
nyingi kutanipa usalama. Huwezi! Yesu anawaambia wale wafuasi wa Yohane
Mbatizaji, “Mnatafuta nini?” Wanafunzi wale wakamjibu, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?”
Yoh 1:38. Anapokaa Yesu ndipo kwenye usalama kupita vitu vyote na hali zote
tunazoweza kufikiria. Mt. Augustino anasema, “mioyo yetu haitulii mpaka
itakapotulia kwako Ee Bwana.”
Ndugu yangu, utajiri
unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza
kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na
Mungu. Hawa ni mbegu zile “zilizoanguka
penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia,” Lk 8:8a. Mt. Augustino anatuwasa kutoka kwenye
kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na vichache kuliko kuwa na
vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo uchache na huo wingi.
Uzima wetu upo katika neno la uzima nalo ndilo ngao yetu katika ulimwengu huu
kigeugeu.
Ili
neno la Mungu liwe tumaini la kweli, na ushuhuda wa kweli ndani yetu, na kwa
wale wanaotuzunguka, lazima neno hilo tulisikie, tulipokee, kulitafakari,
kulishirikishe, na mwisho tuwe sehemu ya neno hilo kwa kuwa mashahidi wa neno
hata ikibidi kufa kwa kweli hiyo. Kulipokea neno lazima uwe na utayari wa
kulisikia neno. Usipokuwa na utayari huu ni sawa na mbegu
zile “zilizoanguka
karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila,” Lk 8:5. Na huu ndio
ufafanuzi wa Yesu; kwamba, “Wale wa karibu
na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao,
wasije wakaamini na kuokoka,” Lk 8:12
Kulitafakari neno la
Mungu kunakuhitaji kulisikia neno hilo na liguse maisha yako. Kutafakari neno
ni kama kucheua kile ulichokula. Kama hili halikufanyika ni sawa na mbegu zile “zilizoanguka penye mwamba; zilipoanza kumea
zikakauka kwa kukosa rutuba,” Lk 8:6. Na hapa Yesu anatuambia kwa kuifafanue
lugha ile ya picha, kwamba, “wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo
hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na
wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13. Kulipokea neno kwa furaha na kukosa
mizizi ndani yake, ni kukosa tafakari ya kina juu ya kile ulichokisikia au
kukisoma. Ni kutokulicheua neno, na hivyo neno hilo kutokuwa sehemu ya maisha
yako, na kutokukupa uwezekano wa kulishirikisha kwa wengine. Huwezi kutoa
usichokuwa nacho. Je, itawezekana kweli kushirikisha kwa wengine kile
usichokuwa nacho?
Wapendwa wana wa Mungu,
kuwa na uwezo wa kulishirikisha neno la Mungu kunategemea sana namna
tunavyolicheua neno la Mungu, yaani, uwezo ule wa kulitafakari neno la Mungu na
kuleta mabadiliko kwanza ndani yetu. Tunaposhindwa kufanya hivyo ni sawa na
mbegu zile “zilizoanguka
kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga,” Lk 8:7. Kumbe tunaweza
kushirikishana neno la Mungu vizuri pale tunapokuwa na mazingira mazuri ya
kulitafakari neno la Mungu kama lilivyo, na siyo tulivyo kwa kujionea huruma.
Na hapa Yesu anafafanua lughu hii ya picha na kusema, mbegu zile “zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na
katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya,
wasiivishe lo lote,” Lk 8:14. Leo ni wangapi
tu sehemu ya Jumuiya ndogo ndogo iliyopo kwenye eneno lako, ikiwa ni pamoja na
kwenda kwenye jumuiya hiyo na kuwa sehemu ya familia hiyo, ukiumega mkate na
kushirikishana neno la Mungu?
Leo jumuiya hizi sehemu nyingi zimekuwa
kundi la watoto, akina mama, tena wajane, na wazee. Hakuna vijana, na wala
hakuna akina Baba. Je, hayo malimwengu unayoyakubatia yana uzima ndani yake au
umebaki kujifariji katika upumbavu? Tukifanikiwa katika
hatua hii, yaani, kuliishi neno la Mungu, ni wazi tu mashahidi wazuri wa neno
la Mungu ndani yetu na wale wote wanaotuzunguka.
Kuwa mashahidi na washuhuda wa neno ni sawa na
mbegu zile zilizoanguka “zilizoanguka penye udongo mzuri; zikamea,
zikazaa moja kwa mia,” Lk 8:8a. Hiki ndicho atakacho Yesu kwako na kwangu,
yaani, tuwe mashahidi wa kweli wa neno la Mungu. Na huu ndio ufafanuzi wa Yesu
juu ya udongo mzuri; “ndio wale ambao kwa
unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda
kwa kuvumilia,” Lk 8:15. Kuzaa huku
matunda kwa kuvumilia kunatokana na nguvu ya Roho ile isukumayo ufahamu wetu
juu ya neno ambalo sasa siyo tu tumelisika, bali tumelipokea. Na siyo tu
tumelipokea, bali tumelitafakari kwa kina na kulicheua. Na siyo tu
tumelitafakari kwa kina na kulicheua, bali kwa sasa tumelishirikisha vyema kwa
wengine (uinjilishaji upya).
Na mwisho siyo tu
tumelishirikisha neno hilo kwa wengine bali tumekuwa sehemu ya neno hilo, kwa
kuwa mashahidi na washuhuda wa kweli kwa sababu maisha yetu yanaakisi kweli
hiyo. Kumbe haitoshi kufanya mambo mazuri katika ukamilifu wake, bali yakupasa
kuwa mkamilifu katika maana halisi ya ukamifu kama anavyotuasa Yesu, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa
mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48.
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa tafakari hiyo ya kina kutoka somo la Injili ya leo, inatusaidia
kulifahamu somo letu la kwanza kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho kama
tulivyokwisha kulisikia. Somo hili linaongelea juu ya maisha ya uzima wa milele
na mwonekano wake. Jambo la maana na la msingi katika maisha yako hapa duniani
leo na sasa ni kulenga katika ukamilifu ingawa udhaifu upo. Ni kulishika neno
la Mungu na kuwa shahidi na shuhuda wa neno hilo.
Ni
kujitahidi kila siku kufanya mambo yote katika ukamilifu na kuwa mkamilifu
licha hapa na pale tunadongoka. Na pale tunapodongoka tusiiache Huruma na Neema
ya Mungu kwa kupatanishwa naye. Swali labda mtu atafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili
gani? 1Kor 15:35, halina maana sana kama hatutajianda vyema kwa muda huu mfupi
tukiwa hapa duniani.
Aulizaye swali kama
hili bila kufanya chochote, Mtume Paulo anamfananisha na mpumbavu. Na mpumbavu
ni mtu yule ajifanyaye anajua kumbe hajui chochote. Naye Paulo Mtume anasema, “Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule
utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo,” 1Kor 15:36-37.
Ni wazi kwamba miili yetu katika maisha ya umilele haitakuwa na mwonekano huu
tulio nao. Miili baada ya ufufuko ni miili ile iliyotufukuzwa, na isiyo
shikiliwa au zuiliwa na wakati na nafasi.
Kiyama, yaani, hukumu
ya mwisho inategemea sana na haya unayoishi leo na sasa. Siku ya hukumu ya
mwisho kitakachofanyika ni kuridhiwa-‘ratification’ kwa kile ulichokiishi.
Kumbe kwa namna tunavyoishi ndivyo tunavyojiandalia palipo pema ama pabaya.
Hivyo, “kadhalika na kiyama ya watu.
Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika,” 1Kor 15:42.
Katika ishi yako leo ambayo upingana na matamanio ya ulimwengu huu, kwa wengine
ni aibu na udhaifu, ila kwa Mungu ni fahari na nguvu. Na siri ya maisha ya
uzima wa milele ndiyo hii kwamba, “hupandwa
katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa
katika nguvu,” 1Kor 15:43.
Tungali hapa duniani
Mungu ametuita kama tulivyo, yaani, binadamu aliyeumbwa na sura na mfano wake.
Na katika ubinadamu huo na udhaifu wake, tukiishi kwa uaminifu na kuushinda
ubinadamu huo, hapo ndipo ulipo pia utakatifu wetu. Hivyo utakatifu huo,
ukamilifu, huo, “hupandwa mwili wa asili;
hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko,” 1Kor
15:44. Ndugu yangu, usitamani kuwa kitu kingine ambacho sicho kusudi la Mungu
ndani yake, yaani, hasa wale wenye matamanio ya kuyabadili maumbo yao na hata
jinsia zao.
Wapendwa katika Kristo,
wakutugeuza na kuwa kitu kingine na kwa namna nyingine ni yule yule lifanya
hilo mwanza, yaani, Mungu aliyekuumba wewe na mimi na sura na mfano wake, Mwa
1:27. Ni katika mantiki hii, Mtume Paulo anafanya linganisho la mtu wa
kwanza-Adamu, na Adamu wa mwisho-mwili ule uliotukufuzwa. Na “Ndivyo
ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni
roho yenye kuhuisha,” 1Kor 15:45. Na kuupata mwili huu uliotukufuzwa-wa roho,
yatupasa kuishi mwili huu wa asili katika ukamilifu wake licha ya udhaifu wake.
Ni kwa maana hiyo, “hautangulii ule wa
roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho,” 1Kor 15:46. Hakuna utukufu
pasipo Msalaba, na penye teso ndipo penye utukufu.
Baada ya maelezo hayo
ya kina kuhusu ubinadamu wetu na asili yake hadi kutufukuzwa kwetu, Mtume Paulo
anatupeleka hatua ya pili kwa kufanya linganisho la sisi kama wanadamu, na Neno
aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Huyu ndiye Kristo Yesu. Na hii
ndiyo maana ya maneno haya kwamba, “Mtu wa
kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo (mwanadamu). Mtu wa pili atoka mbinguni
(Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu),” 1Kor 15:47. Ni katika maana hii
tunaweza sasa kuongelea hali zetu katika ubinadamu wetu, na hali zao
walioufikia ukamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu, Mt 5:48. Na Neno kufanyika
mwili na kukaa kwetu, alichukua asili mbili, yaani, Mwanadamu na Mungu.
Na kwa Ubinadamu wake
na Umungu wake, Kristo Yesu aliikamilisha kazi ile ya kumkomboa mwanadamu
katika ubinadamu wake kutoka utumwa wa dhambi na kumwinua katika hali ya umungu
kwa Umungu wake Kristo Yesu. Ni kwa namna hiyo kwamba, “Kama
alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa
mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni,” 1Kor 15:48. Na huu ndio ukweli kwamba, ndani na katika
Kristo Yesu, “kama tulivyoichukua
sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa
mbinguni,” 1Kor 15:49. Hili liliwezekana tu ndani na katika Kristo Yesu,
aliyekuwa na asili hizo mbili, yaani, Mungu na Mwanadamu angali hapa duniani.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ewe
mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo
uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au
nyingineyo,” 1Kor 15:36-37
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tufanye udongo mzuri. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario