JUMAPILI YA 24 YA MWAKA-C
Somo
I: Kut 32:7-11, 13-14
Zab/Kit: 51:1-2, 10-11, 15, 17 (K)
Lk 15:18
Somo II: 1Tim 1:12-17
Injili: Lk 15:1-32
Nukuu
“Tena
Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye
shingo ngumu basi sasa niache,
ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa
kuu,” Kut 32:9-10
“Na Bwana akaughairi
ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14
“Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa
sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo
kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata
rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani,” 1 Tim
1:12-13
“Ni
neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu
alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi,” 1Tim
1:15
“Mafarisayo na waandishi
wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,”
Lk 15:2
“Ni
nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini
na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?” Lk 15:4
“Nawaambia,
Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja
atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya
kutubu,” Lk 15:7
“Nitaondoka, nitakwenda
kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele
yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi
wako,” Lk 15:18-19
“mleteni ndama yule
aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu
alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza
kushangilia,” Lk 15:23-24
“Akamwambia, Mwanangu,
wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako,” Lk 15:31
TAFAKARI:
“Neema, Upendo na Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 24 ya mwaka “C” wa Kanisa. Kwa namna
ya pekee, masomo yetu yote ya leo yanakutafakarisha wewe na mimi kuiona ‘Neema,
Upendo, na Huruma ya Mungu ambayo ni kubwa kuliko dhambi zetu. Na zaidi ya wazo
kuu hilo la leo, masomo yetu haya ya leo yanahusisha ‘Neema, Upendo, na Huruma
hiyo ya Mungu, Uzima na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.
Somo la kwanza Mungu
anaonyesha huruma kwa watu wake kupitia Mtumishi wake Musa. Musa akiwa mlimani
kupokea amri za Mungu, waliobaki chini wakisubiri maelekezo hayo ya Mungu,
wanajifanyia mambo yao kwa kujichongea sanamu zoa kama utambulisho wa Mungu wao
wa kutengeneza. Tendo hili lilikuwa chukizo kubwa kwa Mungu. Kwa hasiri hii
Mungu anataka kuliangamiza taifa lote la Israeli kwa kutokuwa na subira. Bwana
akamwambia Musa, “Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo
ngumu. Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize,” Kut
32:9-10.
Kutokana na hasiri hii
ya Mungu, Musa analiombea taifa lake, kwa kumkumbusha Mungu ahadi zake
alizozitoa na kuzifanya na Ibrahimu, Isaka na Israeli. Kwa huruma yake Mungu,
anaghairi hasira yake. “Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba
atawatenda watu wake,” Kut 32:14. Mungu wetu ni Huruma na mara zote yupo tayari
kuhurumia na kutusamehe tunapoyakiri makosa yetu na kumrudia. Unapodondoka
katika ubinadamu wako usisahau njia ya kumrudia Muumba wako, yaani, kufanya
toba ya kweli na majuto ya dhambi zako.
Sakramenti ya
Upatanisho/Kitubio ndiyo mlango sahihi wa kupita baada ya kuvurugwa na dhambi,
na ndicho kisima sahihi na andaliwa cha kukoga na kujitakasa baada ya kuchafuka
kwa dhambi. Kwenye Mlango huu na kisima hiki ndipo tunapokutana na Neema,
Upendo, na Huruma ya Mungu. Huruma hii ya Mungu iwe pia ndani yangu hasa pale
ninapotakiwa kutoa huruma hiyo bila masharti katika kusamehe. Huu ndio mwito
wako na wangu ninapomwamini Mungu, na Mwanaye Yesu Kristo.
Wapendwa
wana wa Mungu, kama wewe umebatizwa elewa kuwa unaishi ndani ya wokovu
aliokupatia Bwana wetu Yesu Kristo kwa kifo chake pale msalabani. Ni jambo la
kusikitisha sana kwamba tulio wengi hatuoni thamani ya wokovu huu tuliopewa
bure kwa Upendo wa Mungu Baba kupitia Mwanaye Yesu Kristo. Tendo hili kwetu ni
heshima kubwa sana, kwani tumenyanyuliwa katika udogo wetu kama vyombo vya
udongo, 1Kor 15:49; 2Kor 4:7, na kuinuliwa palipo juu kabisa alipo Kristo na
Mungu wetu.
Ndugu
yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, licha ya mastahili haya aliyopewa
wanadamu, Mungu hakumuondolea mwanadamu huyu uhuru wake wa kuamua kutenda
yaliyo mazuri au mabaya. Uhuru tuliopewa na Mwenyezi Mungu ni changamoto kubwa
sana katika kuiishi Imani yetu. Uhuru huu mara nyingi unatutoa katika mstari wa
kuyaishi yale yampendezayo Mungu. Ni kwa kupitia uhuru huu pia tunaweza
kuziacha njia zetu mbaya na kumrudia Mungu kwa toba na majuto.
Hivyo
basi, kila siku ya maisha yangu ninaitwa katika wongofu wa roho yangu. Siyo
kuokoka, bali kuongoka kwani wokovu kesha tupatia Kristo. Wokovu ambao ni
uwezekano wa kufanywa wana wa Mungu kesha tupatia Kristo mwenyewe kwa sadaka ya
mateso na kifo chake pale msalabani. Hivyo yanipasa kuziishi ahadi zangu za
ubatizo muda wote wa maisha yangu hapa duniani.
Ndugu yangu, miaka ile
mitatu ya mwisho ya Yesu hapa duniani inathibitisha furaha ya Mungu, na hasa
kwa yule mwenye kutubu na kuacha njia yake mbaya. Na huu ndio mpango wa Mungu
katika historia nzima ya wokovu wa mwanadamu. Naye Mungu anasema, “sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu
mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi,” Eze 33:11a. Furaha ya Mungu
ni kuanza naye upya, na Yeye utuchukulia katika upya wetu bila kuyahesabu
yaliyopita. Mungu usamehe yote bila kuhoji historia yako ufanyapo toba ya kweli
na majuto ya dhambi zako. Mfano mzuri ni simulizi hili la Mwana Mpotevu kutoka
Somo letu la Injili, Lk 15:11-32.
Katika Injili hii ya
leo, Yesu anazihoji dhamiri zetu katika kweli na haki, na kusema, “Ni
nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini
na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?” Lk 15:4.
Ujumbe hapa ni kwamba, wewe na mimi kama viongozi na wenye dhamana mbele ya
umma, tuwe tayari kukitetea kile kilicho dhaifu kwa sababu furaha ya kweli si
usalama tu wa wengi bali sote tuwe salama. Kama kiongozi ni wajibu wangu kwamba
wote niliokabidhiwa wafike salama na asipotee hata mmoja. Kiongozi
anayekimbilia ukamilifu wa wengi, na kuwapoteza wachache na wakati mwingine
bila kujua “kulikoni,” kiongozi huyo ni dhaifu sana. Yesu anasema, “Kwa maana
jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu
amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16
Kamwe Mungu hawezi
kufurahia tendo hilo la kutomjali mmoja katika hali na mazingira yake kwa
sababu hata huyo unayemuona si mkamilifu kwa vigezo vya kibinadamu, ilhali mtu
huyu yupo tayari kuiacha njia yake mbaya na kumrudia Mungu, ila wewe kwa
kuishikilia sheria, tena mbovu haupo tayari kufikiri nje ya sheria ile, Mungu
anakiu naye, Yoh 19.28. Ndugu yangu, tambua kwamba mtu huyo ameumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu, Mwa 1:27. Na kwa sababu hiyo Mungu hachoki kutafuta kile
kionekacho dhaifu na kilichopotea. Katika hili Yesu anasema, “Vivyo
hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye,
kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk
15:7
Tunahesabiwa haki si
kwa matendo yetu mema tu na ukaribu wetu mbele ya Mungu, bali kwa utayari wetu
wa kuona udhaifu ndani yetu na kufanya toba ya kweli na majuto ambayo kwa
kutenda dhambi ndiyo sababu kubwa leo ya mwendelezo wa mateso ndani na katika
Kristo Yesu.
Wapendwa katika Kristo,
leo huruma na msamaha huo tunaupata kupitia Kristo mwenyewe ambaye ndiye “Neno alifanyika mwili, akakaa
kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa
Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Leo pia kwa namna ya pekee huruma na
msamaha huo wa dhambi tunaupata kupitia Mama Kanisa kama Sakramenti ya wokovu
wetu.
Mamlaka hayo (Kanisa
kama Sakramenti ya wokovu) kayatoa Kristo mwenyewe katika Kanisa, na kwa
watumishi wake waliohesabiwa haki hiyo na Mama Kanisa kabla ya kupaa kwake
Mbinguni. “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni
Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote
mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Hivyo ndugu yangu, Mungu
Baba kupitia Mwanaye Mpenzi na Kanisa lake, ananialika kupatanishwa naye kila
ninapo pumzi yake. Je, ni kwa nini sasa yatupasa kupita kwa Kristo ili niupate
huo upatanisho na Mungu?
Wapendwa wana wa Mungu,
sehemu ile ya 2Kor 5: 17-21, inatupatia jibu halisi na kamili ‘kwa nini lazima
Kristo.’ Ni kwa kupitia Kristo na ndani ya Kristo tunakuwa viumbe vipya na
kuanza upya katika safari ya uzima wa milele. Ni kwa sababu hiyo, “hata
imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita
tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17. Na nikupitia Kristo tu ambaye, “Yeye
asiyejua dhambi (Mungu) alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate
kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor 5:21. Hivyo kwa mantiki hii, hakuna
miongoni mwetu awezaye kujihesabia haki pasipo Kristo. Haitawezekana hata
kidogo ndungu yangu!
Ni kwa ukweli huo
kwamba, ‘siwezi jihesabia haki pasipo Kristo,’ kweli ambao inapingwa vikali na
Mafarisayo na Waandishi. Watu hawa walijihesabia haki pasipo haki ya kweli
ambayo yatoka kwa Mungu mwenyewe. Yesu anawakemea wazi wazi na kutoa angalizo
kwetu kwa kusema, “Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha
Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa
mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt
23:2-3. Kwa mtazamo huu wa Mafarisayo na Waandishi, hawakuona haja ya
majuto ya dhambi zao, na hata kufanya toba ya kweli.
Mafarisayo na Waandishi
walijiona safi na kamili, na hivyo hawakuhitaji Huruma na Msamaha wa Mungu.
Ukaribu wa Yesu na ushiriki wake na wokosefu kwa lengo la kuwatoa katika hali
zao duni na udhaifu ulio tokana na dhambi, tendo hili linaonekana kikwazo kwa
Mafarisayo na Waandishi. Na hii ndiyo sababu ya manung’uniko yao kwa Yesu, “Mtu
huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,” Lk 15:2. Mfano wa Mwana
Mpotevu katika Injili ya leo unajibu manung’uniko hayo ya Mafarisayo na
Waandishi. Mfano huu unaweka wazi ukweli huu kwamba, ‘Neema, Upendo, na Huruma
ya Mungu ni KUBWA kuliko dhambi za mwanadamu pale mwanadamu huyo afanyapo
majuto na toba ya kweli.’
Kwa kujibu manung’uniko
waliyokuwa nayo Mafarisayo na Waandishi juu wa ukaribu aliokuwa nao Yesu kwa
wadhambi, Injili inahainisha wahusika wakuu watatu; Baba Mzazi, Mwana Mpotevu,
na Kaka ya Mwana mpotevu. Wengine ni watumishi au watumwa wa Baba mzazi wa
Mwana Mpotevu, na marafiki wa Mwana Mpotevu. Mwana mpotevu, tena aliye mdogo
katika familia hii, anafanya kitu ambacho si cha kawaida katika jamii. Kitendo
cha kuomba urithi au sehemu ya mali yake kabla ya kifo cha baba yake,
kilimaanisha kumtakia mabaya Baba yake. Ni kutokumtambua Baba yake. Ni
kumchukulia Baba yake kama marehemu.
Kwa upande wa Baba, na
kwa tabia na asili yake, anaonyesha mambo makuu matatu; Ubaba Kamili, Upendo
usiyo shaka na mipaka, na Ustahimilivu katika tendo zima la Huruma ya kweli.
Hivyo ni kutokana na Upendo huo aliokuwa nao kwa wana na familia yake,
anakubali aibu hiyo, na kufanya kadiri ya matakwa ya mwanaye. Baba anampa
sehemu ya urithi wake. “Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo
akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa
maisha ya uasherati,” Lk 15:13.Yaliyompata kijana huyu wote tunafahamu vizuri
simulizi hili.
Ndugu yangu, kutenda
makosa ni hali yetu sote wanadamu. Ila tofauti ipo hapa; unapotambua umefanya
kosa na kuchukua hatua kwa uliyoyafanya ndiko kunakokurejeshea hadhi na heshima
yako tena. “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi
wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa
njaa,” Lk 15:17. Baada ya kutindikiwa vingi na mambo kwenda ndivyo sivyo, Mwana
Mpotevu analiona kosa lake na anakiri kwa matendo na maneno, “Nitaondoka, nitakwenda
kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk
15:18-19. Ndugu yangu, hii ndiyo toba na majuto ya kweli juu ya dhambi.
Tunachoangalia si aibu tutakayopata, bali Huruma, Msamaha, na Mastahili
tunayotarajia kuyapata kwa Upendo wake Mungu kwa kufanya toba ya kweli.
Mpendwa katika Kristo,
ninapodondoka kwa sababu ya dhambi, nisione aibu kuamka na kuomba msamaha kwa
Muumba wangu. Yeye Mungu anasema, “mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho,
aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” Ufu 1:8. Je, kuna mwingine
wa kumkimbilia zaidi ya Mungu wetu?
Mungu aliye Upendo hana mipaka wala masharti ya pekee ninapomrudia. Mungu
anasema, “nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,”
Mit 8:17.
Upendo wa Baba hauna
mfano. Baba huyu anapomwona mtoto wake, hapendi na wala haitaji kujua historia
ya yale maovu aliyofanya. Furaha yake ni kumwona kama alivyo na anajua kurudi
kwake ni toba ya kweli. Na hivi ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu wa Upendo, Huruma,
na Neema. Anachofanya Baba katika simulizi hili la Mwana Mpotevu ni kumrudishia
stahili na hadhi yake kama mwana na mmoja wa familia yake. Alipomwona tu
mwanaye, “baba aliwaambia
watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete
kidoleni, na viatu miguuni,” Lk 15:22. Mwana Mpotevu anarudishiwa hadhi na
mastahili yake kama mwana familia kama ilivyo na itakavyo kuwa mbele ya Mungu
tunapofanya majuto na toba ya kweli.
Tendo hili la Baba,
wapendwa wana wa Mungu, linakuwa sononeko la Kaka ya Mwana Mpotevu. Haoni maana
ya furaha hii na sababu ya kuwa hai mdogo wake. “Akakasirika,
akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi,” Lk 15:28. Ndugu
yangu, katika safari ya wokovu, usipende kujitazama mwenyewe. Wokovu ni kwa
wote na nifuraha ya Mungu na kwa wote wenye mapenzi mema, yaani, Watakatifu wa
Mungu. Tendo la wokovu ni furaha na sherehe kwa wote kwa sababu tunairudia sura
yetu halisi, yaani, sura ile na mfano ule wa Mungu tulioumbwa nayo, mwa 1:27.
Sura hii ufifishwa na kufubaishwa na hali yetu ya dhambi.
Kwa furaha ya kumuona
tena Mwana wake aliyepote, Baba anatoa maelekezo na kusema, “Mleteni
ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu
mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.
Wakaanza kushangilia,” Lk 15:23-24. Katika mfano huu, Yesu anawakemea
Waisraeli na hasa Mafarisayo na Waandishi ambao wanahuzunika kwa yale
ayafanyayo Yesu kuufunua Upendo wa Mungu Baba.
Wapendwa katika Kristo,
yatupasa kutiana moyo na kufurahi mwenzetu anapomwongokea Mungu na kuishi
maisha ya kumpendeza Mungu. Mara nyingi hatuachi kuwasema vibaya wale
wanaojitahidi kuishi njia impendezayo Mungu. Tunawapachika majina mengi, na
kuwakatisha tamaa kabisa. Kwa upande wetu, mwenzetu anapojitahidi kuishi
vizuri, basi iwe changamoto ya mimi kufanya vizuri. Hivyo basi tulio karibu na
mwanga wa Mungu, na kuenenda kadiri ya upendo wa Mungu, tuwe na huruma kwa wote
wanaomrudia Muumba wao tukijua kwamba, tu pamoja na Baba na Upendo wake
sikuzote, na vyote alivyo navyo ni vyetu sote, Lk 15:31. Hivyo yanipasa kuuvua
ubinafsi wangu na niwe na huruma ili nione hitaji ya mwingine, mwili na kiroho.
Ndugu yangu, wakati
ndiyo sasa! Kaa na tafakari namna utendavyo. Je, ninafanya kadiri ya mapenzi ya
Mungu au najitazama mwenyewe? Urithi wako ni fursa uliyo nayo sasa katika
utendaji. Niepuke sononeko la Mwana yule Mkubwa, “Tazama, mimi nimekutumikia
miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi
mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana
wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama
aliyenona,” Lk 15:29-30. Je, kwa kuwa karibu na Baba ninatumia fursa hiyo
vizuri kuonja Huruma na Upendo wake kwangu? Na kama Mwana Mpotevu, Je, baada ya
kuishi ovyo kwa muda wote huo, nipo tayari kufanya toba ya kweli na kuiacha
njia hiyo?
Basi yanipasa nielewa
kwamba nafasi niliyo nayo ni leo na sasa tu. Ni vyema nikachukua hatua sasa na
kuutafuta uso wa Bwana. “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa
dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu;
huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3. Kukengeuka kwangu na kunakonifanya kuwa nje ya Imani yangu
kunatokana kwanza kabisa na ujinga wangu, yaani, kutokujua thamani ya Imani
yangu, na lengo lake katika safari ile ielekeayo katika uzima wa milele.
Mtume
Paulo ni mmoja ya watu walioishi vibaya na baada ya kujitambua, hasa pale
alipojeuzwa na Kristo anayasema haya kinabaugaba. “Nami namshukuru Kristo
Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka
katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi
watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga,
na kwa kutokuwa na imani,” 1 Tim 1:12-13. Kristo akishakutembelea na kukugusa
huwezi kubaki katika hali yako ya zamani.
Tendo
hili ndilo lijulikanalo kama KUONGOKA. Mt. Augustino ni mfano mwingine wa wale
walioacha njia zao mbaya na kuongoka. Tusomapo kitabu chake cha Maungamo
tunaona wazi tendo hili la kuongoka. Mt. Augustino anafafanua kwa undani
alivyoutafuta ukweli sehemu mbalimbali na kusahau kwamba ukweli huo alikuwa nao
ndani yake. Alipoigusa Neema ile ya Wokovu wa Kristo ndani yake yote
yalifunuliwa na akawa mpya ndani na katika Kristo.
Ni vyema
nikaelewa vizuri njia ya wokovu wangu kwa mimi niliye batizwa na mfuasi wa
Kristo. Ni kweli kwamba pasipo Kristo na ndani ya Kristo Wokovu huo kwangu
hautawezekana. “Ni neno la kuaminiwa,
tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni
awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi,” 1Tim 1:15. Hata pamoja na
ukweli huo, yote hufanyika kwetu siyo kwa mastahili yetu, bali kwa kuhesabiwa
haki na Mungu na kwa kupitia Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Na “kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi
wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa
wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele,” 1Tim 1:16.
Kuhesabiwa haki na Mungu
na kwa kupitia Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo, kunaturejesha katika uhasili wa
Mungu, yaani; Neema, Upendo, Huruma, Haki, na Msamaha. Naam, Yeye ni “Mfalme
wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe
heshima na utukufu milele na milele. Amina,” 1Tim 1:17.
Mama Valensa Misalaba
alibahatika kupata watoto watatu, mmoja wa kiume ambaye ndiye wa kwanza, na
wawili wakike. Mtoto wake wa kiume-Mathayo, alikuwa na umri wa miaka 7, na hao
wa kike wawili, moja alikuwa na miaka mitatu na huyo wa mwisho alikuwa na miezi
sita.
Ndoa ya Mama Valensa
Misalaba haikuwa na furaha hata kidogo. Kipigo kutoka kwa mme wake kilikuwa
kitu cha kawaida na kufikia hasa anapokuwa amelewa. Na ikipita siku mumewe
hajalewa ndiyo furaha na amani ingawa katika hali kama hiyo mmewe haachi kuwa
mkali na katili katika mazungumzo ya kawaida tu.
Siku mmoja jioni, na
baada ya mmewe kuondoka kwenda kulewa pombe za kienyeji, Mama Valensa Misalaba
alichukua uamuzi mgumu wa kutoroka na watoto wake kwenda kwa Kaka yake ambaye
alikuwa anaishi umbali wa mwendo wa masaa sita hivi kwa bus. Mama Valensa
hakuwa na wazazi kwani wote walifariki kipindi yeye akiwa na miaka 11. Mfukoni
Mama huyu alikuwa na shilingi 50 TU.
Usafiri wa wakati ule
kutoka hapo alipo hadi kufika kwa Kaka yake iligharimu shilingi 250. Hata hivyo
kutokana na hali na mazingira yale ya mateso hakuwa na namna nyingine zaidi ya
kutoroka. Kwa vile alikuwa anaishi karibu na Barabara kuu ya Mabasi,
Singida-Babati, alikuwa na uhakika wa kupata usafiri kuelekea eneo la Babati
alipokuwa anaishi Kaka yake.
Kufika tu barabara kuu
alipunga mkono na bus moja lililokuwa
linatoka Singida kuelekea Arusha lilisimama. Akaingia ndani ya bus yeye na
watoto wake huku Konda wa bus lile akimwambia, “Mama uandae nauli yako mkononi.”
Baada ya mwendo wa nusu saa hivi, Konda alimwendea Mama Valensa na kudai nauli.
Mama Valensa kabla ya kutoa nauli ile alianza kumwomba radhi Konda yule na
kusema, “Kama yangu na mdogo wangu, nina shilingi 50 tu hapa nilipo, na ninajua
nauli ni shilingi 250. Nimelazimika kusafiri muda huu kuelekea kwa Kama yangu
huko Babati kuepuka kipigo na kifo kutoka kwa mume wangu,” Mama Valensa alikuwa
anayasema hayo huku akimwonyesha makovu na majeraha aliyokuwa akiyapata kutoka
kwa Mume wake.
Kwa hasira na bila kuwa
na chembe ya huruma, Konda alimjibu, “Wewe Mama acha kuuza sura. Hizi hadithi
nimezisikia sana huku barabarani. Ninachotaka ni nauli kamili la sivyo unashuka
mbugani hapa uliwe na simba.” Jambo la ajabu katika sintofahamu ile kati ya
Konda na Mama Valensa, huku watoto wake wakilia kwa hofu ya kushushwa, hakuna
mtu yeyote kati ya abiria wale aliyefungua mdogo wake kumsaidia Mama Valensa.
Ndipo kwa hasira Konda
alimwamuru Dereva asimamishe bus na Mama Valensa na watoto wake washuke.
Walishuka na kutupiwa vitu vyao nje kusiko na utaratibu. Baada ya mwendo wa
dakika kama tano hivyo, dereva wa bus lile aliona kwa mbele kundi kubwa la
simba wakielekea kule walipotoka. Hakika alijua kitakachotokea hata hivyo
akufanya chochote.
Na baada ya kama nusu
saa hivi simba wale waliwakaribia, na Mama Valensa alijua kitakachotokea.
Alimwambia mwanaye Mathayo apande juu ya Mti ulikuwa karibu, naye na watoto
wake wawili wa kike aliwakumbatia kwa kuwafunika kanga. Simba wale mbarara
waliokuwa na njaa waliwavamia na kuwachana vipande vipande. Mathayo alipiga
yowe kwa nguvu zake zote lakini sauti ile haikusikika popote.
Kulipoanza kupambazuka,
Mathayo aliona gari dogo kwa mbali na ndipo alipopiga kelele kupata msaada.
Gari lile lilisimama na ndipo Mathayo aliposimulia haya yote. Watu wale na gari
lile walikuwa ni maafisa wa wanyama pori.
Ndugu yangu, simulizi
hili ambalo lilitokea miaka mingi ya nyuma iliyopita, (miaka ya 90),
linanikumbusha wajibu wangu na nafasi niliyo nayo kwa mwitaji yeyote yule.
Katika hali na mazingira kama ya Mama Valensa, yanipasa kuvivaa viatu vyake, na
kuwa na huruma na upendo. Konda angeyaokoa maisha ya Mama Valensa na binti zake
wawili kama angevivaa viatu vya Mama Valensa, yaani, kusikiliza shida na
mahangaiko yake. Jamii yetu leo wapo wengi kama Mama Valensa wanao hitaji
upendo na huruma kama Mungu anavyotukirimia kila siku bila mipaka.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwanangu,
wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe
ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa
amepotea, naye ameonekana,” Lk 15:31-32
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nijalie moyo wa huruma na upendo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario