JUMATATU
WIKI YA 25 YA MWAKA-C
Somo: Mit 3:27-34
Zab/Kit: 15:2-3ab,
3cd-4ab, 5
Injili: Lk 8:16-18
Nukuu
“Usiwanyime
watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda,” Mit
3:27
“Usimwambie
jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile
karibu nawe,” Mit 3:28
“Hakuna mtu
ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali
huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake,” Lk 8:16
“Jiangalieni basi
jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu
atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho,” Lk 8:18
TAFAKARI: “Mwenye kitu
atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa
nacho.”
Wapendwa wana wa Mungu, ufahamu wa kawaida waonyesha wazi kwamba aliye
tayari kushirikisha alivyo navyo kwa wengine, ikiwa ni pamoja na vipaji vyake,
kwa njia hiyo uvikuza vipaja vyake na kugundua mambo mengine zaidi na yenye
uhusiano na kipaji kile. Hakuna apotezaye muda wake kwa kumsaidia mwingine
kufahamu jambo fulani ambalo yeye ana ufahamu nalo. Ni kadiri ufanyavyo jambo
hilo mara kwa mara ndivyo unavyo lifahamu vizuri na kugundua vingine zaidi.
Hivyo, karama au vipaji tulivyojaliwa na Mungu hukua na kufikia
‘ukamilifu’ wake pale tunapovitumia, na kuvishirikisha kwa wengine. Kwa maana
hiyo, “Hakuna
mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali
huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake,” Lk 8:16. Kama kilivyo kioo waweza kuiona sura yako, ndivyo hivyo hivyo mtu
mwingine ukuwezesha kujiona vizuri pale unaposhirikisha vipaji vyako na kuwa
wazi kwa kile ulicho. Ni katika uelewa huu, neno hili la Yesu ubeba maana yake,
yaani, “Mwenye
kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa
kuwa nacho,” Lk 8:18.
Na kile ulicho ni sawa na ‘kikohozi’ kiasi kwamba huwezi kukizuia
ikiwa wakiishi na kukishirikisha kwa upendo. “Kwa
maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa
ambalo halitajulikana na kutokea wazi,” Lk 8:17. Katika kweli hii, Kristo Yesu
ndiye kielelezo chetu na upendo ule wa Mungu ambao kwa wakati wake alipenda
kutushirikisha, Gal 4:4-5. Upendo huo wa Mungu umewekwa wazi kwa Neno kufanyika
mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na hivi ndivyo ilivyompendeza Mungu kwamba, “jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa
Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,”
Yoh 3:16
Kinyume
chake, yaani, “yule asiye na kitu atanyang'anywa hata
kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho,” Lk 8:18b, ni pale tunapoongozwa na choyo
na ile roho ya ‘kwa nini.’ Kutoshirikisha vipaji na karama zako kwa wengine na
kubaki nazo kwa kujiinua, huzidumaza karama na vipaji hivyo. Ni sawa na kuwa na
shilingi 1000 na kuihifadhi kwenye kopo zuri la dhahabu na kuifungua kabatini.
Fedha hii itabaki katika upya wake, ila kila kukichwa upungua thamani yake, na
hasa pale penye mdororo wa kiuchumi. Kumbe kila mmoja wetu ni vyema akavijua
vipaji na karama zake. Na karama na vijaji hivyo ujionyesha kwa huduma
tuzitowazo kutokana na wito na nafasi tulizokuwa nazo katika jamii.
Hivyo, “usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika
uwezo wa mkono wako kuyatenda,” Mit 3:27.
Kufanya hivyo, yaani, kuwanyima watu mema yaliyo haki yao, hakuna tija yoyote
katika ufanyizi wako na nafasi uliyo nayo, na wala hakuna tija kwa wale
unaowahudumia. Kile uwezacho kufanya kwa wengine leo na sasa kadiri ya uwezo na nafasi, kisisubiri kesho. Kwa
maana hiyo “usimwambie jirani yako, Nenda,
urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe,” Mit 3:28. Kwa kutokufanya hivi unakoswa fadhila nyingi
kutoka kwa Mungu.
Ni kweli kabisa pale
ulipo wapo wengi wenye imani nawe, na kwa upande mwingine wanakuchukulia kama mfano
wa kuigwa. Ikiwa hali ndivyo ilivyo, basi elewa huo ndio mwito sahihi wa kuishi
na kila mtu bila mwelekeo wa kubaguana. Ni mwito pia wa kuchukuliana kwa upendo
na upya kila siku. Si wakati wa kuhama au kutembea na kumbukumbu mbaya za watu.
Hivyo “usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe
na kujiona salama,” Mit 3:29. Kila mmoja anaye hitaji uwepo wako mpe nafasi
kadiri ya nafasi uliyonayo.
Hatari
katika maisha ya ‘ujirani mwema’ ni pale tunapopenda kuishi maisha linganishi
na shindanishi pasipo kujua kwa nini nafanya kama ninavyofanya. Si mbaya wala
vibaya kuwa na wivu wa maendeleo katika maana ya kufanya vizuri zaidi kila siku
kwa kuona mfano mzuri kutoka kwa mwengine. Ila wivu huu usinipeleka katika
uharibufu, yaani, kuharibu kile cha mwenzangu ili changu kionekane. Ndugu
yangu, “usishindane na mtu bila sababu,
Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote,” Mit 3:30. Mara zote nijiuze hivi kabla ya
kutenda lolote; Je, na fanya hivi kwa sababu gani, na ili iwe nini?
Kushindana
na watu pasipo lengo chanya ni sawa na kuotesha upepo na mwisho wa siku utavuna
kimbunga. Hivyo “usimhusudu mtu mwenye
jeuri, Wala usiichague mojawapo ya njia zake,” Mit 3:31. Ikiwa twaishi
ulimwenguni hapa kama jukumu la muda mfupi, basi hatuna sababu ya kupoteza muda
kwa yale yasiyotujenga mwili na roho. Je, una sababu ya kushindana na mtu jeuri
na kaidi? Hapana! “Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali siri
yake ni pamoja na wanyofu,” Mit 3:32. Katika mazingira na hali hii, ni mwito
kwetu pia kuishi maisha ya unyofu kwa sababu hatutopungukiwa kitu.
Ikiwa
amani ile tuipendayo ndani yetu na kwa wenzetu ni muhimu pale tunapoishi zaidi
ya mmoja, basi tuelewe amani hiyo ni tunda la haki. Hivyo tutende haki kwa kila
mtu ili tupate matunda yake, yaani, amani. Kwani “Laana
ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki,” Mit
3:33. Na maskani ya kwenye haki ujengwa na unyenyekevu. Unyenyekevu ni kukubali
pia yapo mambo mengine yaliyo juu ya uwezo wangu, na kuyafahamu hayo yanipasa
kujinyenyekeza. Katika lugha ya picha na yenye kueleweka vizuri kati yetu ni
kwamba, Mungu “huwadharau wenye dharau,
Bali huwapa wanyenyekevu neema,” Mit 3:34. Ndugu yangu, kuijua siri ya Mungu na
maarifa yake, yanipasa kujinyenyekeza mbele yake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Usishindane
na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote,” Mit 3:30
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
nijalie moyo wa kujitoa bila kujibakiza kadiri ya karama na vipaji
ulivyonijalia. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario