martes, 6 de septiembre de 2016

ALHAMISI WIKI YA 23 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 23 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 8:1b-7, 11-13
Zab/Kit: 139:1-3, 13-14ab, 23-24
Injili: Lk 6:27-38
Nukuu
 “Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye,” 1Kor 8:3 

 “Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake,” 1Kor 8:11 

Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo,” 1Kor 8:12

 “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi,” Lk 6:27-28 

 “Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao,” Lk 6:32 

 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu,” Lk 6:35

Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma,” Lk 6:36

TAFAKARI: Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.”

Wapendwa wana wa Mungu, Upendo wa kweli huvunja mipaka yote na kuta zote zinazotuzuia kuuona upendo wa Kristo na sadaka yake pale msalabani. Upendo huu utusukuma kupenda hata pale tunapoumia kama binadamu kwa kufanya tendo hilo kutokana na yaliyotusibu na yaliyopita na kutufanya kile tulicho. Upendo huu ujenga tena daraja Imara la kuwapenda hata wale maadui wetu. Tendo hili la upendo linatukutanisha na Yesu aliyependa hata kuutoa uhai wake kwa ajili yetu. Kwa tafsiri hii, upendo unakuwa AMRI.

Hivyo Yesu anatuambia leo neno hili la uzima sisi tusiosikia, “wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi,” Lk 6:27-28. Tendo hili ndilo linalotofautisha kati ya anayemjua Kristo na aliye mfuasi wake Kristo, Mpagani na anayeongozwa na hofu ya Mungu, na Mkristo wa kubatizwa na anayeishi ahadi za ubatizo.

Upendo wa kweli unakupa mtazamo mpya wa vitu na hasa watu wale wote unaokutakana nao na kuishi nao. Huruma huwa msukumo wako wa ndani katika kuuona kweli, kuitafakari, na kuitenda hata kama mazingira ukuwiya vigumu kufanya hivyo. Tendo hili kimtizamo kwa yale yote unayokutana nayo, ukuweka karibu sana na Mungu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma,” Lk 6:36. Huruma hii ufunua undani wetu ambao huwa kielelezo sahihi cha kuona upendo wa Mungu kwa wenzetu hasa pale tunapotoa hukumu kwa wenzetu.

Mzaburi anatufikirisha ukweli huu kwa kusema, “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Ndugu yangu, hapa tunaalikwa kuwa na huruma kama Mungu alivyo na huruma nasi. Mara tulifanyapo tendo hili ndani na katika Kristo ambaye ndiye ufunuo ulio kamili wa Mungu, tendo hili huwa baraka na mizania ya kuhesabiwa haki mbele za Mungu. “Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38b. Je, walifahamu jambo hili? Mwisho wa maisha yetu hapa duniani tuwe tayari kwa maswali haya matatu mbele ya Mungu:
1.      Ulipenda vipi katika maisha yako niliyokupa hapa duniani?
2.      Umetumiaje vipaji nilivyokupa?
3.      Je, maisha ya Mwanangu mpendwa Yesu Kristo yalikuwa na maana yoyote kwako?

Wapendwa katika Kristo, tukiwa tunajiandaa vyema kuyajibu maswali hayo, hatutakoswa na chochote endapo upendo utakuwa ndiyo namna yetu ya kuona na kutenda. Kwa kuwa “twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga,” 1Kor 8:7b. Utambulisho wako na kujulikana kwako kwa Mungu hakutakuwa kwa njia nyingine zaidi ya ‘kupenda.’ Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye,” 1Kor 8:3. Upendo wa kweli utakuwajibisha katika kweli na haki yale yahusuyo wewe na wengine unaoishi nao.

Na mwenye kuishi katika kweli na haki, hujua ni nani anayemtumikia na kumwabudu. Kama wafuasi wa Kristo, tunayemwambudu na kumtumikia ni Mungu wa kweli na aliye hai. Naye Mtume Paulo anasema, Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu,” 1Kor 8:4. Leo tunazungukwa na imani za ajabu na hofu zisizo na kikomo. Mungu tunayemwabudi siyo Mungu wa vitisho.

 Mungu wetu ni huruma, neema na msamaha. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi; lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo,” 1Kor 8:5-6. Hakuna sababu ya kujawa na hofu ukiwa ndani na katika Kristo Yesu.

Ni wazi kwamba siyo wote wenye kujazwa ufahamu wa kweli kati ya imani na matendo yao. Ni kweli kwamba, ujuzi huu haumo ndani ya watu wote; ila wengine kwa kuizoelea ile sanamu hata sasa hula kana kwamba ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri zao, kwa kuwa dhaifu, hunajisika,” 1Kor 8:7. Ikiwa mtu ni tokeo la historia na makuzi yake, ni wazi kabisa imani za walio wengi bado zimesongwa na mila na desturi zao.

Hatumwendei Mungu kwa mtindo wa kuuchengesha ukweli kuhusu Yeye. Kumbe kwa wewe ujuaye kweli kuhusu Kristo yakupasa kuwa chumvi na mwanga pale ulipo. Ukweli ni kwamba, tusipokuwa mwanga na chumvi pale tulipo,yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake,” 1Kor 8:11. Kumbuka kuwa mbatizwa yeyote na mwenye kuishi ahadi zake za ubatizo ni Kristo mwingine pale alipo. Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo,” 1Kor 8:12. Usimuhuzunishe Kristo kwa matendo yako ambayo hata kwa kutokuyafanya hautapungukiwa chochote.

Ni vyema ukawa mfano wa kuigwa hasa pale unapozungukwa na wale wenye imani changa. Si vyema kuwa makwazo kwao. Mfano wa hili la makwazo Mtume Paulo anasema, Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu,” 1Kor 8:13. Ni vyema nikajizua kufanya yale yawakwazayo wenye imani changa hata kama kwa kufanya hivyo kwangu ni stahili.

Tumsifu Yesu Kristo!

Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo,” 1Kor 8:12


Tusali:-Ee Yesu, nifanye chombo cha upendo na imani ya kweli pale nilipo. Amina.

No hay comentarios:

Publicar un comentario