SIKUKUU YA KUZALIWA MAMA BIKIRA MARIA
Somo I: Mik 5:1-4a
Zab: 13:6ab, 6c
Injili: Mt 1:1-16, 18-23
Nukuu:
“Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee
binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake
kwa fimbo,” Mik 5:1
“Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye
mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja
atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani
za kale, tangu milele,” Mik 5:2
“Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa
ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa
Roho Mtakatifu,” Mt 1:18
“Naye Yusufu, mumewe, kwa vile
alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt
1:19
“Basi alipokuwa akifikiri hayo,
tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa
Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho
Mtakatifu,” Mt 1:20
“Naye atazaa mwana, nawe
utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi
zao,” Mt 1:21
“Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake
Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi,” Mt 1:23
TAFAKARI: “Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee
binti wa vikosi; yeye amemhusuru.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anasheherekea sikukuu ya
kuzaliwa kwa Mama Bikira Maria. Bikira Maria alikuwa mwanamke Myahudi aliyeishi kati ya karne ya 1 KK na
karne 1BK. Kadiri ya mapoke, wazazi wake walijulikana kama Ana na Yoakimu. Mama
Bikira Maria ni mke wa Yosefu, na alimzaa Yesu Kristo kwa uwezo wa Roho
Mtakatifu. Kwa sababu hiyo na kwa utakatifu wake anapewa heshima ya pekee
katika madhehebu mengi ya Ukristo. Hata hivyo, Maandiko Matakatifu yanawasifu
watu mbalimbali kutokana na jinsi walivyomuamini. Mungu na kutenda makuu kwa
ajili ya taifa lake.
Abrahamu alimuamini Mungu akawa tayari kumtolea sadaka mwanae
Isaka, tukio lililomfanya apate baraka ya pekee ya kuwa baba wa
waamini. Na mambo yalikuwa hivi, “Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara
ya pili kutoka mbinguni akasema,
Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala
hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika
kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za
mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui
zao; na katika uzao wako mataifa
yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:15-18.
Yosefu, mwana mpenzi wa Yakobo, alikuwa mwaminifu hata akaliokoa taifa
lisiangamie kwa njaa Naye akawaambia ndugu zake, “Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali
Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo,” Mwa 50:20
Musa ndiye mkomozi wa Taifa la Mungu katika Agano la
Kale: aliongoza Israeli kutoka utumwani
Misri akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai.
Maandiko ya Agano la Kale yanakiri, “Wala
hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa
uso; katika ishara zote na
maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao,
na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; na katika ule mkono wa nguvu wote,
tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote,” Kumb 34:10-12.
Waliofuata ni Yoshua, Debora, Gideon, Ruthu, Samweli, wafalme Daudi na
Solomoni, manabii Eliya, Isaya, Yeremia, Ezekiel na wengineo. Mwishoni Yesu
Kristo akamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza
kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini?
Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini
mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye
mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda
kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama,
namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale
waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo
katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye,” Lk 7:24-28
Elizabeti,
mama wa Yohane, alijiona hastahili kutembelewa na Bikira Maria, Mama wa Yesu,
akamuita, Mama wa Mungu. Naye Elizabeti anajiuliza, “Limenitokeaje neno
hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” Lk 1:43. Bikira
Maria si mtu wa ziada katika mpango wa Mungu bali ni mshiriki mkuu
wa ukombozi wa binadamu. Maria amechangia wokovu kwa kukubali mpango
wote wa Mungu aliyetaka amzae Mwanae, amlee na kumfuata kiaminifu hadi
msalabani, aliposhiriki kumtoa kama sadaka ya kutuokoa. Msimamo wake ulikuwa
mmoja tu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa
Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Tukichunguza nafasi yake katika
fumbo hilo, tunaweza kukiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi
Mungu aliyemtendea makuu, Lk 1:49, kwa kuwa, “Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka
mbinguni,” Yoh 3:27. Yale yote
ambayo Wakristo wengi wanayasadiki kuhusu Bikira Maria, hakujipatia
bali alijaliwa na Mwenyezi Mungu huku akiitikia kwa hiari fumbo la
mpango wake.
Jambo la
pili kumfahamu Mama Bikira Maria itatupasa kumwona Mama huyu katika maisha ya
Yesu. Yesu, kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu na kuwatii wazee wake: “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii;
na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake,” Lk 2:51. Na ishara ya kwanza
kwenye maishaya hadhara ya Yesu iliongozwa na Bikira Maria katika
arusi ya Kana ya Galilaya, akisukumwa na
huruma kwa wenye shida: kwa ombi lake Yesu aligeuza maji kuwa
divai, na wanafunzi wake wakamwamini. Yohane alisimulia hivi, “Siku ya tatu
palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.
Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai
ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, ‘Hawana divai’. Yesu akamwambia, ‘Mama
tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia’. Mamaye akawaambia watumishi, ‘Lo
lote atakalowaambia, fanyeni’. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo
yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya
nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, ‘Jalizeni mabalasi maji’. Nao wakayajaliza
hata juu. Akawaambia, ‘Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza’. Wakapelekea.
Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue
ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maj), yule mkuu wa
meza alimwita bwana arusi, akamwambia, ‘Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo
njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka
divai iliyo njema hata sasa’. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya
Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini,” Yoh
2:1-12
Bikira Maria
anasifiwa kwanza kwa imani yake kuu kabisa, kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni
tu. Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya roho kuliko ya
mwili. “Mtu
mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka
kusema nawe. Akajibu, akamwambia
yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? Akawanyoshea mkono wanafunzi wake,
akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa
maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye
ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu,” Mt 12:47-50.
Vilevile,
wakati wa utume wake, alimsikia “mwanamke mmoja katika lile kundi la
watu akisema, “Heri tumbo
lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini
yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika,” Lk
11:27-28
Kwa hiyo wapendwa wana
wa Mungu, tunapotafakri fumbo hili la kumwilishwa kwa Neno na kukaa kwetu,
tutambue kwamba licha ya udogo wetu, udhaifu wetu, mapungufu yetu, na unyonge wetu, sasa ni wakati wa kuinuliwa
kwetu kutoka katika utumwa wa dhambi na kuwa watu wapya. Mungu anapenda kuanza
upya na kila mmoja wetu na kuusimika ufalme wake milele. Nabii Mika nawaambia
wana wa Israeli, “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa
miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa
mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale,
tangu milele,” Mik 5:2. Udogo na unyenyekevu huo anauchukuwa Mama Bikira Maria.
Tendo
la Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu limewezekana kutokana na “NDIYO” ya Mama
Bikira Maria. Na Neno huyo, yaani, Mwanaye Yesu Kristo, ndiye atakayechomolewa
kutoka katika Taifa hili la Israeli, atasimama na kulilisha kundi lake kwa
nguvu za Bwana. “Naye atasimama, na kulisha
kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao
watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia” Mik 5:4. Utawala wake
siyo kwamba utaleta amani tu, bali Yeye mwenyewe ni Amani. “Na
mtu huyu atakuwa amani yetu,” Mik 5:5.
Wapendwa katika Kristo,
utendaji wa Mungu ni wa ajabu sana! Uteuzi wake hauna upendeleo hata kidogo.
Ila jambo ambalo lililo wazi ni hili; Mungu hupenda kuwainua wanyonge na hasa
wale waliodharauliwa, na wakati huo huo kuwanyenyekesha wale wote wanaojiinua
na kujikweza. Historia nzima ya wokovu wetu inaufunua ujumbe huu wa Mungu. Embu
watazama watu hawa; Zakaria, Elizabeti, Manoa na Mke wake, Samsoni, Mariamu, na
wengine wengi tu, walikuwa watu wa kawaida kabisa na wakati mwingine
walidharauliwa kutoka na mtindo wa maisha yao na mitazamo ya nyakati. Ila Mungu
hupenda kuvitumia vile vilivyodhaifu na kuvinyeyekeza vile vijikwazavyo.
Ndiyo
“Alifanyika mwili, akakaa kwetu:”-hapa ndipo alipochukua hali yetu ya kibinadamu,
ikiwa ni pamoja na mazingira yetu isipokuwa hakutenda dhambi. “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana
kinywani mwake,” 1Pet 2:22. Hata hivyo anakubali kuzaliwa katika hali na mifumo
ya kwetu katika asili zetu. Hivi ndivyo ilivyokuwa, “Kitabu cha
ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Yakobo akamzaa Yusufu
mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo,” Mt 1:1, 16. Historia ya familia
ya Yesu, Ukoo, Kabila na Taifa, unaufunua mpango mzima wa Mungu katika historia
hii ya wokovu wetu.
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna hata mmoja wetu aliyechakugua kuzaliwa katika familia
hiyo aliyopo. Hii ni pamoja na ukoo wake, kabila lake na Taifa lake. Yote ni
mapenzi na mpango wa Mungu. Tusema vipi basi pale tunapowaona baadhi yetu
wakizisifia familia zao, koo zao, makabila yao na Mataifa yao? Hivi kweli kuna
sababu yoyote ile ya kujisifia? Jibu ni HAPANA! Basi kama ni kujisifu,
Yesu angekuwa wa kwanza kufanya hivyo.
Lakini Yesu, “ambaye
yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali
alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa
wanadamu,” Flp 2:6-7
Wapendwa
katika Kristo, kwa tendo la Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu akichukua hali
yetu ya kibinadamu na mazingira yetu, ni heshima kubwa sana kwetu. Pili,
Mwokozi huyu anatufundisha unyenyekevu uliotukuka. Nasi tujifunze kwa mwalimu
wetu Yesu Kristo kwani kwake kuna
ufahamu wote.
Wapendwa
wana wa Mungu, sehemu hii ya Injili tuliyoisoma leo, na hasa, Mt 1:18-19,
inatufanya tujiulize swali hili. Kwa nini Yusufu alikusudia kumwacha Mariamu
ikiwa walikuwa bado kuoana? Ukweli ni kwamba, mila na desturi za Kiyahudi
zilikuwa tofauti na zetu. Mwanaume na mwanamke waliunganishwa pamoja wakati
wanapopeana miadi ya kuoana (uchumba), ingawa hawakuruhusiwa kuhusiana kimwlili
hadi baada ya harusi. Yusufu alikuwa anapanga kuuvunja uchunba wao rasmi baada
ya kugundua kuwa Mariamu ana mimba ili hali hakuwahi kukutana naye kimwili.
Yusufu anataka
kulifanya jambo hili kuwa siri ili kumnusuru Mariamu kifo cha aibu ambacho
kingempata kama jambo lile lingegundulika katika jamii. Kama Yusufu angetaka
kutafuta haki yake, sheria ilisema hivi kuhusu ubikira; “Mtu akitwaa mke, akamwingilia na
kumchukia, kisha akamshitaki
mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami
nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira; Lakini likiwa ni kweli neno hili, la
kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira; na wamtoe nje yule kijana (kike)
mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata
afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika
nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako,” Kumb 22:13-14,
20-21. Kwa hali aliyokuwa nayo Mariamu si tu tatizo la ubikira, ila alionekana
ana mimba. “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama
yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba
kwa uweza wa Roho Mtakatifu,” Mt 1:18
Kwa vile Yusufu
alimpenda sana Mariamu aliona ni vyema kumwondoa katika aibu ile, ili asife kwa
kupigwa mawe. “Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki,
asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:19. Hapa ndipo tunapoona
utu wa Yusufu. Utu huu ndio unaomfanya kuhesabiwa haki na Mungu kama mtu wa
haki. Yusufu hakupenda kulihukumu jambo lile asilolijua. Yusufu alimjua vizuri
Mariamu ikiwa ni pamoja na malezi aliyopata kutoka kwa wazazi wake. Hata hivyo
tukio hili la mimba lilibaki kitendawili kikubwa kwa Yusufu. Kwa upande
mwingine hapa tunafundishwa kwamba ukiwa na mashaka na kitu fulani usitende
chochote. Jambo au kitu kile kipe kwanza Muda. Kitendo cha Yusufu kutaka
kumwacha kwa siri Mariamu ilikuwa kulipa jambo lile muda. Je, ingetokea kwako
au kwangu kwa namna yoyote ile ungelipa jambo hili muda?
Swali lingine ambalo
linatujia katika habari hii, Mt 1:18 ni hili; Je Mariamu alikuwa na mimba kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu, au Yesu alikuwa uzao wa viuno vya Daudi kwa mujibu wa
Mdo 2:30?-(“Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya
kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake
atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi”). Mariamu alikuwa bikira;
Biblia inasema Roho Mtakatifu "alimfunika" Mariamu, si kwa jinsi ya
kuhusiana kimwili. Yusufu alikuwa baba pekee wa kisheria aliyemuasili Yesu,
hakuwa baba halisi. Lakini Yesu alikuwa mzao halisi wa ukoo wa Daudi kupitia
Mariamu, kama orodha ya vizazi yenye kupitia kwa Mariamu ya Lk 3:23-37
inavyoonyesha. Aya nyingine zenye kusema kuwa Yesu ni mtoto (mzao wa ukoo) wa
Daudi ni Mat 12:23; 15:22; 20:30; 21:9,15; Marko 10:47-48; 12:35; Luka 10:41;
18:38-39; Yoh 7:42; 2 Tim 2:8; Ufu 5:5; 22:16. Je, Mat 1:23 (Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana;
Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi) inatafsiri Isa 7:14 (Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba,
atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli) kimakosa kwa
kutumia jina "bikira?"
Jibu ni hapana. Si tu kwamba neno la Kiebrania lililotumiwa
hapa linamaanisha amaa "bikira" ama "msichana", lakini pia
tafsri ya Kigiriki ya Agano la Kale (Septuagint) imelitafsiri neno hili kuwa
“parthenos,” yaani bikira. Swali lingine ambalo tunaweza kujiuliza ni hili:
Kwenye Mat 1:23 na Lk 1:26-35, inawezekanaje Yesu aliyezaliwa na bikra awe mzao
wa ukoo wa Daudi? Hapa kuna mambo matatu ya kuzingatia;
1. Yesu hakuwa mtoto halisi wa Yusufu. Kama angekuwa, Yer
29:32 ingekuwa ni unabii wa uongo.
2. Yesu
alikuwa mtoto wa Yusufu kisheria. Leo hii, mwanaume anayemuoa mwanamke aliye na
mtoto anakuwa baba wa mtoto huyo kisheria, ingawa si baba halisi.
3. Yesu alikuwa mtoto
halisi wa Mariamu. Yesu alikuwa wa ukoo wa Daudi kisheria kupitia Yusufu, na
Yesu alikwa wa ukoo wa Daudi kuuhalisi kupitia Mariamu. Kadiri ya Mat 1:25, “asimjue
kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU,” Mt 1:25”. Je Mariamu alikuwa na watoto wengine wowote?
Mstari huu hautakuwa na maana yeyote na wenye kupotosha kama Yusufu na Mariamu
hawakuwa wamewahi kuwa na uhusiano wa kimwili.
Zaidi ya hapo, Mat 13:55-56; Mak 6:4; Gal 1:19; na Yuda 1 pia
zimerekodi kuwa Yesu alikuwa na wadogo wake wa kiume (ndugu). Eusebius, katika
kitabu chake kiitwacho Ecclesiastical History (karibu mwaka 360 BK) 2:23 na d
3:20 pia anasema kuwa wadogo wane wa kiume wa Yesu walikuwa Yakobo aliyeitwa
mwenye haki), Yose (au Yusufu), Yuda na Simoni.
Moja ya majibu yatolewayo na Kanisa Katoliki ni kuwa Yusufu
alikuwa na watoto kupitia ndoa yake ya awali, lakini si kupitia kwa Mariamu.
Hata hivyo, hakuna ushahidi toka kwenye historia ya Kanisa kuwa Yusufu aliwahi
kuwa na ndoa nyingine kabla ya ile na Mariamu, au mdogo wake yoyote wa kiume
hakutokana na Yusufu na Mariamu.
Jibu lingine la Kanisa Katoliki ni kuwa kwenye jamii za
Kimediteranian neno "ndugu" linaweza kumaanisha binamu na ndugu/jamaa
wa karibu wenye umri unaofanana, na si tu kaka au wadogo wa mtu. Hata hivyo,
Ambrose wa Milani alikuwa wazi kuwa Yesu hakuhitaji msaada wowote ili aweze
kuwaunganisha watu na Mungu, na Mariamu hakupaswa kusujudiwa (On the Holy
Spirit kitabu cha 3 sura ya 11 na.80 mwaka 381 BK). Alisema, "Na mtu
yeyote asihamishie jambo hili kwa Bikira Mariamu; Mariamu alikuwa hekalu la
Mungu. Na kwa hiyo Yeye (Mungu) pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa Yeye afanyaye
kazi katika hekalu lake (mwenyewe)."
Wapendwa wana wa Mungu,
pamoja na kuona ukweli huo hatuwezi kupinga kwamba yote hayo yalifanyika chini
ya mpango mzima wa Mungu. Mungu hawezi kujikanganya mwenyewe. Hivyo Nabii
Yeremia anasema, “Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia
Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye
atafanya hukumu na haki katika nchi,” Yer 23:5. Huyu ndiye Bwana wa haki na utawala wake ni
utawala wa hekima na hukumu zake ni za haki. Ujio wa Masiha ni habari ya wokovu
na kuwekwa huru mwili na roho. “Katika
siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa
ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 23:6. Basi na tuwe watu wa haki, tukitenda
yaliyo kweli na haki, na kuhukumu kwa haki. Kuyatimiza hayo, tujifunze
unyenyekevu wa Mama Bikira Maria.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Naye atazaa
mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake
na dhambi zao,” Mt 1:21
Tusali:- Ee Yesu,
tujalie unyenyekevu na utayari wa kufanya mapenzi yake. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario