JUMAPILI YA 25 YA
MWAKA-C
Somo
I: Amo 8:4-7
Zab/Kit: 113:1-2, 4-6, 7-8, (K) 1,
7
Somo II: 1Tim 2:1-8
Injili: Lk 16:1-13
Nukuu
“Lisikieni
hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini,
tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na
kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu; tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na
wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano,” Amo 8:4-6
“Akamwita,
akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili
wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena,” Lk 16:2
“Yule
wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea
uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya,” Lk 16:3
”Hakuna
mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na
kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia
Mungu na mali,” Lk 16:13
“Basi,
kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike
kwa ajili ya watu wote,” 1Tim 2:1
“kwa
ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani,
katika utauwa wote na ustahivu,” 1Tim 2:2
“Kwa sababu Mungu
ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo
Yesu,” 1Tim 2:5
TAFAKARI:
“Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.”
Wapendwa wana wa Mungu, maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo, “Hamwezi
kumtumikia Mungu na mali,” kwetu ni mwito wa kuyachunguza maisha yetu vyema. Na
kwa maneno hayo ya Yesu, anatoa elekezo sahihi na salama kuhusu maisha yako ya
yangu katika umilele, na yenye kibali mbele ya uso wa Mungu licha ya mapungufu
na udhaifu wetu. Kama kwayo ni mwito wa kuyachunguza maisha yangu, yanipasa
kujua uhusiano wa maisha yangu ya kiroho, nafasi yangu katika jamii, na
mali/utajiri nilizo nazo/nilio nao. Na swali ni hili; kati ya hivyo vitatu
(maisha ya kiroho, nafasi/cheo, na mali/utajiri), ni kipi/vipi
kinasukuma/vinavyosukuma maisha yako? Mali au utajiri na cheo vikiwa ndivyo
vinavyoyasukuma maisha yako, ni hatari sana kudondoka katika dhuluma, na hasa
kwa masikini na wanyonge.
Na huu ndio ujumbe wa
Mungu anaoutoa Nabii Amosi kwa matajiri
na mwenye mamlaka waliokuwa sababu ya dhuluma kwa masikini. Ujumbe huu
unawataka waziache njia zao mbaya na kumrudia Mungu. Naye anasema: “Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na
kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate
kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na
kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu; tupate
kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka
za ngano,” Amo 8:4-6. Leo Nabii Amosi angalikuwa katika jamii yetu angeongelea
ugumu wa maisha uliosababishwa na unaosababishwa na watu wachache waliolifisidi
taifa letu na wanaoendelea kulifisidi. Hawa ndio wale wajulikanao kwa ‘umaarufu
wao’ kama ‘mafisadi.’ Wito ni kuonja moyoni na kughairi uovu kwa sababu waovu
na uovu ni chukizo mbele ya uso wa Mungu. “Laana ya Bwana i katika nyumba ya
waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki,” Mit 3:33
Lolote
lile lililo ovu halina umilele ndani yake. Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu
(Yesu Krito), sadaka hii ya Mwana wa Mungu pale Msalabani, na ufufuko wake,
ndicho kikomo cha uovu wote. Hii ndiyo njia aliyoichangu Mungu kuushinda uovu.
Na tunaushinda uovu tukiwa ndani na katika Kristo Yesu. Kristo ndiye mizania
yetu katika kweli, upendo, haki, na amani.
Wapendwa katika Kristo,
Injili ya leo inatupatia hali halisi kuhusu hesabu yetu siku ya mwisho. Yesu
analisema jambo hilo akitolea mfano wa Tajiri mmoja na Wakili wake
dhalimu. Bila kujua siku wala saa, Wakili huyu dhalimu anatakiwa na Tajiri
yake kutoa hesabu ya uwakile wake, baada ya Tajiri yake kupata habari ya
kutapanywa kwa mali zake. Ni vyema tukaona kwa undani kidogo msukumo wa maisha
unaoongozwa na mali/utajiri na
sifa/cheo, na hatma yake katika maisha ya kiroho.
1.
Watu wengi wanaongozwa na mali
Watu wa mtindo
huu, tamaa yao ya kupata vitu linakuwa
ndilo lengo la maisha yao yote. Kweli hili haijalishi upo wapi na ndani ya
mfumo upi wa maisha. Msukumo huu wa kutaka zaidi kila siku una misingi yake
katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa
wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo yote matatu si ya kweli. “Lakini
hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi
zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na
uharibifu,” 1Tim 6:9. Mali huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na
sababu kubwa ndugu yangu, vitu havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka
vipya, vikubwa, na bora zaidi.
Kuna imani pia kwamba
nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na umuhimu unaotegemea
ulivyo navyo ndugu yangu ni vitu viwili tofauti. “Maana
shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali
wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim
6:10. Thamani yako haitegemei mali
zako, Mungu anasema kitu cha muhimu maishani mwako si vitu! Imani ya watu wengi
kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo nyingi kutanipa usalama. Huwezi!
Ndugu yangu, utajiri
unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza
kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na
Mungu. “Kwa maana hatukuja na kitu duniani,
tena hatuwezi kutoka na kitu,” 1Tim 6:7. Mt.
Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na
vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo
uchache na huo wingi.
2. Watu wengi wanaongozwa na kutaka sifa
Ndugu yangu, wakati mwingine watu hawa wanaruhusu
matarajio ya wazazi, waume, au wake, watoto, waalimu au rafiki zao kutawala
maisha yao. Watu wazima bado wanajaribu kupata sifa kwa wazazi wao ambao
hawajafurahi kamwe. Wengine wanasukumwa na vikundi vya marafiki, wanahofu
wenzao watawafikiriaje. Kwa bahati mbaya, wale wafuatao kundi au maoni ya mtu
binafsi hupotea ndani yake.
Ndugu yangu, kwa nini kujifungia katika gereza hili la
fikra na maoni? “Mtu awaye yote akifundisha
elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo,
wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna,”
ITim 6:3-4b. Sifa yetu kubwa ni kulitenda lile alilofundisha Bwana wetu Yesu
Kristo kwani ndilo lenye uzima wa milele. Mara nyingi kupenda sana sifa huku na
wakati mwingine kunakoendana na matumizi mabaya ya madaraka, huwa kilio kwa
wanyonge na ukandamizaji wa haki za watu, hasa wanyonge.
Ndugu yangu, sijui funguo zote za mafanikio, lakini
funguo moja ya kushindwa ni kujaribu kumpendeza kila mtu. Kutawaliwa na maoni
ya watu wengine ni njia wazi ya kukosa makusudi ya Mungu katika maisha yako.
Bwana wetu Yesu Kristo anatupa angalizo kwa jambo hili, "hakuna mtu
awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu,
ama atashindana na huyu na kumdharau huyu: hamwezi kumtumikia Mungu na
mali." Mt 6:24.
Kuna nguvu nyingi zinazoweza kuongoza maisha yako
lakini zote mwisho wake ni mfu: kutotumia vipawa ulivyo navyo, mahangaiko ya
moyo, na maisha yasiyo ya utoshelevu. “Bali
wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo,
saburi, upole,” 1Tim 6:11. Kuishi katika mfumo huu ndiko kutakako kupa amani ya
kweli na utulivu wa ndani.
Ndugu yangu, kuishi maisha yanayoongozwa na malengo,
ni kutawaliwa, na kuelekezwa na makusudi ya Mungu. Hakuna kitu cha muhimu zaidi
kama kujua malengo ya Mungu kwa maisha yako, na hakuna mbadala kwa hilo-siyo
mafanikio, utajiri, kujulikana, au anasa. Bila malengo, maisha ni
mwendo usio na maana, shughuli bila mwelekeo, na matukio bila sababu. Bila
malengo, maisha ni kitu duni, kidogo sana, kisicho na umuhimu wowote.
Hivyo, alichokifanya
kwa haraka Wakili yule ni kurejesha uhusiano wa haraka na wateja zake ambao
ndio hatma ya maisha yake kwa sasa. Katika jambo hili ilimpasa kutoa msamaha wa
madeni bila kuhathiri utajiri wa Tajiri yake. Hivyo, “Yule bwana
akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa
ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru,”
Lk 16:8. Kwa kuyasema haya, Yesu anatuacha na swali zito la kujibu. Swali hilo
ni hili: Mimi na wewe tunasubiri nini kurejesha uhusiano wetu na Mungu kwa muda
na nafasi tuliyonayo sasa tukiwa bado kwenye nuru, yaani, kwa ubatizo wetu na
agano letu katika maisha, iwapo Wakili huyu na udhalimu wake aliweza kurejesha
uhusiano wake na wateja zake? Wokovu ndiyo sasa.
Je, kwa hali na
mazingira haya yaliyo jaa uovu na yasiyo rafiki na maisha yako na yangu kiroho
tufanye nini? Kama wabatizwa na wafuasi wa Kristo Yesu, na wenye hofu ya Mungu,
Mtume Paulo anatupa changamoto ya maisha ya kiroho, na wosia pia. Ni kweli bila
Mungu kwa nguvu zetu wenyewe hatutoweza chochote. Ili kitu au jambo hilo lidumu
katika hali yake, yatupasa kumshirikisha Mungu katika kila jambo tulifanyalo.
Hivyo, “kabla ya mambo yote, nataka dua, na
sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote,” 1Tim 2:1.
Hapa tunawaombea wote; yaani wema na waovu katika maana ya kwamba, wema Mungu
azidi kuwasimamia katika kila jambo kwa lengo la kuushinda uovu kwa wema, na
wale waovu Mungu awabadili tabia na nia zao mbaya.
Ni wajibu wetu pia kama
Kanisa kwa imani yetu, na wananchi kwa kuzaliwa kwetu na uzalendo wetu
kuwaombea viongozi wetu wadumu katika kweli, upendo, haki, na amani kwa wote
bila kumbagua yeyote. Tunawaombea haya viongozi wetu kwa sababu wengi kutokana
na nafasi walizopewa na umma wa watu wanazitumia vibaya kwa ulevi wao wa
madaraka. Ni kwa namna hiyo tunasali na kuwaombea “wafalme
na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na
ustahivu,” 1Tim 2:2. Pamoja na kufanya hili ambalo ni wajibu msingi kabisa, na
tukiiombea amani nchi yetu, tusisahau
kuwa amani ni tunda la HAKI. Tutende haki kila mmoja kadiri ya wito na nafasi
yake katika jamii, na siyo kuihubiri amani bila kutenda haki. Kufanya hivi ni
chukizo kwa Mungu, na maigizo kwa mwanadamu.
Kuiombea amani nchi
yetu, na wakati huo huo kutenda haki kwa mujibu wa sheria na Katiba tuliyo nayo
kama sheria Mama, jambo hilo “ni zuri, nalo
lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye
hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli,” 1Tim 2:3-4.
Tusipoongozwa na kweli hii, huko mbele ni giza tupu. Marehemu Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, na Mtumishi wa Mungu, katika uchanga wa Taifa letu
miaka ya sitini aliyatamka haya juu ya Uhuru na Maendeleo na kusema, “Tanzania
ni ya Watanzania; na, Watanzania ni wote. Mtu mmoja hana haki kusema ‘Mimi ni
wote.’ Na hakuna Mtanzania kwenye haki ya kusema ‘najua lililo zuri kwa
Tanzania na wengine lazima walifanye.” Tatizo
letu kubwa leo kama Taifa ni pale tunapotanguliza “u mimi wetu.”
Tunapofanya hilo (kuendeleza ubinafsi
wetu), taswira ya Mungu ndani yetu utoweka, “kwa
sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja,
Mwanadamu Kristo Yesu,” 1Tim 2:5. Hata Waswahili wanasema, “kidole kimoja
hakivunji chawa.” Na hata pale
tunaposimama wenyewe, basi tusimame kwa maslahi mapana ya wote katika kweli na
haki kama Kristo Yesu “ambaye
alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira
yake,” 1Tim 2:6. Na mwisho wa siku historia hubaki kuwa mwalimu mwaminifu
kwetu.
Ajenda binafsi yenye malengo binafsi
mwisho wake ni kuumbuka kwa sababu Mungu hachezewi kamari wala kupigiwa bao.
Pasipo imani dhabiti na kweli kwa yale yote tuyatendayo, mwisho wa siku
tutajulikana kama waigizaji ambao hatukumaanisha tuliyokuwa tunafanya ingawa
machoni mwa watu yalivuta hisia kubwa sana na zenye matumaini. Na kwa upande wa
Mtume Paulo anasema wazi kwamba ndani na katika Kristo Yesu (mpatanishi kati ya
Mungu na wanadamu), naye-Paulo “kwa
ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo),
mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli,” 1Tim 2:7. Haya ndiyo maisha
yanayoongozwa na malengo. Na katika hili, Mtume Paulo anasema, “nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku
wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano,” 1Tim 2:8. Tufanye
yote tukiwa na tumaini lile KUU kwamba, ‘Kristo Yesu ndiye mpatanishi kati ya
Mungu na wanadamu, na bila Yeye hatuwezi tukafanya lolote lile, liwe dogo au
kubwa,’ Yoh 15:5. Amina!
Yohane Masikio au kwa jina la utani na
kwa kazi yake, “Galibi Mchuuzi” hujidamka kila siku alhajiri na mapema akiwa na
kapu lake lenye bidhaa mbali mbali, kuelekea kituo cha mabasi kufanya biashara.
Kwa mfumo huu wa maisha yake, Galibi Mchuuzi kila siku kwake ni biashara,
jumatatu hadi jumapili, liwe jua au mvua, baridi au joto. Jambo lingine la
ajabu na la pekee, Galibi Mchuuzi hutembea na pesa zake zote, yaani, faida ya
kila siku. Pesa hii uificha ndani ya kaputula ambayo juu yake huvaa suruali,
mara zote huvalia kibarakashee-kofia ambayo mara nyingi huvaliwa na Ndugu zetu
Waislam.
Siku moja jumapili mchana akiwa kwenye
mizunguko yake ya kusaka hela kwa biashara yake ile ya umajinga, ghafla
alijisikia vibaya na hatimaye ilimbidi kujilaza pembezoni mwa barabara. Na kwa
bahati nzuri ni muda huo huo Paroko wa eneo lile, Padre Ombeni, alikuwa anarudi
kutoka vigangoni kuadhimisha Misa Takatifu.
Mara Paroko alisimama na kwenda kujua
nini kilichomjiri Galibi Mchuuzi kwani mara kwa mara Paroko upishana naye
njiani. “Rafiki kulikoni. Mbona umejilaza hapa?,” Padre Ombeni alimuuliza. Bila
kusema chochote, Galibi aliingiza mkono ndani ya suruali yake na kuchomoa
burungutu la pesa na ndani ya mfuko mdogo wa plastic kulikuwa na kitambulisho
cha ubatizo. Vyote alimkabidhi Padre Ombeni. Na hapa ndipo Paroko alipogundua
kuwa Galibi alikuwa Mkristo, na jina lake ni Yohane Masikio, aliyebatizwa
Parokiani hapo miaka 37 iliyopita.
Kwa sauti ya mbali, Yohane Masikio
aliomba kuungama. Paroko alifanya hilo ikiwa ni pamoja na kumpa mpako wa
wagonywa, na Ekarist Takatifu. Baba Paroko akamwinua pamoja na kapu lake
kumwingiza kwenye gari na kumwahisha hospitalini ambayo haikuwa mbali na
parokia. Baada ya siku tatu, Yohane Masikio alipona kabisa na kuja kutoa
shukrani kwa Paroko.
Na mambo yalikuwa hivi, “Baba Paroko
aksante sana kwa kuyaokoa maisha yangu. Baada ya huduma ile nilijisikia
kuinuliwa juu kwa nguvu za ajabu na kuingizwa Kanisani na kundi la watu
walikuwa wamevaa nguo nyeupe. Walinipeleka mpaka chini ya Msalaba Mkubwa
uliokuwa pembezoni kwa Altari ya Kanisa hilo, na kuniambia, ‘Mtazame huyo
unayeendelea kumtesa hadi sasa,’ wakinielekezea kwa Yesu Msalabani. Baada ya
hapo sikuwaona tena wale watu, nami ndipo niliposhtuka na kujiona nipo
Hospitalini na ufahamu wa kutosha.” Je, kwa hili nifanye nini?
Baada ya ukimwa kidogo, Paroko Ombeni
alimjibu na kusema, “kamwe usimtese tena Yesu. Njia unayoifuata siyo nzuri,
hivyo yachunguze maisha yako ya kiroho, na biashara yako. Mungu bado
anakupenda, na ndiye aliyewatuma wale watu waliovalia nguo nyeupe. Hao ni
malaika.”
Padre, “naweza kuungama tena?” Yohane Masikio,
aliuliza kwa shauku kubwa. “Mwanangu, jisikie huru kupatanishwa na Mungu.
Nifuate kwenye sanduku la maungamo,” Paroko Ombeni alisema kwa upole na upendo
mkubwa.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mungu
ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo
Yesu,” 1Tim 2:5
Tusali:-Ee
Yesu na Kimbilio letu, tufanye chombo chako cha haki, upendo na amani, na mwisho
tuandae kwa kifo chema. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario