JUMANNE
WIKI YA 25 YA MWAKA-C
Somo: Mit 21:1-6, 10-13
Zab/Kit: 119:1, 27,
30, 34, 35, 44
Injili: Lk 8:19-21
Nukuu
“Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa
Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo,” Mit 21:1
“Kila njia
ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo,” Mit 21:2
“Kutenda
haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka,” Mit 21:3
“Akaletewa habari
akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe,” Lk
8:20
“Akawajibu
akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na
kulifanya,” Lk 8:21
TAFAKARI: “Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno
la Mungu na kulifanya.”
Wapendwa
katika Kristo, hofu ya Mungu licha ya kutuongoza katika kweli, haki na upendo
wa dhati, utuunganisha kuwa kitu kimoja katika Kristo. Sote huwa ndugu katika
Kristo si kwa njia hii ya kibailojia, bali ufanywa ndugu kiroho na kuvushwa
katika mitizamo ya kibinadamu isiyo beba umilele ule tunaoutamani. Hivyo Yesu
analisema jambo hii akifafanua maana ya ndugu pale alipoletewa taarifa ya uwepo
wa Mama yake na ndugu zake wakimsubiri nje ya Hekalu. Naye anasema, “Mama yangu na ndugu
zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya,” Lk 8:21. Ni kwa hofu ya
Mungu tu twaweza lisikia neno la Mungu na kulifanya.
Hivyo Yesu anamaanisha
kweli asemavyo, “Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na
kulifanya,” Lk 8:21. Kwa maneno haya
haikumaanisha kwamba Yesu anaukana uhasili wake na familia yake, bali anakwenda
zaidi ya mipaka ya kifamilia, koo, kabila na utaifa. Sote kwa kupitia Yesu
Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, tunaunganishwa na
upendo wa Mungu. Na tunapolisikia na kulifanya neno hilo la Mungu bila
mawaa, baraka na neema huwa matunda yake.
Bila hofu ya Mungu
binadamu huweza kufanya matendo maovu yasiyo na mfanano hata na wanyama.
Wanyama waweza kuwa mfano kwetu kwa matendo yao. Je, wabisha? Hivi ulishawahi
kuona Simba akimuua simba mwenzake hivi hivi tu? Je, ni wangapi wamepoteza
maisha yao kwa mkono wa binadamu wenzao? Je, ushaona Nyani akinyonga kichanga
chake? Je, ni vichanga vingapi kila dakika vinanyongwa duniani leo? Hakika
wanyama wanasomo zuri kwetu la kujifunza pale tunapoikosa hofu ya Mungu.
Kwa upande wa kijamii,
kiongozi asiyekuwa na hofu ya Mungu ni hatari sana. Kwa mamlaka yake aweza
kufanya lolote, hasa pale anapozungukwa na magoigoi wanaosukumwa na hofu ya
woga. Hadhi ya kiongozi yeyote yule ni kuwa na hofu ya Mungu, kusimama katika
kweli na haki. Hivyo, “Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama
mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo,” Mit 21:1. Mfalme au kiongozi
yeyote yule mwenye hofu ya Mungu ufikiri papana na kwa undani kabla ya kusema
chochote. Kubwatuka hovyo na kunakoleta sintofahamu kati ya wale anaowaongoza
siyo dalili za kiongozi mwenye hofu ya Mungu.
Kiongozi
au hata mtu mwingine yoyote yule upimwa njia zake kwa kile alicho. “Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali
Bwana huipima mioyo,” Mit 21:2. Na ndani ya kila mtu ipo nguvu fulani
inayoongoza maisha ya mtu huyo. Maisha ya mtu huweza kuongozwa au kusukumwa kwa
hatia, sifa, mali, na hata umaarufu fulani. Njia salama ni kusukumwa na hofu ya
Mungu. Ni kutenda katika, kweli, upendo haki, na amani. Hivyo, “kutenda
haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka,” Mit 21:3. Sadaka yoyote ile isiyokuwa na uhusiano na Mungu
katika kweli, haki, upendo, na amani, ni chukizo kwa Mungu, na igizo kwa
mwanadamu.
Hivyo ni vyema kila
siku, na hasa pale ambao tuna dhamana mbele za watu kujiepusha na majigambo,
kiburi, na sifa pasipo siha. Kwani “macho
yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi,” Mit
21:4. Kama Mkristo na mwenye kujali na kuwajibika elewa kwamba hu mfano wa
Kristo mwenyewe pale ulipo kama Mfalme. Na Ufalme wake Kristo ni Ufalme wa
kweli na haki, upendo na huruma, unyenyekevu, na msamaha.
Tunapoishi
ufalme huu wa Kristo katika kweli, utuepusha na udanganyifu wa ulimwengu wa
vitu na ushindani. Hivyo yapo maonyo ambayo yatupasa kuyaelewa na kuepukana
nayo. Kwanza kabisa lazima kujua kwamba, “Mawazo
ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji,”
Mit 21:5. Je, mawezo yako mwisho wa siku ukufikisha pale Kristo alipo?
Jambo
la pili ni kuishi katika kweli, na kupata yote ikiwa ni pamoja na mahitaji yako
kwa njia ya haki. Kinyume chake ni kwamba, “kupata
akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti,” Mit
21:6. Je, ni wangapi leo tunaishi katika mauti haya tunapoutafakari utajiri
tuliokuwa nao kwa njia ya dhuluma na udhalimu?
Tatu,
ni vyema ukajua kwamba leo ikiwa wewe na mimi, upo kama ulivyo kutokana na
historia yako, na makuzi yako. Hivyo penye nafsi ya mtu ndipo penye muhimili
wake wote. Nafsi ipo kati ya mwili na roho. Nafsi yako ikiegemea mwili, basi
kuna uwezekano mkubwa kuangamia, ila nafsi yako ikiegemea roho, hapo kuna uzima
wa milele, Gal 5:19-23. Na kwa
namna hivyo uovu wa mtu ni pale nafsi yake inapoegemea mwili na kutamani
matendo ya mwili.
“Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili
machoni pake,” Mit 21:10.
Nne,
maisha ni shule pale ulipo. Matokeo ya shule hii ya maisha ni utakatifu wako.
Hivyo cheza vizuri kwa kila jambo huku ukilenga umilele wako. Na “Mwenye
mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea
maarifa,” Mit 21:11. Maarifa na ufahamu wako ukujenge kuiona nuru ya Mungu, na
nuru hiyo iangaze matendo yako.
Tano,
ishi katika haki na kwa kila mmoja pale ulipo, iwe una dhamana juu yao au
hauna. Kwa sababu, “mwenye haki huitafakari
nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia,” Mit 21:12. Palipo
na haki pana amani, kwani amani ni tunda la haki. Na mwisho, kuishi katika hofu
ya Mungu ni kujifunza kusikiliza zaidi kuliko kuongoa na kujitetea tu pasipo
siha yoyote ile. Kwa kuutoa muda wako kusikiliza mahangaiko ya wengine
kunakufanya kushiriki pia uchungu na maumivu yao. Hivyo tendo hilo hubadili pia
namna ya kutenda kwako. Kinyume chake ni
kwamba, “azibaye masikio yake
asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa,” Mit 21:13.
Kusikiliza mahangaiko ya wengine ni moja ya tiba kwa mwenye mahangaiko hayo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kutenda
haki na hukumu humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka,” Mit 21:3
Tusali:-Ee Yesu, tujalie
neema ya kuvuka mipaka ya familia zetu, koo zetu, kabila zetu na utakifa kwetu,
ili uonekane katika wote na katika yote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario