domingo, 4 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 23 YA MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 23 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 6:1-11
Zab/Kit: 149:1-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili: Lk 6:12-19
Nukuu
Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?” 1Kor 6:2 

Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake?” 1Kor 6:5

 “Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu,” 1Kor 6:11

Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu,” Lk 6:12 

Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume,” Lk 6:13 

Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:14-16 

TAFAKARI:Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk 6:43-44. Maneno haya mazito ya Bwana wetu Yesu Kristo, yanaturudisha katika hali halisi ya ubinanadamu wetu. Mtakatifu Thomasi wa Akwino katika mafundisho yake, anasema, “neema hufanya kazi katika uhalisia.” Kwa maana nyingine, kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kile mtu alicho na matendo yake. Kwa ufahamu wa kawaida-‘common sense,’ inatuwia vigumu kuelewa kwa undani kilichopo ndani ya mtu kwa kile atakacho kuwa au aombacho kuwa na hasa pale kinapo kinzana na kile atendacho.

Ni vigumu kuamini na kuelewa mama ambaye anakesha kila siku akiomba neema na baraka za Mungu kuwa mama na mlezi mzuri ilhali kila apatapo ujauzito-mimba huitoa. Huku ni kucheza na neema na baraka za Mungu. Tutapigwa na mshangao mkuwa pale tutakapo hukumiwa na wale wanaoishi kweli hii, yaani, mlandano wa maisha yao na matendo yao. Hawa ndio wateule na watakatifu wa Mungu. Naye Mtume Paulo katika hili anasema, Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?” 1Kor 6:2. Mara nyingi na baadhi ya watu na hasa viongozi wa kisiasa kwa kutaka huruma ya wanyonge walio wengi, wamelitumia vibaya jina la Mungu kama kichaka cha kuficha uovu wao na kuwapumbaza wanyonge wanaotaka kusikia heri za peponi zisizo na kweli katika uhalisia.

Ndugu yangu, fumbua macho yako na ona vizuri. Si vyema kuruhusu Jina la Mungu kunajisiwa mimbarini na baadhi ya watu na hasa viongozi wa kisiasa kwa kutafuta umaarufu na kuonewa huruma na umma wa watu na kufanya eneo hilo kama kichaka cha kuhalalisha uovu wao. Tunapo ruhusu hali na mazingira kama hayo, tujiandae kwa adhabu ya Mungu. Mungu hafanyiwi dhihaka hata kidogo. Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake?” 1Kor 6:5. Maneno yetu yaendane na matendo yetu. Na maombi yetu yaakisi maisha yetu na kile tutakacho kuwa. Kinyume chake ni dhihaka mbele ya Mungu, na maigizo mbele wa wanadamu.

Ni jambo la kushangaza kwa Mkristo na anayeamini ufufuo siku ya mwisho mwenye kuishi kwa chuki na visasi, na asiye tayari kusamehe. Na mara nyingine tunaonyesha hali hii hata kwa wale wasio na imani thabiti. Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini,” 1Kor 6:6. Hili ni sikitiko kubwa kwa Kristo aliyekukomboa wewe na mimi pasipo mastahili yako au yangu. Kwa nini basi tunakoswa huruma? Kwa nini tunaendeleza sera za chuki na kupandikiza mbegu hiyo hata kwa watoto wetu? Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi,” 1Kor 6:9-10. Hakika katika haya hakuna mbingu.

Ndugu yangu, unapoendekeza ubinadamu na ubinafsi wako ni vigumu kumwona Kristo kwa wengine. Kwa matendo haya ya mwili, yaani,  uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Usalama wako na wangu upo kwenye tunda la roho, yaani, upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria,” Gal 5:22-23. Kiongozi kama kioo cha jamii anayoiongoza hanabudi kuwa na tunda hili la roho. Kiongozi mwenye kupandikiza mbegu ya chuki na visazi ajiandae kuvuna tufani la machafuko.

Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa hu hai leo na sasa basi jua kwa Mungu bado hujachelewa hata kwa wingi wa dhambi zako. Tumia muda wako vizuri leo na sasa ukiyachunguza mapungufu yako, ile uenende katika njia sahihi ya Mungu. Huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zako. Ni kwa huruma na neema hiyo ya Mungu, baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu,” 1Kor 6:11. Jeuri na kiburi ya nafasi, cheo, na madaraka uliyo nayo ni kwa muda tu. Ipo siku utagundua kuzungukwa kwako leo kote na watu kulimaanisha tu nafasi uliyokuwa nayo na wala  sio utu kwako na watu uliokuwa unawaongoza. Majuto ni mjukuu!

Yesu Kristo kama kiongozi wetu na aliyeishi kile alichokisema, ili kutimiza hazma ya kile alichokijia, yaani, kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi, aliyaweka yote wazi tangu mwanzo. Iwaya ya yote, Yesu Kristo alikuwa na kauli mbiu kama dira ya kila mmoja kufuata ili kufika kule alikotaka sote tufike-uzima wa milele. Kauli mbiu hii ilikuwa hivi; “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Kwa maana nyingine, huruma na neema ya Mungu hufanya kazi yake pale tunapoipokea huruma na neema hiyo kwa kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi.

Na hata baada ya kutoa kauli mbiu yake hiyo, Yesu alionyesha wazi mpango kazi wake mwanzoni kabisa kabla ya kufanya chochote. Na mambo yalikuwa hivi;  “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:16-19. Mpango kazi mzima wa Yesu hauna uchochezi wa aina yoyote ile, wala vitisho. Ni habari njema kweli kweli na iliyojaa matumaini.

Baada ya kutoa mpango kazi wake, Yesu akiwa Mungu na Mwanadamu, alihitaji watu wa karibu naye ili kuitenda kazi ile aliyoijia kama tulivyoona hapo mwanzo. Kuwapata watu hawa, Yesu hakukurupuka, bali aliyaweka yote mikononi mwa Baba yake aliye mtuma. Hivyo, Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu,” Lk 6:12. Ni baada ya maombi haya, Yesu anawachagua wanafunzi wake. Na hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume,” Lk 6:13. Hawa ndio wale Thenashara-Mitume kumi na wawili, Mt 10:2-5, yaani,  Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:14-16.

Hawa Thenashara ndio waliokuwa wasaidizi wake wa karibu katika kutimiza lile alilolijia yaani, kukuweka wewe na mimi huru kutoka utumwa wa dhambi. Na hawa Thenashara, “akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi,” Lk 9:1. ‘Aliwapa mamlaka’ ikimaanisha uhuru wa kufanya yale yampendezayo Mungu. Katika kweli hii, Yesu aliruhusu ubunifu katika utendaji kila mmoja kadiri ya karama zake. Hakika Kristo Yesu ni kiongozi kweli kweli, na mfano kwetu ulio hai. Tujifunze kwake.

Baada ya kufanikisha mpango huu, ikiwa ni pamoja na kuweka wazi kauli mbiu yake, mpango kazi wake, na kuwachagua watu wake wa karibu, yaani, Thenashara, alianza mara moja kazi ile aliyoijia. Hivyo “waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote,” Lk 6:17b-19. Yesu kamwe hakupoteza muda wake kupambana na watesi wake. Kwa maana nyingine, Yesu hakuwa na muda wa kupoteza kupambana na wapinzani wake; Mafarisayo, Waandishi, na Wazee, bali aliutumia muda wake wote wa miaka ile mitatu kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mbinguni. Matokeo ya kazi yake ni uwepo wa wewe na mimi leo kama Wakristo na wafuasi wake wenye hofu ya Mungu. Ni wajibu msingi kwa matiki hiyo kwamba wewe na mimi yatupasa kuwa mawakili wa Kristo pale tulipo.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu,” Lk 6:12


Tusali:-Ee Yesu, tufanye mawakili wako wema pale tulipo kila mmoja kadiri ya wito na karama zake. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario