JUMANNE
WIKI YA 24 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 12:12-14, 27-31a
Zab/Kit: 100:1-2, 3, 4, 5
Injili: Lk 7:11-17
Nukuu
“Maana
kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule,
navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12
“Kwa
maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu
Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote
tulinyweshwa Roho mmoja,” 1Kor 12:13
“Takeni sana
karama zilizo kuu,” 1Kor 12:31a
“Na
alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana
pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye,”
Lk 7:12
“Bwana
alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13
“Akakaribia,
akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana,
nakuambia, Inuka,” Lk 7:14
“Yule
maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:15
TAFAKARI: “Takeni sana karama zilizo kuu.”
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na sheria
ya Bwana, yaani Torati, leo kielelezo chetu kuufikia uzima wa milele ni Kristo
Yesu kwa wote walio na ufahamu juu yake (dhamira safi na hofu ya Mungu), na kwa
namna ya pekee wabatizwa wote.
“Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa
kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa
au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja,” 1Kor 12:13. Ni katika kweli hii kwamba wapo
wengine kwa dhamiri zao safi na hofu yao juu ya Mungu watapata wokovu.
Wapendwa katika Kristo,
Mungu wetu ni Mungu wa wanadamu wote licha ya tofauti zetu za kiimani. Hakuna
anayeishi katika ulimwengu huu kwa sababu yake mwenyewe, Rum 14:7. Kila mmoja
wetu anayo chapa ya Mungu ndani yake, Mwa 1:27. Ulimwengu huu ukiwemo na vyote
vilivyomo ni Mali yake Mungu, Zab 24.1. “Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu
wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja,
atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa
atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo,” Rum 3:29-30. Ukweli ni kwamba
kila anayeongozwa na mwenye dhamiri hai na safi ataokolewa siku ya mwisho.
Mafundisho
ya Kanisa hasa tunaposoma Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 847, inafundisha
juu ya dhamiri hai na safi ambapo hata wale wasiomjua Kristo ndiyo ponya yao.
Ukweli huu pia umefafanuliwa vizuri katika mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa
Vatikano, Konstitusio ya Kichungaji juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa leo,
“Gaudium Et Spesteaches,” “Furaha na Matumaini,” inaelezea ukweli huu kama
ifuatavyo; “Kwa kweli ni katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili
tu kwamba fumbo la binadamu linaangazwa. Maana Adamu, mtu wa kwanza, alikuwa
mfano wa yule atakayekuja, yaani Kristo Bwana. Naye Kristo, aliye Adamu mpya,
akilifunua fumbo la [Mungu] Baba na la upendo wake, hudhihirisha kikamilifu kwa
binadamu, binadamu alivyo, na kumjulisha wito wake mkuu. Jambo hilo haliwahusu
wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema ya Mungu
hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana. Maana Kristo alikufa kwa
ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa
hiyo lazima tuwe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano
wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu,” (no. 22)
Somo letu la leo Mtume Paulo anaongelea vizuri
sana kuhusu Kristo kama Kanisa nasi tukiwa viungo vyake. Ni kwa Sakramenti ya
ubatizo tunafanywa wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake. Lakini tunaishi na
kupata uhai tukiunganika na Kristo kama viungo vya huo mwili yaani Kanisa. “Maana kama vile mwili
ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi,
ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12. Kanisa kwa mtazamo huu, ni mwili wa Kristo, yaani
wabatizwa wote, na Sakramenti ya wokovu wetu. Basi tukiwa viungo vya Kristo
vyenye kujenga mwili wa Kristo ambao ni Kanisa, kila kiungo kina kazi yake na
kwa kutimiza kazi yake ndiyo afya ya mwili mzima. “Kwa
maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi,” 1Kor 12:14.
Hivyo kila mmoja wetu, yaani mbatizwa
ana umuhimu wake wa pekee kuujenga mwili huu, yaani Kanisa, na kufanya vizuri. “Basi ninyi mmekuwa
mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake,” 1Kor 12:27. Umoja katika
utofauti wetu ndio uzuri wa mwili huu wa Kristo yaani Kanisa. Karama zetu
mbalimbali ni kwa ajili ya Kanisa na kufaidiana. Hivyo, “Mungu
ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu
waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na
maongozi, na aina za lugha,” 1Kor 12:28.
Utofauti huo katika huduma na karama ni kwa ajili ya Kanisa zima la wana wa
Mungu. Sote kwa pamoja twaufanya mwili huu, yaani Kanisa kuwa hai.
Wapendwa katika Kristo, ni vyema ukajua
karama zako na huduma yako katika Kanisa. Si vizuri kupoteza muda wako kwa
kuishi maisha linganishi, yaani, maisha ya mfanano na mwingine, bila kuvitambua
vipaji vyako ambavyo ndiyo njia bora ya kutumika katika mwili huu, yaani
Kanisa. Na kuvijua vipaji na karama zako ni kutokukata tamaa pale unaposhindwa
kufikia lengo lako kusudiwa maisha au huduma unayoitoa. Wote hatuwezi fanana. “Je! Wote ni mitume?
Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa?
Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?” 1Kor 12:29-30. HAPANA! Kila mmoja wetu
anakarama yake ambayo Mungu anapenda uitumie hiyo kuudhihirisha Utukufu wake na
Furaha yake.
Wapendwa wana wa Mungu,
ukweli ni kwamba kila jambo lina kusudi lake, hivyo litazame jambo hilo kwa
jicho la imani, na wala usiruhusu manung’uniko na kujihukumu pale mambo
yanapokwenda ndivyo sivyo. Tazama mara zote tumaini lile lililopo mbele yako.
Mfano wa mtu aliyetazama tumaini
lililopo mbele ya maisha yake ni Mama yule wa mji wa Naini kadiri ya Injili ya
leo, na aliyefiwa na mwanaye wa pekee, Lk 7:11-12. Mama huyu na tukio lake hili
kiimani linatufundisha kuishi kwa tumaini pale tunapokumbana na sintofahamu
katika maisha.
Injili ya leo inatupa
simulizi hili kwa namna ya pekee. Yesu Kristo katika safari zake za kuihubiri
habari njema ya wokovu akiwa na wanafunzi wake, wanakutana na msafara uliobeba
maiti ya mwana pekee wa mama mjane. “Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na
maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa
mjini wengi walikuwa pamoja naye,” Lk 7:12. Bila shaka msafara ule wa maiti ile
na hali za watu kama zilivyokuwa kwa kusikitika juu ya msiba ule, na hasa mama
huyu ambaye anaonekama kuwa mwema kwa jirani zake, unamsikitikisha Yesu pia. “Bwana
alipomwona (mama mfiwa) alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13.
Neno ‘usilie’ katika
mazingira haya limebeba ujumbe, ‘ondoa hofu na uwe na matumaini.’ Tumaini
lenyewe hapa na katika uhasilia wake ni Kristo Yesu mwenyewe. Kwa upendo wa ajabu na huruma ya Kimungu,
ambaye kwa sasa ni Mungu na mwanadamu, Yesu “Akakaribia,
akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana,
nakuambia, Inuka,” Lk 7:14. Baada ya tukio
hili la pekee kabisa na ajabu, “Yule
maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:15. Bila shaka
mimi na wewe tungekuwa katika msafara huo tungetimua mbia kwa hofu!
Pamoja na hofu
waliokuwa nayo watu wale katika msafara ule, walibaki na tumaini kubwa mbele
yao. “Hofu
ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na,
Mungu amewaangalia watu wake,” Lk 7:16. Hili ni fundisho kwetu pia. Twapaswa
daima kumshukuru Mungu na kuliweka tumaini kwake tu aliyetutendea mambo ya
ajabu, badala ya kujitafutia utukufu binafsi, na hata kutaka kuabudiwa. Pili,
tuwe vyombo vya kusambaza habari njema kwa wengine, badala ya chuki. “Habari
hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando,” Lk
7:17. Je, ndugu yangu, hapo ulipo watumika kama chombo cha habari njema ya
wokovu, au ndiyo upande wa pili, yaani, mzalisha chuki?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bwana
alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tujalie Neema na Baraka ili tudumu katika tumaini lako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario