JUMAPILI YA 18 YA MWAKA-C
Somo
I: Mhu 1:2; 2:21-23
Zab: 95:1-2, 6-7, 8-9
Kol 3:1-5, 9-11
Injili: Lk 12:13-21
Nukuu:
“Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa
maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu
yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu,” Mhu 2:21
“Basi
mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi
mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1
“Hapo
hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala
mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11
“Akamwambia,
Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Lk 12:14
“Akawaambia,
Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu
vyake alivyo navyo,” Lk 12:15
“Lakini
Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu
ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo
alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21
TAFAKARI: “Na jina lake Mataifa watalitumainia. Kristo ni yote,
na katika yote.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 18 ya mwaka “C” wa Kanisa.
Tunapoyatazama masomo yetu ya leo tunazamishwa na Mama Kanisa kutafakari na
kushirikishana kweli hii, kwamba, “Na jina lake Mataifa watalitumainia. Kristo
ni yote, na katika yote.” Somo la kwanza kadiri ya Mhubiri, anayaona maisha si
kitu wala chochote, bali ni ‘ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni
ubatili,’ Mhu 1:2. Swali la msingi na la kujiuliza ni hili, nitawezaje
kuitamani hiyo kesho kama sioni maana ya leo? Kama tumeumbwa ili tuishi milele,
na Mungu akaona inafaa tuwepo ulimwenguni hapa, iweje tena niwe na mawazo haya
kwamba mtu apata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake
alivyojitahidi chini ya jua?’ Mhu 2:22.
Ndugu yangu, ni vyema
nikaelewa kwamba vyote vinavyoonekana na visivyoonekana alivyoviumba Mungu kwa
asilimia kubwa vinamlenga huyu mwanadamu aliyepewa heshima ya juu kabisa kwa
kuumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni katika mantiki hiyo, “Bwana aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu;
ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa,
aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18.
Pamoja na mahangaiko na sintofahamu za maisha, ulimwenguni hapa pana kusudio la
Mungu katika maisha yetu. Hapa ndipo uwanja wa kujua kusudi la kuumbwa kwetu na
kujiandaa katika uzima ule wa milele. Na kwa kusudi la kuumbwa kwetu, hapa
duniani ndipo tutakapo mjua Mungu, mpenda Mungu, mtumikia Mungu, na mwisho
kurudi kwake mbinguni.
Ni
kweli kabisa hapa na pale tutakatishwa tamaa, ila isiwe sababu ya kutokuona
kusudi la Mungu katika upana wa uumbaji wake. Ufanyalo zuri leo, kesho laweza
kufutwa kwa hila tu na kutoweka. Ila pamoja na hali hiyo, hatuwezi kufuta wema
wa lililo jema mbele ya macho ya Mungu. Na hata jambo hilo linapobaki katika
historia yake, huendelea kuwa somo kwa vizazi na vizazi.
“Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na
kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu
yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu,” Mhu 2:21. Pamoja na mtizamo huu
wa Mhubiri, maisha ni zaidi ya yale tuyafanyayo leo au kuyamiliki. Jambo la
maana na muhimu ni kuwa huru nje ya yale tuyafanyayo na kuyamiliki.
Tusipojibadua katika haya, maisha hukosa maana na hasa pale yanapotoweka yale
tuyafanyayo na kuyamiliki. Ni swala la wakati kwamba itafika mahali hatutaweza kufanya chochote.
Je, katika hali hiyo ya
kutokufanya chochote, utu wetu utatoweka kwa sababu tu wazee? Utajiri na mali
tulizonazo tumemilikishwa kwa muda tu na wakati ukifika watamilikishwa wengine,
nasi tutaondoka kama tulivyokuja bila chochote kwa sababu, “Nchi
na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab
24:1. Ndugu yangu, tunapojimilikisha yale ambayo kwa asili siyo yetu, mwisho wa
siku huwa ni ubatili na masikitika makubwa. “Kwa
kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku
moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili,” Mhu 2:23.
Wapendwa Taifa la Mungu, Injili ya leo,
inatutaka tutafakari kwa undani maisha yetu na uhusiano wake na mali. Ndugu
moja anamwendea Yesu mbele ya mkutano na kumwamuru amwambie ndugu yake amgawie
urithi wao, Lk 12:13. Badala yake, Yesu anamuuliza swali la msingi na la
kushangaza. “Akamwambia,
Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Lk 12:14. Swali hili linatutaka kuweka bayana
nini maana ya maisha yetu na mahusiano yake na mali. Ndugu yangu unayesafiri
nami katika tafakari hii, elewa leo kwamba maisha yako ni dhamana hapa duniani,
na mali tulizo nazo tumeazimwa tu kwa muda. Mali ni za Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
muda wetu hapa duniani na nguvu zetu, akili, nafsi, mahusiano, na mali zetu
zote ni zawadi toka kwa Mungu ambazo ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia vizuri.
Sisi ni mawakili wa yale Mungu atupayo. Wazo hili la uwakili huanza na utambuzi
wa kuwa Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu na kila mtu duniani. "Nchi na
vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake." Zab
24:1. Hivyo Yesu anamtahadharisha kijana yule na sisi pia kwa kutuambia kwamba,
“Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu
vyake alivyo navyo,” Lk 12:15. Uzima wako na furaha yako ya kweli haitokani na
wingi wa mbali ulizokuwa nazo. Kwa maana nyingine, vitu hivyo kwa kuwa navyo
kwa wingi havituhesabii haki mbele za Mungu. Ndugu yangu, kama humwamini yule
aliyefufuliwa kutoka wafu yaani, Kristo Yesu, wingi wa utajiri wako ni bure
kabisa kwa sababu mali zote ni za Bwana ukiwa na wewe mwenyewe. Mtume Paulo
anasema, “sisi tunaomwamini yeye
aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye
alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki,”
Rum 4:24b-25. Hivyo wingi wa mali zako bila Imani juu ya Kristo mfufuka ni
bure.
Hakika "hatumiliki"
chochote kwa wakati wetu mfupi wa kuishi duniani. Mungu "hutukopesha"
dunia tunapoishi hapa. Ilikuwa mali ya Mungu kabla hujaja, na Mungu anamkopesha
mtu mwingine ukifa. Je unabisha? Ndugu, ukweli ni kwamba unaifurahia dunia hii
kwa muda mfupi tu. Injili ya leo inatuambia kwamba asiyefahamu ukweli huu ni
MPUMBAVU kama mkulima yule tajiri aliyetaka kufurahisha nafsi yake kwa kusema,
‘pumzika basi, ule, unywe, ufurahi,” bila kujua ni nani aliye sababu ya uzima
wake. “Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu
wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari
vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo
mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21. Ndugu yangu bado furaha yako ipo kwenye mali?
Mungu alipowaumba Adamu na Hawa,
aliwakabidhi uangalizi wa uumbaji wake na akawaweka kuwa wadhamini wa uumbaji
wa mali yake. "Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale
samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho
juu ya nchi," Mwa 1:28
Kazi ya kwanza ambayo Mungu aliwapa
wanadamu ni kuangalia na kutunza "vitu" vya Mungu duniani. Wajibu huu
haujaondolewa kamwe. Ni sehemu ya malengo yetu leo. Kila kitu tunachokifurahia
yapasa tukione kama dhamana ambayo Mungu ameiweka mikononi mwetu. "Hapo
tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu."
1Kor 4:2
Yesu mara kwa mara anaonyesha kuwa
maisha ni dhamana na anatoa mfano wa talanta, mfanya biashara alikabidhi
watumishi utajiri wake alipo safiri. Aliporudi alitathmini kazi ya kila
mtumishi na kumpa ujira sawasawa na kazi yake. Yule tajiri anasema, "vema, mtumwa mwema na mwaminifu;
ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya
Bwana wako," Mt 25:21.
Ndugu, mwisho wa maisha yako duniani
utatathminiwa kulingana na ulivyotumia yale Mungu aliyokukabidhi. Hii inamaana
kwamba mambo yote unayofanya, hata yale mambo madogo madogo ya kila siku, yana
matokeo ya umilele.
Kama utaona mambo yote kuwa dhamana,
Mungu anaahidi zawadi tatu katika maisha ya milele. Kwanza, utapewa
"uthibitisho". Atasema, "kazi nzuri! umefanya vyema." Kisha
"utapandishwa" daraja na utapewa jukumu kubwa katika umilele:
"nitakuweka uwe mwangalizi wa vitu vingi." Na mwisho utakaribishwa
katika "karamu." "Njoo ushiriki katika furaha ya Bwana wako.
Watu wengi wanashindwa kufahamu kuwa
pesa ni jaribu na dhamana toka kwa Mungu. Mungu anatumia pesa kutufundisha
kumtegemea; na kwa watu wengi fedha ni jaribu kuu kupita yote. “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni
kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na
kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10. Mungu anaangalia jinsi tunavyotumia
pesa ili kupima jinsi gani tunaaminika. "Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu
katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?" Lk
16:11. Huu ni ukweli wa muhimu sana. Mungu anasema kuna uhusiano wa moja kwa
moja baina ya ninavyotumia pesa zangu na hali yangu ya kiroho. Jinsi
ninavyotawala pesa zangu "utajiri wa dunia" ni kigezo cha kiasi gani
Mungu anaweza kunikabidhi baraka za kiroho, "utajiri wa kweli".
Hebu jiulize ndugu yangu, Je, namna
ninavyotumia fedha zangu yaweza kumzuia Mungu kufanya mambo zaidi maishani
mwangu? Je, ninaweza kuaminiwa katika utajiri wa kiroho? Wapo watu wachache
katika mazingira na maisha yetu, waliweza kuthibitisha uhusiano wa moja kwa
moja baina ya walivyotumia pesa zao na hali ya kiroho ya maisha yao. Pesa au
utajiri wao havikuwa kipao mbele katika maisha yao. Watu na maisha yao ya dhiki
ilikuwa kero zake na mara zote alijitahidi kutafuta suluhu ya kero hizo za
watu. Mtu wa namna hii ndiye tunayeweza kuumpa dhamana ya kusimamia mali ya
umma. Alilolisema ndilo alilolifanya. Dhima hii ndiyo iliyompa nguvu ya
Kimaadili. Mfano wa mtu huyu ni Baba yetu wa Taifa; Julius Kambarage Nyerere,
aliyetutangulia katika haki. Apate rehema kwa Mungu apumzike kwa amani. Sina
shaka katika maisha yake. Ipo siku atapewa uangalizi mkubwa zaidi na Mama
Kanisa na kuwa Mwombezi wetu-Mtakatifu.
Yesu Kristo anasema, "na yule
asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa
vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake
huyo watataka na zaidi." Lk 16:48. Maisha ni dhamana. Na kadiri Mungu
anavyokupa zaidi, ndivyo anakutaka uwajibike zaidi.
Ndugu
yangu, pamoja na kuishi leo na sasa na changamoto zake, yanipasa kujua shabaha
ya maisha yangu ipo wapi. Kama Mkristo na mfuasi wa Kristo, Kristo ndiye
shabaha maisha yangu. ‘Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Kristo ni yote, na katika yote.’
Kwa nini Kristo ndiye
shabaha ya maisha yako kama Mkristo na mfuasi wake? Ndugu yangu, wakati fulani
wanafunzi wa Yohana Mbatizaji walimwona Yesu akiwa anabatiza, nao walimwendea
Yohana Mbatizaji ili kujua juu ya kile afanyacho Yesu, na nafasi yake katika
ufahamu na umaana wake. “Yohana akajibu,
akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni,”
Yoh 3:27. Kwa jibu hili la Yohana ilithibitisha Kristo ndiyo njia sahihi na
hapana shaka juu yake. Pamoja na ukweli kwamba “vyote vilifanyika
kwa huyo (NENO-CHRISTO); wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika,” Yoh 1:3, kwa kinywa
chake Yesu Kristo analithibitisha hili na kusema, “hakuna
mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 14:65. Ni ndani
na katika Kristo kuna njia, kweli, na uzima. Naye Yesu anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa
Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ndugu
yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, nje ya Kristo una nini
kilichochako zaidi ya dhambi zako?
Kristo ndiye shabaha
ya maisha yako unapotazama fumbo zima la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Tendo hili la UFUFUKO wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo fursa ya pekee kwa wale
wote wamuaminio Kristo, ambaye ndiye mwisho wa shaka yote. Naye Mtume Petro
analisema tukio hili katika undani na upana wake. “Wala
hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini
ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Ndugu
yangu hapo ulipo Kristo yupo? Hapo ulipo usalama upo bila Kristo? Ndugu yangu
hata nikipoteza vyote katika ulimwengu huu kama ninaye Kristo ndani ya maisha
yangu sitokuwa nimepungukiwa na chochote.
Na
hivi ndivyo asemavyo Mtume Paulo hasa kwa wale wanaaminio ufufuo wa Kristo, na
upya wa maisha yao ndani na katika Kristo; “Basi
mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi
mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Tendo
la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo linatusukuma toka ndani ya mioyo yetu na
imani yetu kuyatafuta yaliyo juu kule Kristo aliko. Kwa Mkristo yeyote hapa
duniani asipolifanya jambo hili kuwa kielelezo cha maisha yake, basi ajue kwake
ufufuko hauna maana ye yote. Mtume Paulo anasema hivi kuhusu ufufuko, “tena
kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure,”
1Kor 15:14. Ufufuko wa Kristo ndiyo kiini cha Imani yetu.
Ndugu yangu, mambo
yaliyo juu aliko Kristo ni yale yote yanayotuongoza huko aliko, yaani ufalme wa
mbinguni na umilele wake. Kwa maneno
mengine ni “kuvaa utu mpya,
unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba,” Kol 3:10. Utu huu upya ni tendo la kupiga vita aina zote za
dhambi kwa sababu dhambi ufifisha na kuzorotesha utu wetu wa ndani ambao ni
nafsi na roho.
Jambo la pili na lenye maana kabisa
katika maisha ya kiroho ni kufikiri muda wote yale yaliyo juu na siyo yaliyo
katika nchi. Hapa Mtume Paulo anaongelea sana swala la nafsi ya mtu. Nafsi
inapoegemea zaidi katika mwili matokea yake ni anguko kuu na mwisho wa
matumaini yote ya kuurithi ufalme wa Mungu. Hapa ndipo binadamu anapoonekana
mara zote kufikiri yaliyo katika nchi na yasiyo na umilele. Kuepukana na kadhia
hii, Mtume Paulo anatoa angalizo kwa kusema,
“Basi,
vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya,
mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu
ya Mungu,” Kol 3:5-6. Ghadhabu ya Mungu hapa ni kuukosa ufalme wake na
kuangamia milele pasipo kuwa na nuru yake.
Ndugu yangu, pale nafsi inapoegemea roho,
ndipo tunapojazwa tumaini jipya na kufanywa upya siku kwa siku. “Kwa hiyo hatulegei;
bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa
upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Kuishi ukweli
huu ndani na katika Kristo ni kuchuchumilia cheo chetu halisi, yaani UTAKATIFU
WAKO! Cheo hiki kila mmoja wetu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ndiyo
stahili yake, na anaipata kwa kuishi kweli kwa mafundisho ya Kristo, na
kutimiza ukweli huo kwa uaminifu. Hivyo hasili zetu katika maana ya mila na
desturi zetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na utaifa wetu hazina
uhalalisho wowote katika cheo hiki kama hatunaye Kristo katika maisha yetu ya
kila siku. Ni kwa sababu hii Mtume Paulo anawapa angalizo watu wa nyakati zake,
na sisi pia kwa kusema, “hapo hapana
Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi,
mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11.
Wapendwa katika Kristo,
angalizo la mtindo huo alilotoa Mtume Paulo na lenye kutuweka katika mstari
sahihi kuelekea urithi tulioandaliwa na wenye hadhi ya cheo chetu, ndiyo
changamoto kubwa kama wafuasi wake Kristo. Na changamoto ya Mkristo ni kupenda
hata pale pasipopendeka, ikiwa kipimo cha upendo huo ni kupenda bila kipimo.
Kwa kupenda kwa mtindo huu, mimi na wewe tuwe tayari kuyapokea yale
aliyoyapokea Kristo Yesu, ila kwa sasa na kwa tumaini kubwa ni kwamba, Kristo
kesha yashinda mateso hayo, Kristo kesha ushinda Msalaba.
Ni katika pendo hilo
Kristo anapomponya mtu yule aliyepooza mkono, Mt 12:13, Mafarisayo wanafanya
shauri la kumwangamiza, Mt 12:14. Ila kwa mbinu hizi hawatafanikiwa kama
ulivyokuwa utabiri wa Nabii Isaya, akisema, “Tazama,
mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye;
Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu,” Mt 12:17-18.
Kumbe usalama wangu na wako upo kwa Kristo mwenyewe, na huu ndio ule “Mwanzi
uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo
hukumu ikashinda,” Mt 12:20. Naam, “Na jina
lake Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21. Je, bado una mashaka na Kristo Yesu?
Upendo Katete, binti
aliyetoka familia masikini sana ya Bwana na Bibi Lazaro Katete, alisoma kwa shinda
sana hadi kufikia kiwango cha kuwa Daktari bingwa wa magonjwa ya akina Mama na
Watoto. Kuhitimu masomo yake hayo ilikuwa mwanzo mpya wa maisha mapya katika
familia yao. Baada ya miezi sita ya kuajiriwa kwake, ulilipuka ugonjwa wa Ebola
katika nchi yake na hivyo aliona ni wakati wa kuitumia elimu na utaalamu wake,
na kama sadaka katika nchi yake.
Baada ya mwenzi mmoja
akiwa anatoa huduma hiyo katika kambi rasmi ya wagonjwa wa Ebola, hali
ilibadilika ghafla kwani naye alionekana ana dalili za kuambukizwa ugonjwa huo.
Kambi nzima iliingiwa na hofu, si kwa sababu ya ugonjwa ule ambao kwa wakati
ule ulikuwa si kitu cha kuepukika, bali waliingiwa hofu kumwana mtu ambaye
alikuwa karibu nao na kujitoa bila kujibakiza kuwahudumia hawezi tena kufanya
hivyo.
Na baada ya wiki mbili,
Upendo Katete alifariki. Hakika lilikuwa pigo kubwa sana kwa jamii ile na hasa
wazazi wake na familia yake kwa sababu nuru ile iliyokuwa inang’aa ilizimika
ghafla. Familia yake haikupata hata nafasi ya kumwona na hata kumpa heshima ya mwisho
kwa kuuaga mwili wake, kutokana na hathari za wao pia kuambukizwa.
Baada ya miaka mitano,
na kwa kutambua mchango wake na historia ya maisha yake, jamii yake na msaada
kutoka nje ya nchi ile, waliamua kujenga hospitali kubwa sana kwa heshima yake
yenye kutoa huduma kwa akina mama na watoto. Kumbe tukio hili linatukumbusha
maneno haya ya Yesu, “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka
katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao
mengi,” Yoh 12:24. Ndugu yangu, ni wazi leo Upendo Katete hayupo tena katika
hali ya kushikika, ila bado na kwa kiasi kikubwa anaendelea kuishi na kutoa
hudumu kwa jamii yake kupitia hospitali hii; “Upendo Katete Hospital.”
Tumsifu
Yesu Kristo
“Hapo hapana Myunani
wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala
mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11
Tusali:-Ee
Yesu, maisha yetu yana maana ndani na katika wewe. Tupe ujasiri wa kuyatafuta
katika maisha yetu kila siku yale ya juu pale ulipo. Amina