lunes, 6 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 10 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 10 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 18:20-39
Zab: 16:1-2a, 4, 5, 8, 11
Injili: Mt 5:17-19
Nukuu:
Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17 

Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie,” Mt 5:18 

 “Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno,” 1Fal 18:21

 “Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie,” 1Fal 18:37 

TAFAKARI: Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.”

Wapendwa wana wa Mungu, Sheria ya Bwana ni utaratibu wa kuyaishi yale yampendezayo Mungu, na kuwa na mahusiano mazuri naye kwani Yeye ndiye uhai na uzima wetu. Wana wa Israeli walipewa sheria kama mwongozo wa kutenda na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. “Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe,” Kut 24:12. Sheria hizi zilipaswa kufuatwa kiaminifu na bila kuzichakachua. “Mioyo yenu na iwe kamili kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.” 1Fal 8:61.

Ukamilifu na uaminifu wa mtu ulipatikana katika kuzishika sheria za Bwana. Kwa sababu, “sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.” Zab 19:7. Hivi ndivyo ilivyopaswa kuzishika sheria za Bwana. Na hilo ndilo lililokuwa kusudi la sheria. Jambo la kushangaza wakati wa Yesu, Wayahudi hawakuwa wanafuata Torati kama iliyokuwa mwanzo, yaani, nyakati za Musa. Wayahudi walikuwa wanafuata tafsiri ya Torati ambayo iliendana na matamanio yao na siyo ya Mungu. Huu ndio ugomvi uliokuwepo kati ya Yesu na Waandishi na Mafarisayo.

Matamanio haya ya Mafarisayo na Waandishi katika ubinadamu wao ambayo yalienda kinyume na tamanio la  Mungu juu ya sheria nyakati zile za Yesu, ndiyo hayo yaliyojitokeza pia nyakati zile za Nabii Eliya na wale wafuasi wa miungu ya Baali. Kuwarudisha kwenye mstari wa kweli na haki, ikiwa ni kumfuata na Mungu wa kweli na wakuabudiwa, Nabii Eliya anawaasi na kusema, “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno,” 1Fal 18:21.

Kwa kuwafundisha ni Mungu yupi aliye hai na anayepaswa kuabudiwa, Nabii Eliya anatoa ushauri wa kumtolea Mungu huyo sadaka ya kuteketezwa kama ishara iliyo hai. Kadiri ya somo letu la leo tumesikia jinsi wafuasi wale 450 wa miungu ya Baali walivyotoa sadaka yao, na kuliita jina hilo la Baali bila mafanikio licha ya kujichanja na kutokwa damu. Na ndipo Eliya alipomjeukia Mungu wake aliye hai na kufanya  ishara zilizobeba kumbukumbu ya safari ya ukombozi ya wana wa Israeli. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu,” 1Fal 18:31-32. Eliya anatambua kuwa Mungu aliyewafikisha hapo walipo hawezi kamwe kuwakana kwa sababu wanamwamini na wana matumaini makubwa juu yake.

Baada ya watesi wake Nabii Eliya kushindwa na kuikubali aibu yao na mungu wao wa uongo, na ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako,” 1Fal 18:36. Kwa jambo hili ambalo Nabii Eliya anataka kulifanya siyo kwa kujiinua yeye mwenyewe wala kujitukuza, bali huyu Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli ajulikane na kuabudiwa milele. Eliya anafahamu nafasi yake katika jambo hili, yaani, yeye ni mpelekwa tu wa kuwapa watu ujumbe ule maalumu wa Mungu. Na kwa namna hiyo, Eliya anajikabidhi hivi mbele ya Mungu na kusema, Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie,” 1Fal 18:37. Eliya hatangulizi maslahi yake mbele wala kujulikana kwa lolote lile. 

Maandalizi yalipo kamilika, na kuwahakikishia watu wote kuwa Mungu amuombaye ni mwaminifu na mwenye nguvu kwa kuimwagia sadaka ile ya kuteketezwa maji mapipa manne mara tatu, Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji,” 1Fal 18:38. Huyu ndiye Mungu aliye hai na anayepaswa kuabudiwa. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu,” 1Fal 18:39. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, kwa hiki kilichotokea, Wayahudi hawakupaswa kukengeuka katika imani yao. Ila kadiri tusomapo historia ya Taifa hili la Israeli na kutafakari, tunaona mambo hayakuwa kama yalivyopaswa kuwa. Hali ya uvuguvugu wa imani ya kweli ilikuwa hivyo hata nyakati za Yesu hata pamoja na kupewa torati kama mwongozo wa kufuata na kuwa karibu na mapenzi ya Mungu.

Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu, Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi), iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati, (Mt 15:2-3, 6; Mk 7:3, 5, 8, 9, 13). Naye Yesu anawaambia, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:8. Mapokea haya ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Mtume Paulo baada ya kuongoka na kuujua ukweli kuhusu sheria ya Bwana anawaambia Wakolosai, Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Ukweli ni kwamba, Mtume Paulo kama Mfarisayo kabla ya kuongoka kwake aliyafuata mapokeo haya ya wazee ambayo yalikuwa ni ‘ukweli wa Mungu uliopotoshwa.’ Paulo anakiri jambo hili na kusema, Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal 1:14.

Kwenye jambo hili, yaani kweli ya Sheria ya Bwana, Yesu anawakemea Mafarisayo na Waandishi na kusema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17. Hapa Yesu akubaliani nao kwa swala la kuichakachua Torati kama walivyokwisha kufanya. Yesu anarudisha mpango mzima wa Mungu katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Yesu anatoa zaidi maana ya sheria na ushikaji wa sheria hiyo. Yesu anawakosoa Mafarisayo kwa unafiki wao katika sheria na kusema, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache,” Mt 23:23

Utimilifu wa sheria kadiri ya mpango mzima na mtazamo wa Yesu umebebwa katika upendo. Hii ndiyo amri mpya. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Mtakatifu Agustino anatuambia kwamba, “ukipenda utafanya yote.” Ni katika mantiki hii kwamba, “mkipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Je, leo hatushangai kuona baadhi ya viongozi wakiichakachua Katiba ya nchi zao kwa ajili ya matamanio yao na uchu wao wa madaraka? Jambo hili limekuwa chanzo kikubwa cha machafuko mengi duniani na hasa kwenye bara letu la Afrika. Ni ukweli usiopingika kwamba, vikundi vingi vya kigaidi vimejitokeza pale sauti ya wengi katika mkondo sahihi, yaani, demokrasia ilipoganyagwa, kubezwa, na hata kubakwa kwa manufaa wa watu wachache tu katika kundi zima la walio wengi. Ni vyema tukasoma alama za nyakati.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno,” 1Fal 18:21


Tusali:-Ee Mungu Mwenyezi, na Baba yetu upasaye kuabudiwa, waongoze viongozi wetu waliopewa dhamana na umma, mara zote wayaone maslahi mapana ya watu wao, na siyo ubinafsi wao. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario