IJUMAA WIKI YA 10 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 19:9a, 11-16
Zab: 27:7.8a, 8b-9abc, 13-14
Injili: Mt 5:27-32
Nukuu:
“Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa
nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana
hakuwamo katika upepo ule,” 1Fal 19:11b
“na
baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la
nchi,” 1Fal 19:11c
“na
baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule;
na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu,” 1Fal 19:12
“Ikawa,
Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama
mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa,
Eliya?” 1Fal 19:13
“Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini
mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati,
amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini,” Mt 5:31-32
TAFAKARI: “Toka, usimame mlimani mbele za
Bwana.”
Wapendwa wana wa Mungu, ‘kutoka na kusimama mlimani mbele za Bwana’ ni
uthibitisho wa maisha bila hatia, na kielelezo cha kuisimamia hukumu ya Bwana
iliyo haki na kweli. Mlima kama kitu kilicho juu, chochote kilicho juu yake
uonekana vizuri kwa wale walio chini yake. Hivyo hiki kilicho juu ili kionekane
na wote chapaswa kuonekana bila kuzongwa na uvuli, yaani kitabia kisiwe na
hatia. Ni kusimama katika kweli bila kuwa na ‘dhania’-“bias” katika hukumu ya
haki na kweli. Hali na tabia hii humpa mtu ‘nguvu ya maadili’ katika kusema,
kuonya, na hata kuamrisha pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo. Hali na nguvu
hii ya kimaadili haijalishi maumbile ya mtu katika udogo wake, au ukubwa wake.
Kwa kuwa Bwana alipendezwa na Nabii Eliya, anamkubusha nguvu aliyonayo
na aache woga katika kutenda kwake hata kama mazingira yanayomzunguka yamejawa
hofu, 1Fal 19:11a, 14. Katika mazingira kama hayo yatupasa kwenda kwa utulivu
wa ndani, na siyo kukurupuka. Mungu kamwe hapatikani katika ghasia au machafuko
yanayotuzunguka. Hivyo ni wito kwetu kuwa na busara na utulivu wa ndani ‘palipo
machafuko na sintofahamu’ kuona uhalisia wa mambo, na kutoa suluhu lenye heri.
Hapa ndipo tunapoona busara ya kiongozi anavyokabiliana na sintofahamu katika
maisha ya wale anaowaongoza. Lengo siyo wepesi wa kutoa majibu ‘mepesi kwa
maswali magumu’ bila kufikiri kwa kina, bali kuwa na uelewa mpana wa kile
kisichojulikana vizuri kwako na kwa wengi. Na usemapo iwe mara moja na
kueleweka kwa wote.
Kwa
upande wetu binadamu kuelewa mafumbo mazito kama haya twaitaji utulivu wa
ndani. Ni katika utulivu Mungu hujidhihirisha. Mfano, Mungu anajidhihirisha kwa
Nabii Isaya kwa namna hii: “Na tazama,
Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba
mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo,
tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na
moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu,”
1Fal 19:11-12. Tunapopatwa na jambo la kutuhuzunisha au tusilolifahamu, moyo
wetu hupitia hatua mbalimbali kama upepo wa nguvu, tetemeko la nchi, na moto.
Katika hali hizi zote za uchungu na hasira Mungu hawezi kamwe kujidhihirisha
ndani yetu. Hivyo katika hali kama hiyo yakupasa kutulia na kutokufanya
chochote zaidi ya kutafakari hali ile. Kwa maana nyingine usifanye maamuzi
yoyote ukiwa katika hali ya hasira. Mwisho wa hasira yako, maamuzi uliyoyafanya
yatakugharimu maisha yako, na hali yako. Mtu yeyote yule mwenye kutoa maamuzi katika hali isiyo ya utulivu, madhara
yake ni makubwa sana, na mbaya zaidi akiwa yeye ndiye kiongozi au mzazi. Ni
wanyenyekevu tu uweza kurudi nyuma na kusawazisha mambo kwa kukiri kudondoka
kwao na kuomba msamaha kwa maamuzi yao mabaya na yasiyokuwa na tija. Mwenye
kiburu uzidi kujitetea na kuhalalisha alichokifanya, na hapo ndipo huaribu
kabisa.
Wapendwa wana wa
Mungu, hapa ndipo tunapoweza kuona udogo wa kitu unavyokuwa na kufikia ukubwa
wake ambao unatuwia vigumu kujinasua. Huu ndio mtazamo wa dhambi kadiri ya Injili ya leo. Kumbe
kadiri ya Injili ya leo dhambi haihesabiki tu kwa kufanya tendo halisi, bali
hata kwa kuwaza na kuvutwa kwa hisia ya kufanya dhambi hiyo. Mizania ya dhambi
ipo sawa kwa kufanya au kutokufanya ili hali tu tamaa ile ya kufanya jambo hilo
ipo ndani yako. Kilichokosekana hapo ni mazingira halisi ya kulitenda jambo
hilo, ila uzito wa dhambi ni ule ule. Tafsiri hii ya dhambi inatupeleka mbali
zaidi na kututoa katika mtazamo wa kizamani wa kusema kuna dhambi ndogo na
kubwa. Yesu anatupa angalizo katika jambo hili: “Mmesikia
kwamba imenenwa, Usizini; lakini
mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini
naye moyoni mwake,” Mt 5:27-28. Je, si yale yamtokayo mtu moyoni mwake ndiyo
yamtiayo unajisi? Je, si ndani ya moyo wa mtu ndipo kwenye vyanzo vya yale yote
yamjazayo mtu na kumfanya kile alicho? Pasipo utulivu wa ndani viongoza
matamanio yako ya nje (jicho, au mkono, Mt 5:29-30) hukosa mwelekeo. Nuru ile
ya ndani inapofifishwa yote ya nje huenda mrama.
Wapendwa
wana wa Mungu, “Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho
kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? Bali
vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi,” Mt
15:17-18. Utulivu wa ndani ndiyo taswira halisi ya mtu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“lakini
mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini
naye moyoni mwake,” Mt 5:28
Tusali: Ee Yesu Mwema,
tujalie utulivu wa ndani katika kuona, kuamua na kutenda. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario