JUMATANO WIKI YA 11 YA MWAKA-C
Somo: 2Fal 2:1, 6-14
Zab: 31:20, 21, 24
Injili: Mt 6:1-6, 16-18
Nukuu:
“Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha,
Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha
akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu,” 2Fal 2:9
“Akalitwaa
lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana,
Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha
akavuka,” 2Fal 2:14
“Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya
kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 6:1
“Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu
kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini
atakujazi,” Mt 6:17-18
TAFAKARI: “Baba yako aonaye
sirini atakujazi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo natulitafakari neno hili “Baba yako aonaye sirini
atakujazi.” Hatuna sababu ya kuwa na hofu tunapojisalimisha kwa Mungu bila
kujibakiza, na hasa pale tunapofunga kwa ajili ya kujitakatifuza, na tunapoomba
kwa ajili yetu na wengine. Hatuna chochote cha kumficha Mungu, wala
kujinyambulisha na kuwa kile tusicho. Mungu anatujua vizuri kuliko tujijuavyo
kwa sababu Yeye ndiye aliyetuumba, tena kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Naye
Mungu, yaani, Neno aliyemwilishwa na kukaa kwetu, Yoh 1:14, anatuambia, “Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope
basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi,” Lk 12:7. Hakiti tu kito chenye samani
mbele ya Mungu licha ya udogo wetu. Hivyo ni vyema tukaacha maigizo katika
maisha.
Somo letu
la leo linaelezea “maisha ya ukaribu.” Na kama ilivyo hada, linatupa ukaribu wa
Eliya na Elisha kama ilivyokuwa ukaribu Yesu Kristo na wanafunzi wake. Nabii
Eliya yupo wazi kwa Elisha, na kabla ya kuondoka kwake anamtaka Elisha aombe
chochote naye atatenda. “Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha,
Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha
akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu,” 2Fal 2:9.
Kwa upande wa Yesu, sharti la kupata
kile tuombacho yatupasa kukaa ndani ya Kristo, na kuachana na michanganyo katika imani. Naye Yesu anasema, “Ninyi mkikaa ndani
yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi
mtatendewa,”
Yoh 15:7. Yesu anaenda mbali zaidi na kusema, kama imani tunayao bila michanganyo tuombalo hata sasa tutalipata, “Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni,
nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu,” Yoh 16:24. Furaha ya kweli katika maisha na hasa
ya kiroho hukamilishwa na Kristo mwenyewe.
Uwezo wa mwanadamu wa
kujenga mawazo (taswira) ya kufikirika ni moja ya njia azitumiazo mwanadamu
kugundua vitu na hata kuviboresha vile vinavyomzunguka. Lakini ubaya wa mawazo
fikirika ni pale mwegemeo wake unapoelekea kwenye ubinafsi wa mtu husika. Hii
ni hatari kwa sababu uwezekano huo waweza kuwa hatari kwa mtu binafsi na hata watu
na mazingira yanayomzunguka. Jibu la Nabii Eliya kwa kile alichokiomba Elisha
kwamba “umeomba neno gumu,” 2Fal 2:10, linaonyesha mwegemeo huo wa ubinafsi.
Jibu hili halina tofauti na jibu la Yesu kwa kile walichokiomba (mmoja wao
aketi upande wa kuume wa Yesu na mwingine upande wa kushoto) wana wa Zebedayo,
“Hamjui
mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo
nibatizwao mimi?” Mk 10:38. Hata baada ya kujidhihirisha kwamba wapo tayari kubatizwa
ubatizo huo, Mt 10:39, bado Yesu anawataka wafikiri vizuri zaidi kwa sababu
hicho wakiombacho kinavigezo vyake. Naye Yesu anawaambia, “lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au
mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,”
Mk 10:40
Kuondoka kwa Nabii
Eliya kulikuwa kwa namna ya pekee sana. Nabii Eliya nachukuliwa na gala la
moto, na farasi wa moto. Na “walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea
gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda
mbinguni kwa upepo wa kisulisuli,” 2Fal 2:11. Moto ni ishara ya uwepo wa Mungu
na Utakatifu wake. “Pumzi zake huwasha makaa, Na miali ya moto hutoka kinywani
mwake,” Ayu 41:21. Moto licha ya kuwa ishara na uwepo wa Mungu, ni ishara ya
kutakatifuzwa, kufundishwa na hata onyo kutoka kwa Mungu. Na hili ndilo neno la
faraja kutoka kwa Mungu kupitia Nabii Isaya, “na mkono wa Bwana utajulikana,
uwaelekeao watumishi wake, naye atawaonea adui zake ghadhabu. Maana Bwana atakuja na moto, na magari
yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa
moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto,” Isa 66:14b-15
Namna hii ya
kuondoka Nabii Eliya kunafanana na kupaa kwake Bwana wetu Yesu Kristo Mbinguni
ingawa Yeye haikuwa kwa gari na farasi wa moto. Hata hivyo kitu cha kutazama
hapa ni ujumbe ule ulioachwa na namna ulivyopokelewa na wale walioachiwa ujumbe
husika. Kwa upande wa Elisha ilikuwa hivi; “Naye
Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda
farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua
vipande viwili,” 2Fal 2:12. Kuondoka kwa Eliya ni huzuni kubwa kwa Elisha. Ni
hali na ujumbe wa huzuni. Yesu alivyopaa
alituhaidi kutupatia Roho Mtakatifu, na kutotuacha mayatima kwani atatujia, Yoh
14:18. Na zaidi ya hilo, alituachia kazi ya kufanya, yaani, kuwafanya mataifa
yote kuwa wanafunzi wake kwa kuwahubiria habari njema na kuwabatiza, Mt
28:19-20.
Kanisa linaachiwa kazi
ya kufanya hadi mwisho wa nyakati. Huu ndio uwezo uliopewa Kanisa, yaani, kwa
kila aliyebatizwa na mwenye kuziishi
ahadi zake za ubatizo vyema. Hili ni sawa na vazi lile la Eliya lililomwangukia
Elisha, na kumwezesha kufanya aliyofanya mtanzulizi wake. Elisha “Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji,
akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika
huku na huku, Elisha akavuka,” 2Fal 2:14. Vazi na ishara aliyoifanya Elisha
ina mfanano
wa fimbo ya Musa aliyopewa na Mungu kwa kuzifanya ishara. Naye Mungu ananena
juu ya fimbo ile, “Nawe utatwaa
fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara,” Kut 4:17, ikiwa ni
pamoja na kuyagawa maji ya baharí, watapita kati ya bahari katika nchi kavu,14:16. Ndugu yangu, uwezo
aliokupa Mungu yaani karama na vipaji ulivyonavyo ndiyo ni sawa na fipo ile ya
Musa na vazi hili la Eliya ambao sasa ameachiwa Elisha. Leo kama wewe ni mzazi
unayejali na kuwajibika, urithi mkubwa kwa mwanao ni elimu. Mpe mwanao ufahamu
huo kwa sababu, "Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima;
Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu,” Mit 9:9. Hata pamoja na
elimu hiyo kuwa muhimu, usisahu pia kumjengea mwanao hofu ya Mungu kwa sababu,
“Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu,” Mit 9:10
Njili
yetu leo inatupa kinagaubaga namna ya kufanya na inavyompendeza Mungu. Na hii
ndiyo maana halisi ya kumacha Bwana na kumjua, Mit 9:10. Leo tulio wengi
tunapowasaidia wahitaji na hasa; wazee, mayatima na wajane, tunatenda tendo
hili kwanza kwa kuwakusanya watu ili waone tunachokitoa. Pili, tuna viita
vyombo vya habari ili wautangazie ulimwengu jinsi tunavyotoa na tulivyo wema.
Tufanyapo tendo hili kwa mfumo na mtazamo huu twajisikia raha nafsini mwetu, na
kujipongeza kwa kufanya kazi nzuri ya kijamii na hata kichunguji. Je, kuwa Baba
au Mama mwema na mkarimu na karibu kwa familia yako unaitaji kuvaa au kubeba
bango lenye maandishi kama haya; “Baba mwema na mkarimu,” ili familia ijue
ukweli huo? Nafikiri hapa kwa kiasi kikubwa tunakosea sana tunavyofanya hivyo.
Yesu anatoa onyo na angalizo kwa kusema, “Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya
kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 6:1. Tendo kama
hili halina dhawabu yo yote machoni mwa Mungu.
Ni
kweli watu watatusifia na kutuandika kwenye magazetu yao, ambayo kesho yake
magazeti hayo hayo yaliyopambwa jana kwa utoaji wetu yatafungia vitumbua na
historia yote inaishia hapo. Je, imani na matumaini yako ipo kwa watu? “Bwana asema hivi, “Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu,
Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5. Bali, “Amebarikiwa
mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa
kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari
ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa
mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda,” Yer 17:7-8. Tunapowategemea wanadamu hasa
kwa matendo yetu ili yawapendezeshe hatuna tofauti na Mafarisayo nyakati zile
za Yesu.
Leo
Yesu anatupeleza mbali zaidi na hasa matendo yale tuyafanyayo ilikwa ni
kumrudishia Mungu sifa na shukrani, hatupaswi kuyafanya kama maonyesho mbele za
watu ili watuone. Jamii yetu leo kwa kiasi kikubwa imetawaliwa na maigizo na
habar iza kufikirika tu kila kukicha. Yesu anatutaka leo tuyaone matendo yetu
ya huruma tuyafanyayo kwa watu ni sehemu ya sadaka, sala, na kufunga.
Anayetukirimia neema na baraka katika matendo hayo ya kiroho ni Mungu mwenyewe.
Hakuna maana yo yote ya kuomba huruma kwa watu mara tuyafanyapo mambo haya. “Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue
ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka
yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi,” Mt 6:3b-4. Ni kweli
utoapo kwa siri, ndivyo hivyo Baba yako aonaye sirini atakujazi. Ila tusimwibie
Mungu au kumdanganya Mungu kwa kumpa kile kisicho halali. Mfano mdogo ni huu;
ukiangalia shilingi hamsini hadi mia mbili huwezi kukuta maneno haya, “Fedha
halali kwa malipo ya shilingi, mia tano, elfu moja au elfu kumi,” ambayo yapo
pia kwenye noti ya shilingi elfu mbili, na elfu tano. Je, unapotoa sadaka yako
jumapili shilingi hamsini, mia moja, au mia mbili, unatoa fedha halali
ukilinganisha kwa kipato chako cha mwezi? Kama kuna uwiyano hautakuwa umetenda
kosa, na hautakuwa umejifungia baraka na neema za Mungu. Kama unacho kingi na
unasema kwa matendo yako unacho kidogo, Mungu atakipunguza kadiri ya matendo
yako. “Wakamkasirisha kwa matendo yao; tauni ikawashambulia,” Zab 106:29. Mungu
aweza kukufanya chochote kadiri ya uchoyo wako.
Na
tusalipo yatupasa kuunganika na Mungu katika undani wetu na siyo kupayukapayuka
ili watu wajue tunasali. “Bali wewe
usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako,
usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi,”
Mt 6:6. Hatumpendezeshi yeyote tunaposali, bali Mungu ambaye ni yote katika
yote, na tunauonja ukaribu wetu na Mungu, kwa njia ya kumshukuru, kumtukuza, kumwomba
na kumsifu.
Na
mwisho tunapofanya tendo la kufunga kuwe na malengo. Licha ya kuwa ni tendo la
kiroho, kufungu ni tendo la kiafya pia. Je, ninavyojinyima nafanya hivyo kwa
sababu gani hasa? Na kwa kufunga kwangu kumelenga maisha yangu ya kiroho? Je, ninalenga
hasa utakaso ndani mwangu, au nalifanya tendo hilo kwa vile imekuwa mazoe kila
kipindi fulani cha mwaka watu hufanya hivyo nami nafanya? Pili, tendo hilo
mwisho wa siku linawalenga watu gani kama shukrani kwa Mungu? Haya ni maswali
muhimu sana ya kujiuliza kabla ya kufanya zoezi hili la kiroho, mfungo. Maswali
hayo yakipata majibu yake fanya hivi, “wewe
ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye
sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi,” Mt 6:17-18. Kujipaka mafuta ni kutokuwavuta watu kujua
unachokifanya kwa sababu tendo hili ni la kiroho zaidi.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bali
wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili
usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako
aonaye sirini atakujazi,” Mt 6:17-18
Tusali:-Ee Yesu, ujuaye
undani wetu, tuongoze katika kweli na haki ili tuwe kweli tunda la upendo wako.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario