JUMANNE WIKI YA 11 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 21:17-29
Zab: 51:3-4, 5-6a, 11, 16
Injili: Mt 5:43-48
Nukuu:
“Neno
la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka,
ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika
shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki,” 1Fal
21:17-18
“Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua,
ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa
walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako,”
1Fal 21:19
“Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani?
Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?” Mt 5:46
“Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
TAFAKARI: “Maana
mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Basi ninyi mtakuwa
wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”
Wapendwa wana wa Mungu, pasipo shaka yoyote ile, mwisho wa maisha yetu
na mbele ya kiti kile cha hukumu tutahukumiwa katika mizania ya upendo. Bila
shaka msoma mashtaka yetu, yaani, Yesu Kristo akiwa mbele ya Mungu Baba
atakuuliza wewe, na mimi kila mmoja kwa nafasi yake hivi; “Je, ulipenda kwa
kiasi gani? Nikiwa kielelezo chako nilikupenda upeo, Yoh 13:1, na kuyatoa maisha
yangu na kufa kifo cha aibu kwa ajili yako. Swali la pili nafikiri litatoka kwa
Mungu Baba. Nalo ni hili; Mwanangu, niambie umetumia vipi vipaji nilivyokupa?
Kumbe kujibu vizuri maswali haya mbele ya safari yakupasa wewe na mimi kuishi
vyema katika hofu ya Mungu, na wale wote wanaotuzunguka bila kujali hali zao na
historia zao.
Somo letu la leo, linafafanua vizuri namna tupasavyo kuishi, yaani
kuwa na hofu ya Mungu, na mahusiano yetu na jirani. Jana tuliona kile
kilichojiri kwa Mfalme Ahabu na Mkewe Yezebeli. Kwa uovu wao na kutokuisimamia
haki wanakuwa sababu ya kifo cha Nabothi mtu mwenye haki. Mungu wetu yu hai na
huona yote tuyafanyayo. Mungu huchukizwa sana pale tunapoipoteza nuru yake
ndani yetu kwa kujipenda zaidi. Na kwa sababu hiyo, Mungu anavunja ukimya ili
haki itendeke. Na “Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu
mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la
Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki,” 1Fal 21:17-18. Nabii Eliya Mtishbi anakuwa mjumbe halali wa
ujumbe maalum wa Mungu. Hii ndiyo maana halisi ya kuwa Nabii. Mungu hutumia
watu wake aliowateua kwa kazi maalum ili ujumbe wake uwafikie walengwa, na hawa
ndio manabii kama Nabii Eliya. Ujumbe wa Mungu kwa mfalme Ahabu kupitia Nabii
wake Eliya wasema hivi; “Ukamwambie,
ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema,
Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa
watairamba na damu yako, naam, damu yako,” 1Fal 21:19. Mungu anatangaza kiama
kwa mfalme Ahabu kwa uovu wake. Ni ujumbe kwetu pia kuyatumia vizuri mamlaka ya
Mungu tuliyopewa kupitia watu wake kwa njia halali ya kupiga kura, yaani,
demokrasia huru na ya haki.
Mungu
huitangaza na hata kuionyesha wazi hasira yake pale tunapokengeuka na kukataa
wazi upendo wake. Na hii ndiyo maana ya dhambi, yaani, kuukataa upendo Mungu
tukiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu kile tukitendacho. Kwa kuukataa upendo huu
wa Mungu (mfalme Ahabu), Mungu kwa kupitia Nabii Eliya anasema, “Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami
nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa
katika Israeli,” 1Fal 21:21. Ndugu yangu, Mungu amekuumba kwa malengo, yaani,
umjue, umpende, umtumikie, na mwisho urudi
kwake. Kwa kutokutambua wajibu huu na kutenda kinyume chake, Mungu uchukizwa
sana, na huweza pia kuzidisha adhabu yake pale tunapomkasirisha kwa kutokuwa
kusudi la kuumbwa kwetu. Hivyo katika ukweli huu Mungu anasema zaidi kuhusu
Ahabu, “Kisha nitaifanya nyumba yako
iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa
Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha
Israeli,” 1Fal 21:22
Wapendwa katika Kristo,
Mungu uchukizwa zaidi na yule asababishaye makwazo na hata kudongokwa kwa mtu
katika hali ya dhambi. Na hii ndiyo adhabu ya mke wa mfalme Ahabu aliye gushi
nyaraka za mfalme na kusababisha mauti ya Nabothi mtu mwanye haki. Naye Mungu
anasema kupitia kinywa cha Nabii Eliya juu ya Yezebeli mke wa mfalme, “Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli,” 1Fal
21:23. Dhambi hii ya makwazo Yesu anaisema kwa msisitizo mkubwa, kwamba, “Na
ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe
jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini,” Mk 9:42. Ni wito kwetu pia kutokuwa vikwazo kwa wengine.
Adhabu yake ni kubwa. Katika hili, yeyote yule kwa njia moja au nyingine, kwa
kujua na kushiriki kosa la wengine au mwingine hatokuwa salama. Kama ni kichapo
ni kile kile! Naye Mungu anasema, “Mtu wa
nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa
angani watamla,” IFal 21:24. Unapoujua ukweli
wa jambo na kukaa kimya bila kufanya chochote katika kweli na haki, washiriki
uovu ule ule. Tendo hili ni sawa kabisa na yule aliyejua na kushiriki moja kwa
moja katika uovu ule ule.
Wapendwa wana wa Mungu,
haki ya Mungu huyafanya tena upya agano jipya na watu wake. Mungu husahau
historia ya mabaya yetu na kutupa tena nafasi ya kuwa wapya katika yote. Naye
anasema, “Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu
machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea,” 1Fal 21:25. Mimi na wewe hulivunja agano na Mungu kwa kuasi
kwetu na kwenda kinyume na upendo wa Mungu. Na kumwasi Mungu ni kutokuwa na
nafasi naye. Na ndiyo ilivyokuwa kwa watu wa utawala ule wa mfalme Ahabu. Mungu
“akachukiza mno, kwa kuzifuata
sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana
wa Israeli,” 1Fal 21:26. Unapokosa nafasi ya Mungu ndani ya moyo wako, nafasi
hiyo hupata mpangaji mwingine ambaye huyabomoa maisha yako.
Tunapomkosea
Mungu ni vyema kukajirudi na kufanya toba ya kweli. Hivyo ndivyo Mfalme Ahabu
alivyoupokea ujumbe ule wa Mungu kupitia mtumishi wake Nabii Eliya na kufanya
toba ya kweli. “Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake,
akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa
upole,” 1Fal 21:27. Neema na Huruma ya Mungu
kwa mfanya toba ya kweli na majuto ni kubwa kuliko dhambi zake. Naye Mungu
anasema, “kwa sababu amejidhili
mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake,” 1Fal 21:29a.
Ndugu
yangu, maisha ya ufufuko ni ushindi dhidi ya uovu. Na upendo ndio kielelezo
chake. Naye Yesu katika upendo wa kweli anasema, “wapendeni
adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili
mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake
waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,” Mt 5:44-45. Kumbe
kupenda siyo tu kwa wale wanaotupenda. Yatupasa kufanya zaidi na kupenda zaidi.
Tumwone Kristo kwa kila mmoja bila kujali historia yake iwe nzuri au mbaya.
Kristo anatupa nafasi tena na tena ya kuwa wapya. Wakati fulani Mtume Petro
alitaka kujua kipimo cha kusamehe, naye Yesu akamjibu, “sikuambii hata mara
saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22. Kwa maneno mengine, ‘mpe
uliyechukuzwa nawe muda wa kutosha.’
Upendo
wa Mkristo anayeishi maisha ya ufufuko hana kipimo cha kuutoa upendo wake zaidi
ya kupenda bila kipimo akiitafakari thamani ya kuokolewa kwake kwa sadaka ile
ya mwenye haki pale Msalabani, yaani, Yesu Kristo. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu
kwetu; “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani?
Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?” Mt 5:46. Upendo wa kweli na maisha mapya ya ufufuko
hayafungamanishwi na uhasili wetu wa kuzaliwa, bali kila siku ni vita ya
kuushinda ubinadamu wetu na kuelekea nuru ile ya milele, yaani maisha ya
milele. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Tena
mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa,
je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:47. Kuushinda ubinadamu wetu ndiyo dira na
kuishi maisha ya malengo hapa duniani.
Tunaishi kwa malengo, na malengo yetu ni kuufikia uzima ule aliyotuhaidia Yesu
Kristo, “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni
haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa
milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:40. Kusudi la kila mmoja wetu ni kuwa
kama aliyetuumba, yaani, kuupata ule ukamilifu. “Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt
5:48. Ukamilifu huu, ambao ndio Utakatifu, ndicho kigezo cha kuishi maisha hayo
ya umilele na Baba yetu wa Mbinguni huko Mbinguni.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Ikawa,
Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini
mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole,” 1Fal 21:27
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
tuhurumie kwa kuwa tumetenda dhambi na tujalie neema na huruma yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario