JUMAMOSI WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Tim 4:1-8
Zab: 71:8-9, 14-15ab, 16-17, 22
Injili: Mk 12:38-44
Nukuu:
“lihubiri neno,
uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa
uvumilivu wote na mafundisho,” 2Tim 4:2
“Maana
utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia
zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya
utafiti; nao watajiepusha
wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo,” 2Tim 4:3-4
“Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili,
kiasi cha nusu pesa,” Mk 12:42
“Akawaita
wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi
kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali
iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,
ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:43-44
TAFAKARI: “Maana
utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima.”
Wapendwa wana wa Mungu, baadhi ya sehemu ya Kanisa la Magharibu
limekumbwa ukavu mkubwa wa Imani. Baadhi ya maeneo hayo ni vigumu wakuwakuta
vijana na watu wa umri wa kati makanisani. Na kama utawakuta basi elewa wapo tu
kwa matukio au maadhimisho ya masakramenti ambayo kwa kiasi kikubwa hufanywa tu kutimiza utaratibu fulani, na kwa kuwa
imekuwa mtindo fulani wa maisha. Leo maeneo haya utawakuta vikongwe tu
makanisani.
Pamoja na sababu nyingi zitolewazo kwa mujibu wa historia ya Kanisa
hili la Magharibu, hii ni dhahiri; kutokuwepo kwa Katekesi ya kina. Kwa kiasi kikubwa
Kanisa lilijisahau. Watu/Waamini walilishwa mafundisho ya Kanisa bila
kuyacheua. Mafundisho ya mtindo huu yalimzunguka mtu kila kona. Mtu alikutana
na mafundisho ya mtino huo Kanisani, na kwenye mfumo mzima wa kijamii na siasa.
Matokeo yake ni kwamba mtu alijiona kama mfungwa katika mtindo fulani wa maisha
uliokuwa vigumu kuuhoji na kujinasua. Kwa mtindo huu, uasi wa dini na imani
uliza kujitokeza taratibu, kwani binadamu anapobanwa sana utafuta pa kutokea.
Kulianza pia taratibu kujengeka chuki kwa baadhi ya watu juu ya Kanisa. Kanisa
lilionekana kuuchukua kabisa uhuru wa mtu.
Ni vyema mtu ajue vizuri kile akiaminicho, na siyo kukimeza tu bila
kucheua. Usipo kijua vizuri kile ukiaminicho ni vigumu pia kukitetea au kuwa
sehemu ya maisha yako. Mtume Paulo anampa angalizo Timotheo, ambalo leo
tungelihusiha na utoaji wa Katekesi ya kina. Naye anasema, “lihubiri neno, uwe
tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa
uvumilivu wote na mafundisho,” 2Tim 4:2. Tusipo jali leo kuwapa waamini
katekesi ya kina juu ya imani ya kweli, muda si mrefu nasi tutakumbana na hiki
kinachoendelea katika Kanisa la Magharibi. “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho
yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi,
kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao
watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo,” 2Tim
4:3-4. Sambamba na kutoa katekesi ya kina, tuliopewa dhamana hiyo na Kanisa
yatupasa kujifunza kwa kina juu ya ‘teología ya mawasiliano.’ Pasipo
mawasiliano katika uinjilishaji vyote uvurugika. Ni sawa na kuujenga mnara wa
babeli. Waamini wanapaswa kushirikishwa vizuri maswala ya uinjilishaji kadiri
ya nafasi zao. Makleri hawawezi kufanya mambo yote. Tujifunze historia ya
Kanisa la mwanzo na changamoto zake. “Wale Thenashara wakawaita jamii ya
wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu
mezani,” Mdo 6:2. Hii ni faida ya kujifunza Teología ya mawasiliano. Kielelezo
cha Teología hii ni uwepo wa Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja nafasi tatu.
Teología hii ya
mawasiliano katika utekelezaji wa katekesi ya kina inatutaka tuwe na kiasi, na
kila mmoja katika familia ya wana wa Mungu awajibike kadiri ya nafasi yake.
Hivyo Mtume Paulo anamwambia Timotheo, mimi na wewe leo kwamba, “Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote,
vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako,” 2Tim
4:5. Mtume Paulo analiona hili na umuhimu wake kwa sababu umri wake unakwenda,
na nguvu pia zinapungua. Hawezi tena kuyanya kwa nguvu kama zamani, na kufanya
yote mwenyewe. “Kwa
maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika,” 2Tim 4:6.
Haya ni mang’amuzi binafsi kutoka kwa Mtume Paulo. Mang’amuzi katika maisha ni
mwalimu mzuri wa kutusaidia kuzisoma alama za nyakati. Kanisa katika historia
yake, limepata mang’amuzi makubwa sana. Ni vyema tukaitumia elimu hii, kuzisoma
alama za nyakati zetu.
Hii ndiyo vita ya
kiimani aisemayo Mtume Paulo kwamba, “Nimevipiga
vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7. Kila
mmoja kadiri ya nafasi yake katika Kanisa lazima ailinde imani yake licha ya
changamoto tunazokumbana nazo kila siku. Leo tunaishi katika ulimwengu wa umimi
na vitu. Ni vigumu kwa mtazamo huo kuwa na Teología ya mawasiliano kama kila
mtu atakuwa amejifungia katika kiota chake. Kumbe leo kwa namna ya pekee
twahitaji kuziimarisha jumaiya zetu ndogondogo za Kikristo. Hapa ndipo
tunapoweza kutoa katekesi ya kina na kuumega mkate kwa kina. Mtindo huu wa
maisha ya Jumuiya Ndogondogo za Wakristo, ndiyo ulivyokuwa kwa Kanisa lile la
mwanzo. Ni mahali hapa tunapoambiwa
kwamba, “wakawa wakidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika, na
katika kuumega mkate, na katika kusali,” Mdo 2:42. Je, waijua Jumuiya yako?
Kama waijua huwa unajumuika nao katika ushirika, kuumega mkate, na katika
kusali?
Wapendwa wana wa Mungu,
ni katika kutimiza wajibu huu muhimu juu ya imani yetu ndipo tunapoweza kusema
kama Mtume Paulo, kwamba, “baada ya hayo
nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile;
wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake,” 2Tim 4:8.
Umoja na mshikamano katika Kanisa, yaani, wabatizwa wote, ni muhimu kufanikisha
hazma hii ya uinjilishaji wa kina. Kwa namna hiyo, sote ni ndugu na
tumehesabiwa haki na kuwa wana na warithi wa Mungu kwa sadaka ile ya Yesu pale
Msalabani. Kwa kutambua upendeleo huo yatupasa kuwa waangalifu na matendo yale
yote yatakayo dhuru afya ya kuwa wana wa Mungu.
Katika Injili ya leo,
Yesu katika mafundisho yake anatupa maangalizo hayo na kusema, “Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa
mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni,” Mk 12:38. Hakuna sababu ya kupoteza
muda mwingi kwa kufanya maigizo badala ya kuwajibika kila mmoja kadiri ya
nafasi yake, na wito wake. Huu ndio ule unafiki alioukemea Yesu tuisomapo sura
yote ya 23 ya Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo. Maigizo haya
yasiyo na tija ni ya wale ambao hupenda “kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya
mbele katika karamu; ambao hula
nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo
kubwa,” Mk 12:39-40. Hawa ni wale wanasisasa wa wetu wa leo ambao hupenda
kucheza na akili za watu kwa sababu wanaujua udhaifu na mapungufu ya wananchi
wao. Wakiwa na masikini hujifanya kuwa nao bega kwa bega na kuwahaidia mbingu
isiyofikika. Wakiwa na matajiri hujifanya kuwa nao karibu wakiwahaidi kulinda
maslahi yao, na wakiwa Makanisani na Misikitini hujipambanua kupiga vita dhidi
ya ufisadi na uovu wa kila aina kumbe ndani mwao wasukumwa na roho hiyo hiyo ya
kufisidi.
Ni
vyema kila mmoja wetu akawa kile alicho na kujitoa bila kujibakiza. Na huu ni
ule mfano wa mwanamke mjane na masikini. Mwanamke huyu alijitoa bila
kujibakiza. “Akaja
mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa,” Mk
12:42. Ni vyema kila wakati maneno yetu yaseme matendo yetu, na matendo yetu
yaseme maneno yetu. Hili lisipoonekana
kwa kiongozi yeyote yule humuondolea ile nguvu ya kimaadili. Mwanamke huyu
mjane na masikini kwa nafasi yake anaonyesha nguvu yake ya kimaadili. Kwa
msisitizo juu ya hili Yesu “Akawaita
wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi
kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali
iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,
ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:43-44. Je, ndugu yangu, kadiri ya nafasi
yako na wito wako, umetia yote hapo ulipo; katika imani yako, uinjilishaji
wako, na jamii inayokuzunguka?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Jihadharini na
waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na
kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa
unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa,” Mk 12:38-40
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
tufanye daima vyombo vya Amani yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario