jueves, 23 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 12 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 12 YA MWAKA-C
Somo: Omb 2:2, 10-14, 18-19
Zab: 74:1-2, 3-5a, 5b-7, 20-21
Injili: Mt 8:5-17
Nukuu:
Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi,” Omb 2:10 

Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa,” Omb 2:14 

 “Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7

 “Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10

TAFAKARI: “Nitakuja niwaponye.”

Wapendwa wana wa Mungu, Injili ya leo ni uthibitisho na mwendelezo wa Mungu wetu aliye hai na mweza wa vyote. Kumbe hatuna sababu ya kubaki na majonzi yoyote yale tunapokutana na sintofahamu katika maisha kama wanavyokabiliana na hali hiyo wana wa Israeli. Ndani na katika Kristo hatupaswi kuishi katika ukiwa, hata kama hatuna jibu la moja kwa moja, ‘tumaini katika maisha’ liwe jibu la sintofahamu yako. Wana wa Israeli wanaliweka tumaini kwa lao kwa Mungu kwa njia ya kufanya toba kweli na majuto. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi,” Omb 2:10. Toba ya kweli na majuto huwa jibu na matumaini ya kweli pale tunapoona kweli kwa kupotoka kwetu bila kutafuta sababu zozote zile za utetezi au kuhalalisha dondoko letu.

Hata hivyo, nyakati kama hizi katika maisha tunahitaji manabii wa kweli, na wasioyumbishwa na mivumo yoyote ile katika jamii. Tunahitaji watu wa kuuona ukweli kama ulivyo hata kama utawagharibu maisha yao. Leo na hasa katika jamii yetu ya Tanzania, tunahitaji nabii wa kweli ‘wa sauti ya wasio na sauti’ ambao ndio wengi. Ni katika mazingira kama haya ndipo ‘tunapoliona Kanisa la Kristo’ aliye hai na aliyekufa kwa ajili ya wewe na mimi ili tuwe huru na hai. Na hii ndiyo maana ya maneno haya tuyasomayo katika somo letu la leo, kwamba; Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa,” Omb 2:14. Kanisa ambalo ndilo Mwili wa Kristo na Sakramenti ya Wokovu wetu, linapoufumbia macho uovu wa namna yoyote ile kwa sababu zozote zile, historia itakuwa hakimu wa kweli na haki kwa wakati wake.

 Hivyo kwa mantiki hii, Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu, Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu,” Omb 2:19. Kanisa, yaani, Mwili wa Kristo, na kila mbatizwa kama sehemu ya mwili huo, lisipo simama kama ‘sauti ya wasio na sauti’ katika kweli na haki, litakuwa limekwishapoteza jukumu msingi katika safari nzima ya ‘kuumba ulimwengu,’ ‘kuukomboa ulimwengu,’ na ‘kuutakasa ulimwengu.’ Kanisa katika maana ya wabatizwa wote, ni viungo shirikishi katika uumbaji wa pili wa Mungu, ambao mimi na wewe twaushiriki kadiri ya vipaji vyetu, wito wetu, na nafasi zetu katika jamii inayotuzunguka.

Wapendwa katika Kristo, tukiirejea Injili ya leo, Mungu hutujibu mara tunapomwelekea bila shaka yoyote. Imani ndiyo msingi wa yote tuyaombayo kwa Mungu. Tunapomwelekea Kristo katika mahangaiko yetu, na kuwa imara katika imani, jibu lake ni moja tu.Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7, na kwa maana pana ni kwamba, ‘nitakuja niwaponye.’ Tunakosa neema hii pale tunapoanza kubabaika katika imani. Mara nyingi twapenda kupata majibu mepesi ya haraka kwa maswali magumu kwa kile kinachotusumbua bila la kujua hathari zake, na hasa hatma ya mahangaiko yetu. Hatma ya mahangaiko yetu ni uponyaji wa kweli. Tunaposukumwa na majibu tu mepesi ya yale yanayotusumbua, tunaishia kwanye ufahamu wa haraka na usio na uweledi wa kiimani. Hapa ndipo Wakristo wengi hudondoka. Rejea ‘kikombe cha Babu wa Loliondo.’ Tupo kati yetu tunaoamini kwanza majibu ya waganga wa kienyeji kabla ya kupeleka kesi hiyo mbele ya ufahamu wetu wa kibinadamu, yaani tafiti za kisayansi, na mwisho tukikosa jibu, kwa hakimu mwenye haki na mamlaka yote, yaani, Yesu Kristo, ambaye ndiye tumaini letu. Pamoja na utayari wa yule akida juu ya Imani aliyokuwa nayo kuhusu Yesu, haoni sababu ya Yesu kufanya safari na kuleta uponyaji huo ili hali uzima upo ndani na katika Kristo. Hivyo anaonyesha imani yake isiyo na shaka kwa Yesu na kusema, “Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona,” Mt 8:8. Ndugu yangu, hiki ni kikomo cha hali ya juu kwa kile tukiaminicho.

Kwa upande mwingine, Yesu alifumbii jambo hili macho bila kulisemelea. Hapa ndipo mahali Yesu anapotuonyesha nini maana ya Imani ya kweli. Pamoja na mamlaka aliyokuwa nayo yule Akida, alitambua mamlaka aliyokuwa nayo Kristo Yesu. Kujishusha kwa Akida huyu ndipo kunapo muhesabia haki. Hivyo Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10. Je, ni wangapi kati yetu tulio tayari kuuvua ubwana wetu na kuuvaa utwana?

Ndugu yangu, katika Imani ya kweli ndipo penye uponyaji wa kweli. Uponyaji wa kweli ndani yetu tunatembea nao ila hatujua ni wapi pa kushika. Jambo hili linajidhihirisha wazi kwa maneno ya Yesu mwenyewe. Naye anamwambia yule Akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini,” Mt 8:13. Ndugu yangu, bila shaka unafanya maombi kwa nia mbalimbali. Leo ngoja nikumegee siri ya kufanikiwa katika maombi yako. Kwanza, kuwa na imani kwa kile unachokiomba kana kwamba umeshakipata tayari. Pili, kila neno ulitamkalo kwa imani hiyo, nena maneno hayo hivi; “nani nasimama katika neno hili nililolitamka bila shaka.” Hapa ndipo Mungu ulitimiza lile tuliombalo na ulitamkalo kadiri tulivyoliamini.

Kristo mara zote anatutakia uhai, tena uhai wa kweli. Ni kwa namna hii,ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu,” Mt 8:17. Yesu anamponya mama mkwe wa Petro na mama huyu anawahudumia. Kristo mara zote anatwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu, na madhaifu yetu. Ndugu yangu, magonjwa yako wayapeleka wapi? Achana na ‘Kalimanzila!’

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini,” Mt 8:13b

Tusali:- Ee Yesu, nakuamini. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario