miércoles, 15 de junio de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 11 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 11 YA MWAKA-C
Somo: YbS 48:1-15
Zab: 97:1-2, 3-4, 5-6, 7
Injili: Mt 6:7-15
Nukuu:
“Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu yeyote,” YbS 48:12b

 “Lakini kwa ajili ya hayo yote watu hawakutubu wala hawakuziacha dhambi zao, hata walipochukuliwa mateka kutoka nchi yao, wakatawanyika juu ya uso wa dunia yote,” YbS 48:15

 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi,” Mt 6:14

Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mt 6:15 

TAFAKARI: Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, kusamehe hakumaanishi kusahau ulichotendewa, bali ukumbukapo ulichotendewa badala ya kubaki katika hali ya uchungu, mateso na majonzi, unajazwa furaha ndani ya moyo wako kwa sababu unaonja furaha ya Utukufu ule alioupata Yesu Kristo kupitia kifo kile cha Msalaba. Kusamehe kweli ni kutambua kweli thamani ya ushindi wa msalaba dhidi ya uovu. Na ndiyo maana yakupasa kujua, ‘hakuna utukufu pasipo msalaba.’ Na niutazamapo Msalaba Mtakatifu unikumbushe Mti ule wa ajabu na wenye bahati ambao wokovu wangu ulitundikwa juu yake. Mahangaiko yetu katika maisha ndani na katika Kristo hupata bahati kama ya mti huu kwa sababu mwisho wa mateso hayo upo wokovu. Kumbe siyo vyema kumlaumu Mungu na kukasirika juu ya Yesu pale ninapopatwa mateso pasipo hatia yoyote. Je, Kristo Yesu alikuwa na hatia alipoukabili msalaba zaidi ya kuukubali ili tuwe huru kutoka kifungo cha dhambi?

Hata pamoja na hali hiyo ya mateso makubwa, Yesu Kristo hakuacha kutoa msamaha. Akiwa amewambwa Msalabani aliweza kutamka maneno haya pasipo shaka yoyote,  “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo,” Lk 23:34a. Je, ninao ujasiri huo wa kutamka maneno hayo hata pale ninapotambua wazi kuwa nimeonewa? Hakika ni changamoto kubwa sana leo, hasa kwenye ulimwengu huu wa ‘haki sawa.’ Lakini pamoja na wigo huu mpana wa ‘haki sawa’ Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mt 6:15. Je, kwa maendeleo ya leo twaweza sema alichokisema Yesu kimepitwa na wakati? La hasha! Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho,” Yoh 12:48. Maandiko Matakatifu yana uzima nyakati zote, na ya hai muda wate.

Yapo mambo mawili tunayoweza kujifunza katika Injili ya leo. Jambo la kwanza ni kuhusu Sala. Na jambo la pili ni namna ya kusala. Sala anayo tufundisha Bwana wetu Yesu Kristo leo, na ili kuyapata yote tuyaombayo kuna sharti moja lazima tulitimize, yaani, makosa yetu husamehewa na Mungu kwa mizania ile ile tuitumiayo kuwasamehe wale waliotukosea.Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu,” Mt 6:12. Pili kuzama katika sala ni kusali katika utulivu. Hivyo Yesu anasema,Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi,” Mt 6:7. Je, sala hii ya Baba Yetu ina maana yoyote kwa wabebao mzigo wa visasa, chuki, na kutokusamehe?

Wapendwa katika Kristo, mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mt 6:14-15. Je, kunafaidha gani kutembea na gunia hili la chuki, visasi, na kutokusamehe? Kwa nini hutaki kumsamehe huyo uliyembeba muda wote katika kichwa chako, moyo wako, na maisha yako yote? Kwa nini hutaki kujiweka huru? Yawezekana aliyekutenda hilo usilotaka kusamehe hana habari na ugomvi wako nawe. Yeye yupo huru ila wewe bado upo kwenye maabusu hiyo ya kutokusamehe bila kujua tarehe rasmi ya kusikilizwa kesi yako.

Pamoja na mkwano huo tunaojijengea wenyewe, Jambo la pili tunalofundishwa leo ni namna ya kusali. Yesu anatufundisha namna ya kusali na mapaswa yake. Anatoa angalizo katika sala. Sala ya kweli na yenye utulivu ni kule kusali bila kupayuka. Ni sala ya kumsikiliza mtu wa ndani. Ni kujisikiliza na kusikiliza matakwa ya Mungu. Ni utulivu wa ndani ambapo katika utulivu huu tunakutana na Mungu. Hivyo kuabudu kuliko kwa kweli ni kuabudu katika usahihi, uhalisi, tafakuri, na matendo hai. Kama haya mambo hayafanyiki, kuabudu kweni ni kupayuka payuka. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba,” Mt 6:7-8

Sala hii ya Baba yetu ni ufupisho kwa yale yote tunayotakiwa kufanya kila dakika tunapopumua. Mahitaji yetu, utulivu wetu, matakwa yetu, uhusiano wetu na wengine, mahangaiko na vishawishi vyetu vyote hupata majibu katika sala hii. Je, tunatafakari hayo tusalipo sala hii ya baba yetu? Mfano swala la MSAMAHA. Kusamehe ni amri na sio ombi. Yatupasa Kusamehe na hiki kicho kipimo cha sisi kusamehewa. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi,” Mt 6:14. Ndugu yangu, kusamehe siyo kusahau kama nilivyo kwisha kusema. Ukweli ni kwamba hatuwezi kufuta aliyofanyiwa Yesu na kufa kifo kile cha aibu msalabani. Ila tunasema msalaba ni ushindi tunapotazama Utukufu wa Msalaba. ‘Huu ndio ule uti wa msalaba, ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake.’ Maneno haya ya ushindi na matumaini husemwa siku ile ya Ijumaa Kuu unapofunuliwa msalaba uliofunikwa.

Unapomsamehe mtu mbele yako upo Utukufu. Tunapokumbuka uchungu tuliofanyiwa tunapata faraja kwani katika hilo tumeshinda kwa kusamehe. Ni faraja ya kweli na tumaini jipya. Tusibaki kwenye uchungu na mateso ila tukumbatie Utukufu ule wa milele. Hili ndilo fumbo la kusamehe na Utukufu unaopatikana katika tendo hilo. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mt 6:15. Na kwa kufanya hivyo ndugu yangu, yaani kutokusamehe kwako, mbele huko ya safari hakuna Utukufu wala Mbingu-Uzima wa milele.

Kudumu katika mambo haya mawili yaani, sala kwa ujumla wake, na namna ya kusali, utujengea urafiki wa karibu na Mungu pasipo woga. Tunakuwa tayari kumwendea na kuzungumza naye siyo nyakati zile tunazomwitaji tu, yaani, nyakati za shida, bali nyakati zote kama rafiki mwema na wakaribu. Ni kutambua kwa kina kwamba wakuogopwa licha ya kwamba ni rafiki yetu, ni Mungu tu. Binadamu pamoja na ukuu na mamlaka yake si wa kuogopwa bali kuheshimiwa kwa kile anachokisimamia katika kweli na haki. Hivyo katika kweli na haki, mtawala au kiongozi anapaswa kuulizwa na kufikika kwa sababu nguvu alizokuwa nazo kapewa na umma anaouongoza. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Nabii Elisha kwamba, “Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu yeyote,” YbS 48:12b. Kwenye kuisema kweli na kuitetea haki pale ambapo hapana fursa ya kufanya hivyo, huleta mateso na sintofahamu nyingi. Hata hivyo kukaa kimya siyo jibu.

Kweli na haki huwezwa kudhoofishwa lakini haiangamizwi bali ujikusanya na kuwa na nguvu zaidi katika umilele wake. Hii ni kwa sababu kweli na haki ni asili ya Mungu kwenye umilele.  Hii ndiyo iliyokuwa tabia ya Nabii Elisha mbele ya kweli na haki, yaani “Hakukutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini mwili wake ulitoa unabii,” YbS 48:13. Hapa ndipo pale Yesu anaposema, Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28. Kilicho haki hudumu katika umilele wake hata kama kitahujumiwa kwa wakati kwa kukinyamazisha.

Masimulizi ya maisha ya Nabii Elisha yanathibitisha ukweli huu kwamba, “Kama alivyofanya miujiza katika maisha yake, kadhalika na katika mauti yake kazi zake zikawa za ajabu,” YbS 48:14. Ni nani basi mwenye uwezi wa kuinyamazisha Roho ya Mungu ndani ya mtu mwenye haki? Ni kweli kabisa kwamba kuwa kipofu siyo kwamba huna uwezo wa kuona, bali upofu mbaya ni ule wa kutokuikubali kweli kwa sababu tu wewe siyo wa upande huo wa pili wenye kuiona kweli kama ilivyo. Mungu hakosi kutuwajibisha pale tunapoichezea kweli ambayo ni moja ya sifa yake. Hivyo pamoja na Elisha kuipigania kweli hadi mauti yake, “watu hawakutubu wala hawakuziacha dhambi zao, hata walipochukuliwa mateka kutoka nchi yao, wakatawanyika juu ya uso wa dunia yote,” YbS 48:15. Kwani leo miongoni mwetu hawapo wenye kuutetea uovu ilihali wakijua madhara yake?

Mpendwa tuliyeongozana pamoja katika tafakari hii, turudi kwa swala letu kuu la kusamehe na kama umeguswa na tafakari hii, embu tulia na fikiri uliyembeba kwa muda mrefu bila kumsamehe. Leo au kesho tafuta njia ya kumsamehe. Ni vizuri akijua pia umemsamehe. Kwa tendo hilo unaleta pia uponyaji kwako na kwake. Na fanya hivyo kwa upendo na uhuru. Wakati ndio sasa!

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi,” Mt 6:14


Tusali:-Ee Yesu Mwema, nikumbushe daima kuwa kipimo cha kusamehe ni kusamehe bila kipimo kama ulivyojitoa sadaka pale Msalabani kwa upendo mkubwa bila kujibakiza na kusamehe yote. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario