martes, 7 de junio de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 10 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 10 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 18:41-46
Zab: 65:10, 11, 12-13
Injili: Mt 5:20-26
Nukuu:
 “Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli,” 1Fal 18:45

Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli,” 1Fal 18:46

Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20

 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23-24

Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25

TAFAKARI:Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”

Wapendwa katika Kristo, Injili yetu ya leo yatutaka tuyapime matendo yetu vyema hasa katika mizania ya kusamehe na kusamehewa. Yesu katika hili anatoa angalizo kubwa na kusema, "haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni," Mt 5:20. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki kuwa ni watu wema, na ndiyo kipimo cha kweli. Ndugu yangu, Mungu pekee ndiye hutuhesabia haki, tena si kwa matakwa yetu, bali kwa matakwa yake kwa sababu Yeye tu ndiye HAKI. Sisi binadamu tunashiriki tu ukamilifu wa Mungu kwa kuwezeshwa naye. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki na kuwa miungu watu. Huu ni upofu uliopitiliza. Kuwajua vizuri Mafarisayo na Waandishi nakualika usome sura yote ya 23 ya mwinjili Mathayo. Ni kwa sababu hiyo Yesu anatoa angalizo kwanza kama kweli tunataka uponyaji, lazima kusamehe kama hatua muhimu na mizania ya  kusamehewa.

Kusamehe ni amri kama kweli na sisi tunataka kusamehewa. Sala ya ‘Baba yetu’ imeliweka jambo hili wazi kama sharti la upatanisho na Mungu. Cha ajabu sala hii tunaisali wengine kila siku na kila mara kwa siku, ila bado kusamehe ni shiiida! Je, utaponywaje kama tatizo lako ni kuvunjika mguu, ila "P.O.P" umefunga shingoni? Mbona kila siku unatibu ugonjwa usioumwa kwa dawa tofauti? Kwa nini inakuwiya vigumu kusamehe na kupatana na ndugu yako? Je, wewe ni mkamilifu sana? Unatofauti gani na mafarisayo na waandishi wanachukuwa nafasi ya Mungu kwa kujihesabia haki?

Wapendwa wana wa Mungu, ukitaka sala yako, na maombi yako yapate kibali mbele ya Mungu, jipatanishe wewe mwenyewe, wewe na uliyekosana naye, na pia wewe na Mungu. Hivyo basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,  iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23. Wengi na hasa wale tuliokosewa hupenda kuyarefusha mambo sana, na wakati mwingine tungependa tunyunyuziwe ubani kwa cheteso cha dhahabu ili tuwe tayari kwa kuyaongelea yale yaliyotutatiza.

Ila baraka na neema hutujia pale tunapokuwa na uhusiano mzuri na wenzetu, mazingira, na Mungu Muumba wetu.  Nabii Eliya ni mfano wa kweli hii kama tulivyosikia somo letu la leo. Pamoja na ukame ulioikumba nchi, Mungu anawarudishia tena uhai kwa kuinyeshea nchi mvua, Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele,” 1Fal 18:41. Alisemalo Eliya ni uthibitisha wa ukaribu wake, na urafiki wake na Mungu. Hana shaka lolote juu ya Mungu kwani hakuwahi kuuvunja uhusiano wake na Mungu. Hivyo Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli,” 1Fal 18:45. Furaha ya Mungu kwetu ni kuuishi upendo wa kweli na kuwa na mahusiano mazuri kati yetu na viumbe vyake vingine. Mahusiano haya mazuri huufunua utukufu wake Mungu. Nabii Eliya ni uthibitisho huo wa mahusiano mazuri na Mungu. Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli,” 1Fal 18:46. Maisha kama safari, yatupasa yatupasa kuulinda uhusiano huo na ndugu zetu, mazingira na Mungu kadiri tunavyosafiri hadi mwisho wa safari yetu hapa duniani.

Ni kwa mantiki hiyo agizo la Yesu lakutaka wewe na mimi, "patana na ndugu yako uwapo naye njiani," Mt 5:25. Maana yake ni nini? Kupatana na ndugu yako mngali njiani ni kufanya juu chini kupatana na ndugu yako angali yu hai. Msivute muda pasipo sababu. Kengele ikishagongwa hakuna tena pa kujitetea. Maapizo na laana hazikusaidii chochote. Unazidi jizibia riziki zako bure na baraka kutoka kwake mwenyezi Mungu. Unaposamehe unajiponya na kumponya mwenzako pia. "Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi," Yoh 13:35.

Wapendwa wana wa Mungu, ibada na sadaka zetu kwa Mungu huwa safi na za kumpendeza Mungu pale tunapokuwa na amani ya kweli ndani mwetu, na ndugu zetu, mazingira yetu, na Muumba wetu. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23-24. Amani hii ni pale unapokuwa tayari kupatana na kusamehe bila kipimo.

Wapendwa wana wa Mungu, ukitaka sala yako, na maombi yako yapate kibali mbele ya Mungu, jipatanishe wewe mwenyewe, wewe na uliyekosana naye, na pia wewe na Mungu. Wengi na hasa wale tuliokosewa hupenda kuyarefusha mambo sana, na wakati mwingine tungependa tunyunyuziwe ubani na kupigiwa cheteso cha dhahabu ili tuwe tayari kwa kuyaongelea yale yaliyotutatiza.

Wengi tumeshuhudia watu hawapendi kupatana na kuishia kuapizana pasipo sababu. Wapo wengine hata baada ya kuzidiwa wakiwa kitandani karibu ya kufa wanapoomba upatanisho na ndugu yake kunakuwa na mkwamo bila mwitikio wowote na mwisho mtu huyo hufariki katika hali ya  majonzi makubwa. Hivi unajisikiaje ndugu yako kufa akikuomba upatane naye nawe kwa kiburi chako hukusikia na hatimaye ndugu yako anafariki? Ndugu yangu, Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25. Je, kwa kutokupatana na ndugu yako angali hai, utajibu nini mbele ya Kadhi-Mungu mwisho wa siku?

Tumsifu Yesu Kristo!

Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25


Tusali:-Ee Yesu Mwema na Mungu uliye Huruma, Msamaha na Upendo; tujalie Moyo wa kusamehe muda wote tusafiripo hapa duniani. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario