JUMATATU WIKI YA 11 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 21:1-16
Zab: 5:2-3, 5-6,-7
Injili: Mt 5:38-42
Nukuu:
“Lakini
mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume,
mgeuzie na la pili,” Mt 5:39
“Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe
urithi wa baba zangu,” 1Fal 21:3
“Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri
yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa
katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi,” 1Fal 21:8
“Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini
mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka
alizowapelekea,” 1Fal 21:11
“Na hao
watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa
wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na
mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa,” 1Fal
21:13
TAFAKARI: “Msishindane na mtu mwovu.”
Wapendwa wana wa
Mungu, leo Bwana wetu Yesu Kristo anatushauri kwa msisitizo tusishindane na mtu
mwovu. Ukweli ni kwamba kitokacho kwa Mungu ni chema na kama kilivyo kina
umilele kwa sababu Mungu wetu ni Mtakatifu, Mkamilifu, na Wamilele. Ni kwa
mantiki hii kwamba “hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya
uzaao matunda mazuri; kwa kuwa
kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini,
wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk 6:43-44. Wito wa Yesu kwetu wa
tusishindane na mtu mwovu unalenga katika dhana nzima ya uovu, yaani, uovu kama
ulivyo hauna umilele. “Msishindane na Mtu mwovu,” badala yake ni kuliweka
tumaini lote kwa Bwana ambaye kwake ndiko kwenye chanzo halisi cha wema na
jema, haki, na kweli. Ni kumcha Bwana na kuuchukia uovu. Hivyo “kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na
njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia,” Mit 8:13.
Ndugu yangu, uovu kwa wingi wake
hauna ‘umilele.’ Kama umilele ni maisha ya Utukufu wa Mungu wetu, uovu ambao
kutokuwa na uzuri/mafaa, ni dhahiri kwenye umilele huo (Utukufu wa Mungu)
hakuna uovu. Uovu ni swala la muda tu. Kwa maana nyingine haki lazima itawale
kuona kwetu, kufanya kwetu, na kuhukumu kwetu. Kwani “Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki
huokoa na mauti,” Mit 10:2. Wapo wengi kati
yetu huishi kwa dhuluma au kuwezeshwa kwa dhuluma, au vyote viwili kwa wakati
mmoja. Ndugu yangu, tenda haki kwa kila mmoja apitaye katika mikono yako nawe
utalipwa mema. Uovu ni andaki la dhambi, na aliye zama katika andaki hili la
dhambi ni vigumu kuubaini uovu wake kwa sababu hakuna nuru tena. “Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki
atalipwa mema,” Mit 13:21. Ni wazi lazima kuuchukia uovu, na kutenda haki.
Kwa nini basi Yesu anatuambia
tusishindane na mtu mwovu? Kujua ukweli huu yatupasa kuutafakari wasifu wa mtu
mwovu. Ushirika na mtu mwovu au ushindani na mtu mwovu mavuno yake ni udhalimu.
Njia salama ni kumwepa mtu mwovu kwa kuchukia tabia yake hiyo
ili ajirudi. Na kwa sababu hiyo, “usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa
udhalimu,” Kut 23:1b. Tabia hii ya mtu mwovu humtenga na Mungu kama asemavyo, “kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye
mwovu,” Kut 23:7c. Hivyo kama wewe ni kiongozi hapo ulipo, kwa nafasi yako wewe ni msimamizi wa kweli na
haki kama Mungu anavyoamuru, “basi, usikie
mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia
njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki
yake,” 2Nya 6:23. Kiongozi asiyefanya hili, bali elewa wazi wale waliochini
yake utawaliwa na hofu na ugumu wa maisha. Je, kama zipo mamlaka za kuwajenga
hofu kwa watu tukae kimya kama makaburi? La hasha!
Kukaa
kimya kama kaburi kwa kuogopa kuchukiwa
katika vita dhidi ya uovu na mtu mwovu ni kujivika aibu yako mwenyewe.
Ila kuishinda hali hii ni kuushinda uovu na mtu mwovu. Hivyo “hao
wakuchukiao watavikwa aibu; Nayo hema yake mwovu haitakuwako tena,” Ayu 8:22.
Kadiri ya historia ya ulimwengu huu na watu wake, hasa watu waovu, mwisho wao
hauna mema. Kwa nafasi wanazokuwa nazo na kuzitumia vibaya hasa kukataa kweli
na kuikandamiza haki, kilio cha wanyonge huamsha hasira ya Mungu. Hakuna mwenye
hati miliki ya ulimwengu huu, na wengine kubaki kama wasindikizaji tu. Na “hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu, Na
urithi wa hao waoneao, waupokeao kwa Mwenyezi. Watoto wake wakiongezeka ni kwa
upanga; Na wazao wake hawatashiba chakula,” Ayu 27:13-14. Mungu huweza ruhusu
kucheleweshwa kwa haki ya watu na yule mwovu kwa nia ya kumpa nafasi mwovu huyo
kujirudi na kutenda haki, bali Mungu hawezi kufumbia macho kuchezewa milele
upatikanaji wa haki hiyo kwa watu wake. Kila mmoja wetu ndani yake anayo chapa
ya Mungu, Mwa 1:27. Je, mtu mwovu
hupata wapi kiburi chake?
Tabia ya mtu mwovu
huamini utetezi wa nguvu zake na kuiondoa kabisa hofu ya Mungu ndani yake. Ni
kuishi kwa kujiamini kuliko pindukia. Huku ni kuiasi ile kweli iliyo ndani
yako, yaani, ‘umeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,’ Mwa 1:27. Na kwa sababu
hiyo, “Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya
Mungu mbele ya macho yake,” Zab 36:1. Pamoja na ujasiri huu usiokuwa na
mwelekeo wa mtu mwovu, “Bwana hataiacha
nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali,”
Mit 10:3. Hakika mwisho wa mtu mwovu hauna heri! “Mtu
mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika,” Mit
11:18. Katika hali kama hii ni vigumu kumshauri mtu mwovu lile lililo jema kwa
sababu hupenda kusikia yale ayapendayo na yaliyoujaza moyo wake. “Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu,” Mit 17:11a.
Hali na mazingira haya ya mtu mwovu kutamalaki katika uovu wake, na mtu mwenye
haki kukandamizwa na kile kilicho kweli na haki yake, inatupeleka kuelewa
vizuri uongozi wa mfalme Ahabu na mkewe Yezebeli kwa upande mmoja, na Nabothi
kwa upande mwingine kama mdhulumiwa kwenye haki.
Kosa
na sababu ya kuuwa kwa Nabothi ni kuitetea haki yake kama urithi kutoka kwa
baba zake, yaani, shamba lile la mizabibu lililokuwa karibu na nyumba ya mfalme
Ahabu, 1Fal 21:2. “Nabothi akamwambia
Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu,” 1Fal 21:3. Nabothi
hakuwa na lugha nyingine zaidi ya hiyo kwa sababu kwa Myahudi vitu vitatu
ndivyo vilivyo ulinda uhai wake. Navyo ni ardhi, Torati kama neno na amri ya
Mungu, ilikwa ni pamoja na Hekalu kama sehemu ya kumsifu Mungu na kumtolea
shukrani, na jambo la mwisho ni uongozi bora. Kwa hali hii tunaona wazi mambo
mawili muhimu yanatikiswa, yaani, ardhi na kutokuwa na uongozi wa haki. Kwa
vile mfalme Ahabu aliiruhusu dhuluma ndani ya moyo wake, neno lile la Nabothi lilimnyima
raha na usingizi kabisa, “akajilaza
kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula,” 1Fal 21:4b. Je, Ahabu
atafikiri zaidi kama kiongozi na kuzuia umwagaji wa damu? La hasha!
Kwa
vile mtu mwovu hukataa ushauri wa kweli, na badala yake hupenda kusikia yale
yaliyoujaza moyo wake, mke wake anatumia nafasi hiyo kuiondoa huzuni aliyokuwa
nayo mume wake, yaani, mfalme Ahabu. Yezebeli mke wa mfalme Ahabu anamwamasisha
mumewe kwa kusema, “Je! Sasa wewe
unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi
nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli,” 1Fal 21:7. “Sasa wewe
unaumiliki ufalme wa Israeli,” maneno
haya ni maneno ya uchokozi na chokonozi. Ni sawa na kusema, “iweje ushindwe
katika hili ilihali wewe ni mfalme wa Israeli?” Leo tungeweza kuyaweka maneno
hayo katika mazingira yetu na kusema, “Je, wewe siye Rais wa Tanzania?” Na
tungeweza kwenda mbele zaidi na kusema
kama alivyotaka kusikia mfalme; “iweje ushindwe katika hili ilihali
serikali hii ni yako?” Hakika washauri kama Yezebeli ni hatari katika swala la
kusimamia kweli na haki kama ilivyo.
Kwa kumfurahisha mfalme
na kuirudisha furaha yake, Yezebeli mke wa Ahabu mfalme “akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake,
akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika
mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi,” 1Fal 21:8. Mnyonge anapodhulumiwa, tena
kwa wale ambao walitakiwa kumtetea, ni vigumu sana kujinasua katika janga hilo.
Kila njia na mbinu usukwa ili hazma mbovu na dhuluma itimizwe. Na ndivyo
ilivyokuwa kwa mwenye haki Nabothi. Nyaraka ile iliyogushiwa na Yezebeli kwa
wazee iliwataka wazee wale kuwainua watu wawili na kuandaa ushahidi wa uongo
dhidi ya Nabothi, “ili wamshitaki, na
kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige
kwa mawe, ili afe,” 1Fal 21:10. Je, leo tupo tofauti na mazingira kama haya
yaliyomkuta Nabothi? Wapo wengi kati
yetu wamehukumiwa kwa kesi ya kugushi kama hizi, na bado zipo keshi nyingi za
mtindo huu mitaani mwetu. Nani basi wa kutunasua katika mazingira haya? Wale
wazee wenye nguvu katika jamii bila kujua na kuchunguzi kwa kina wito ule, nao
wanaingia mkenge na “wakafanya kama
Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea,” 1Fal
21:11. Ndugu yangu, penye uovu hata wenye ufahamu siyo wakutegemewa kabisa.
Hapa ndipo ule usemi huwa kweli kwamba, “machozi ya samaki huenda na maji.”
Uovu
una tabia moja. Unapousukuma huendelea kushirikisha wengi na mengi, na mwisho
wa siku ni mauti. “Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia,
wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu,
wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji,
wakampiga kwa mawe hata akafa,” 1Fal 21:13. Ni kweli kwamba Nabothi hakupigwa
mawe na wale watu wawili watoa ushahidi wa uongo juu yake. Ni mara ngapi
tunakutana na matukio ya kuchomwa watu barabarani nasi kwa kutokujua
kilichojiri tunashiriki moja kwa moja katika uovu huo? Je, tunatoa hata muda
kidogo kuhoji kwa nini mambo yamekuwa kama yalivyo? Je, ni kweli wanaopatwa na
matukio kama hayo wanastahili kufa katika mtindo kama huo? Hata kama kuna
sababu, je ni halali kuutoa uhai wa binadamu mwenzako kwa mtindo huo? USIUE!
(Kut 20:13, Kumb 5:17, Mt 5:21; 19:18; Mk 10:19; Lk 18:20; Rum 13:9, na Yak
13:9)
Msukumwa
na uovu hana mshipa wa aibu, bali ufurahia uovu wake. Hivyo utekelezaji wa
tukio lile linamfikia Yezebeli. “Wakampelekea
Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa,” 1Fal 21:14.
Yezebeli bila shaka anafarijika kwa tendo lile kwa sababu limekwenda kama
alivyolipanga. Hivi ni vifo vya kimfumo ambavyo si ajabu kuvisikia au kuviona
katika jamii yetu leo. Tunachoshuhudia ni hili; ‘Sauti usikika kwa kishindo,
watu wanapoteza uhai na mali zao, na mwisho kimya kama hakijatokea kitu.’ Hali
na matukio kama haya ni faraja tu kwa mtu mwovu, tena faraji hiyo ni kwa muda
mfupi tu. Ni kwa mantiki hiyo, “Yezebeli
aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia
Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa
kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa,” 1Fal 21:15. Kwa vile
mtu mwovu hupenda kuyasikia yaliyo ndani ya moyo wake tu, tena yaliyomaovu, “Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa,
akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili
alitamalaki,” 1Fal 21:16. Je, damu ya Nabothi na haki yake itapotea bure? La
hasha! Mungu wetu hayupo usingizini kama asemavyo, “mawazo yangu si mawazo yenu, wala
njia zenu si njia zangu,” Isa 55:8
Wapendwa
katika Kristo ni wito kwako na kwangu kwamba
tuwe watu wa kusimama katika kweli na haki mara zote. Tuuchukie uovu kwa sababu
hufifisha nuru ya Mungu ndani mwetu. “Msimlipe
mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote,” Rum 12:17.
Tutende haki, na tuanze pale tulipo. Tuwe watetezi katika kweli na haki kwa
wanyonge na wale wote wanaominywa haki zao. Hivyo “neno
lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye
kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia,” Efe 4:29. Huku ndiko kuwa nabii kwa
wakati wako.
Tusifu Yesu Kristo!
“Nabothi
akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu,” 1Fal
21:3
Tusali:-Ee Yesu uliye haki
na kweli yetu, tutumie vyema kama vyombo vyako vya kweli na haki pale tulipo
kama ushuhuda hai kwa wote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario