JUMAPILI YA 10 YA MWAKA-C
Somo
I: 1Fal 17:17-24
Zab: 30:1, 3-5, 10-12 (K) 1
Somo
II: Gal 1:11-19
Injili:
Lk 7:11-17
Nukuu:
“Akamwambia
Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu
ikumbukwe, ukamwue mwanangu?” 1Fal 17:18
“Akamwomba
Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu
ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe,” 1Fal 17:20
“Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia,
akafufuka,” 1Fal 17:22
“Kwa maana, ndugu zangu,
injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu,”
Gal 1:11
“Kwa
kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo
wa Yesu Kristo,” Gal 1:12
“Bwana alipomwona
alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13
“Akakaribia,
akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana,
nakuambia, Inuka,” Lk 7:14
“Yule
maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:15
TAFAKARI:
“Kila jambo linakusudi lake, litazame kwa jicho la imani, na wala usiruhusu
manung’uniko na kujihukumu. Tazama tumaini lililopo mbele yako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kumi ya Mwaka ‘C’ wa Kanisa. Kwa namna
ya pekee tunaalikwa kuwa na mtazamo chanya
pale tunapokutana na changamoto za imani. Masomo yetu yote matatu ya leo
yanatuelekeza katika fundisho hilo. Ukweli ni kwamba kila jambo lina kusudi
lake, litazame kwa jicho la imani, na wala usiruhusu manung’uniko na kujihukumu
pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo. Tazama mara zote tumaini lile lililopo
mbele yako. Tusomapo masomo ya leo tunapata mifano mitatu ya watu waliotazama
tumaini lililopo mbele ya maisha yao. Watu hawa ni Mama Mjane yule wa Sarepta,
IFal 17:9, Mtume Paulo wa Tarso, mji wa Kilikia, Mdo 22:3, na mwisho ni Mama
yule wa mji wa Naini aliyefiwa na mwanaye wa pekee, Lk 7:11-12. Watu hawa na
matukio yao kiimani yanatufundisha kuishi kwa tumaini pale tunapokumbana na
sintofahamu katika maisha.
Baada ya mateso na
mahangaiko mengi nyikani, ikiwa ni pamoja na kukata tamaa ya kuishi, Nabii
Eliya kwa mwongozo wa Mungu, 1Fal 17:9, anapata ufadhili na kukirimiwa na
mwanamke yule mjane wa Sarepta. Mama huyu alijaliwa kuwa na mtoto mmoja tu wa
pekee. Hata pamoja na ukarimu wa familia hii jambo la ajabu linatokea, yaani,
katika mazingira yasiyo ya kawaida mtoto huyu anafariki. Tendo hili ni uchungu
na huzuni kubwa kwa mama huyu majane, na fedheha kubwa kwa Eliya. Ni wazi kama
binadamu, na akiyatazama mateso yake ya huko nyuma, Eliya alijiuliza ‘kwa nini
haya yote yanitokee mimi?’ Kwa upande mwingine mjane huyu alipatwa na mashaka
juu ya mgeni wake, yaani, Eliya. “Akamwambia Eliya,
Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe,
ukamwue mwanangu?” 1Fal 17:18. Ni
dhahiri swali hili lilimsononesha sana Eliya aliye kirimiwa kwa upendo mkubwa
katika familia hii, ambayo ilikuwa tayari kushikiri kile kidogo walichokuwa
nacho, 1Fal 17:12-13. Pamoja na huzuni hii, bado Eliya aliyaweka matumaini yake
kwa Mungu. Eliya “Akamwomba Bwana,
akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake
hata kumfisha mwanawe,” 1Fal 17:20. Eliya hakuanza kumtafuta mchawa kuhusu kifo
kile, ila machozi, huzuni na fedheha ile aliipeleka mbele ya Mungu.
Ndugu
yangu, Mungu upatikana pale tunapo mtafuta pasipo shaka na kwa nia na moyo
thabiti, Isa 55:6. Hivyo Eliya “Akajinyosha
juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu,
nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena,” 1Fal 17:21. Kwa tumaini
hili alilokuwa nalo Eliya, Mungu hakukawia kujibu ombi lake, na kumwondolea
fedheha ile ugenini. Hapa Mungu anadhihirisha uwepo wake na kutowatupa wale
wamgemeano na kumwamini pasipo shaka. Na “Bwana
akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka,” 1Fal 17:22.
Ni fundisho kwetu pia kwamba upatwapo na tatizo usiishie kulalama tu, bali
mwambie Mungu ‘anataka kukufundisha nini kutokana na tatizo hilo.’ Hivyo omba
kwa Mungu nguvu na uwezo wa kutatua tatizo hilo. Hapa ndipo tuwezapo kuliona
tatizo katika mwono na jicho la Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
fudisho kubwa la tukio hili lipo kwa Eliya mwenywe, mwanamke mjane, na kwetu
sisi. Kwa mwanamke mjane anaelewa na kuamini nguvu za Mungu kupitia mtumishi
wake Eliya. “Mwanamke akamwambia
Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana
kinywani mwako ni kweli,” 1Fal 17:24. Kwa uthibitisho huo, Eliya pia anatambua
upendo wa Mungu kwake, na kamwe Mungu hawezi kumtupa hata akiwa katika shida za
mtindo gani. Tumaini halisi na lenye uhakika ni kwake Mungu tu. Nasi
tunafundishwa kumwelekea Mungu hata pale tunapopatwa na hisia mbaya kwa wale
tuliojitoa kwao na mara kuona kama ndiyo sababu ya mateso yetu. Swali la
kujiuliza katika sintofahamu kama hiyo hi hili: Je, ‘Mungu wataka kunifundisha
nini katika hiki nisichokifahamu vizuru?’ Na mwisho yatupasa kuliweka tumaini
lote kwake Mungu, kama asemavyo Mtume Paulo; “Jaribu
halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni
mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile
jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13. Mungu
hawezi kutugeuzia kisogo tunapomtumainia.
Mtu wa pili
anayetufundisha tumaini la kweli pale tupatwapo na sintofahamu nyingi katika
maisha ni Mtume Paulo. Mtume Paulo hakuwa na historia nzuri katika maisha yake
kabla ya kuongoka. Bila shaka nawe pia ukiitazama historia yako na hayo
yanayokutokea leo unakata tamaa na kujihukumu kila kukicha. Tazama tumaini
lililo mbele yako, na hasa ukitazama historia ya Mtume Paulo na kuongoka kwake.
Katika hili, Mtume Paulo mwenyewe anatusimulia kwa ufupi historia ya maisha
yake. Naye anasema, “Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji
wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa
sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi
nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi
watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na
wanawake,” Mdo 22:3. Historia hii ya Mtume Paulo inasema chochote kuhusu hali
na maisha yako? Kama haitoshi, mtazame Yesu pale msalabani, kwani kaubebe
ujumbe mzito sana juu ya maisha yako. Kwa kuwambwa kwake Msalabani anakuambia
hivi; “ona nilivyo hapa. Nimeyafanya haya yote kwa sababu na kupenda upeo.”
Hakika hakuna sababu ya kujiona mnyonge na mtu aliyetengwa ninapoutafakari
Msalaba Mtakatifu. Kristo ndilo tumaini la kweli, na Yeye ndiye njia, kweli, na
uzima wetu, Yoh 14:6.
Mtume Paulo baada ya
kuongoka kwake, ikiwa ni msukumo wa moja kwa moja wa Kristo mwenyewe baada ya
kutupwa chini, Mdo 9:4-5, tumaini lake lote alilielekeza kwa Kristo Yesu. Naye
kwa kutoa ushuhuda wa kweli hiyo anasema, “Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo
niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu,” Gal 1:11. Kwa
maneno mengine ni kwamba kile alicho na anachokihubiri Mtume Paulo siyo tokeo la nguvu zake au maarifa yake
binafsi, bali ni neema ya Kristo iliyo ndani yake.
“Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu (Injili hiyo) wala
sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo,” Gal 1:12. Mtume
Paulo hafichi historia yake mbaya na kuona aibu kuisema mbele za watu. Ila
anataka mimi na wewe tuelewe kwamba misimamo yetu iliyojengwa na inayojegwa na
mila na desturi zetu potofu, ndani yake hakuna uzima. Naye anasema, “Maana
mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba
naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu,” Gal 1:13. Ndugu yangu,
kama wewe ni mmoja wa kujipambanua kwa ubora wa kabila lako, misimamo ya kabila
lako isiyo na mwono wa Kimungu, na hata umaarufu wake, basi elewa haupo njia
sahihi kama wataka kuwa mfuasi wa Yesu. Mtume Paulo anakuambia wewe na mimi
kwamba, “Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio
hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya
baba zangu,” Gal 1:14. Hata kwa kufanya hayo yote, Mtume Paulo anagundua
hapakuwa na tumaini lolote, zaidi ya kupotea kwa misimamo isiyo na mwelekeo wa
Kimungu na kuikosa njia ile sahihi.
Wapendwa katika Kristo,
usipotambua uwepo wa Mungu katika maisha yake, chochote ujengacho juu yake
hukosa msingi imara, na mwisho wake uporomoka. Baada ya kuongoka kwake, Mtume
Paulo anagundua nguvu na uwepo wa Mungu katika maisha yake. “Mungu aliyenitenga tangu tumboni
mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,” Gal 1:15. Hivyo kile alicho Paulo
baada ya kuongoka kwake, yaani, kurudi katika njia iliyo sahihi, Kristo ndiye
kila kitu kwake. Ni kwa sababu hiyo Paulo anasema kwamba, Mungu “alipoona vema kumdhihirisha
Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri
na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa
hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi
tena Dameski,” Gal 1:16-17. Je, umeyapitia machungu na mahangaiko kama Mtume
Paulo?
Na mwisho, mtu wa tatu
mwenye kutupa tumaini la kweli katika udogo na mahangaiko yetu ni mwanamke yule
wa mji wa Naini aliyefiwa na mwanaye wa pekee, Lk 7:11-12. Injili ya leo
inatupa simulizi hili kwa namna ya pekee. Yesu Kristo katika safari zake za
kuihubiri habari njema ya wokovu akiwa na wanafunzi wake, wanakutana na msafara
uliobeba maiti ya mwana pekee wa mama mjane. “Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na
maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa
mjini wengi walikuwa pamoja naye,” Lk 7:12. Bila shaka msafara ule wa maiti ile
na hali za watu kama zilivyokuwa kwa kusikitika juu ya msiba ule, na hasa mama
huyu ambaye anaonekama kuwa mwema kwa jirani zake, unamsikitikisha Yesu pia. “Bwana
alipomwona (mama mfiwa) alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13. Neno
‘usilie’ katika mazingira haya limebeba ujumbe, ‘ondoa hofu na uwe na
matumaini.’ Tumaini lenyewe hapa na katika uhasilia wake ni Kristo Yesu
mwenyewe. Kwa upendo wa ajabu na huruma
ya Kimungu, ambaye kwa sasa ni Mungu na mwanadamu, Yesu “Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa
wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka,” Lk 7:14. Baada ya tukio hili la pekee kabisa na
ajabu, “Yule maiti akainuka,
akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:15. Bila shaka mimi na wewe
tungekuwa katika msafara huo tungetimua mbia kwa hofu! Pamoja na hofu waliokuwa
nayo watu wale katika msafara ule, walibaki na tumaini kubwa mbele yao. “Hofu
ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na,
Mungu amewaangalia watu wake,” Lk 7:16. Hili ni fundisho kwetu pia. Twapaswa
daima kumshukuru Mungu na kuliweka tumaini kwake tu aliyetutendea mambo ya
ajabu, badala ya kujitafutia utukufu binafsi, na hata kutaka kuabudiwa. Pili,
tuwe vyombo vya kusambaza habari njema kwa wengine, badala ya chuki. “Habari
hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando,” Lk
7:17. Je, ndugu yangu, hapo ulipo watumika kama chombo cha habari njema ya
wokovu, au ndiyo upande wa pili, yaani, mzalisha chuki?
Siku moja jioni nikiwa
na Babu yangu Mzee Ngilishi, ambaye sasa hupo mbele za haki, alinisimulia
hadithi hii kuhusu Jogoo. Nyakati zao Babu waliweza kudamka mapema asubuhi kwa
msaada wa vitu viwili. Moja, ilikuwa kuwika kwa Jogoo, na pili, sauti ya
Kengele kutoka Parokiani. Pamoja na msaada wa viashiria hivyo viwili vya kuujua
muda, Jogoo hakuweza kuwasaliti isipokuwa pale mwezi unapoandama.
Lakini Babu aliendelea kusema,
“pamoja na kuwika kwake Jogoo, nasi kujua kumekuchwa, Jogoo alikuwa ana tafsiri
yake ambayo ni tofauti kidogo. Jogoo hufikiri kwamba asipowika hakuwezi
kukakuchwa.” Baba aliendelea kusimulia, “kwa ukweli wa jambo hili kama wapo
jogoo wawili watatu, hukosi kusikia ushindani wao kwa wao katika kuwika. Moja
huanza hivi, “mimi ni wa kwanzaaaaaa,” na mwingine huitikia, “umekoseaaaaaa,
haaaaa!” Babu na mimi tuliangua kicheko!
Mwisho, Babu akasema,
“mara nyingi twaweza kuwa tunafanya mazuri na mwisho tukajifananisha nayo huku
tukisahau yule aliyetuwezesha kuyafanya hayo yote. Unapokosa msingi huu, na
kujiweka katikati ya yote yale uyafanyayo, mambo yanapoharibika au kutokwenda
vizuri kadiri ya mazoea yetu, ni rahisi kukata tamaa kabisa. Na hapa ndipo unapolikosa
lile tumaini la kweli la kusonga mbele kwa sababu yote umeyaweka pamoja nawe
ukijiaminisha ndiyo yote katika yote. Hivyo huwezi kuona mbele upatwapo na
sintofahamu katika maisha. Mjukuu wangu usiwe ukuta wako mwenyewe na kushindwa
kuona mazuri zaidi yaliyopo mbele yake. Sasa nenda kalale na uyasikilize vizuri
Majogoo,” Baba alimalizie simulizi lile.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bwana
alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13
Tusali:-Ee
Yesu na Mwokozi wangu, usiniondolee lile tumaini ndani yangu. Nijalie niweze
kuyaona yote katika tumaini la kweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario