JUMAMOSI WIKI YA 11 YA MWAKA-C
Somo: 2Nya 24:17-25
Zab: 89:4-5, 29-30, 31-32, 33-34
Injili: Mt 6:24-34
Nukuu:
“Hata
baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia.
Naye mfalme akawasikiliza maneno yao,” 2Nya 24:17
“Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani;
naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi
kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana,
yeye naye amewaacha ninyi,” 2Nya 24:20
“Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia
huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi
kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24
TAFAKARI: “Hakuna mtu awezaye kutumikia
mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu.”
Wapendwa wana wa Mungu, tafakari ya leo inatuzamisha katika dhana
nzima ya ‘uaminifu’ katika maisha, na hasa kwa yule mwenye kutuwezesha yote
katika yote. Huyu si mwingine bali ni Mungu mwenyewe. Ni kuishi maisha
yanayoongozwa na malengo, yaani, maisha ya hofu ya Mungu. Ikiwa ni maisha yenye
malengo na yanayoongozwa na hofu ya Mungu, ni wazi maisha hayo
‘yatakuwajibisha.’ Hiki ndicho asemacho Bwana wetu Yesu Kristo kwamba, “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana
atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu.
Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Sehemu ya pili ya angalizo ya Yesu
limejikita kwenye Mungu na mali. Mara nyingi uwezo wa mtu kwa upande wa mali
alizonazo zimekuwa chanzo cha kiburi chake na kuuvaa upofu wa kutokuona nafasi
ya Mungu katika maisha yake, na mwisho kujisadikisha kuwa na uwezo wa kufanya
kila jambo kwa mali alizonazo. Mali ikiwa ni pamoja fedha alizokuwa nazo mtu,
Mtume Paulo analiona jambo hili wazi pale fedha hiyo inapo mtawala mtu. “Maana shina moja la
mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo
wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10
Tukiachana na fedha,
jambo lingine ambalo ni hatari ni matumizi mabaya ya mamlaka aliyonayo mtu.
Nguvu ya mamlaka kwa wengine huwatia kiburi hasa pale mamlaka hiyo inapokuwa na
mwelekeo ‘neno la mwisho’ dhidi ya mali, maisha, na uhai wa watu, yaani,
mamlaka isiyohojiwa wala kukosolewa pale ambapo mambo yanapokwenda ndivyo
sivyo. Ni rahisi kwa mwenye nguvu hizi kimamlaka kujisahau na kuchukua nafasi
ya Mungu. Mwenye kufanya hivyo ni kuusahau pia ubinadamu wake ikiwa ni pamoja na mapungufu yake. Hivi ndiyo hali
ilivyokuwa kwa mfalme Yoashi aliyesahau historia nzima ya ufalme wake mara
baada ya kufa kwake kuhani Yehoyada. “Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda
wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao,” 2Nya
24:17. Sujudio la watu kwa mfalme ni kiashirio cha anguko kimahusiano kati ya
Mungu na mamlaka ya kibinadamu. Ndugu yangu, wakusujudiwa ni Mungu tu. “Ni
nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u
Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa
matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa,” Ufu 15:4. Jaribu la kufanywa Mungu
watu liliwakuta pia Mtume Paulo na Barnaba uko Likoania katika safari yao ya
kimisionari.
Tendo la uponyaji wa
mtu mwenye udhaifu wa miguu-kiwete tangu tumboni mwa mamaye, linaibua hisia za
watu hawa wa Likaonia na kuwaona Paulo na Barnaba kama miungu ya kuabudiwa. “Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo
wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya
wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu,
na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji,” Mdo 14:11-12. Tendo hili
ni moja ya mambo hatari sana katika utume au utumishi wa aina na ngazi yoyote
ile. Ukiona hali hii ndani mwa watu inajitokeza na kuacha kumwabudu Mungu na
kuanza kukuambudu wewe kama mchungaji wao au kiongozi wao, ujue wazi ufanyacho
si matakwa ya Mungu bali shetani amechukua nafasi yake. “Tazama, nakupa walio
wa sinagogi la Shetani…, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na
kujua ya kuwa nimekupenda,” Ufu 3:9
Hivyo kwa kutambua
kasoro hii, Mtume Paulo na Barnaba wanatoa angalizo kwa Walikaonia na kusema,
“Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi;
twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na
kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha
mataifa yote waende katika njia zao wenyewe,” Mdo 14:14-16. Hatari kubwa katika
jambo hili ni kwamba, binadamu anapoukataa ubinadamu wake, anajeuka kuwa mbaya
kuliko shetani, kwani shatani alishaukubali ushetani wake pale alipomwasi
Mungu. Na ndivyo ilivyokuwa katika utawala ule wa mfalme Yoashi kwamba, “Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao;
wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu
ya hiyo hatia yao,” 2Nya 24:18.
Katika hali na
mazingira kama haya, Mungu haachi kuwainua watumishi wake kutoa maonyo kwa watu
wake waliokengeuka katika imani ili wabaki katika kweli.
“Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada,
kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi
kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana,
yeye naye amewaacha ninyi,” 2Nya 24:20. Mara nyingi walio kolea katika uovu ni
vigumu sana kutazama nyuma na kuanza upya kwani “tamaa ikiisha kuchukua mimba
huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti,” Yak 1:15. Ni kwa
namna na ugumu huo hawakumsikia Zekaria mwana wa Yehoyada, na badala yake
wakaazimia kumuua, 2Nya 24:21. Mfalme Yoashi anasahau historia yake na namna
alivyookolewa kuuwawa akiwa mtoto mdogo na hata kutawazwa kuwa mfalme. “Basi
hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia,
bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya,
akayatakie kisasi,” 2Nya 24:22. Katika kweli na haki, Mungu kamwe hafumbi macho
licha ya kuchelewa kwake kutimiza kweli na haki hiyo. Yeye anatujua ni wakati
gani unafaa. Pamoja na kuvamiwa na mataifa ya jirani, mfalme kwa kosa lake la
kuruhusu maabudu ya miungu mingine katika utawala wake linayafanya maisha yake
kutokuwa na mwisho mzuri. “Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha
ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa
ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika
mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme,” 2Nya 24:25. U
ndumilakuwili katika maisha siyo mzuri. Ni heri kuwa joto au baridi, kuliko
kuwa vuguvuvu.
Ni kwa mtazamo huo,
Yesu katika Injili ya leo anatupa angalizo na kusema, “hakuna
mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda
huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na
mali,” Mt 6:24. Hata ukifanikiwa ni kwa muda mfupi tu. Je, kwa nini twapaswa
kumtumikia bwana mmoja? Sababu ya wazi na ya moja kwa moja ni kuondoa ile roho
iliyojigawa vipande vipande. Mfano; kama umepata mialiko miwili ya harusi
inayofanyika muda ule ule na siku ile ile, yakupasa kuchagua moja wapo
utakayokwenda hata kama zote zina uzuri au zimetofautiana. Kuchagua huku ndiko
Yesu anapotushauri kuutafuta kwanza ufalme wa Mbinguni, na kuondoa roho ya
kujigawa vipande vipande. Naye Yesu anasema, “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33. Ndugu yangu, unaloneno zaidi ya ukweli huu wa
Bwana wetu Yesu Kristo?
Ni ukweli usiotia
shaka kwamba ukishaingia katika mfumo huu, na mtazamo huu wa fundisho hili ya
Yesu, kuutafuta ufalme wa mbinguni kwanza, huwezi kupata presha unapowaona watu
wakipigana vibega kwa kumwangaikia mfalme tumbo na utajiri wake. Kristo
anapokuwa katikati ya yote, yeye atakupatia kadiri ya mahitaji yako na kwa
wakati wake. “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia
yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Mt 6:34. Ndugu yangu yatupasa kumuishi
Kristo leo na sasa katika yale yote yampendezayo. Ingawa kesho inasikika
akilini mwetu, tuelewe kesho hiyo ipo mikono mwa Mungu katika uhalisia wake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33
Tusali:- Ee
Yesu, uwe kitoshelezo chetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario