SHEREHE YA
MT. PETRO NA PAULO, MITUME
29/6
Somo: Mdo 12:1-11
Zab: 34:1-3, 4-5, 6-7, 8-9
Somo II: 2Tim 4:6-8, 17-18
Injili: Mt 16:13-19
Nukuu:
“Hata
Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka
malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa
taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11
“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani
nimeilinda,” 2Tim 4:7
“Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike
ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18
“Simoni
Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16
“Nami
nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu;
wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18
“Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa
limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa
mbinguni,” Mt 16.19
TAFAKARI: “Utume si lelemama,
bali ni kuvumilia hadi ushindi wa kweli.”
Wapendwa
wana wa Mungu, neno utume si geni masikioni mwenu. Ila tusikiapo neno utume
yatupasa kwanza kabisa tuelewa ukweli huo na uhasilia wa maisha hayo ya kiutume
kwamba hayana uhusiano na faida binafsi. Ni utumishi uliotukuka, na
usiojifungamanisha na maslahi binafsi. Ni msukumo wa maisha unaotutaka kujitoa
zaidi kwa ajili ya wengine bila kujali faida yetu binafsi. Utume kamwe hauwezi
kuwa na malengo ya faida binafsi. Mtu anapokuambia ametoka utume, au anaenda
utume ni vyema kuelewa kwamba anaenda kumenyeka, kutaabika na kujichosha kwa
ajili ya wengine. Msukumo huu haupaswi usukumwe na ufahamu au vigezo vya wale
tunaowahudumia, ila kwa kila tunayemuhudumia bila kujali anatujua au la.
Hivyo leo
Mama Kanisa anavyosherehekea siku ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume,
anasadifu ukweli huu, yaani watu hawa walikuwa ni MAJITU YA SIFA, katika maana
ya kwamba waliyatoa maisha yao bila kujibakiza pasipo woga wowote. Ingawa
sitazama sana katika wasifu wa Petro na Paulo Mitume, ila historia ya maisha
yao inaonyesha jambo hili. Petro anajulikana zaidi kama kiongozi na mwakilishi
wa Kristo katika kundi la wale wa mwaminio Kristo na kuyaishi maagizo yake.
Paulo anasimama kama mmisionari shupavu aliyeyafanya yote ndani na kwa ajili ya
Kristo. Hivyo leo Kanisa linasheherekea zawadi ya maisha yao katika kutenda na
kulisimamie lile alilolianzisha na kuliacha Kristo, na kulipeleka duniani kote
kama Kanisa la kimisioni na Sakramenti ya wokovu.
Ni wazi
watu hawa wawili yaani Petro na Paulo wanayafanya mambo haya makubwa katika
maisha yao ‘kwanza kwa kujitambua wao wenyewe,’ na pili ‘kuishi utambuzi huo katika
kukutana na Kristo kila siku.’ Ukomvu wao wa Imani ni matokea ya kumtaabikia
Kristo kila siku katika kuutoa ushuhuda wa kweli. Somo la kwanza linaeleza kwa
undani ni kwa namna gani Petro aliutoa ushuhuda huo bila woga. Mwisho anasema
maneno haya baada ya kutoka gerezani kwa miujiza. “Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa
katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo
12:11. Ufahamu huu kwa Petro hauna tena shaka juu ya kile anachokiamini.
Injili ya leo kwa namna nyingine inatupa wasifu wa Petro
kwa undani na kutuelekeza nini hasa maana ya kiti chake na nafasi yake kati ya
Mitume. Mtume Petro ndiye pekee aliyejibu swali ya Yesu kwa ufasaha, licha
kwamba kwa mujibu wa Yesu jibu lile ni ufunuo kutoka kwa Mungu. Yesu
anapowauliza wanafunzi wake, Je, watu wanasema kuwa mimi ni nani, Petro anajibu
baada ya ukimya mkuu (tafakari): “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Yesu
anaridhika na jibu hili, na hapo hapo anamnyenyekesha Petro kwa kusema, “Heri
wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba
yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Ufahamu huu wa Petro, na kufunuliwa huku kwa
siri hii juu ya Kristo, kunamhesabia haki juu ya kiti kile alichokikalia hadi
leo, Petro kama halifa wa kwanza, na Mababa watakatifu waliomfuata kama maalifa
wa Kristo. Yesu mwenyewe anaweka kiti hiki rasmi kwa kusema, “wewe ndiwe Petro,
na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu
haitalishinda,” Mt 16:18. Wapendwa, Kanisa letu linamisingi yake. Moja ya
misingi yake hiyo ni uongozi Imara usio wa yumbishwa.
Wapendwa wana wa Mungu, baada ya kuwekwa rasmi kiti hicho
kama alama ya uongozi imara kichungaji, anayekalia kiti hicho anapewa mamlaka
kamili juu ya wale watakao kuwa chini ya uongozi huo. Yesu anayatoa mamlaka
hayo kwa kusema, “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa
mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na
lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19.
Kwa kupitia kiti na mamlaka haya, Kanisa linakuwa rasmi chombo cha msamaha na
huruma ya Mungu. Na hii ndiyo maana ya Kanisa kama Sakramenti ya wokovu. Kanisa
pia linapewa mamlaka ya kufundisha, kuonya, kukataza na hata kufungia yale
yanayoenda kinyume cha Imani na ufuasi wa Kristo.
Ndugu yangu, chuma kinapoitwa “Iron Steel,” kimepita katika
moja mkali sana. Uimara wa chuma hiki ni tokeo la chuma hicho kuvumilia joto
hilo kali bila kupoteza uhasilia wake. Mitume, na hasa Petro na Paulo ambao leo
Mama Kanisa anawasherekea, walitaabika vya kutosha kuhusu jina la Yesu. Somo la
Pili linaeleza kwa undani mahangaiko na taabu alizozipata Mtume Paulo. Mtume
Paulo anasema kama ni vita ameishinda na mwendo ameumaliza. “Nimevipiga vita vilivyo
vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7. Faida kubwa aliyoipata
katika utume wake huo wa pekee ni kuilinda Imani ambayo si kwa faida yake
mwenyewe, bali kwa Kanisa zima. Msingi wa maisha ya Mtume Paulo ni kauli mbiu
yake hii: “kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.” Flp 1:21.
Hii ni hatua ya juu kabisa kwa mfuasi wa Kristo. Hapa ni kuishi kile
unachokiamini na kukubali kuyapata yote kutokana na imani hiyo.
Wapendwa
wana wa Mungu, hatua aliyoifikia mtume Paulo ni hatua ya kutokutishika na jambo
lolote. Ni hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa
tunajua wote lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikono ya Kristo, na kuacha
yeye atende kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka yoyote juu ya: sababu ya
kuja kwake Yesu Kristo kwetu, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na
ufufuko wake. Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: “Bwana ataniokoa na kila
neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye
milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18. Je, ninaweza kuyatamka maneno haya bila
hofu yoyote ninapokabiliwa na changamoto za maisha yangu ya kila siku? Ndugu
yangu Utume si lelemama, bali kuvumilia hadi ushindi wa milele.
Tumsifu
Yesu Kristo!
Wewe
ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya
kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18
WATAKATIFU
PETRO NA PAULO MITUME, MTUOMBEE. AMINA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario