sábado, 11 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 11 YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 11 YA MWAKA-C
Somo I: 2Sam 12:7-10, 13
Zab: 31:1-2, 5, 7, 11 (K) 5
Somo II: Gal 2:16, 19-21
Injili: Lk 7:36-8:3
Nukuu:
Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni,” 2Sam 12:9 

Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10

Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:13

 hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki,” Gal 2:16 

 “Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure,” Gal 2:21

Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu,” Lk 7:38 

Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi,” Lk 7:39 

TAFAKARI: “Neema na Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Matendo yetu tu kama yalivyo hayatoshi kutuhesabia haki mbele ya Mungu. Ila kwa Neema ya Mungu yote mema kwetu yawezekana. Sote twaalikwa kufanya toba ya kweli na majuto.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 11 ya mwaka “C” wa Kanisa. Wazo kuu la tafakari yetu la leo kadiri ya masomo yake ni hii: ‘Neema na Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Matendo yetu tu kama yalivyo hayatoshi kutuhesabia haki mbele ya Mungu. Ila kwa Neema ya Mungu yote  mema kwetu yawezekana. Sote twaalikwa kufanya toba ya kweli na majuto.’ Kwa kutambua kosa lake na huitaji wa huruma ya Mungu, Mfalme Daudi akamwambia Nabii Nathani, “Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:13 

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, kunatofauti kubwa kuusema ukweli na kuuishi ukweli. Kuna tofauti kubwa pia ya kuhubiri haki na kutenda haki. Vile vile kunatofauti kubwa sana ya kusema kuhusu upendo na kuishi upendo. Kuyasema mambo kwa ufasaha ni taaluma ambayo mtu anaweza kuipa kwa kupitia njia na miongozo inayohusu jambo hilo. Kuishi jambo fulani ni kugeuzwa na jambo hili na kuwa sehemu ya jambo hilo. Kumbe kwa namna nyingine kama wasemavyo waswahili, ‘kuna kusoma na kuelimika.’ Hivi ni vitu viwili tofauti.

Nabii Nathani anatumwa na Mungu kwenda kwa Mfalme Daudi na kumwambia chukizo alilomfanyia. Nathani anamweleza Daudi uzito wa tatizo na dhambi aliyoifanya kwa jamii, kwa yeye mwenyewe na kwa Mungu. Kwa nafasi aliyokuwa nayo Daudi kama Mfalme ilimpasa awe mtetezi wa kweli, haki, Amani na Upendo. Ufalme wake kama ulivyo uliwakilishwa na taswira na fadhila hizo. Badala yake, Daudi anakuwa muhujumu wa hiyo kweli, haki, Amani, na Upendo. Huu ndio ule mfano wa mtu yule aliyekuwa na kondoo wake mmoja na aliyempenda kupita vitu vyote, 2Sam 12:1-4. Nathani hapa anamaanisha, mtu yule ni Uria, na kondoo wake ni mkewe Bath-sheba Daudi aliyezini naye, na matokeo yake kupelekea umauti wa Uria. Kama Kondoo, yaani wanawake, Daudi alikuwa nao wengi na ofisi yake kama Mfalme iliruhusu kuwa na wake hao wengi.

Mazungumzo ya Nabii Nathani na Mfalme Daudi kwa kupitia mfano wa Mtu na Kondoo wake aliyekuwa anampenda na hivyo kudhulumiwa, yanaamasisha sifa kuu na uwepo wa falme yoyote ile iliyo kwa ajili ya watu, yaani: ufalme wa haki, amani, kweli, na upendo. Hivyo Mfalme Daudi anaguswa na mfano ule na kumwambia Nabii Nathani, “Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma,” 2Sam 12:5-6. Mfalme Daudi anajiweka kitanzi mwenyewe kwa makosa yake. Ndugu yangu, kumbuka maneno ya Yesu, Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38. Ni kwa mizania hii, Nabii Nathani anamwambia Daudi bila kupepesa macho, Wewe ndiwe mtu huyo,” 2Sam 12:7. Hivyo kosa na adhabu inamstahili yeye mwenyewe.

Mungu anatoa adhabu kwa Mfalme Daudi kwa kosa lile ambayo ni chukizo kwake mwenyewe kama Mfalme na mtetezi wa haki za watu, chukizo na makwazo kwa jamii, na chukizo kwa Mungu aliye haki, kweli, amani, na pendo. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10. Kwa kutambua kosa lake na kulikiri, Mungu anathibitisha kuwa Yeye ni Upendo na Huruma na kumwondolea adhabu ya kifo Mfalme Daudi. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:12. Pamoja na hayo, kiumbe kile kama tokeo la uzinifu wa Daudi hakikuishi.

Wapendwa katika Kristo, wewe na mimi kwa njia moja au nyingine tumefanya kama Daudi na wakati mwingine zaidi hata ya Daudi. Hakuna njia nyingine ya kujikwamua katika hali hii zaidi ya kufanya toba ya kweli na majuto. Mungu aliye mwingi wa rehema, neema na upendo yu tayari kutusamehe. Kwa maana Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli,” Zab 86:15. Amina 

Injili ya leo tunamwona Yesu anaalikwa nyumbani kwa Mfarisayo mmoja kwa chakula. Tukio hili kwa kiasi fulani linaakisi tukio lile kubwa la mlo wa mwisho wa Yesu na wanafunzi wake. Tukio lile la mlo wa mwisho Yesu aliandaa na kuwaalika wanafunzi wake, na kuonyesha kwa upendo jinsi ilivyowapasa kuishi, na kuwapa rasmi majukumu yako kama watumika na siyo wanaotumikiwa. Katika tukio hili lenye kuakisi mlo ule wa mwisho; upendo, huruma, na msamaha wa Mungu unajidhihirisha. Upendo, huruma, na msamaha wa Mungu hautokani na mila na desturi zetu wanadamu, bali ni kweli iliyo ndani ya Mungu mwenyewe ambayo ina uhusiano wa karibu kabisa na wa moja kwa moja kwa namna tulivyoumbwa, yaani, ‘kwa sura na mfano wake,’ Mwa 1:27. Sheria zetu licha ya ukweli unaoufunua kadiri ya mazingira yetu na wakati mwingine katika mapungufu yake, siyo sababu ya upendo, huruma, na msamaha wa Mungu kwetu, “kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria,” Rum 3:20.

Karne ile ya kwanza katika ulimwengu ule wa kiyahudi ulitawaliwa na ‘dini’ ya matendo ya sheria. Matendo haya ya sheria yalitafsiriwa ndivyo sivyo kama sababu ya kuhesabiwa mtu haki mbele za Mungu. Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu,” Rum 10:3. Upofu huu katika tafsiri halisi ya Sheria ndiyo iliyowapoteza Mafarisayo na mwisho wa siku hawakuifuata Torati kama ilivyokuwa, bali tafsri yake ambayo  ililenga ubinafsi wao na matamanio yao. Hivyo Yesu anatupa angalizo na kusema, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20. Mtume Paulo anayafahamu fika matendo ya sheria ambayo ndani yake hapakuwa na uzima wowote, bali kupotea na kupotoka kwa kujiridhisha nafasi na kujisadikisha kama asemavyo, wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa,” Mdo 26:5. Mtazamo huu na umbumbumbu huu ndiyo Yesu anausema kama mzigo kwa Mafarisayo.  Wao (Mafarisayo) hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao,” Mt 23:4 

Hivyo ndugu zangu, waraka kwa Wagalatia kama tulivyokwisha usoma leo, Wayahudi waliwataka Wagalatia kuzishika mila zao (kiyahudi), na desturi za Mafarisayo. Matendo ya sheria hayakuhusiana kabisa na ‘dini’ ya Musa na Agano la Kale, ambayo ndiyo Torati. Matendo ya sheria hayakuwa kweli kuhusu Torati, bali tafsiri ya Torati ambayo ilikuwa ukweli wa Mungu ulipotoshwa kama tutakavyoona baadaye kidogo. Wakristo wengi na hasa baadhi ya Madhehebu ya Kiprotestanti hawatofautishi ukweli kati ya matendo ya sheria na sheria yenyewe (Torati).

Wengi hufikiri matendo ya sheria ni kutokuifuata Torati. Hii si kweli. Mtume Paulo anaposema matendo ya sheria anamaanisha Talmud, yaani ukweli kuhusu Mungu uliopotoshwa kutokana na tafsiri ya Torati yenyewe. Kwa ujumla mafundisho ya Mtume Paulo yalilenga au kukazia juu ya Yesu Kristo, yeye mwenyewe Paulo, yaani kuongoka kwake, na swala zima la neema ya Mungu. Katika fundisho hili Mtume Paulo anasema,  Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu,” Gal 2:20. Kuhusu Neema ya Mungu kwetu ambayo kwayo yote mema yawezekana, Mtume Paulo anasema, Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure,” Gal 2:21. Sheria isemwayo hapa siyo Torati, bali matendo yale ya sheria ambayo kwayo kama yalivyo hayana uzima wowote ndani yake. Ni mbwembwe tu!

Pamoja na ukweli wa fundisho hilo, kinyume chake ni kwamba, Mtume Paulo anawafundisha Wagalatia kutii sheria na amri za Mungu, ‘dini’ ya kweli, ikiwa ndiyo njia ya maisha-Agano la Kale-Torati, angali wakiishi katika neema ya Mungu iliyowezeshwa na Kristo mwenyewe kwa sadaka yake pale msalabani. Ndiyo maana kwa mshangao mkubwa Mtume Paulo anawauliza Wagalatia, Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:1-2. Kwa matendo ya Sheria hapa, Mtume Paulo haipingi Torati bali anazungumzia yale yaliyotafsiriwa na kuchukuliwa kama mapokeo ya wazee na siyo Torati yenyewe, Mk 7:9. Ukweli ni kwambamwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki,” Gal 2:16 

Kuishika sheria ya Bwana kama ilivyo Torati si laana au kulaaniwa, bali Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima,” Zab 19:7. Lakini kinyume chake ni kwamba, wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye,” Gal 3:10. Bila shaka Mtume Paulo analisema hili na kusimamia ukweli huu kama ulivyo na ilivyopaswa kuiishika Torati bila kuichakachua.  Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina,” Kumb 27:26

Ndugu yangu, kuna usalama na ukamilifu katika kuishika sheria ya Bwana kwani wana,  Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana,” Zab 119:1. Ni kwa ukweli huu kuhusu sheria ya Bwana Mtume Paulo anasema, torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema,” Rum 7:12. Naye Yesu kwa msisitizo anatuambia, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17. Na zaidi kuhusu amri, Yesu anamwambia yule Bwana tajiri kwamba,  “ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri,” Mt 19:17 

Yesu anautambua udhaifu huu wa sheria za wanadamu, na hasa katika jamii yake ambayo waliachana na torati na kufuata tafsiri ya torati na masimulizi yake, yaani, TALMUD. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi,” Lk 7:39. Ni kweli kwamba wote ni wadhambi, yaani, mwanamke yule asiyejulikana, na huyu mfarisayo anayemshangaa Yesu kuguswa na huyu mwanamke. Huyu mfarisayo anaonyesha upendo mdogo, ana mashaka na Yesu, ana moyo mzito na mgumu, na hivyo kumfanya aonyeshe upendo kidogo. Kinyume chake, mwanamke huyu anakuwa karibu na Yesu, anamgusa Bwana Yesu, anaufungua moyo wake na kujiweka wazi mbele ya Mungu wake aliye Huruma. Mwanamke huyu anaonyesha upendo mkubwa na kupenda kwa sababu anapenda na anajisikia kupendwa na Bwana aliye Huruma, Yesu Kristo. Huyu mwanamke mdhambi hajisikii aibu kwa kulia na kuyatoa machozi yake mbele za watu waliokuwa wanamwangalia na kumuhukumu ndani ya mioyo yao.

Kristo amekuja na kujitoa kwa wadhambi kwa urafiki wake na kuwapatia wokovu. Kwake Yesu ni muhimu sana na furaha kwa mdhambi kuupokea urafiki huu na kutambua umasikini wake, yaani, dhambi zake. Yesu Kristo anafanya urafiki na mdhambi kwa huruma ya hali ya juu. Hapa tunagundua ukubwa na upendo wa Mungu usiopimika. Yesu hawabagui watu. Yesu anawapenda watu na kukaa nao karibu, na kuutwaa wokovu kwa wote. Yesu anajua vyema nani yule mwanamke aliyekuwa karibu naye. Yesu anajua mwanamke huyu ni mdhambi na yupo tayari kuanza upya naye kwa sababu anahitaji kukombolewa. Hata hivyo kinachowakwaza Wayahudi ni kuona kwa nini Yesu anamwacha mwanamke huyu aendelee kumgusa ili hali wanajua ni mdhambi. Katika tendo hili Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami,” Lk 7:23. Kwa nini basi tunakwazika tuonapo upendo wa Mungu kwa watu wake? Yohana Mbatizaji alihubiri ubatizo wa toba na watu waliongoka. Lakini kwa makusudi Mafarisayo waliupinga ubatizo ule kwa vile walikwishajihesabia haki. Ndugu yangu, bado hatujamaliza kuamini na kuelewa huu upendo wa Mungu. Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye (Yohana),” Lk 7:30. 

 Jambo la kushangaza zaidi wakati wa Yesu, Torati ile ambayo ndiyo ilikuwa mstakabali wa Taifa la wana wa Mungu-Waisraeli, ilikwisha chakachuliwa vya kutosha na hivyo Taifa hili lilikuwa linafuata Tafsiri yake tu kwa sehemu kubwa. Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi) iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati. Ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa.

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu hana macho tuliyo nayo sisi ambayo yana kikomo na umbali fulani wa kuona. Macho ya Mungu, au kwa namna nyingine muono wa Mungu uvuka hata uwezo wetu wa kuona na matokeo yetu ya kufikiri. Hivyo Yesu anaurejesha uhai wa Mungu kwa maisha ya kweli na sababu ya kuumbwa huyu mwanadamu. Hivyo kwa tukio hili la mwanamke huyu mwenye dhambi nyumbani mwa Mfarisayo, Yesu anasema bila kupepesa macho yake, kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo,” Lk 7:47. Licha ya udhaifu wake kama mwanadamu, mwanamke huyu akuacha kuonja upendo wa Mungu na kurudisha upendo huo kwa Yesu kadiri ya uwezo wake. Anafanya tendo hili kwa  kumdondoshea machozi miguu ya Yesu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, hakuacha kumbusu sana miguu ya Yesu, na kumpaka miguu ya Yesu marhamu. Ni ukweli kwamba, “hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipenda, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu,” 1Yoh 4:12. Msukumo huu wa upendo haumzuii Yesu kumwambia mwanamke huyu kuwa, “Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani,” Lk 7:50. Kila mmoja wetu anahesabiwa haki mbele za Mungu si kwa kile alicho, bali ni upendo, huruma, na msamaha wake Mungu mwenyewe. “Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu,” IKor 2:11.

Yesu anaonyesha ugumu wa mioyo ya hao wasiopenda kuongoka na wasiopenda kuwatambua wadhambi. Ukweli ni kwamba wote walio wana wa Mungu hutambua hekima ya Mungu. Hekima hii ya Mungu ndiyo Huruma yake. Hivyo wenye mioyo migumu hawawezi kufurahia kuongoka kwa wengine. Dhambi kubwa ya mtu ni pale anaposhindwa kujua kuwa yeye ni mdhambi mbele ya Mungu. Mtu wa leo hakubali dhambi zake, na hajisikii kuwa ni mdhambi. Hali hii utuweka mbali na habari njema ya wokovu. Ni kweli kwamba kadiri tunavyokuwa katika maisha ya kiroho ndivyo hivyo tunavyojisikia masikini zaidi na wahitaji wa huruma ya Mungu. Neema ya Mungu utufanya tuishi katika kweli na utuwezesha kugundua hitaji kubwa la kuwa na Mungu.

Je, ndugu yangu unalo la kumficha Mungu? Basi kama kweli tunataka kuponywa kama mwanamke huyu na kama alivyoponywa Mfalme Daudi, yatupasa kujisalimisha kila siku mbele za Mungu. Tunafanya hivyo tukijua kwamba, “wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu,” Ebr 4:13. Hapo vipi ndugu yangu?

Padre huruma ya Mungu ni mhamasishaji mzuri sana wa maisha ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Kama tujuavyo jumuiya hizi ndilo taswira ya wazi la Kanisa kama mwili wa Kristo. Hapa tunajuana vizuri siyo tu katika urefu na ufupi wetu, wembamba na unene wetu, bali pia tabia zetu na historia zetu nzuri na mbaya. Hivyo, Padre huruma ya Mungu kwa wiki mara mbili husali na moja ya jumuiya zake katika Parokia yake ya Bikira Maria Mama wa Mateso.

Dada Natalia ni mmoja wa wana Jumuiya ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambayo ndiyo zamu yao kutembelewa na Padre huruma ya Mungu. Dada huyu Natalia ni mwana jumuiya wa kawaida, ila mwenye furaha, uchangamfu na mwenye kujitoa kwenye jumuiya yake hasa katika swala la mapambo na maandalizi ya altare pale kunapokuwa na adhimisho la Misa Takatifu katika jumuiya. Huduma hii kwa baadhi ya wanajumuiya hawakuwa wanapendezwa nayo kwa sababu historia ya maisha Dada Natali haikuwa nzuri.

Licha ya kufanya toba ya kweli na kumrudia Mungu, Natalia hakupenda kuficha hali yake na afya yake kwa baadhi ya wana Jumuiya, ikiwa ni pamoja na viongozi wake wa Jumuiya. Na kwa sasa Dada huyu ni mwadhirika. Ukweli huu kwa wana jumuiya wengine waliuchukulia kwa woga sana kiasi kwamba walitaka pia kumzuia kuendelea kutoa huduma ile aliyokuwa akiitoa kama nilivyosema hapo juu. Mbaya zaidi hawakupenda asalimiane na Padre huruma ya Mungu. Mmoja wa kiongozi wa Jumuiya hii aliwahi hata kumvuta sikio na kumwambia asiwe anasalimiana na Padre kwa kumshika mkono kabla ya Misa na hata wakati wa kutakiana amani.

Hakina Dada huyu alikuwa na wakati mgumu sana. Hata hivyo hakukatishwa tamaa kutoshiriki na wana jumuiya wenzake katika sala. Basi siku ile katika adhimisho la Misa Takatifu na ulipofika muda wa kutakiana amani, Padre huruma ya Mungu bila kujua chochote alimwendea moja kwa moja na kumpatia mkono wa amani kwa sababu alimwona kasimama mwenyewe tu kwa muda mrefu. Dada Natalia kwa tendo lile ya Padre kumpa mkono wa Amani lilimfanya ashindwe kujizuia na kuanza kububujika machozi. Padre hakuelewa chochote na aliendelea na adhimisho lile la Misa hadi mwisho.

Mwisho wa adhimisho lile la Misa ile Takatifu, Padre huruma ya Mungu alitaka kujua kulikoni. Natalia alimweleza Padre huruma ya Mungu historia yote ya maisha yake. Na mwisho Natalia alimwambia Padre; “pamoja na hayo yaliyotokea huko nyuma katika maisha yangu, leo najisikia furaha kubwa sana kunitakia amani. Hakika nimeonja upendo wa Mungu na nina furaha kubwa sana moyoni mwangu. Asante sana Padre,”

Padre huruma ya Mungu alimwambia Dada Natalia huku akiwa amelishika bega lake, “Mungu asingekuwa na huruma na kusamehe dhambi, mbinguni kungekuwa wazi kabisa. Watakatifu tayari wana historia yao ya jana, mimi na wewe tulio wadhambi bado tuna leo na kesho yetu kama tukijaliwa. Basi tuitumie leo yetu vizuri na kesho na kesho hiyo kama tukijaliwa, ili nasi siku moja tuwe na historia yetu kama watakatifu.” Padre huruma ya Mungu alimkubatia, na kisha kuingia naye ndani kwa ajili ya chakula kile kilichoandaliwa na jumuiya.  Baadhi ya wanajumuiya hawakuacha kumkazia macho Natalia kama mijusi.

Tumsifu Yesu Kristo!

na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao,” Lk 8:2-3


Tusali: Ee Yesu, uliyetupenda upeo, nijalie pendo lako hilo la kweli na  lisilo na ubaguzi kwa kila mmoja ninayekutana naye na katika hali yoyote ile. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario