sábado, 18 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 12 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 12 YA MWAKA-C
Somo: 2Fal 17:5-8, 13-15a, 18
Zab: 60:1-3, 10-11
Injili: Mt 7:1-5
Nukuu:
Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine,” 2Fal 17:7 

Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya,” 2Fal 17:8 

kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu,” 2Fal 17:13

 “Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa,” Mt 7:2 

Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?” Mt 7:3 

TAFAKARI: Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.” 

Wapendwa wana wa Mungu, kama kweli tu wana wa Mungu aliye hai, basi twapaswa kufanana na ule uwana uendanao na ufalme wake. Ufalme wa Mungu ni Ufalme wa haki na uzima, Ufalme wa Utakatitifu na Neema, Ufalme wa Mapendo na Amani. Historia ya wana wa Israeli mara kwa mara Inaonyesha ukaribu wao na Mungu, na wakati mwingine uasi, na Mungu kuwa mbao nao. Unapotokea uasi huu Taifa hili la wana wa Israeli upoteza amani na maisha huwa magumu sana na kutumikishwa kama mateka kwa nchi jirani zao. Katika somo la leo kama tulivyosikia, hali kama hiyo, yaani, kuchukuliwa mateka inatokea katika kipindi cha kumi cha Hoshea, kwamba, yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine,” 2Fal 17:7. Tatizo kubwa lilikuwa ni kuiga mambo yasiyofaa kutoka kwa majirani zao na kwenda kinyume na amri na Upendo, na Huruma ya Mungu. Hivyo,  wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya,” 2Fal 17:8 

Wapendwa wana wa Mungu, katika sintofahumu hiyo, Mungu hakuacha kuwainua watumishi wake Manabii na kukemea kukengeuka kwao. Hata hivyo kama ilivyo sikio la kufa halisikii dawa, ilikuwa vigumu kwao kuamini na kusikia sauti hiyo ya kinabii. Kwani kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu,” 2Fal 17:13. Mungu akuacha kutoa hukumu yake na hata kuruhusu mateso kwao kama dawa ya kuwaponya na uasi wao. Hukumu hii ya Mungu ilikuwa ya haki na kweli kwani hata kabla ya hukumu hiyo aliwapa viashirio vingi na hata kuwatuma Manabii wake kufundisha njia ipasayo kufuatwa, kukemea uovu husika, na kuonya. Hata pamoja na adhabu hizo Mungu alizokuwa anazitoa hakuwa na lengo la kuwapoteza, bali kuwapata wana wake, lakini pale tu wanapoikumbatia huruma na upendo wake na kuziacha njia zao mbaya kwa toba ya kweli na majuto. Hukumu hizi na adhabu zake zilitumika kama ‘dawa ya kiroho’ ili wautambue Upendo na Huruama ya Mungu. Na ndiyo maana kwa upendo huu, “hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Huyu ndiye ‘NENO’ aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, yaani, Yesu Kristo.

Injili ya leo inaongelea kwa undani juu ya utoaji wa hukumu. Jambo la msingi kabisa kulifahamu, Yesu apingi utoaji wa hukumu ulio haki na kweli. Tatizo lipo pale tunapo wahukumu watu pasipo haki na kweli. Jambo la pili ni hili; hukumu ile uitoayo kipimo chake kiwe kweli iliyo ndani yako mwenyewe, yaani, nguvu ya maadili uliyo nayo. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu kwamba, “kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa,” Mt 7:2. Hatua hii inaturudisha kwenye Imani thabiti kwa kile ukiaminicho na ufanyacho katika ufahamu wake na umaana wake. Imani hii asili na chanzo chake ni Mungu mwenyewe aliyeamua kujifua kwetu kama zawadi. Imani ni tunda la Neema na Upendo wa Mungu kwetu. Hivyo tufanyapo hukumu yoyote ile, Mungu apaswa kusimama katika tendo hilo, yaani, haki ya kweli. Hapa ndipo tunapozungumzia hofu ya Mungu. Licha ya kwamba bado tunabaki kuwa wanadamu katika nyama na mifupa yetu, hupaswi kutawaliwa na hisi zako utoapo hukumu. Ukifanya hivyo, basi haki na kweli huwa matatani. Haki na kweli lazima itendeke kama ilivyo.

Hatua ya pili yenye neema na inayotutofautisha na wengine kama wafusasi hai wa Kristo katika katoa hukumu, hata pamoja na haki kutendeka kama ilivyo, UPENDO wa Mungu lazima utawale. Lengo lisiwe kumpoteza yule unaye muhukumu katika kweli na haki, bali lengo liwe kumpata. Ni kufanya zaidi kwa yule unaye muhukumu katika kweli na haki. Katika hili Yesu anasema, “nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo,” Lk 6:33. Tenda yetu katika kutoa hukumu iwe ya haki na kweli, na kipimo kiwe upendo, yaani, kumpata yule aliyepotoka au potea.

Kwa mantiki hiyo, hukumu ya kifo haina nafasi katika maana halisi ya mafundisho ya Yesu. Kifo hakikuwa sababu ya ujio wake wa kumkomboa mwanadamu. Naye Yesu anasema, Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele,” Yoh 10:10. (Rejea habari ya kondoo mia na kupotea mmoja, Lk 15:4-7, Mwanamke mwenye shilingi kumi akipotelewa na moja, Lk 15:8-11, Mtu aliyekuwa na wana wawili-habari ya mwana mpotevu, Lk 15:11-32). Mifano hii yote mitatu inatupa picha pana ya furaha ya Mungu pale mmoja anapoziacha njia zake mbaya na kuukumbatia uzima wa milele. Mungu hufurahi sana pale mwenye dhambi anapoziacha njia zake na kumrudia. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk 15:7 

Hukumu yenye mizania ya upendo haibebwi na hisia za chuku, wala kulipiza kisasi, na wala lengo lake siyo kumpendezesha mwanadamu. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?” Mt 7:3. Hukumu tuitoayo ibebwe na nguvu ya maadili tuliyonayo. Tusipolifanya hili, hukumu yetu itakuwa ya kinafiki kabisa mbele ya jamii na mbaya zaidi mbele ya Mungu.Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako,” Mt 7:5. Vibanzi vyetu ni mapungufu yetu tuliyonayo. Mara zote tujitahidi kuyasafisha na kuachana nayo mapungufu yetu ili hukumu tuitowayo kwa wenzetu ibebwe na nguvu ya kimaadali tuliyonayo. Kinyume chake hatutakuwa tofauti na kemeo lile alilolitoa Yesu kwa mafarisayo walionekana kukimbizana na masikini na wanyonge, huku wenye majina yao, fedha zao, ushawishi wao katika jamii wakiachwa kufanya watakavyo. Ni katika taswira hii Yesu anatuambia wewe na mimi tusiohukumu katika kweli na haki kwamba, “viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,” Mt 23:24. Je, hili halina ukweli katika jamii yetu tunapopambanua ‘rushwa kubwa’ na ‘rushwa ndogo?’ Mafisadi ‘Papa’ na vifisadi dagaa?’ Lugha hii inatoka wapi kama siyo haya asemayo Yesu, ‘kuchuja mbu na kumeza ngamia?’

Tumsifu Yesu Kristo!
Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya,” 2Fal 17:8


Tusali:-Ee Yesu Mwema, ulie kielelezo halisi katika kweli, haki, na upendo, tufanya watumishi wako na wasimamizi wako katika kweli, haki na upendo pale tulipo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario