JUMANNE WIKI YA 12 YA MWAKA-C
Somo: 2Fal 19:9b-11, 14-21, 31-35a, 36
Zab: 48:2-3a, 3b-4, 10-11
Injili: Mt 7:6, 12-14
Nukuu:
“Alituma wajumbe kwa Hezekia mara ya pili, kusema, Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda,
maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema,
Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru,” 2Fal 19:9-10
“Naye Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu
wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa
falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi,” 2Fal 19:15
“Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu,
nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12
“Bali
mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni
wachache,” Mt 7:14
TAFAKARI: “Huruma na Neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Moyo wa toba
na majuto ya kweli huyajenga upya mahusiano yetu na Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu, tulitafakaripo neno la uzima wetu tunagundua
kwamba, ‘Huruma na Neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.’ Na hata pamoja
na ukweli huu, ‘moyo wa toba na majuto ya kweli huyajenga tena upya mahusiano
yetu na Mungu.’ Mungu wetu ni hai na hutujalia uhai kila siku bila kujali njia
zetu nzuri au mbaya. Je, hujiulizi pamoja na maovu yako bado anakupa pumzi ya kupumua?
Je, tungeitajika kulipa kodi ya hewa tunayopumua, ni nani kati yetu angelipa
kwa wakati na muda wote? Je, hili lisingekuwa jambo la kukufanya ujirudi na
kumrudia Mungu ambaye anao uwezo wa kusimamisha mtiririko wa pumzi unayovuta
bure? Kama nakuambia uongo, basi niambie ni siku gani utakufa hata kama kufa ni
kweli isiyopinga.
Ndugu yangu, unapojaribu kupata maana ya maisha yako hapa duniani, na
bila kuchoka kudadisi kesho itakuaje, lazima utakiri tu kwamba kuna sehemu
kubwa ya maisha yako bado haijulikani sawasawa, na inabaki kuwa fumbo kwako
kama mwanadamu mwenye ukomo fulani wa asiyeyajua yote katika ukamilifu wake.
Hili tusilolijua sawasawa na hatuchoki kutaka kujua ukweli wake, uwazi huo
unatusukuma kadiri ya ufahamu wetu kujua lazima kuna kitu zaidi yetu na chenye
ukamilifu wote kwa sababu cha fanya na kusema kile tusichokijua. Uwazi huu
unazibwa na Mungu mwenyewe anayejifunua kwetu kupitia Maandiko Matakatifu, na
yale yote tunayokutana nayo kila siku katika maisha yetu. Kwa ufahamu wetu
hatuupi maana yoyote kwa ulimwengu huu tunaishi kama jukumu la muda mfupi, bali
kadiri tuutafakaripo ulimwengu huu tunaoishi kwa muda mfupi unatupa maana ya
maisha yetu. Hatua hii ya kutokuona yote sawa na yapo kama yalivyo, ndiyo
itusogezayo katika uwepo wa Mungu kama nguvu na uwezo wa yote kama yalivyo kwa
utaratibu na ujumla wake pasipo ugonganishi wowote ule. Nguvu hii ya ndani na
yenye kuyafanya yote kila moja katika upekee wake, na yote katika mwelekeo wa
utulivu na wenye kuufunua umilele katika kila kimoja wapo, ndiye Mungu
Mwenyewe.
Wapendwa wana wa Mungu,
tuutazamapo ukweli huu ambao hujionyesha wazi katika maisha yetu ya kila siku,
kwa hofu ya Mungu tunatambua kwamba pamoja na udhaifu wetu wa kibinadamu,
‘Neema na huruama ya Mungu ni kubwa kuliko udhaifu wetu, yaani, dhambi zetu.’
Pamoja na Mamlaka na nguvu za kifalme walizokuwa nazo Taifa la Israeli,
walijikuta mateka pale walipoukataa uwepo wa Mungu katika maisha yao na
kutegemea nguvu na akili zao. Kejeli kama hizi ndizo hata mataifa
yaliyowazunguka walizifanya pale walipowanyanyapaa. Mfalme Ashuru anatuma
ujumbe kwa mfalme wa Yuda-Hezekia kumkejeli kuhusu Mungu waliyekuwa wana
mwamini. Maneno ya ujimbe huo yalisema hivi; “Asikudanganye
Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme
wa Ashuru,” 2Fal 19:9-10. Hata hivyo, Mfalme Hezekia hakushtushwa na ujumbe
ule, 2Fal 19:14, licha ya kwamba alionja udhaifu wao kama Taifa mbele ya Mungu.
Bado walimtegemea Mungu atafanya tu chochote wanapomwelekea kwa majuto ya
kweli. “Naye
Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu
ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia;
wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi,” 2Fal 19:15. Toba yao kama Taifa
inautambua uwepo wa Mungu, tena aliye hai. Wanatambua pia si haki Mungu wao
aliye hai kuziakiwa, 2Fal 19:16. Wito wao ni mwamba Mungu atege sikio lake tena
na kuwatoa katika mtego na mkono wa adui wao. “Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na
mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe
ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako,” 2Fal 19:19. Sala hii ya Mfalme Hezekia ni
sala ya kujiachia pasipo kujibakiza. Kama ni silaha ya vita bali katumia risasi
ya mwisho na yenye matumaini yote. “Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe
kwa Hezekia, akisema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba
juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia,” 2Fal 19:20.
Tunapojiachi kwa Mungu bila kujibakiza katika toba na majuto ya kweli kama Taifa
au mmoja mmoja ya chukizo lake mbele ya Mungu, neema na huruma ya Mungu ni
dhahiri kwetu. Mungu kamuumba kila mmoja wetu aishi milele na asipotee. Raha ya
Mungu ni kutupata tena na tena.
Ndugu
yangu, ufanyapo toba na majuto ya kweli, Mungu haishi kukupa neema na huruma
yake tu, bali uyapanga upya maisha yako katika mwelekeo ulio sahihi na wenye
umilele. Na hivi ndiyo alivyofanya kwa wana wa Israeli chini ya Mfalme Hezekia
kupitia mjumbe wake Nabii Isaya; “Basi Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa
Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele
yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake,” 2Fal 19:32. Je, tunapoteza nini
tunapojisalimisha mikoni mwa Mungu, ambaye yupo tayari kuanza yote katika
maisha yetu? Tatizo ni kiburu na kutokushindwa kwetu. Mwisho wa siku tunakupali
kufa na tai zetu shingoni, na siyo kuukubali udhaifu wetu kama wanadamu. Mungu
yupo tayari kuyafanya yote sasa na baadaye pale tu tunapoukiri kwa utashi wetu
uwepo wake. Kwa kufanya toba na majuto ya kweli, Mungu haturudishii tu imani
tuliyoipoteza, bali ufikiria pia mambo yajayo kuhusu maisha yetu. Na hivi
ndivyo alivyofanya kwa Mfalme Hezekia na watu wake, kwamba, “nitaulinda
mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi
wangu,” 2Fal 19:34. Na ndiyo alivyotekeleza ahadi yake, “Ikawa usiku uo huo
malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na
themanini na tano elfu,” 2Fal 19:36b. Basi Mungu anavyotutendea mambo makuu
kama haya ni wito kwetu pia kutenda wema kwa kila mmoja wetu. Huku ni kusadhifu
neema na huruma ya Mungu kwetu.
Wapendwa wana wa Mungu, kwa neema na huruma yake Mungu,
katika Injili ya leo, Bwana wetu Yesu Kristo anatupatia suluhu lenye upana
uliozidi mipaka ya kifamilia. Suluhu hilo ni kuwa macho muda wote katika kujali
na kuwajibika tukifanya jambo hili la msingi, yaani, “yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo
hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Maana yake ni kwamba,
jambo lililo jema ni jema tu siyo kwako ila na hata kwa mwenzako. Basi litende
kama lililovyo na vizuri zaidi litende kama lako. Hufanyavyo hivyo, jua ndiyo
Mungu apendavyo liwe hivyo kwani hiyo ndiyo hamu ya moyo wake, ambayo kwetu ni
sheria. Sheria hii ya “upendo,” twaifanya
si kwakushurutishwa, bali ndicho kiini cha maisha yetu, na hofu yetu kwa Mungu.
Ndugu
yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, jambo hilo hapo juu tusipolifanya,
na hasa kwa ndugu na wale wote wanaotuzunguka, bado hatujajua thamani ya utu
wetu, na upendo wa Mungu Baba kwetu. Hapa tunapewa angalizo: “Msiwape
mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije
wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua,” Mt 7:6. Mara nyingi
tunavipa vitu heshima kuliko utu wa mtu. Leo na hasa ulaya, mbwa au paka
anaweza kugaramiwa na kupewa upendo wa hali ya juu kuliko ombaomba aliye
mlangoni mwa Kanisa siku nzima. Mbwa huvalishwa nguo za joto wakati wa baridi,
ila masikini huyu hana hata koti kuufunika mwili wake. Binadamu na utu wake
atabakia kuwa hivyo hata kama mfumo wa maisha yake utakuwa mbovu au
kutokuridhisha. Mbwa au Nguruwe atabakia kuwa nguruwe hata kama tutajaribu
kumpandisha na kuwa na hali kama sisi. Sababu ni kwamba yale tuwafanyiayo yenye
mastahili ya kibinadamu kwao hayana maana na hayana thamani yoyote kwao.
Wanyama wapewe stahiki za wanyama, na binadamu apewe heshima yake kama binadamu
licha ya umaskini wake. Ujumbe hapa ni kwamba tuwe na busara kadiri ya stahiki
yatu kama wanadamu. Kutokufanya hivyo ni kukosa busara na kupoteza hadhi yetu
na utu wetu. Tendo hili ni sawa na pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe ambayo
ulinganishwa na mwanamke asiye na busara/akili. Kwa nguruwe pete hiyo haina
thamani. Nguruwe uweza kuiburuza atakavyo. Na hii ndiyo maana ya maneno haya, “kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika
mwanamke mzuri asiye na akili,” Mit 11:22.
Hapa
ndipo penye mtihani mkubwa wa maisha, na tafsiri nzima ya maisha ya umilele
ikiwa ni pamoja na hukumu yake. Yesu Kristo anatupatia njia ya kufuata
tusijepigwa na mshangao siku ya mwisho. “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni
mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango
huo,” Mt 7:13. Uzuri wa njia pana ni kwamba
kunauwezekano mkubwa wa kubeba kila kitu, yaani ponda mali kadiri ya uwezo
wako, ila usisahau kifo kwani huja kwa mtindo huo huo. Na hapo ndipo penye
ubaya wa njia pana. Njia nyembamba hutukataza baadhi ya mambo kutokuchukuliana
nayo. Wembamba wa njia hutunyenyekesha namna ya kutembea katika njia ile ili
tufike kwa usalama mwisho wa safari. Hatuwezi kujiendea kama tutakavyo.
Yatupasa kufuata mwelekeo wa njia kama ulivyo. Njia nyembamba inatuadhabisha
namna ya kuenenda kwa faida yetu wenyewe. “Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao
waionao ni wachache,” Mt 7:14. Waionao njia hii ni wachache kwa sababu hulka ya
binadamu si kupata mateso. Hulka ya binadamu ni kuitafuta furaha. Ndugu yangu,
elewa hakuna utukufu pasipo msalaba. Hivyo njia nyembamba ndiyo njia sahihi
kuelekea uzima wa milele, licha ya machungu na mapaswa yake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Basi yo yote myatakayo
mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na
manabii,” Mt 7:12
Tusali:-Ee Yesu, tujulishe
njia yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario