IJUMAA WIKI YA 11 YA MWAKA-C
Somo: 2Fal 11:1-4, 9-18, 20
Zab: 132:11,12, 13, 14, 17-18
Injili: Mt 6:19-23
Nukuu:
“Na
Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka,
akawaharibu wazao wote wa kifalme,” 2Fal 11:1
“Ila
Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa
Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake,
na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo
hakuuawa,” 2Fal 11:2
“Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa
mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya Bwana;
akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa Bwana, akawaonyesha huyo mwana wa
mfalme,” 2Fal 11:4
“Ndipo
akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya
mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na aishi,” 2Fal
11:12
“Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia. Naye
Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme,” 2Fal 11:20
“Msijiwekee
hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba,” Mt 6:19
“kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo
wako,” Mt 6:21
“Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na
giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!” Mt 6:23
TAFAKARI: “Kisichotoka kwa Mungu kwa ajili ya watu na kupitia watu, hakiwezi
kikadumu hata kama kitalazimishwa. Tuwekeze kwa Mungu kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi
hawavunji wala hawaibi.”
Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya historia nzima ya wokovu wetu, ni
dhahiri kwamba, “Kisichotoka kwa Mungu kwa ajili ya watu na kupitia watu,
hakiwezi kikadumu hata kama kitalazimishwa.” Swali hapa ni kwamba kwa nini
nyakati fulani tunalazimisha vitu na mwisho vinakuwa madhara makubwa kwetu?
Jibu ni hili: ‘hatupendi kuona vitu kama vilivyo, bali hupenda kuviona vitu
hivyo kama tulivyo.’ Kwa maana nyingine, hatupo tayari kuupokea ‘ukweli na
uhalisia wa jambo kama ulivyo, bali kama tujionavyo.’ Mang’amuzi katika maisha
ni mwalimu mzuri sana pale tunapoivaa miwani ya ‘kweli na haki.’ Tatizo kubwa
wewe na mimi, tunapenda kuvaa miwani ya kuubadili uhalisia wa jambo kwa kuleta
unafuu au urahisi katika ‘mwonekano wa jambo husika.’ Ni kuvaa miwani ya giza
wakati uhalisi wa kitu umemulikwa kwa mwanga au nuru ya jua. Je, imani yetu
kama Wakristo, na tena Wakatoliki imejengwa katika msingi gani?
Ndugu yangu, pasipo UFUNUO wa Mungu kwetu, ni vigumu kuzungumzia swala
zima kuhusu imani yenye kuaminika. Mungu kwa upendo wake na mpango wake wa
kumkomboa mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, anajifunua kwa
mwanadamu huyu katika historia kwa hatua, na mazingira halisi na hali ya
mwanadamu kama alivyo muumba. Kumbe wewe na mimi kama tulivyo leo siyo kwa
bahati mbaya, bali ni makusudi mazima ya Mungu katika mpango wake wa ukombozi.
Hivyo tunapoitazama historia hii, na kadiri ya Maandiko Matakatifu, na
utumilifu wa unabii, tunaona ugoto huo unafikia kilele kwa Neno aliyefanyika
mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, yaani, Yesu Kristo. Hapa ndipo maisha upata
maana na tumaini kule tuendapo kulipo beba yote katika yote.
Hivyo, fikra na udadisi wetu katika fumbo hili hausadifu au kuufanya
ufunuo wa Mungu kuwepo, bali unatusaidia kuuelewa kama njia mojawapo ya
mwitikio wa fumbo hili la Mungu kujifunua kwetu. Ufunuo kama ulivyo
unajitosheleza kama ulivyo. Kwa ufunua kama ulivyo kuna mambo mawili lazima
tuyajue, yaani, moja; ‘kiini na kibebwa katia ufunuo huo,’ na pili ‘tendo la
ufunuo lenyewe.’ Kiini na kibebwa katika ufunuo wa Mungu katika ujumla wake ni
kweli isiyowezwa onyeshwa katika undani wake kwa sababu ya toka kwa Mungu
mwenyewe ambaye katika asili yake sisi kama viumbe hatujui kina chake. Ila kwa
upande wa ‘tendo la ufunuo,’ kibinadamu na kwa uwezo wa akili na ufahamu
tuliopewa, kwa kupitia matukio ya kihistoria yenye kubeba kusudi la wokovu
wetu, ulifumbua funuo la Mungu kwetu. Hapa ndipo tunapozungumzia ukamilifu wa
unabii. “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma
Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini
ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Matendo haya
kwa namna ya pekee umuhusu mtu na hubeba maana katika maswala yale yote
yanayomuhusu mtu. Hapa ndipo tunapoweza kuona swala zima la imani likiwajibika
kutoa suhulu la mambo mengi yamuhusuyo mwanadamu. Je, katika maana hii ya
ufunuo wa Mungu, tweza badili dhamira ‘kweli’ ya Mungu katika mpango wake juu
ya ukombozi wa watu wake? Jibu ni hapana!
Kadiri ya mang’amuzi ya
kijamii katika historia yake, mwanadamu huweza kuutafsiri uhalisia wa kitu kama
ajionavyo yeye na sivyo uhalisia wa kitu ulivyo. Hapa ndipo penye matatizo
makubwa, fujo, na uovu. Kuanzia hapa tunaweza kulielewa somo letu la leo kuhusu
sakata zima la Athalia aliyejitwalia ufalme pasipo matakwa ya Mungu na kwa
ajili ya watu na kupitia watu, na kile kitakachojiri kwa Yoashi ambaye ndiye
aliyekuwa mlengwa kwa ajili ya watu na kupitia watu. “Na
Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka,
akawaharibu wazao wote wa kifalme,” 2Fal 11:1. Utawala dhalimu utumia nguvu
nyingi sana kufifisha kweli inayoakisi dhamiri na matakwa ya watu. Hata pamoja
na ubatili na udhalimu kama huu, pasipo njia Mungu huifanya njia, 1Kor 10:13.
Hivyo, “Yehosheba, binti wa mfalme
Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni
mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba
cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa,” 2Fal 11:2.
Kadiri ya masimulizi, Yoashi mwana wa Ahazia aliwekwa katika mafisho haya kwa
miaka takribani sita, 2Fal 11:3. Hapa tunafundishwa kwamba, ‘kisichotoka kwa
Mungu hata kama kikilazimishwa kina mwisho wake wakati utimiapo. Na “Hata
mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa
walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya Bwana; akapatana nao, akawaapisha
nyumbani mwa Bwana, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme,” 2Fal 11:4. Huyu
Yehoyada ni kuhani, na yupo kwa ajili ya watu katika kweli na haki. Je,
makuhani wetu leo wanasimama katika kweli na haki au ndiyo njaa na unafiki
unaowasongo kila kikicha na kuisaliti kweli na haki? Kwa jamii yetu ya Tanzania leo sitashangaa
kwa njaa hii na unafiki huu kupata na kusikia ‘matamko mbadiliko kama kinyonga’
kutoka kwa makuhani wetu wa kimtindo. Hakika alichofanya Yuda Eskariote kumuuza
yule mwenye haki, Bwana wetu Yesu Kristo kwa vipande thelathini vya fedha, Mt
26:15, kinaendelea leo kufanywa na makuhani hawa feki na wa kimtindo.
Malengo
na hazma ya Mungu, mwanadamu hawezi kuizuia kwa uwezo wake. Na hivi ndivyo
ilivyokuwa kushindwa kwake Athalia. “Ndipo
(Yehoyada) akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda;
wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na
aishi,” 2Fal 11:12. Kuhani Yehoyada anatimiza kazi yake, na anakuwa nabii wa
wakati wake katika kuisimamia kweli na haki. “Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia,
majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye ye yote amfuataye
mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa Bwana,” 2Fal
11:15. Lengo la kuhani yeyote yule ni kuwa daraji kati ya watu na Mungu ambaye
watu wake uweka matumaini kwake. Kuhani kwa kutokuwa daraja katika hofu hii ya
Mungu ulipoteza na kuliangamiza kundi zima lenye unyofu na imani ya kweli kwa
Mungu. Hata hivyo jambo hili halikutokea kwa Yehoyada. Badala yake, “Yehoyada akafanya mapatano kati ya Bwana na
mfalme na watu, ili wawe watu wa Bwana; tena kati ya mfalme na watu,” 2Fal
11:17. Utawala wowote ule usio akisi sauti ya watu ambayo pia ni sauti ya
Mungu, “Vox populi vox Dei,” huwa mateso kwa watu, lakini ni kwa muda tu. Na
ndiyo maana baada ya miaka sita ya mateso, Mungu akawajibu watu wake. “Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia.
Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme,” 2Fal 11:20.
Ujumbe kwetu ni kwamba si vyema kulazimisha vitu hata pale kwa uwazi kabisa
watu wamelikataa jambo hilo, ila wewe kwa uroho wako wa madaraka na ubinafsi
wako wapenda kuwa kile kisicho akisi matakwa ya wengi. Mungu hachezewi hata
kidogo! Na usipowekaza kwa Mungu katika kweli na haki, basi jiandae kwa
uharibufu!
Wapendwa wana wa Mungu,
Injili ya leo kwa upekee wake, inakazia swala zima la kuwekeza kwa Mungu. Vyote
tulivyonavyo ni mali ya Mungu, Zab 24:1. Kilicho chako ni dhambi zake. Hivyo,
vipaji na karama tulizojaliwa lazima ziwe na mwono wa Mungu kwa faida yako
ukivitumia vyema, na kwa ajili ya watu wake. Utajiri huo uwe sababu ya kuufikia
ukamilifu ikiwa ndilo hitimisho lako. Kwa maana hii, vitu na mali tulivyokuwa
navyo huwa na maana tu kama furaha yetu imejengwa kwa kuyaona madhaifu yetu, na
kuishi kuelekea ukamilifu. Kwa hiyo vitu hivi havitakuwa ndio mwisho wa
mahangaiko yetu kwa uwepo wake kwa vyenyewe. Vitu hivi huwa uwezekano tu wa
kutufikisha katika ile furaha ya kweli. Yesu anatoa onyo na angalizo kuhusu
mali tuzifanyazo ndio kwisho wa kila kitu. “Msijiwekee
hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba,” Mt 6:19.
Mfano mzuri kwa hiki akisemacho Yesu, tazama wakati wanapofariki matajiri na
kuzikwa. Je, uzikwa na mali zao ambazo ndizo zilizokuwa sababu ya furaha yao?
Matajiri wengine hupendekeza kuzikwa na baadhi ya mali zao, na hata wengine
uenda mbali zaidi na kupendekeza kuzikwa na “vizima moto.” Je, mateso na moto
wa jehenam twaweza kuuzima kwa kutumia vizima moto hivi? Tunachopaswa kufanya
muda wote tuishipo hapa duniani ni kuwekeza katika uzima wa milele.
Kuwekeza
katika uzima wa milele ni kujitahidi kila siku ya maisha yetu kuishi katika
ukamilifu hata kama udhaifu upo. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu
wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Mt 5:48. Ukamilifu huu ni kuishi katika saburi
ya kweli. Ni kuishi maisha yampendezayo Mungu, licha ya udhaifu wetu
kibinadamu. Mungu katuumba wanadamu, na katika uwanadamu wetu ndivyo atakavyo
tukomboa. “Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu
bila kupungukiwa na neno,” Yak 1:4. Ndugu yangu unawekeza katika benki ipi hadi
sasa?
Wapendwa
niwashauri sote kwa wingi wetu tuwekeze katika “BUM,” yaani, Benki ya Uzima wa
Milele. Benki hii ina usalama kuliko benki zote hapa duniani unazoweza
kufikiria. Benki hii ndiyo anayoisema leo Bwana wetu Yesu Kristo, “jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu
kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi,” Mt 6:20. Je, ipo benki
hapa duniani yenye usalama kupita BUM?
Mt.
Agustino anasema, “Mioyo yetu haitulii mpaka itakapo tulia kwako Ee, Bwana.” Ni
kwa namna hiyo basi tunapowekeza ndipo unapokuwa mtima wetu. Ndipo ulipo moyo
wetu na mahangaiko yake. Ndipo palipo na hitimisho la yote tuyatarajiayo katika
safari hii iliyosongwa na giza nene mbele yetu. Hivyo, “hazina
yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:21. Ndugu yangu, chunguza
mwenendo wako mzima wa maisha. Chunguza vizuri na wala usijipendelee kwa lolote
kama kweli unataka kuenenda katika njia iliyo salama, haki, na kweli. Mungu
ametupa sote UFAHAMU na UHURU wa kumrudia au kumkana, na kuifuata njia iliyo
salama. Ufahamu na uhuru huu ndiyo taa ya mwili. Ufahamu na uhuru wetu ndilo
jicho la kutazama na kubaini mema na mabaya. “Taa
ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na
nuru,” Mt 6:22.
Ufahamu
na uhuru huu Mungu aliotupa tusipoutumia vyema hakika tunaangamia mchana
kweupe. Ufahamu na uhuru huu ni kama kisu. Twaweza kutumia kisu kukata mkate,
na twaweza kutumia kisu kwa kujiua au kuwadhuru wengine. Yesu anasema ni kwa
namna hiyo, “jicho lako likiwa bovu, mwili
wako wote utakuwa na giza,” Mt 6:23. Je,
wataka kutembea katika kiza hili la umauti milele yote?
Tumsifu Yesu Kristo!
“kwa
kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:21
Tusali:-Ee
Yesu Mwema na Kiongozi wetu, tukumbushe daima kuyafanya mapenzi yako na Baba
yetu wa mbingu kwa wale tuliopewa dhamana hiyo kama viongozi. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario