lunes, 20 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 12 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 12 YA MWAKA-C
Somo: 2Fal 22:8-13; 23:1-3
Zab: 119:33, 34, 36, 37, 40
Injili: Mt 7:15-20
Nukuu:
“Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali,” Mt 7:15

“Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya,” Mt 7:17

“Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri,” Mt 7:18 

 “Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema, Enendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya Bwana ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa,” 2Fal 22:12-13 

Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile,” 2Fal 23:3 

TAFAKARI: “Maisha yako ni dhamana.”

Wapendwa wana wa Mungu, ‘maisha yako hapa duniani ni dhamana.’ Maisha ni dhamana tunapo utafakari mfano ule wa talanta, Mt 25:14-28. Ni kwa mtazamo huo masomo ya leo yanatutaka tuyaone maisha yetu kuwa ni dhamana hapa duniani. Hapo ulipo yakupasa “kuwa zaidi” ya kile ulicho katika kweli, haki, na wema. Ni kwa mizania hiyo “kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mt 25:29. Kuyaona maisha kuwa dhamana ni kukubali kutojihesabia haki kwa chochote kile ufanyacho hata kama ni sababu ya furaha yako na wale wanaokuzunguka. Kwa maana nyingine ni kutokukubali kujilinganisha na vitu. Wewe kama mwanadamu, uliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na  ndivyo niaminivyo, umeumbwa ili uishi milele. Kuyaona maisha katika mtazamo huu ni hatua muhimu sana ya kuyaishi maisha huru katika unyenyekevu wa kweli.

Maisha huru na ya unyenyekevu wa kweli kamwe hayasukumwi na kile tulicho katika maana ya nafasi na madaraka tuliyonayo katika jamii. Ila ni maisha yenye utayari wa kusikia yasemwayo juu yako, na kusikia zaidi ya kusema. Ni maisha yanayosukumwa zaidi na tafakari ya ndani kwani kile tusichotaka kusikia mara nyingi ndicho tulicho. Huwezi kufika kule usipotaka kupasikia kama huna maisha ya tafakari ya ndani. La sivyo mambo yako na maamuzi yako yataongozwa na vionjo vyako na wale wanaokuzunguka ili mradi tu kuujenga uhusiano bandia na usiodumu.

Mfalme Yosia aliyetawazwa kuwa Mfalme akiwa na umri wa miaka minane, na kutawala kwa muda wa miaka thalathini na moja, 2Fal 22:1, hakuwa kama mtangulizi wake, yaani Baba yake. Mfalme Yosia alijaliwa masikio ya kusikia na kuyatafakari yale aliyoambiwa na wale waliomshauri ambao kwa hakika walikuwa na hofu ya Mungu kama kuhani mkuu wa wakati wake, yaani Hilkia. Mfalme licha ya mamlaka yake na nafasi yake hakuacha kuomba ushauri ili asimame daima katika kweli na haki katika utawala wake. Licha ya kuzirarua nguo zake za kifalme kama ishara ya kukiri udhaifu wake alipoambiwa ukweli juu ya hali yake, 2Fal 22:11, hakuishia hapo. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema, Enendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya Bwana ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa,” 2Fal 22:12-13

Licha ya nafasi aliyokuwa nayo mfalme alifahamu fiki mipaka yake kama mwanadamu kwamba hawezi kufanya yote kwa wakati wote. Na pale aliposhauriwa kwenda kinyume na matakwa ya Mungu hakuacha kufanya agano jipya tena na Mungu. Kiongozi asiyekuwa na hofu ya Mungu ni hatari sana. Mfalme Yosia hakuwa hivyo. Daima aliona uwezo na mipaka yake kama mwanadamu, na alitambua nafasi ya Mungu katika maisha yake, na wale aliopewa dhamana kuwaongoza. Na hivi ndiyo ilivyokuwa pale mambo yalipokwenda ndivyo sivyo,  Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile,” 2Fal 23:3. Wengi wa watawala wetu leo ni sawa na miungu watu. Kumgusa mfalme (viongozi wetu) leo katika kweli na haki katika mazingira yetu ni sawa na kuigusa mboni ya jicho la mamba. Hakika hutakuwa salama!

Katika injili, Yesu anatufundisha hali ya uhusiano wetu na Mungu ipasavyo kuwa. Kitu cha kwanza kabisa katika nyakati zetu, Yesu anatuwasa, kwa kusema, “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali,” Mt 7:15. Watu hawa waongo si kwenye nyanja tu za Imani/kidini, bali hata kwenye nyanja za kijamii. Maneno haya ya Yesu yanaujumbe mahususi hasa kwetu hasa pale tunapoona utofauti mkubwa kati ya kile asemacho mtu (aliyepewa dhamana na umma) na baada ya kukupiga mgongo kufanya tofauti kabisa. Watu hawa wameupata umaarufu wa haraka sana kwa kuihubiri amani midomoni mwao, ila ndani ya mioyo yao wamejaa chuki, visasi, na vita inayosubiri muda tu kulipuka. Tuwapima watu hawa kwa matendo yao kwa sababu, “kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya,” Mt 7:17. Kama historia yake imetawaliwa na wema na hofu ya Mungu, basi kile atuambiacho kitakuwa na mashiko. La sivyo ni sawa na kutegemea ndizi mbuvu kutoka kwenye mti wa limao. “Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri,” Mt 7:18. Mara zote mtu hutoa kile alichokuwa nacho. Huwezi kutoa kile usichokuwa nacho.

Ni kwa mantiki hii ya kutoa kile ulichonacho ndivyo kila mmoja wetu kaitwa kwa namna ya pekee kuishi wito wake hapa duniani. Ni katika kuishi hiki ulicho kwa ukamilifu na uaminifu wake kutakakompendeza Mungu. Tendo hilo litakuwa sababu ya neema zake kwako ili ufikie taji lile alilokuandalia yaani utakatifu wako. Kama wewe ni mlei, hulazimiki kuishi maisha ya kitawa au ukleri ili ufikie taji hili. Kaa pale ulipo kwa uaminifu, na hapo ndipo utakapo kutana naye. Hiyo ndiyo Galilaya yako (Mk 16:7). Kila mmoja wetu akae nafasi yake kwa uaminifu na hapo ndipo tutakapokutana naye. Maneno haya ya Yesu ‘mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri,’ yanatuashiria hukumu yetu ya mwisho. Kwa kuishi kwetu hapa duniani kila mmoja wetu lazima “awe zaidi.” Haupo hapa duniani kwa bahati mbaya. Yakupasa kuwa zaidi pale ulipo kadiri ya wito wako. Usipokuwa zaidi katika mema ujue kifuatacho ni kuhukumiwa milele. “Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni,” Mt 7:19. Je, wasubiri hali hiyo ikufike?

“Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri,” Mt 7:18


Tusali:-Ee Yesu Mwema, yakamilishe yote mema yaliyo ndani ya moyo na nafsi zetu kwa sifa na utukufu wako, na watu wako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario