sábado, 25 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 13 YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 13 YA MWAKA-C
Somo I: 1Fal 19:16b, 19-21
Zab: 16: 1-2, 5, 7-8, 9-10, 11 (K) 5
Somo II: Gal 4:31b-5:1, 13-18
Injili: Lk 9:51-62
Nukuu:
Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake,” 1Fal 19:19b 

Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea?” 1Fal 19:20 

 “wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa,” Gal 5:1b 

uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo,” Gal 5:13b 

 “Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine,” Lk 9:56 

 “Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62

TAFAKARI: “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kumi na tatu ya mwaka “C” wa Kanisa. Kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa anatualika tumtafakari huyu Mwana wa Adamu ‘ni nani kwetu kama wafuasi wake katika mwono wa Kanisa,’ na pili, Mwana wa Adamu ‘ni nani katika maisha yako kama mfuasi wake.’ Msingi wa haya yote mawili umejengwa katika imani ya kweli juu ya Kristo Yesu. Imani hii ndiyo kielelezo na namna tunavyochukulia ufuasi wetu. Mimi na wewe tunayo maswali ya kujibu kwa kina katika uhalisia huu wa Imani ya kweli, yaani, katika ufahamu wa kutosha, na wenye maana. Je, yatosha kukiri na kumfuata Yesu popote atakapo kuwa kama upepo na bendera? Je, katika ufuasi huo natambua mapaswa yake? Je, nipo imara na nitakuwa imara katika nyakati zote na hasa zile nyakati za sintofahamu? Ushirika wako hai na Kristo ndiyo salama na ponya yako. ‘Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa.’ Wokovu huu ambao ni bure kwetu na kusiko kwa mastahili yetu binafsi, unatagemea utayari wako.

Kadiri ya Injili ya leo, Yesu anampa angalizo mtu yule aliyekutana naye njiani na kusema yupo tayari kufuatana naye ko kote atakapokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58. Kwa maneno mengine Yesu anatuambia hakuna maslahi yo yote kibinadamu zaidi ya maisha ya umilele kutoka kwake. Kama ni swala la utajiri na kuwa na maisha mazuri siyo kipaumbele cha kwanza katika ufuasi wetu kwake. “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:9. Kazi yetu ya kwanza ni kuutafuta ‘kwanza ufalme wa mbinguni’ na mengine yote tutapewa kwa ziada na kadiri ya mahitaji yetu.

Jambo la pili na la muhimu tunalofundishwa leo kuhusu Imani ya kweli na ufuasi usio na mawaa ni ‘utambuzi wa kweli na kujua nafasi ya Mungu katika maisha yako.’ Bila shaka wengi wetu tuna hofu ya kifo. Hata hivyo, kifo kipo pale pale tupende au tusipende. Na kama umezaliwa basi ipo siku utakufa. Kuzaliwa si lazima, bali kufa ni lazima kama umezaliwa. Kwa hiyo katika mantiki hii ya kifo na uhalisia wake, hatupaswi kukiogopa. Yatupasa kuishinda hofu ya kifo ili tuwe tayari kukipokea kifo kama njia pekee ya maisha yale baada ya kifo hapa duniani, kuishi umilele. Hakutakuwa na maisha ya umilele baadaye bila kupita katika fumbo hili la kifo.

Hivyo Yesu anamtoa hofu ndugu yule aliyetoa hoja ya kwenda kwanza kumzika Baba yake ndipo amfuate. Naye Yesu anamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu,” Lk 9:60. Je, Yesu anatukataza kuwazika wazazi wetu? La hasha! Kufanya hivyo angekuwa anaenda kinyumbe na ile amri ya nne ya Mungu, “waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12. Yesu anachotaka kukuambia wewe na mimi leo ni kwamba, kifo ni ‘kweli isiyopingika na hivyo shughuli zake na mazingira ya yake, isiwe sababu ya kutokupokea ujumbe wake wa uzima wa milele.

Na jambo la tatu na la mwisho tunalofundishwa leo kuhusu Imani na ufuasi thabiti ni ‘kule kuwa na msimamo thabiti wa wito ulio nao na kutunza kile ulichoitiwa.’ Hii ni pamoja na kutokuwa ndumilakuwili au kigeugeu cha kutaka ‘kutazama au kurudi nyuma ulikotoka kwa malengo ya kujaribu tena.’ Bali lipaswalo ni kujenga uaminifu na utayari wa kutimiza kile ulichoitwa na kukubali bila shuruti kwa sifa na utukufu wake Mungu. Na hicho ulichoitwa na kukubali kwa hiari yake kiwe mwitikio chanya hasa pale linapojitokeza swala ya huduma kwa watu au umma. Wengi wetu baada ya kubatizwa tumerudi kuishi maisha ya kipagani kabisa. Na wengi katika kundi hili wamekuwa washirikina wa kupindukia na kuongozwa na nguvu za giza ili hali wamejivika visakramenti mwili mzima. Ushirikina ‘ni kuamini nguvu fulani kutoka kitu fulani kisicho na uhusiano kimantiki.’ Katika hili Yesu anatupa angalizo, na kusema, “Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62. Kwa maneno mengine ni heri kuwa baridi au joto, kuliko kuwa vuguvugu katika Imani.

Ni katika mwono huu wa kuipokea habari njema ya wokovu wetu, tunaona mshabiano wa maneno ya Yesu na kile alichokifanya Elisha. Elisha kuwa Nabii kulikuwa hivi; Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake,” 1Fal 19:19b. Hizi ndizo ishara au alama zinazotusogeza kwenye kiapo. ‘Ndiyo’ ya Elisha ilikuwa hivi; Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi,” 1Fal 19:20ab. Na ‘ndiyo’ ya Elisha inakuwa ‘ndiyo kweli,’ pale Elisha alipoinuka, akamfuata Eliya, akamhudumia, 1Fal 19:21b. Tendo hili ndilo nililolisema hapo juu kwamba, ‘kujenga uaminifu na utayari wetu wa kutimiza kile tulichokubaliana kwa sifa na utukufu wake Mungu, na hasa pale linapojitokeza swala ya huduma kwa watu au umma.’ Je, kusema tu na kuwa tayari inatosha? La hasha! Wapo Wakristo kati yetu wao ni ‘imani tu inatosha,’ na wapo wengine wao ni ‘kulihubiri neno tu inatosha.’ Kuwa mfuasi wa Kristo kwa kufanya moja ya hayo mawili utakuwa bado hujalifikia lengo na sababu ya ufuasi wako. Kumbe yote mawili yanaitajika na mwisho wa siku yawe chachu ya wewe kuzaliwa upya katika maana ya kuushinda ubinadamu wako ili kuuvaa utu upya kila siku, yaani, utakatifu. Na hili ndilo analotuambia Mtume Paulo leo kwamba,  “wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa,” Gal 5:1b. Kongwa la utumwa ni kuurudia ubinadamu wako katika hali ya upofu, hali ya giza, na kukosa nuru halisi ya Kristo Yesu. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Na wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:9, 12-13.

Kumbe kama asemavyo Mtume Paulo, uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo,” Gal 5:13b. Huwezi kubagua au kujibagua kama kweli una upendo wa kweli. Upendo wa kweli ni  msukomo wa wazi na utayari wa kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu kwa nuru ile ya Kristo iliyoko ndani mwako. Upendo huu ndiyo tunao uona kwa wale wamisionari wa kwanza waliokuwa tayari kwenda wasipopajua kuifikisha habari njema ya wokovu kwa watu wote.

Ni katika mantiki hii ya upendo kwamba sheria hukosa nguvu na wakati mwingine kutohitajika au kuonekana kama upendo wa kweli unatawala maisha ya watu. Na anaye mjali mwenzake na kuwa tayari kutenda jema kwa ajili yake, haki utawala ndani ya moyo wa watu huyo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako,” Gal 5:14. Huku ndiko kuenenda kwa roho na kuvithibiti vilema vya miili wako, ikiwa ni pamoja na tamaa zake, Gal 5:16. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka,” Gal 5:17. Lakini dereva wa maisha yako akiwa Roho wa Mungu, utaruhusu ndani yako moyo usio na ubaguzi na kujitoa kwa upendo bila kujibakiza. Na huu ndio ukweli kwamba, tukiongozwa na Roho hatupo tena chini ya sheria, Gal 5:18 

Devota, Mkatukumeni aliyekuwa anajiandaa kwa Sakramenti ya ubatizo, wiki tatu kabla ya kuipokea Sakramenti ile, yeye na wenzake walipata nafasi ya maongezi na Baba Paroko. Kwa vile kundi hili lilikuwa la watu wazima, Baba Paroko aliwashauri na kusema, “endapo unajua kwamba unaishi uchumba ni vyema kuliweka jambo hilo wazi na ikiwezekana siku ya ubatizo huu Mama Kanisa akaadhimisha pia Sakramenti ya ndoa.” Wote wakaangua kichoko huku wakimtazama Devota.

Baba Paroko alimtazama Devota na kumuuliza, “kuna uhusiano wowote wa kicheko hiki na nilichosema juu ya maisha yako?” “Hapana Baba Paroko,” Devota alijibu huku akiangalia chini.  “Kama unaishi uchumba ni vyema ukaliweka wazi jambo hili ili tuweze kukusaidia zaidi.” Baba Paroko alisisitiza. Devota alikataa katu katu kama anamchumba na wanaishi uchumba. “Baba Paroko hawa wananisingizia tu na wanacheka kwa wasilolijua,” Devota alisema kwa ukali.

Na mwisho Baba Paroko alimwambia Devota, “ikiwa kuna ukweli katika jambo hili, Roho wa Bwana atalidhihirisha kabla ya kuipokea Sakramenti hiyo ya Ubatizo.” Basi baada ya hayo, Paroko alitoa baraka na wote wakatawanyika kila mtu nyumbani kwake.

Siku tatu kabla ya adhimisho la Sakramenti hii ya ubatizo, mapema asubuhi, Baba Paroko aliletewa taarifa ya ‘mwanaume mmoja kufia chumbani mwa Devota Mkatukumeni. Na Devota hajulikani alikokimbilia.’ Ndugu yangu, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58


Tusali:-Ee Yesu uliyekimbilio letu, kwako na itoshe. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario