JUMANNE WIKI YA 10 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 17:7-16
Zab:5:2-3, 4-5, 7-8
Injili: Mt 5:13-16
Nukuu:
“Eliya
akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza
mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao,” 1Fal 17:13
“Kwa
kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala
ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya
nchi,” 1Fal 17:14
“Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika
itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na
watu,” Mt 5:13
“Vivyo
hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema,
wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16
TAFAKARI: “Bwana Mungu huwaifadhi na kuwasitiri wote wamwaminio.”
Wapendwa wana wa Mungu, Mungu hudumu katika uaminifu wake katika
umilele wote. Hii ni moja ya sifa ya Mungu, kwamba uaminifu wake ni wa milele. “Kama sisi hatuamini,
yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:13. Na
huu ndio wito wa Bwana wetu Yesu Kristo anaotutaka tuwe, yaani, wakamilifu kama
Baba yetu wa Mbinguni alivyo mkamilifu, Mt 5:48. Hivyo uaminifu kwa Mungu ni
jambo muhimu sana katika imani na yale yote tuyafanyao kila siku ya maisha
yetu.
Nabii Eliya ni mfano wa kuigwa wa wale
waliomwamini Bwana bila kujibakiza, na
mwisho wa siku Mungu aliwasitiri katika shida zao. Eliya akiwa mgeni na
asiyefahamika vizuri kwa mjane yule wa Sarepta. Hata hivyo, Eliya anamwaminisha
mjane huyu kuliweka tumaini lake lote kwa Mungu licha ya uhaba ule wa chakula. “Eliya
akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza
mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao,” 1Fal 17:13. Hakika
kwa kiasi cha unga na mafuta kilichobaki kiliwatosha tu kwa siku moja. Hata
hivyo Eliya Nabii anatumaini kubwa sana kwa Mungu aliye hai. “Kwa
kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala
ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya
nchi,” 1Fal 17:14. Hii ni imani ya kweli na iliyo hai. Mungu wetu siyo Mungu
aliyebaki tu kwenye historia na matukio mazuri yaliyokwisha tokea, bali yu hai
hata sasa, na tunapomtafuta katika kweli na haki anapatikana, Isa 55:6. Matokeo
yake, “Lile pipa la unga halikupunguka,
wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa
kinywa cha Eliya,” 1Fal 17:16. Mungu kamwe hachoki kuwasitiri wale wote
wanaoweka tumaini lao kwake. Nabii Eliya kwa upande mwingine anatufundisha tuwe
vielelezo hai vya Mungu kwa wale wasioamini na kusadiki uwepo wa Mungu katika
maisha yao.
Wapendwa
wana wa Mungu, Injili ya leo inatupa mifano miwili ya kuwa vielelezo vya Mungu
aliye hai, na wakati huo huo kutoa ushuhuda wa kweli wa maisha yetu ya kila
siku. Vielelezo hivyo ni kuwa chumvi na nuru. “Ninyi
ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?
Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu,” Mt 5:13. Chumvi kwa
matumizi ya kawaida mbali na kuwa
kikolezo cha kuleta ladha nzuri ya chakula, ilitumika kuvihifadhi vyakula ili
vitumike kwa muda mrefu. Ili kidumu kwa muda mrefu, chakula kama nyama na
samaki vilisowekwa chumvi, na hivyo havikuweza kuharibika. Chumvi katika mantiki
hii na hasa katika somo hili la Injili imetumika kama mfano halisi katika
maisha ya kijamii. Mimi na wewe ili tuwe kikolezo katika kujenga ushawishi wa
maisha yenye malengo yatupasa kuchanganyika na watu. Tunaweza tu kuyajua maisha
ya watu pale tunapochanganyika nao na kuwa sehemu ya maisha yao, kwa lengo la
kuwasaidia kutoka katika hali zao duni na huzuni zao. Lengo hili lisipofikiwa
chumvi kama chumvi haina faida yoyote, zaidi ya kutupwa nje na kukanyagwa na
watu, Mt 5:13b
Kielelezo
cha pili katika kutoa ushuhuda wa kweli wa maisha yetu ya kila siku ni kuwa
nuru ya ulimwengu. “Ninyi
ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:14.
Kimaadili yatupasa kuwa nuru. Nguvu ya kimaadili ni ushawishi mkubwa sana wa
watu kutii na kufuata yale tunayowaongoza wayafanye. Nuru ni ushindi katika
giza. Na nuru ni kinyume cha giza. Maendeleo ya watu kwa namna yoyote ili ni
tokeo la ustaarabu wao. Haya ndiyo maadili ya watu katika kuona na kutenda.
Pasipo ustaarabu, maadili pia huwa ovyo. Kwa maana nyingine, palipo na
utaratibu pana akili. Nuru ambayo ndiyo maadili, ustaarabu, na kielelezo cha
ufahamu wa watu, yaani, akili, ni kitu cha kupewa kipaumbele. “Wala
watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo
yawaangaza wote waliomo nyumbani,” Mt 5:15. Watu wengi hupatwa na mshangaa pale
kunapokuwepo na msuguano kati ya kile akisemacho mtu, na ustaarabu wake yaani,
maadili aliyokuwa nayo. Mwenye maadili mazuri, husukumwa na kutawala namna ya
sema yake. Mtu wa mtindo huu uchagua maneno la kusema kadiri ya hadhira yake,
na somo kusudiwa kwa watu husika. Kwa maana nyingine, mtu huwa na uchaguzi wa
maneno ya kusema. Ni kwa maana hiyo kwamba, “Vivyo hivyo nuru yenu
na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu
aliye mbinguni,” Mt 5:16. Nuru ya mtu ni nguvu ya maadili ya mtu, ambayo ni
kama nijamu. Ni vigumu kummiliki farasi katika mwendo kama hauna nijamu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Ninyi
ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?
Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu,” Mt 5:13
“Vivyo
hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema,
wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16
Tusali:-Ee
Bwana Yesu Kristo, nifanye kikolezo halisi pale nitakapo kuwa, na kuwa mfano
halisi wa nuru yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario