domingo, 26 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 13 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 13 YA MWAKA-C
Somo: Amo 2:6-10, 13-16
Zab: 50:16bc-17, 18-19, 20.21, 22-23
Injili: Mt 8:18-22
Nukuu:
kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya mwenye upole,” Amo 2:6b-7a

 “nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha,” Amo 2:8

Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako,” Mt 8:19

Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake,” Mt 8:20

TAFAKARI: “Uongozi ni wito na dhamana. Ni kutumika na siyo kutumikiwa.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni kosa na dhambi ya jamii-‘social sin,’ pale unapotumia nafasi uliyonayo na cheo ulichonacho kuzikanyaga haki za raia wenzako kwa manufaa yako binafsi. Mmomonyoko huu wa maadili amboa ndiyo picha halisi ya nyakati zile za Nabii Amosi, hauna tofauti sana na jamii yetu leo. Ukijaribu kuitazama jamii yetu leo walio na nafasi ya kutoa huduma katika jamii kwa na kwa mujibu wa sheria na mamlaka waliopewa, wamekuwa watu wa ‘ujanja ujanja’ hivi. Kila mwenye nafasi hiyo kwa lugha iliyozoeleka tungesema wamekaa ‘kidili dili.’

Kwa mtizamo huu wa “kidili dili,” wanyonge ambao ndio wengi kwao kilio hakina ukomo. Uovu na uonevu kwa wanyonge ni kitu ambacho Mungu kamwe hatokivumilia. Sote tunamastahili sawa mbele ya Mungu licha ya tofauti zetu kihali. Mungu kwa kupenda kwake yeye mwenyewe aliona inafaa kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Hata hivyo, wanyonge kwa wingi wao leo wanatumika kama daraja-“uwezekano” la walionazo (matajiri wachache), wanasiasa, na watu wengine wenye ushawishi katika jamii, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa dini ili kufikia malengo yao binafsi. Mzaburi anatuambia, “heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu,” Zab 41:1. Watu hawa wasio na uchungu na wanyonge baada ya kuyafikia malengo yao huwasahau wanyonge na huwatumikisha na hadi tone la mwisho.

Jamii inapofikia hali na mazingira kama haya, kuna hitaji kubwa sana la ‘sauti ya wasio na sauti,’ yaani, mtu au taasisi yenye uwezo wa kuona uovu kama ulivyo, kuukemea kwa vitendo, na kuyaponya majeraha kwa kutoa mwanga mpya na njia mbadala kuelekea tumaini la kweli na hai. Wote wale waliovunjika moyo na kuumizwa katika hali kandamizi katika jamii, lazima wajengewe tumaini la kweli na yenye mabadiliko chanya. Nabii Amosi alikuwa ‘sauti ya wasio na sauti’ wa nyakati zake. Naye aliuona uovu na kuusema kama ulivyo. Naye hakusita kusema, wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya mwenye upole,” Amo 2:6b-7a. Ukitaka kujua ukweli huu katika jamii yetu leo, rejea vipindi vyote vya kampeni na mazingira yote ya chaguzi uliyokwisha yashuhudia. Je, ni wangapi wananunuliwa? Wakati mwingine kwa gharama ya sahani ya wali na maharage!

Leo swala la maadili kwa viongozi wa ngazi zote, na kwa namna ya pekee katika familia zetu limeporomoka sana. Tuelewe kwamba familia zisipokuwa na msingi imara kimaadili ikiwa ni pamoja na msisitizo wa kuuchukia uovu, tusitegemee kuwapata viongozi malaika ilihali viongozi hao ni tunda la familia hizi zisizo na maadili na hofu ya Mungu. Nyakati za Nabii Amosi ‘mtu na baba yake waliweza kumwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina la Mungu ambalo ni Takatifu,’ Amo 2:7b. Je, leo hatuna matukio kama hayo? Ni mara ngapi tunasikia binti akijigamba bila kuwa na mshipa wa aibu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Baba yake mzazi?

Hali hii ya maadili mabovu haikuwa tu kwenye maswala ya kijamii, bali ilikwenda hata kwenye maswala ya kiimani. Waliotegemewa kuwa mfano, yaani, ‘viongozi wa kidini,’ walitumia nafasi yao vibaya wakiutazama zaidi ubinafsi wao. Watu hawa waliokosa hofu ya Mungu walijilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha,’ Amo 2:8. Je, vituko kama hivyo vimekoma leo katika jamii yetu? Leo ipo mifumuko mingi ya imani za ajabu ajabu, na kufanya kuchipuka ‘vikanisa’ vingi katika jamii yetu. Ni vyema tukatafakari maneno haya ya Mtume Paulo; “Na roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu,” 1Kor 14:32-33. Hapa ndipo tunapoona uongozi kama wito na dhamana.

Hili ndilo analolizungumzia Yesu katika Injili ya leo. Wito na kuitika wito si swala la kumfuata Yesu popote aendapo, bali kujua nini maana ya kumfuata Yesu, na matakwa yake. Kumfuata Yesu kadiri ya injili ya leo ni “KUACHA” utaratibu, mitazamo, na matamanio tuliyoyazoea ambayo ni kinyume na kile tulichoitiwa. Kauli ya kutangaza nia ya kumfuata Yesu ni rahisi sana kama anavyojinadi mwandishi huyu, na kusema, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako,” Mt 8:19. Akilijua hilo ni jambo rahisi kutamka kama nia, Yesu anamjibu mwandishi huyu, “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake,” Mt 8:20. Kwa maana nyingine Yesu anataka kumwambia jambo hili: je, upo tayari kuyaacha mazuri haya ya ulimwengu na ufahari wake wote,  na kuwa tayari kutaabika na kudharauliwa kwa sababu yangu? Hapa ndipo tunaposhindwa wengi. Ni sawa na kusema, “utawa naupenda, ila ufukara siupendi.” Ni sawa na kusema, “maisha ya ndoa nayapenda, ila uzazi na malezi sipendi.” Huu ni mchanganyo wa hali ya juu.

Kumfuata Yesu Kristo inamaanisha kujibadua kutoka katika mnaso wa mazoea, au uhasili. Hapa yatupasa kujipanga vizuri katika hatua hii. Wengi tumeshindwa kujibandua kutoka mnaso wa kiasili tuliokuwa nao kutokana na uhasili wa maisha yetu kama tokeo la historia yetu (mila na desturi zetu). Hakuna kati yetu aliye kisiwa wala aliyedondoka kama mana jangwani. Sote tumetoka katika familia, na familia hizo zinaushawishi mkubwa kuhusu hatma ya maisha yetu ya kila siku. Ila leo Yesu anasema JIBANDUE KUTOKA JELA HIYO.  Mnaso huu utupelekea kujiuliza moja ya maswali haya ya kifamilia tunayoyaishi kila siku. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu,” Mt 8:21. Ni hekima na busara kwenda kuwazika wazazi na hata kuwahudumia hadi siku ya mwisho ya maisha yao kadiri ya amri ya nne, “waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,  upate heri, ukae siku nyingi katika dunia,” Efe 6:2-3. Ila Yesu anatupa jibu la uhakika tunapoamua kumfuata. Yesu anasema, “nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:22.” Hatukatazwi kuwazika wazazi wetu, bali tunaonywa kuwa “mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria,” Gal 5:18. Je, ndugu yangu wewe unaongozwa na nini?

Tumsifu Yesu Kristo!

Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake,” Mt 8:20


Tusali:-Ee Yesu Mwema na Mchungaji wetu, tuonyeshe njia ya uzima. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario