ALHAMISI WIKI YA 12 YA MWAKA-C
Somo: 2Fal 24:8-17
Zab: 79:1-2, 3-4a, 4b-5
Injili: Mt 7:21-29
Nukuu:
“Yekonia
alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi
mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani
wa Yerusalemu,” 2Fal 24:8
“Akafanya
yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake,” 2Fal
24:9
“Si kila mtu
aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye
afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21
“Wengi
wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina
lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?” Mt 7:22
“Ndipo
nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao
maovu,” Mt 7:23
TAFAKARI: “Alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si
kama waandishi wao.”
Wapendwa wana wa Mungu, masomo
ya leo na hasa somo la Injili, linatutafakarisha mambo makuu mawili. Moja,
‘onja moyoni yale utamkayo mdomoni.’ Na pili, ‘tambua kile kisukumacho maisha
yako.’ Tukianza na hili la kwanza, ‘onja moyoni yale utakayo mdomoni,’ Yesu
anasema, “Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21. Maneno maneno
tu hayatoshi. Yatupasa kuyaishi maneno hayo na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha
yetu. Hapo ndipo penye ufalme wa mbinguni. Kati yetu wapo mabingwa wa kuapa na
wakati mwingine kulitaja jina la Mungu kama ndege yule kasuku. Kumbe yatupasa
kulisikia neno na kulitenda. Kwa kufanya hivyo twaonyesha tu watu wenye ufahamu
wa Mungu, na yale yote tuyafanyayo msingi wake utakuwa imara daima. La sivyo
tuwe tayari kwa karipio hili ya Yesu siku ile ya mwisho, “Sikuwajua ninyi
kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu,” Mt 7:23. Kumbe tuonje moyoni yale
tutamkayo mdomoni.
Hakuna kitu chochote
kitakacho weza kutuyumbisha kutoka kwenye imani hiyo kama kabla ya kutamka kitu
tunakipa tafakari ya pekee. Kwa maana hiyo “Basi
kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye
akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa
maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25. Twaweza kulifanya jambo
hili kama tutaonja moyoni yale tuyatamkayo mdomoni. Fikiri kwa kina na sawa
sawa kabla ya kutamka lolote mbele za watu, na zaidi kama una dhamana juu yao.
Watu wengi wanamshangaa
Yesu mafundisho yake kwa sababu mamlaka yake yamebebwa na maadili yake. Nguvu
ya kimaadili ina kina kirefu kuliko nguvu itokanayo na mamlaka nyingine, mfano;
kisiasa. Nguvu ya kimaadili huja yenyewe kwa kujionyesha nje kadiri ya tabia ya
mtu ilivyo jengwa, njema, na yenye kulenga mara zote katika ukamilifu licha
kwamba udhaifu upo. Waliomzunguka Yesu wanapigwa na butwaa “kwa
maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao,”
Mt 7:29. Je, huyapima maneno yako kabla ya kuyatamka?
Ndugu zangu katika Kristo, jambo la pili katika masomo yetu
ya leo, ‘tambua kile kisukumacho maisha yako.’ Kitu hicho ndicho kinachotakiwa kuwa na
mamlaka juu ya maisha yako. Kwa maneno haya ya Yesu, “Si kila mtu
aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni,” Mt 7:21a, ni
mizania tosha ya kupima kile kisukumacho yale tuyafanyayo au utamkayo. Kwa
maana nyingine unaweza kuwa mbwekaji mzuri sana kwa kuwapendezesha watu wanaokuzunguka
kwa kuwaaminisha pasipo kumaanisha, ukawa kama mbwa anayebweka usiku kucha
kumwaminisha tajiri yake kwamba ulinzi upo imara kumbe ni woga wa miluzi ya
upepo.
Mfalme
Yekonia aliyeanza kutawala akiwa na umri wa miaka kumi na nane, 2Fal 24:8a,
hakujifunza kutoka makosa ya Baba yake, na hivyo naye akawa chukizo machoni pa
Bwana kama alivyofanya Baba yake, 2Fal 24:9. Mfalme Yekonia aliendeleza yale
yale ya Baba yake bila kujali hitaji la wale aliokuwa anawaongoza. Huu ndiyo
udhaifu wa kuridhishana utawala na mamlaka kama ilivyo kitu cha mila na desturi
tena zisizo badilika. Ni kukosa picha pana ya ukweli wa jambo kwa kukubali na
kuendelea kujifungamanisha na mtindo ule ule hata kama hauna tija na maono
chanya kadiri ya hitaji na wakati. Ni kutazama maslahi makubwa kwa kundi dogo
la watu wanao neemeka mfumo huo wa utawala, ingawa wetu wanateketea. Kwa upande
mwingine ni kutokuwa tayari kujifunza kutoka historia ambayo maisha ya watu leo
na sasa ni tokeo lake. Mtazamo na mazingira ya mtindo huu ndivyo ilivyokuwa
rahisi kwa Taifa hili ya Israeli kudondoka mara kwa mara katika mikono ya
maadui zao. Mataifa yaliyowazunguka yaliufahamu udhaifu wao kwa sababu waliijua
historia vizuri. Mfalme Yekonia baada ya kuzidiwa hakuwa na ujanja zaidi ya
kujisalimisha mwenyewe chini ya utawala wa mfalme Nebukadreza wa Babeli kama
mateka katika mwaka wa nane wa utawala wake, 2Fal 24:12b
Tawala
nyingi zisizopenda kubadilika kutokana na hitaji la wakati ikiwa ni pamoja
maono pevu kuelekea kule wasipokujua ila wanapatamani, huwa mwanzo wa anguko
lao. Taifa linaweza kuwa huru, yaani, uhuru wa bendera ila halina nguvu licha
ya rasilimali lilizo nazo. Mali na utajiri wake uchukuliwa kwa mlango wa nyuma
na mataifa majanja yanayoenda na mabadiliko na hitaji la wakati, ikiwa ni pamoja
na maono pevu, yaani, sera sahihi za uchumi wa wakati husika. Na hivi ndivyo
ilivyokuwa katika Taifa la Waisraeli (ambao kwa sasa ni mateka-Babeli) chini ya
utawala wa mfalme Yekonia,
“Akatoa huko hazina zote za nyumba
ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya
dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana,
kama Bwana alivyosema,” 2Fal 24:13. Mfalme huyu akupoteza tu rasilimali vitu,
bali pia rasilimali watu ambayo ndiyo iliyokuwa
nguzo ya taifa na msingi wa
vyote. Mfalme wa Babeli,
Nebukadreza, “Akawachukua
mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu
kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa
wanyonge wa watu wa nchi,” 2Fal 24:14. Hili lilikuwa pigo kubwa sana kwa Taifa
hili la Israeli. Tukiacha haya ya kijamii,
kisiasa na utamaduni, embe kwa sasa tuzame ndani zaidi kwa haya ya kiroho. Kwa
upande huu wa maisha ya kiroho, Yesu anatupa angalizo kwamba, ni yule tu “afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni
(Mungu) ndiye atakayeingia katika ufalme wa mbinguni.” Mt 7:21b. Je, kufanya mapenzi ya Mungu kunamaanisha
nini?
Wapendwa wana wa Mungu, kufanya mapenzi ya Mungu ni “kukaa
katika pendo” la Mungu. “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na
kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na
Mungu hukaa ndani yake,” 1Yoh 4:16. Ni kuwa tayari kuongozwa na mamlaka ya Mungu
katika mfumo wa Upendo. Tunakaa katika upendo wa Mungu kwa kuyatimiza mapenzi
yake pale tu tunapolipokea neno lake, tunapolisoma neno lake, tunapolifanyia
tafiti neno lake, tunapolikumbuka neno lake, na tunapolitafakari neno lake.
Haya mambo matano ni muhimu sana kama tunataka kweli kukaa naye na kuyafanya
mapenzi yake. “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya,
atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha,
mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana
misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25. Hakuna awezaye kutung’oa
kwenye mwamba huu wa imani hata kikija kimbunga cha tsunami.
Tusipo lishika neno la Mungu vizuri tutakuwa
tayari kuongozwa na mamlaka hizi; mila
zetu
(kwa kufanya yale yanayotutia hofu bila kuhoji
sababu yake), desturi zetu (kwa
kufanya kadiri ya mapokea ya wazee wetu katika hali ya upofu), hisia zetu (kwa kufanya kadiri ya
miyeuko yetu na siyo utashi wetu). “Na kila asikiaye
hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba
yake juu ya mchanga; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka;
nalo anguko lake likawa kubwa,” Mt 7:26-27. Hakika kwa hali hii tunabaki kuwa
kama bendera fuata upepo. Na kwa sababu hiyo, kila ajitokezaye na kutushawishi
hatutakuwa na nguvu ya kuimili vishindo vya imani kwani tu wepesi kama pamba.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Akafanya
yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake,”
2Fal 24:9
Tusali:- Ee Yesu Mwema,
tuongoze kwa lililo jema tukitambua kwamba maisha yetu hapa duniani ni jukumu
la muda mfupi, hivyo tutumie vyema wakati na nafasi tuliyo nayo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario