JUMAPILI YA 12 YA MWAKA-C
Somo
I: Zek 12:10-11
Zab: 63: 1-5, 7-8, (K) 1
Somo
II: Gal 3:26-29
Injili:
Lk 9:18-24
Nukuu:
“Nami
nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema
na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama
vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake,
kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza,” Zek 12:10
“Siku
hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya
Hadadrimoni katika bonde la Megido,” Zek 12:11
“Kwa
kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu,”
Gal 3:26
“Hapana Myahudi
wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana
ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu,” Gal 3:28
“Akawaambia,
Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa
Mungu,” Lk 9:20
“Kwa kuwa mtu
atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake
kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24
TAFAKARI: “Nao watamtazama yeye ambaye walimchoma. Maana
ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kumi na mbili ya mwaka “C” wa Kanisa.
Tafakari yetu ya leo yatutaka tuzame katika fumbo zima la ‘Neno kufanyika mwili
na kukaa kwetu,’ Yoh 1:14. Neno huyu ndiye kielelezo chetu, matumaini yetu, na
ukomo wa ufunuo wa Mungu Baba Mwenyezi kwetu. Hivyo tutamfikia Mungu Baba
Mwenyezi kwa kupitia Mwanaye, yaani Yesu Kristo, kama Kristo mwenyewe
anavyothibitisha kwetu kwamba, “Mimi ndimi
njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6.
Kristo kama njia, kweli, na uzima, asili yake katika maana ya lengo lake hapa
duniani ni ‘wokovu wa kila kiumbe,’ binadamu akipewa nafasi ya pekee, Mwa 1:27.
Hivyo
lengo hili-wokovu, Mungu alianza kulifunua tangu kuumbwa kwa ulimwengu, na hasa
kwa manabii wake, na kwa namna ya pekee leo kupitia Nabii Zakaria kama
tulivyokwisha kusikia katika somo letu la kwanza, yaani, “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa
Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma;
nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao
wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya
mzaliwa wake wa kwanza,” Zek 12:10. Ndugu yangu, hiki ndicho kilichotokea siku
ile ya Ijumaa Kuu. Tendo hili la Ijumaa
Kuu ndiyo utimilifu wa wakati ambapo Mungu alisema sasa inatosha kwa watu
wangu. Mtume Paulo anasema, “Hata
ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke,
amezaliwa chini ya sheria, kusudi
awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa
wana,” Gal 4:4-5. Uwana huu wa Mungu, unatuweka sawa mbele za Mungu kwa kuwa
Mungu aliona inafaa na hivyo kutuhesabia haki kwa sadaka ya Mwanaye Mpenzi pale
Msalabani. Hivyo, “Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi
nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu,” Gal 3:28. Umoja wetu huu siyo umoja usiokuwa
na malengo. Ni umoja uliojengwa mwa msingi thabiti wa Imani ndani na katika
Kristo Yesu kama kielelezo chetu hai, “Kwa
kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu,”
Gal 3:26. Je, nini maana ya maneno haya;
“Nao watamtazama yeye ambaye walimchoma?”
Wapendwa
wana wa Mungu, manane haya ya Nabii Zakaria, ‘watamtazama yeye ambaye
walimchoma,’ unabii huu ulikamilika tunaposoma Mwinjili Yohane 19:28-37. Hakika
ulimwengu ulipata maombolezo na kimya kikuu kama alivyotabiri Nabii Zakaria,
kwamba, “Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama
maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido,” Zek 12:11. Na hivyo ndivyo
ilivyokuwa kadiri ya tafsiri ya maneno haya ‘watamtazama yeye ambaye
walimchoma,’ tunapotafakari sehemu hiyo, Yoh 19:29-37.
Yohani Mtakatifu anaunganisha tukio la kifo
cha Yesu na kutukuzwa kwake. Yesu anaonyeshwa akiwa anaiendea saa yake, ndio
saa ya kutukuzwa kwake, kwa kifo, ufufuko na kupaa kwake Mbinguni. Anamwonyesha
Yesu anatoka kwa Baba na anarudi kwa Baba.
Yesu anapokufa msalabani anatoa roho yake,
anatupa roho huyu aliyempokea wakati anaanza kazi yake, aliposema, “Roho wa
Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena,
Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk
4:18-19. Yohani anaunganisha tukio la kifo cha Yesu, tukio la msalaba na
Pentekoste. Pale msalabani Yesu anatoa roho wake, nasi tunampokea kutoka ubavuni
mwake tunapopokea sakramenti zake, “damu na maji”, katika Kanisa
lake. “Lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka
damu na maji,” Yoh 19:34
Sisi tunapobatizwa
tunampokea roho huyu wa Kristo, Roho Mtakatifu. Anatufanya kuwa wana wa Mungu
na wana wa Kanisa. Kwa sakramenti ya Kipaimara, Roho Mtakatifu anatufanya kuwa
askari hodari wa Yesu Kristo kwa njia ya mapaji yake saba tunayopokea. Kuwa
tayari kutoa ushuhuda juu ya Yesu. Na tunafanya hivyo na kuwa hivyo kwa, “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo
mmemvaa Kristo,” Gal 3:27. Ni katika
Kanisa tunapewa karama ya Roho Mtakatifu. “Na Mungu ameweka wengine katika
Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza,
kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za
lugha,” 1Kor 12:28. Anatoa karama mbalimbali kwa wafuasi wa Kristo.
Karama hizi ni kwa ajili ya manufaa ya Kanisa lote, ingawa zinaweza kuwa na
msaada kwa aliyepewa. “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa
kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine
neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye
yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine
matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine
aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote
huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama
apendavyo yeye,” 1Kor 12:7-11. Kanisa lina wajibu wa kupima kwamba karama
inapojitokeza kama kweli ni kutoka kwa Roho Mtakatifu. Kama si kutoka kwa Roho
Mtakatifu, hii si karama bali ni kitu kingine. “Basi pana tofauti za karama;
bali Roho ni yeye yule,” 1Kor 12:4
Kama wafuasi wa Yesu, tunapojaliwa karama na
Roho Mtakatifu, tunavutwa daima kumtazama yule waliyemchoma, yule tuliyemchoma.
Tukifanya hivyo karama na vipaji vyetu havitakosa kuwa vya manufaa kwa Kanisa
zima. Tunapomtazama tunatambua kweli tuna karama. Je, tutamtazama namna gani?
Katika Kanisa lake hasa anapotufundisha kwa njia ya neno lake alilowakabidhi
mitume, viongozi wa Kanisa ambao ndio wenye madaraka ya kututafsiria neno la
Mungu na karama mbalimbali katika Kanisa na kuona kama kweli ni karama au ni
hisia au maigizo au mahangaiko ya kisaikolojia n.k.
Karismatiki katoliki ni karama ya Roho
Mtakatifu katika Kanisa. Ni tofauti na karismati za kilokole na madhehebu
mengine au dini nyingine. Ipo hatari ya kuchanganya Karismatiki Katoliki na
hasa karismatiki ya kilokole. Siku hizi katika Karismatiki Katoliki wapo baadhi
yetu wanaoiga mambo mengi ya kilokole kama nyimbo, namna ya kucheza, namna
ya kuongea na kuhubiri, namna ya kusalimiana na kufurahi, namna ya uponyaji na
kukemea uovu n.k. Je, haya hapa kwetu hayapo? Si tu Karismatiki Katoliki
wamekumbwa na tamaa hii ya kuiga na kutumia mambo ya wengine, bali hata
wakatoliki wengi hutumia nyimbo, muziki, na hisia za kilokole katika tafrija,
sherehe, mikutano na semina zao. Kweli sisi wakatoliki tumechuja kiasi hicho
kwamba tulivyo navyo, mathalani nyimbo zetu hazigusi nafsi na hisia zetu? Kuna kila dalili ya kuweka vya kwetu chini,
au kuvichimbia na kukumbatia vya wengine na kuwasaidia kuvieneza hata ndani ya
Kanisa Katoliki.
Ni vizuri ieleweke kwamba, si dhambi wala
kosa kuiga jambo jema na zuri kutoka kwa mwenzako au jirani yako hata kama
mnatofautikiana kwa namna moja au nyingine. Hata hivyo tunapoyaiga hayo mazuri
kutoka kwa wenzetu, tumeitendea haki ‘teología,’ hasa jumbe za nyimbo
tunazoziimba? Pamoja na mambo mengi yanayobeba ‘teología ya kikatoliki,’ hili
ni dhahiri, yaani, jumbe za nyimbo hizo ni vyema zikabeba haya; Imani ya kweli,
tumaini la kweli, na Upendo wa kweli wa Mungu. Muhimu hapa ni ‘teología ibebayo
ujumbe ule unaoimbwa,’ na siyo namna waimbavyo, wachezavyo, na ishara au
viashiria wavitoavyo ikiwa vinamwelekea Mungu mwenyewe wanayemwimbia na
kumsifu. Zipo njia mbalimbali za kufikisha ujumbe ule ule mahususi kwa Mungu
kadiri ya mila, tamaduni, na desturi za watu. Mungu ufurahi tunavyojiachia
kwake kama tulivyo katika kumsifu, kumshukuru na kumwabudu. Mungu asingependa
tuwe kama ‘maroboti.’ “Basi, ndugu zangu,
nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai,
takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana,” Rum 12:1. Ni
ibada yenye maana, na siyo tu iliyobeba ufahamu, bali yote mawili, yaani,
ufahamu wa kile ukifanyacho, na umaana wake (Rationality and Significativity).
Hivyo wale wanaobeza kuwa Karismatiki kusali kwao na kuimba kwao ni kwa
kupayuka payuka kusikokuwa na maana yoyote, ni sawa na mtu anayepoteza muda
wake kumkemea chura kutoa kwake sauti akiitafsiri kuwa ni kelele. Je, kelele za
chura kama unavyozitafsiri haziufunui utukufu wa Mungu aliyemuumba chura huyo?
Jiulize! Je, nani kakuambia kusali kwako ndiko kuliko bora kuliko kwa wengine
wote?
Tufanyeje basi? Tuanze kumtazama yule
waliyemtoboa, tuliyemtoboa, ndio kutumia vile ambavyo kweli ni mapokeo sahihi
ya Kanisa na kuyaboresha tuliyonayo, yaani, kuyatamadunisha kwa mwanga wa
Injili yale yanayobeba tamaduni, mila na desturi zetu. Tutafanikiwa hili tukiwa
na ushirikiano sisi wenye, na viongozi halali wa Kanisa, tukiwatumia wataalamu
wetu [kwaya zetu, waalimu wa kwaya, makatekista wetu] na pia tukitumia vipawa
tulivyopewa na Mungu. Yapo mengi tunaweza kuiga toka kwa wenzetu yakatusaidia
lakini hii inahitaji umakini wa hali ya juu na ruhusa ya Kanisa kama
nilivyokwisha kusame hapo awali. Si kila mtu anajiamulia kitu chake na kukileta
katika Kanisa Katoliki, kuna utaratibu tangu enzi za mitume ambao unaongozwa na
Roho Mtakatifu. Kila mtu akileta utaratibu wake au kitu chake itakuwa ni fujo
na hakutakuwa na umoja ambao unaletwa na Roho Mtakatifu. Penye migogoro,
ubinafsi na hali ya kupenda kuwa juu ya mamlaka ya Kanisa, ambapo hakuna utii,
hakuna karama, bali kiburi na majivuno ndio vinatawala.
Wafuasi wa Yesu, tunapomtaza yule
waliyemtoboa, tuliyemtopoa/mchoma pale msalabani, sadaka ya Misa ambayo ni
sadaka ya Yesu msalabani, ni kiini, na kilele cha sala na ibada zetu zote.
Tuipe Ekaristi takatifu, Ibada ya Misa Takatifu nafasi ya pekee, kwani pekee
ndipo tunapokutana na kumtazama yule waliyemchoma, yule tulimchoma. Yesu ambaye
anatupa roho wake, ndiye chanzo cha karama na vipaji vyetu vyote. Kazi zetu,
ibada zetu, na sala zetu zituandae kuadhimisha Ekaristi takatifu, Misa Takatifu
na Misa Takatifu iwe chemchemi ya kutuhuisha, na kuhaisha karama na vipaji
vyetu.
Mama Maria ambaye alimleta huyu ambaye
tunamtazama, anatupa sisi na ulimwengu. Yeye hachoki kutuombea na
kutuletea zawadi za ukombozi. Maria alipata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu,
akawa hekalu la Roho Mtakatifu na hekalu la Mwana pekee wa Mungu, Tabernakulo
ya kwanza. Kama Mungu amempa heshima hiyo, kuwa mama wa Mungu, sisi hatuoni
ugumu kwani ni mama yetu. Anatuombea nasi tuwe mahekalu au Tabernakulo ya Roho
Mtakatifu na ya Mwanaye, kwa ubatizo na kipaimara kwa namna ya pekee.
Tutakuwaje tabernakulo la Roho Mtakatifu na Yesu, kama hatuna heshima
kwa mama yake? Kama hatuithamini Misa takatifu, Ekaristi takatifu
ambayo inawezekana na inafanyika kwa uwezo wa Roho Mtakatifu? Tutakuwaje
Tarbenakulo ya Roho Mtakatifu na Yesu, kama hatuna heshima na utii kwa Kanisa
lake, ambamo ndimo tunaweza kujua, karama za Roho Mtakatifu?
Hata hivyo yatupasa kumjua huyu Yesu ni nani kwetu. Yesu
alitaka kujua kutoka kwa watu na hata kwa wanafunzi wake wa karibu kabisa wanamtazamo
gani juu yake. Mtume Petro anatoa jibu sahihi kuhusu Yesu, na lile lililo mpasa
Kristo katika ulimwengu huu. “Akawaambia, Nanyi
mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,”
Lk 9:20.
Mpendwa unayesafiri nami katika tafakari hii nikuulize swali
la msingi; pamoja na majibu ya wengine, na hasa jibu alilolitoa Petro kuhusu
swali alilouliza Yesu, wewe binafsi Yesu kwako ni nani? Jibu la Petro kwa
tafsiri, Kristo yaani Masiha wa Mungu, ndiye yeye tu aliyewekwa katika mpango
mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Hivyo tutaiona mbingu na kuufurahia uhuru wa
kweli endapo tu tutakuwa tayari kushikamana na mwana huyu wa Mungu. “Yeye ndiye
jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la
pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina
lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,”
Mdo 4:11-12. Hivyo kufikia hatua hii la kuokolewa kwetu kupitia jina hili
hatunabudi kushiriki njia ile aliyopitia Bwana wetu Yesu Kristo kama
anavyowanong’onozea wanafunzi wake siri hii na kusema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na
wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka,”
Lk 9:22. Ndugu yangu hakuna PASAKA PASIPO IJUMAA KUU. Ndivyo hivyo kwetu kama
wafuasi wake Kristo tulio hai kwamba hakuna UTUKUFU PASIPO MSALABA.
Padre
Tomasi Songambele akiwa ofisini mwake, alipigiwa simu na mmoja wa viongozi wa
Jumiya ndogondogo kutoka moja ya kigango cha parokia yake. Ujumbe ule ulikuwa
ni taarifa ya mgonjwa aliyezidiwa na alihitaji huduma ya kiroho.
Baada ya
ujumbe ule wa simu, Padre Tomasi Songambele alionekana kutoka na kuingia
sakristia akiwa anatafuta kitu fulani. Mwisho, katekista aliyekuwa karibu,
alijaribu kujua nin hasa, na hivyo
alimuuliza, “Padre kulikoni, mbona wa ingia na kutoka, na unaonekana kuna jambo
linakusumbua?” Padre alimjibu, “natafuta chupa ya kubeba maji ya baraka!”
Katekista
alitabasamu na kumwambia, “Padre, wewe ni ‘PADRE,’ nenda huko kwa mgonjwa
utayafanya yote.” Wote walicheka, na Padre akasema huku akiondoka, “asante sana
Katekista, leo upo juu!” Padre akawasha gari na kuondoka. “Maana ninyi nyote
mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo,” Gal 3:27. Hivyo katika Kanisa kila
mbatizwa yampasa kujua nafasi yake, na kwa namna hiyo, mwili wa Kristo tukiwa
sisi ni viungo vyake, utakuwa na afya.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa
kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza
nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24
Tusali: Ee Yesu, nifanye kiungo chako hai
katika mwili wako, yaani, Kanisa. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario