KUZALIWA KWA YOHANE MBATIZAJI
24/6/
Somo I: Isa 49:1-6
Zab: 139: 1b-3, 13-14ab, 14c-15
Somo II: Mdo 13:22-26
Injili: Lk 1:57-66, 80
Nukuu:
“Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu,
enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo
la mama yangu amenitaja jina langu,” Isa 49:1
“akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika
wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3
“Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli
habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake,” Mdo 13:24
“Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani
mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye
mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake,” Mdo 13:25
“Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto
huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk
1:66
“Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani
hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli,” Lk 1:80
TAFAKARI: “Wewe si bahati mbaya.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake Yohane
Mbatizaji. Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kunajidhihirisha kama utangulizi wa
yale atakayoyafanya Kristo kama hatua ya mwisho ya kumkomboa mwanadamu. Kwa
maana nyingine, Yohane anatambulika katika Kanisa na hasa katika fumbo zima la
historia ya ukombozi wa mwanadamu kama msafishaji njia, mwandaaji njia, mtoaji
taarifa wa kile ambacho kitatokea. Yohane Mbatizaji anawaandaa watu kwa
kumpokea Masiha na Mwokozi wa wanadamu. Hivyo basi, tafakari yetu leo
utaongozwa na neno hili; “Wewe si bahati mbaya.”
Kuzaliwa
kwa Yohane Mbatizaji ni fumbo na muujiza wa pekee wa Mungu kwa wale
wamtumainio. Familia ya Zakaria na Elizabeth ilihuzunishwa sana kwa kukosa
mtoto kwa muda mrefu. Ila wakati ulipotimia Mungu aliyafanya yote kadiri ya
mpango mzima kwa ajili ya watu wake wote. Hivyo tendo hili la kuzaliwa kwake
Yohane Mbatizaji linadhihirisha maneno haya kwamba ‘hakuna aishiye ulimwengu
huu kwa bahati mbaya.’ Kama umezaliwa jua wewe ni wa pekee, na Mungu anampango
mkubwa sana juu yako, na ukombozi wa watu wake. “Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake,
wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa
maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi
kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena
kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia,” Rum 14:7-9. Ni mara
ngapi twajisikia vibaya wakati tunapopigwa na hali ngumu ya maisha hata
tunamtusi Mungu na kumuasi? Wewe si bahati mbaya!
Somo letu
la kwanza linaelezea umuhimu wa uwepo wetu katika dunia hii, na malengo yake. “Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi
kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la
mama yangu amenitaja jina langu,” Isa 49:1. Ndugu yangu, ungali bado hujazaliwa
Mungu kesha fahamu jina lako na makusudi yake. Tendo hili linajitokeza wakati
wa kumpatia jina Mtoto aliyezaliwa na Elizabeth. Jambo la ajabu wote wawili
yaani Elizabeth na Zakaria wanapendekeza jina “Yohane” licha ya kwamba hawakuwa
na mawasiliano kabla yake. Jina Yohane maana yake ni, “Mungu ndiye mwenye
Neema.” Ndugu yangu, Mtume Paulo anasema, “Lakini
kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si
bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni
neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10. Hatuna cha kujivunia kwa kile tulicho.
Kwa sababu hiyo, yapo mambo makuu matatu yatupasa kufahamu ili kujua makusudi
ya Mungu katika maisha yetu hapa duniani. Jambo la kwanza ni hili; kwa hali yo
yote nitakayokuwa nayo lazima nijipokee kwanza, na kwa namna hiyo ndivyo neema
za Mungu zitafanya kazi ndani yangu.
Pili,
Mungu hutupa majukumu ya kufanya hapa duniani. Hatupo hapa kushangaa shangaa na
kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Mtume Paulo anatoa onyo: “Maana
twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao
wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya
katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao
wenyewe. Lakini ninyi, ndugu,
msikate tamaa katika kutenda mema,” 2The 3:11-13. Tupo katika ulimwengu huu wa
malengo maalumu, na kupitia malengo hayo kazi ya Mungu hutendeka. Mungu anawaambia Waisraeli na anakuambia wewe
na mimi pia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli,
ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3. Mungu hutukuzwa tufanyapo vyema yale
tunayoyaishi kadiri ya wito wetu. Wakati mwingine hatutambui wajibu huu mkubwa
mbele ya Mungu kwa kuwajibika vilivyo kwenye tumishi zetu ndogondogo na wakati
mwingine zile zisizo julikana rasmi na jamii.
Mfano Mama lishe anayewahudumia wachimba mifereji pembezoni
mwa jiji. Yawezekana hakuna mwenye kuguswa na huduma hii hata kidogo. Ila
angalia wamama lishe hawa wanavyojituma na kudamka usiku wa manane kuandaa
watakavyovihudumu kwa siku. Faida waipatayo ni ndogo sana ukiliganisha na muda
wanaoutumia kuwahudumia vibarua hawa walio wanyonge kama wao. Hii ni neema ya
Mungu! Katika jambo hili Mungu anasema, “Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi
wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli
waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu
wangu hata miisho ya dunia,” Isa 49:6. Ndugu yangu, yale tujitoayo bila
kujibakiza katika utume wetu, ni nuru kwa watu wa Mungu, na kwetu ni wokovu wa
milele.
Ni kwa namna hii ya pekee, wakati ulipotimia Mungu anatupatia
Yohane Mbatizaji kama mwaandaaji wa yule atakaye hitimisha lengo la kuukomboa
ulimwengu huu kutoka utumwa wa dhambi. Huyu anayeandaliwa ni neno aliyefanyika
Mwili akakaa kwetu. Huyu ndiye Kristo. Yohane Mbatizaji anawaandaa watu kwa kuwahubiria habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake Bwana
wetu Yesu Kristo. “Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani
mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye
mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake,” Mdo 13:25. Je, twaweza kuwa
wanyenyekevu kama Yohane Mbatizaji? Je, tupo tayari kuwaandalia wengine
mazingira mazuri ya utendaji? Ni mara ngapi tunapokabidhiwa kazi twataka
kuharibu vyote tulivyovikuta na wakati mwingine tuondokapo twaharibu yote
tuliyoyafanya ili anayekuja asikute chochote? Je, hii ndiyo sababu ya uwepo
wako katika dunia hii? Wakati mwingine tuyafanyayo hayaendani na maisha na wito
wetu, na matendo hayo wakati mwingine ni heri yale ya kipagani kuliko sisi
tunayemjua Kristo.
Tatu,
tunapoishi hapa duniani maisha yetu yawe barua za kusomwa na wengine, na kwa
kupitia barua hizo wengi wapate wokovu. Maisha yetu yaamshe mvuto wa kumfahamu
Mungu na kupenda kuishi naye. Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji na maisha yake ni
kielelezo cha makusudio ya Mungu kwa watu wake. Hivyo, “Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto
huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk
1:66. Je, maisha unayoishi kuna viashiria vyovyote vya mkono wa Mungu? Kama
hamna ni vyema ukachunguza ukamilifu na uaminifu wa maisha unayoishi kadiri ya
wito wako. Kwa Yohane Mbatizaji jambo hilo lipo wazi kwa sababu tunaambiwa
hivi: “Yule
mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea
kwake kwa Israeli,” Lk 1:80. Ni vyema nijiulize swali hili: Je, hapa nilipo
kadiri ya wito wangu, ninakua, naongezeka nguvu rohoni, ninamatumaini ya
kukutana na Mungu kwa sadaka yangu hiyo niitoayo kila siku (katika jangwa hilo
la Maisha)?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani
hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli,” Lk 1:80
Tusali:-
Ee Mungu twasema asante kwa kutupa sababu ya uwepo wetu hapa duniani. Hatupo
kwa bahati mbaya. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario