viernes, 10 de junio de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU BARNABA MTUME

SIKUKUU YA MTAKATIFU BARNABA MTUME
11/6
Somo: Mdo 11:21b-26; 13:1-3
Zab: 98:1, 2-3ab, 3cd-4, 5-6
Injili: Mt 10:7-13
Nukuu:
 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli,” Mdo 13:1 

Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,” Mdo 13:2 

 “Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7 

Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8 

Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake,” Mt 10:9-10 

TAFAKARI: “Watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana.” 

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha kumbumbuku ya Mtakatifu Barnaba Mtume. Mtakatifu Barnaba anajulikana pia kama ‘Nabii wa wakati wake,’ ‘Mwanafunzi wa karibu wa njia ile ya Yesu,’ na ‘Mmisionari.’ Barnaba ni kati ya wale Wakristo wa kwanza kabisa wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo ya pale Yerusalemu. Barnaba ambaye hapo awali alijulikana kama Yusufu, alitoa mali zake zote na kuziweka chini ya Mitume. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume,” Mdo 4:36-37. Barnaba anatambulika pia kama binamu wa Marko, Kol 4:10. Barnaba na Paulo wanafanikisha vizuri sana Mtaguso ule wa Yerusalemu kama waleta taarifu juu ya uinjilishaji wao na mikwamo wanayokumbana nayo. Vile vile walitumika vizuri kama wapeleka taarifa- vyombo vya kupeleka habari za maamuzi yale ya Mtaguso wa Yerusalemu, Mdo 15:25, 35-37. Licha ya kutokuwa na uthibitisho wa wazi kwa jambo hili, Mtakatifu Tertulian katika maandishi yake anamtaja Mtume Barnaba kuwa ndiye mwandishi wa waraka ule kwa Waebrania. Hata hivyo Maandiko Matakatifu yanatueleza kutokea shida “mashindano” baina ya Barnaba na Paulo wakajitenga, Mdo 15:39. Kutokuelewa kwa Barnaba na Paulo kulitokana na Paulo kutopendezwa na kitendo cha Barnaba kumchukua Yohana alijulikana kama Marko, Mdo 15:38, kwa sababu ndugu huyu aliwaacha huko Pamfilia asiende nao kazini na kurejea Yerusalemu, Mdo 13:13. Na baada ya kazi ngumu ya uinjilishaji wa kina, kadiri ya mapokeo, mauti ya kifo dini kama shahidi wa Kristo yalimkuta Mtume Barnada huko Salamis-Cyprus mwaka 61 BK.

Baada ya historia hiyo fupi kuhusu Mtume Barnaba na mahusiano yake na Mtume Paulo, kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa anatutaka tutafakari mambo makuu matatu; moja, Msingi wa Kanisa la wana wa Mungu ulivyojengwa. Pili, wasifu wa Mitume na hasa Barnaba. Na tatu, maadili yahusuyo kazi hii ya kutumika kwa ajili ya wengine, maisha ya utume

Wapendwa katika Kristo, Msingi wa Kanisa la wana wa Mungu ulijengwa na Kristo Mwenyewe tunapoliangalia fumbo zima la mateso, kifo na ufufuko wake. Tukio la Ufufuko, na baadaye tukio lile la Pentekoste liliwapa nguvu ya ajabu Wakristo wa kwanza. Hawakuwa tena na woga wa kuhubiri habari njema za Ufufuko na uzima wa milele. Wakristo hawa walikuwa tayari muda wowote kwa lolote. Kadiri ya Maandiko Matakatifu na mapokeo ya Kanisa la mwanzo, kutawanyika kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo, kulitokana na kuhujumiwa kwa jumuiya hiyo, na hasa kile kifo cha Shahidi Stefano. Kwa upande mwingine, kupitia mateso haya, habari njema zinafika kila kona na wengi wanamwamini Mungu. Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao,” Mdo 11:19. Kutawanyika huku kwa jumuiya hizi za Wakristo tukienda mbali zaidi ni kutokana na sadaka ile ya pekee aliyoitoa Yesu pale msalabani. Hakika Damu ya Mwana-kondoo wa Mungu haikupotea bure. Damu hii imekuwa ‘ufunguo mkuu wa kufungua kila mahali kwa kulifukuza giza na kuuleta mwanga wa milele. Ni kwa kupitia sadaka hiyo hiyo nasi kwa kila mmoja wetu, Kanisa linakua na kuenea popote duniani.

Ni kwa namna hiyo tunapokuwa na Kristo katika nia na matendo yetu tunabarikiwa kwa sababu tuyafanyayo ni mwendelezo wa kazi yake ya kuikomboa dunia. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21. Hapa tunaona safari ya uinjilishaji ndiyo inaanza, na Kanisa katika maana ya kila Mbatizwa linakuwa Kanisa la Kimisionari. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia,” Mdo 11:22. Kazi hizi za kimisionari ndizo zinazolifanya Kanisa likue na kuenea kila mahali. Kazi hizi pia ndizo zinazo watambulisha wale wazifanyazo. Ni hapa Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi wa Yesu wanaitwa Wakristo. “Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia,” Mdo 11:26b. Kuitwa kwao huku ni kutokana na matendo yao kuendana na kile walichokuwa wakikiamini na kukihubiri.

Wapendwa wana wa Mungu, mtindo huu wa kimisionari unaitajika sana nyakati zetu hata leo. Matendo mema ndani ya Kristo na katika Kristo, umtambulisha Kristo pale ulipo; na kwa namna hiyo kwa ubatizo wetu wote tumeitwa kuwa wamisionari. Umisionari wa kutembea na vipasa sauti kwa sasa hauna nafasi sana. Tunaitaji umisionari wa matendo mema kwa watu wote. Kristo alishaanza kulifanya hili pale ambapo Wayahudi walitaka kupata uhakika kama kweli yeye ndiye Kristo mwenyewe. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia,” Yoh 10:25. Kazi azifanyazo Yesu ndizo zinazomthibitisha na kumtambulisha kuwa yeye ni nani. Ni kwa namna hiyo hiyo kwamba kazi tuzifanyazo kama wabatizwa na Kanisa kwa ujumla wake zitamtambulisha Kristo pale tulipo.

Jambo la pili katika tafakari yetu ya leo ni kuona wasifu wa Mitume na kwa upekee Mtume Barnaba. Mitume kwa ujumla wao walifanya uinjilishaji wa kina ikiwa ni pamoja na kuilinda imani ya kweli. Walikuwa tayari na kwa busara ya hali ya juu wakiongozwa na Roho Mtakatifu walitoa majibu sahihi kwa kile walichoulizwa au kutuhumiwa. Hivi ndivyo Mtume Petro alivyowasihi wenzake na leo kwa upande wetu, Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu,” 1Pet 3:15. Ni kwa mwono huo, Barnaba na Paulo wanakuwa mstari wa mbele kuhubiri habari njema ya ufufuko na uzima wa milele.

Barnaba na Paulo walifanya uinjilishaji wa kina popote pale walipokuwa au kwenda. Safari yao ya umisionari haikuwa rahisi kwani nyakati nyingine walipata upinzani mkubwa kutoka kwa Wayahudi na wale wasiomwamini Kristo.  Pamoja na kutokukubalika kwa Mtume Barnaba, Paulo, na wenzake kutokana na ujumbe waliokuwa wakiutoa ikiwa ni mwendelezo wa kazi ya Kristo, wanakimbilia Listra na Derbe kupata hifadhi. Mtume Barnaba na Paulo wanafanya mambo makuu kwa mkono wa Mungu, na kuleta tafrani kubwa. Tendo hili la uponyaji wa mtu mwenye udhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, linaibua hisia za watu hawa wa Likaonia na kuwaona Paulo na Barnaba kama miungu ya kuabudiwa. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji,” Mdo 14:11-12. Hakika, tendo hili ni moja ya mambo hatari sana katika utume wetu. Ukiona hali hii ndani mwa watu inajitokeza na kuacha kumwabudu Mungu na kuanza kukuabudu wewe kama mchungaji wao, ujue wazi ufanyacho si matakwa ya Mungu bali shetani amechukua mkondo wake. Ni ukweli usiopingika kwamba, tunastahili pongezi kwa yale tuyafanyayo na hata wakati mwingine kuthaminiwa hasa kwa kuitambua kazi tunayoifanya. Ila mtazamo na mwelekeo huu wa kuthaminishwa na kutambulika kwa yale tuyafanyayo usichukue kamwe nafasi ya Kristo na Mungu. Ufahamu huu ndiyo unaotupeleka sasa tuangalie sehemu ya tatu, yaani, maadili yahusuyo kazi hii ya kutumika kwa ajili ya Kristo na wengine.

Hivyo kwa kutambua kasoro ya kutaka kufanywa miungu watu, Mtume Barnaba na Paulo wanatoa angalizo kwa Walikaonia na kusema, “Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe,” Mdo 14:14-16. Hatari kubwa katika jambo hili ni kwamba, binadamu anapoukataa ubinadamu wake, anajeuka kuwa mbaya kuliko shetani, kwani shatani alishaukubali ushetani wake pale alipomwasi Mungu.

Ndugu yangu, usipompa Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yako chochote kile chaweza kuyaongoza maisha yako, na mwisho wake ukawa mbaya kwa sababu kitu hicho kama kilivyo hakina umilele. Maadili ya Mbatizwa yeyote yule ni kuwahubiria watu habari njema ya wokovu na ufalme wa Mungu. Yesu anasisitiza jambo hili na kusema,Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7. Tumeumbwa tuishi milele, na duniani hapa siyo makao yetu ya kudumu. Tupa hapa kwa maandalizi tu huku tukijua maisha ya hapa duniani ni jukumu la muda mfupi. Kila mmoja kadiri ya wito na karama zake, yampasa kutumia vyema karama hizo. Kwa namna hiyo Yesu anatoa wito na kusema, Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8. Pamoja na wajibu huu, Yesu anatoa angalizo pia kuhusu tatizo la kushikamana na mali za dunia hii. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake,” Mt 10:9-10. Kuambatana na mambo haya na kuyapa nafasi ya kwanza upunguza hari na kasi ya kuyatimiza yale tupasayo kufanya.

Ni vyema pia tukawa waangalifu kwa wale watukaribishao na kutupatia ukarimu wao na hifadhi. Maisha ya kutangatanga pasipo mwelekeo sahihi ni hatari sana kwa uchungaji na umisionari kwa ujumla wake. Hivyo Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka,” Mt 10:11. Ni vyema kufanya kile kilichokupeleka pale, na fanya hicho tu. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi,” Mt 10:12-13. Tatizo kubwa hutokea pale tunapobadili nia na sababu ya kuwa pale tulipopaswa kuwa. Tatizo hili ni sawa na “kubadili gia angani ilihali hujui utaangukia wapi kwa maamuzi hayo.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake,” Mt 10:9-10

Tusali:-Ee Yesu, tujalie moyo wa kimisionari pale tulipo. Amina.


Mtakatifu Barnaba Mtume, utuombee.

No hay comentarios:

Publicar un comentario