domingo, 5 de junio de 2016

TAFAKARI: JUAMATATU WIKI YA 10 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 10 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 17:1-6
Zab: 121:1bc-2, 3-4, 5-6, 7-8
Injili: Mt 5:1-12
Nukuu:
Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu,” 1Fal 17:1 

Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani,” 1Fal 17:2-3 

Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito,” 1Fal 17:6

 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu,” Mt 5:11 

Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:12

TAFAKARI: Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, sehemu kubwa ya maisha ya mwanadamu hapa duniani ni kutafuta maana ya maisha yake, na kuipata ile furaha ya kweli. Binadamu huyu ulifanya jambo hili anapoitazama historia yake kama somo kwa lengo ya kuyarekebisha yale ambayo hayakwenda vyema kwa wakati huu aishipo sasa, ili kule aendapo asipokujua vizuri kuwe na tumaini. Hivyo, somo la Injili ya leo kwa upana wake linaelezea hali halisi katika mahangaiko ya mwanadamu, na ulimwengu juu tunaoishi. Na kwa kulisema hilo, Yesu leo anatutaka tuzitafakari kwa kina heri hizo alizozisema, Mt 5:3-12.

Lakini ili tuifikie furaha ile ya kweli ambayo hiyo ndiyo lengo halisi, hatuna budi kuufahamu ulimwengu huu tunaoishi leo. Bila kuujua ulimwengu huu ambapo ndipo tunapoishi, ni vigumu pia kuiona furaha ile ya kweli inayoendana na malengo ya kuumbwa kwetu. Mimi na wewe tumeumbwa ili tuishi milele. Kwa ufupi na kwa kina, Yesu anatupa siri ya hali halisi ya ulimwengu huu tunaoishi leo. Naye anasema, Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Pamoja na mazingira kama haya, na tunaposimama kwa lile lililo kweli na haki, Kristo hatotuacha kamwe. Ni katika kweli hii Mungu anamwahidia Nabii Eliya uhai mbele ya safari ambao kwa akili ya kibinadamu ni vigumu kuamini. Naye Mungu anasema, Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito,” 1Fal 17:6. Ni kwa sababu hiyo Yesu aliyatoa maisha yake, ili mimi na wewe leo tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi na uovu wake wote. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Hivyo tuitafutapo furaha hiyo ya kweli hatuna budu kujua hali ya ulimwengu wetu tunaoishi kama alivyotufunulia Bwana wetu Yesu Kristo. Je, tunafanye nini sasa?

Jambo la kufanya ni kuziishi heri alizotuambia Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo. Katika tafakari hii sintozipitia heri hizo moja baada ya nyingine, bali niwatake tutafakari heri hizo kwa kuyatazama mambo makuu manne ambayo kwa kiasi fulani yanasema juu ya maisha yetu ya leo. Mambo hayo ni kama yafuatayo: Kwanza, kuwa na nafasi ndani ya moyo wako. Pili, hapo ulipo fanya zaidi na achana na mazoea. Tatu, hapo ulipo kuwa mzalendo kwa kujipokea, kuwapokea wengine, na kuipigania jamii yako-Taifa lako. Na nne, kuwa alama na kielelezo hai cha amani ya kweli hapo ulipo.

Wapendwa wana wa Mungu, tuanze na hili la ‘kuwa na nafasi ndani ya moyo wako.’ Huwezi kuwa na furaha ya kweli kama hakuna nafasi ya Mungu ndani ya maisha yako. Hofu ya Mungu ndani yetu ni mizania ya kujipokea kama tulivyo, na kutufanya tujitahidi kufika pale ambapo tunapatamani. Itakuaje basi kufanya hivyo kama huna nafasi ya Mungu ndani yako? Kuwa na nafasi ndani ya moyo wako, Yesu ameizungumzia katika Injili ya leo kwa mtindo huu, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3. Ni umaskini huu wa roho, yaani, kuwa na nafasi ya Mungu ndani yako, kutakao kupeleka katika furaha ile ya kweli, yaani, ufalme ule wa Mbinguni baada ya kuvishinda vita hivi hapa duniani. Haya ndiyo maisha yale ya umilele kama lengo halisi la kuumbwa kwetu, yaani, tumeumbwa tuishi milele.

Pili, ‘fanya zaidi na achana na mazoea.’ Hakuna saratani mbaya katika maisha ya mtindo wowote ule, pale unapofikia hatua ya kuridhika na kila kitu, na kuacha mambo yaende tu kama yalivyo, kwa vigezo kwamba kama juzi na jana ilikuwa hivyo, basi hata leo na kesho itakuwa hivyo hivyo. Mwenendo huu wa maisha ni mwendo wa ‘kufa pole pole’ huku ukiona. Kumbe kuishi maisha yenye malengo ni kufanya zaidi ukijua siyo kwa sababu ya ubinafsi wako, bali kwa ajili ya wengine kwa sasa na hata vizazi vijavyo. Mtume Paulo anatufafanulia vizuri kuhusu kweli hii na kusema, Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake,” 1Kor 10:24. Na tutakuwa tunafanya hivyo siyo kwa kuutafuta utukufu binafsi, bali kuifikia tumaini lile ambalo kila mmoja wetu bila kujali historia yake, itikadi zake, familia au kabila, anatamani kuipata. Kwa Mkristo na mfuasi wa Kristo aliye hai hufanya hivyo akijua ukweli huu kwamba, “hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:7-8. Hivyo ndugu yangu, kulifikia tumaini hili yakupasa wewe na mimi kuwa na njaa ya tumaini hilo. Ni katika mazingira haya Yesu anasema, Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa,” Mt 5:6. Je, hali ipo vipi hapo ulipo? Jamii inayokuzunguka inatenda haki nawe ukiwa mmoja wapo? Kama hilo halipo itakuwaje basi uwe na furaha ya kweli? Changamoto hii ni yangu na yako pia. Tuwe na njaa na kiu ya haki. La sivyo hatutaweza kushibishwa, yaani kuwa na furaha ya kweli.

Tatu, hapo ulipo ‘kuwa mzalendo’ kwa kujipokea, kuwapokea wengine, na kuipigania jamii yako-Taifa lako. Ndugu yangu, mizania ya haki na kweli, ipo ndani ya usafi wa moyo wa mtu. Kuna msemo wa kifalsafa usemao kwamba, “mtu hutoa kile alichokuwa nacho.” Hivyo huwezi kutoa kile usichokuwa nacho. Lakini naweza kuifikia mizania hii ya usafi wa moyo kwa kufanya hatua hii muhimu sana katika maisha yangu, yaani, kujipokea kama nilivyo. Hapa simaanishi tu kuyaona mazuri yako na mabaya yako ukaridhika nayo na kutokufanya chochote. Wito wa kila mmoja wetu ni kuwa wakamilifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo makamilifu, Mt 5:48. Kama hili ndilo lengo msingi la maisha na malengo yangu, sinabudi kuurekebisha udhaifu wangu ili kuufikia usafi ule wa moyo kila siku ya maisha yangu. Hii siyo kazi ya siku moja.

Jambo hili, yaani, ‘kujipokea’ likichukua mkondo wake sawa sawa, mengine hufuata, yaani, kuwapokea wengine, na kuwa tayari kwa maslahi mapana ya jamii inayokuninguka, na Taifa zima. Huu ndio uzalendo tunaouzungumzia hapa, yaani, fanya yote kwa ajili ya wengine kwa kulitazama tumaini lililo mbele yako na kwa wote. Katika kweli hii, jambo hili litawezekana kama Yesu anasemavyo, Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu,” Mt 5:8. Ni katika moyo ulio safi utofautisha namna ya kufikiri kwetu, kuamua kwetu, na kutenda kwetu. Mlolongo huu ndiyo ule unaotupatia cheo chetu halisi, yaani, utakatifu wako. Hivyo tutamwona Mungu tu tukiwa na cheo hiki, yaani, Utakatifu kwa sababu Mungu wetu ni Mtakatifu.

Na nne, ‘kuwa alama na kielelezo hai cha amani ya kweli hapo ulipo.’ Ni moyo safi huo ambao utuwezesha kuona kitu kama kilivyo, na kusema kama kilivyo, ili kibaki kama kilivyo katika hali yake daima. Tatizo kubwa hapa mara nyingi mimi na wewe huvaa miwani ya ‘tulivyo,’ na kupoteza uhalisi wa jambo au kitu kama kilivyo. Miwani hii ya ‘tulivyo,’ yaweza kuwa itikadi zetu kisiasa na kidini. Miwani hii ya ‘tulivyo inaweza kuwa pia familia zetu, koo zetu, na makabila yetu. Kwa mtindo huo, tutawezaje kuwa wapatanishi wa kweli? Ndugu yangu, tunapoambatana na mambo hayo kwa kushikamanana nayo ou kung’ang’ania nayo kama yalivyo, twajisababishia upofu wa kudumu. Ni vyema mimi na wewe tukatoka katika boksi hilo na kupata mwanga halisi wa kuona vizuri ukweli wa kile tukitazamacho. Huku ndiko kuwa ‘wapatanishi’ kama asemavyo Yesu, Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9. Mungu yu mpatanishi wetu katika maana nzima ya Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Ni upananisho huu ambao kilele chake kilikuwa kifo cha Mwanaye Mpenzi pale msalabani, ambacho kifo hicho kilituhesabia haki kuwa wana na warithi wa ufalme wa Mungu. Hivyo leo mimi na wewe tunapokuwa wapatanishi tunamwakilisha Mungu kama watoto wake. Na huu ndio uwana wa Mungu, yaani, kuwa mpatanishi pale ulipo.

Mambo yote manne tuliyoyaona hapa juu yanahitaji sadaka. Sadaka ya kwanza ni kujikatalia nafsi yako mwenyewe ili uwe na mizania ya kweli na haki katika yale yote utakayokutana nayo kwa kufikia malengo ya mambo hayo manne. Somo la kwanza leo linatupa kweli hiyo kwa mfano wa nabii Eliya. Aliyaona mambo kama yalivyo na kuyasema kama yalivyo. Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu,” 1Fal 17:1. Sadaka uitoayo ina maana kwa sababu mbele kuna heri na tumaini. Kielelezo cha heri hiyo na tumaini ni Kristo mwenyewe. Mateso na majaribu lazima tutakutana nayo katika safari hii. Kwa msisitizo mkubwa Yesu anasema, Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Kuna furaha kubwa sana moyoni kuhukumiwa kwa sababu tu umetenda haki na kuishuhudia kweli. Haya ndiyo maisha ya ushuda hasa katika nyakati zetu hizi tunapoona na kushuhudia ubabaishaji kila kona.
Tumsifu Yesu Kristo!

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu,” Mt 5:11


Tusali:-Ee Yesu, furaha ya kweli ni pale ninapokufia katika kweli na haki. Nipo ujasiri ya kukijongea kifo hicho. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario