martes, 31 de mayo de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 9 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Tim 2:8-15
Zab: 25:4-5ab, 8-9, 10, 14
Injili: Mk 12:28-34
Nukuu:
Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9 

Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13 

 “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Mk 12:28b

 Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote,” Mk 12:29-30 

Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:31

Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo,” Mk 12:34 

TAFAKARI: Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.” 

Wapendwa wana wa Mungu, mwanadamu kwa kuumbwa kwake, Mwa 1:27, na uwepo wake hapa duniani, mara zote hutafuta maana ya maisha yake. Hufanya hivyo si kwa bahati mbaya, au udadisi fulani, bali kama alivyo, mwanadamu ni tokeo la historia  yake na kijamii na jamii anayoishi leo na sasa. Hivyo, mwanadamu huyu hapo alipo kadiri ya imani na maadili yake, hakosi kuifikiria kesho ambayo bado kuiishi akiwa na matumaini kuwa ipo. Na kama ni Mkristo achoki kuyafikiria maisha yale ya umilele na hukumu yake ya mwisho, kwa sababu anatambua wazi maisha ya hapa nduniani ni jukumu la muda mfupi tu. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya,” 2Kor 5:10

Kwa hali na mtazamo huo, mwanadamu hakosi kutafuta maana ya maisha yake. Utafutaji wa maana juu ya maisha yake humpa pia maana ya mahangaiko na mateso yake. Katika hali hii Mtume Paulo anasema, Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9. Neno la Mungu ni hai, na pia ni uhai. Tulisadiki neno kama alivyofanya Diwani yule wa Kana ya Galilaya, Yoh 4:46, mwanaye aliyekuwa hajiwezi, naye akapata uponyaji. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia,” Yoh 4:50 

Maisha yakikosa maana, binadamu hujikabidhi katika ‘ovu’ lolote lile bila kujali chochote kwa sababu maisha yake kesha yahesabu kuwa si chochote. Huku ni kutaka tamaa pale tunapokosa tumaini la kweli. Ila kwa upande wa Mtume Paulo ni tofauti. Yesu Kristo ndiye nahodha wa maisha yake, na kwake, yaani kwa Kristo, maisha yake (Paulo Mtume) yamepata maana halisi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13. Huyu ndiye Kristo ambaye kwake kama wafuasi wake, kuna tumaini la kweli.

Hata pamoja na ukweli huo, Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli,” 2Tim 2:15. Ndani na katika Yesu Kristo hakuna sababu ya kuishi kwa hofu. Mmoja wa waandishi ili kupata uhakika na kuiondoa hofu yake, anamuuliza Yesu, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Mk 12:28b. Swali hili ni la msingi kabisa, ingawa yawezekena muuliza swali alifanya hivyo ili kujiridhisha na pengine kujua ameegemea upande upi. Ni vizuri pia kujihakiki kama kweli unatembea njia iliyo salama. Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote,” Mk 12:29-30. Jibu la Yesu linamkumbusha muuliza swali kuwa yeye ni tokeo la historia yake, na hivyo historia hiyo ina nguvu katika maisha yake.

Yesu hakuishia hapo tu, bali anaenda mbele zaidi ile muuliza swali afahamu vizuri ubinadamu wake. Maisha huwa na maana unapoishi tumaini la kweli, yaani, kuelekea ule umilele ambalo ndilo lengo kwa yeyote yule aishie duniani hapa. Naye Yesu anamwambia,  Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:31. Kumbe mimi na wewe siyo tu tokeo la historia yetu, bali pia masisha ya kijamii tunayoishi kila siku. Hapa duniani hatuishi kama visiwa. Mahusiano yetu (ya haki, kweli, usawa, upendo) na wenzetu utujenga kimaadili na imani, na hivyo kutufanya kukua kiroho. Huu pia ni mtihani muhimu sana wa kujipatia taji lile la gharama kupita mataji yote, yaani, utakatifu wako. Bila hili kuiona Mbingu na Mungu ni ndoto! Kuhusu historia yake, na mahusiano yake na wenzake, mwaandishi yule alijibu vyema, Mk 12:32-33. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo,” Mk 12:34. Ndugu yangu, wewe na mimi tuutafakari umbali wetu na ufalme ule wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo,” Mk 12:34


Tusali:-Ee Yesu Mwema, nijalie ufahamu wa kuona maana ya maisha yangu kila siku licha ya changamoto nazokumbana nazo kila kukicha. Amina

lunes, 30 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 9 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Tim 1:1-3, 6-12
Zab: 123:1b-2ab, 2cdef
Injili: Mk 12:18-27
Nukuu:
Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana,” 2Tim 1:3

Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9

 “Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao,” Mk 12:18-19

Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni,” Mk 12:25 

TAFAKARI: “Kuna furaha ya kweli na heshima kuifia ‘kweli na haki’ kwa wajinga ili waijue kweli na haki, kuliko kufa kama mfalme kwa pongezi na makofi ya wapumbavu wadhanio kuijua ‘kweli na haki ilhali hawaijui na wao wenyewe hawajijui.’”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kuwa Mkristo kwa kubatizwa tu haitoshi. Leo kuwa Mkristo kwakuitaji kuwa mpiganaji halisi wa Kristo kama Mfalme wa haki, kweli, upendo, unyenyekevu, huruma, msamaha, na uwazi. Ulimwengu uliojaa dhuluma, ufisadi, na matendo ya uvunjifu wa haki za binadamu, hauwezi kamwe kuukubali Ufalme wa Yesu Kristo kama nilivyosema. Leo tulio wengi, yaani Wakristo, tumewekwa katika kikaangio cha kukubaliana na mtazamo huo (dhuluma, ufisadi, na uvunjifu wa haki za binadamu) au kuukataa kwa gharama kubwa sana hata kuutoa uhai wako. Hakika njia iliyo rahisi na isiyo na mawaa ni kuusaliti Ukristo (kumkana Kristo) wako kwa gharama nafuu kama alivyofanya Yuda Eskariote kwa vipande thelathini vya fedha. Ndiyo maana leo wale tuliotegemea waseme na kuukemea uovu wapo kimya, na wale waliojaliwa ufahamu wa kupembua mema na mabaya wamekuwa wasaliti wa iliyo kweli na haki.

Ndugu yangu unayesafari nami katika tafakari hii, kuwa Mkristo leo ni changamoto kubwa sana, kama ilivyokuwa kwake Yesu Kristo kuutangaza Ufalme wa  Mungu kwa Wayahudi kwa kauli mbiu yake ile, yaani,  “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Jamii ya Yesu wakati ule ilikuwa kama ndoto kuupokea ujumbe huu-kutubu na kuiamini Injili. Je, katika hali hii, Yesu alirudi nyuma katika hili kwa vigezo vya kutokukubalika? La hasha!

Kwa kuushindilia msumari wa moto katika kusisitiza na kumaanisha asemacho, Yesu aliwapa wapinzani wake silabasi ya utendaji wake kwa miaka ile mitatu. Naye anasema juu ya utendaji wake kama ifuatavyo na itakavyokuwa: Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Silabasi hii ndiyo iliyokuwa hatma ya kifo chake kila cha aibu, yaani, kifo cha Msalaba. Msukumo wa kifo hiki ni Upendo na furaha ya kweli katika haki, kwa kujua kile akifiacho siyo kitu cha kubumba bali ndio ukweli wenyewe. Yesu anakuwambia wewe na mimi,  Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Bwana wetu Yesu Kristo amelifanya hili, nasi kama wafuasi wake ni changamoto kubwa kwetu leo. Hakika Kristo amekupenda wewe na mimi upeo, na kwa sababu hiyo alikuwa tayari na yupo tayari hadi sasa kufa kwa ajili yako na mimi. Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1. Kwa nini basi Mkristo mwenzangu unakuwa na imani ya mwono wa chura? Hivi leo nikikuuliza uniambia ukweli kuhusu Chura ‘kama amesimama au kachuchumaa waweze nipa jibu sahihi? Kigugumizi hiki cha kujua mkao wa Chura, ndicho kigugumizi juu ya imani ya Wakristo wengi wa leo.

Wapendwa wana wa Mungu, yote niliyoyasema ni kukuandaa ili uzame vizuri katika tafakari ya leo na kadiri ya masomo yake. Mtume Paulo licha ya changamoto alizozikuta baada ya kuongoka kwake, hakuwa tayari kubadilishwa na mtazamo wa wakati wake na kujivika koti la uovu. Haki na kweli ndani na katika Kristo Yesu ilibaki kuwa msingi wa imani yake. Hivyo Barua yake ya pili kwa Timotheo anapenda wafahamu, na tufahamu kiini na msimamo wa imani yake. Naye anasema, Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana,” 2Tim 1:3. Anaye kumbukwa hapa bila shaka ni Timotheo mwenyewe aliye mfano halisi wa kweli na haki katika jumuiya yake. Leo mambo hayako hivyo hata kidogo. Baadhi yetu kama viongozi wa dini, na wenye kuijua iliyo kweli, na hata kama hatuiamini kwa kupitia utaratibu uliowekwa kwa taasisi husika kama hatua ya kuhesabiwa haki ya kuwa kile ulicho, tumekuwa waogeleaji wa kufuata mawimbi ya maji bila kujali ustadi wa kuogelea kwetu tukitazama ng’ambo ile na iliyo salama tunayotamani wote kuifikia. Hapa ndipo penye chimbuko la unafiki. Hapa ndipo kwa makusudi makubwa kabisa katika fikiri, amua na tenda yetu, wafuasi wetu hutushangaa kwa kwenda kinyume kabisa cha matazamio ya kweli ile tunayoihubiri na matamanio yake. Hapa ndipo tunapoonekana si tu vituko, bali watu tusiokuwa na maono na uelewa wa kile tukisemacho, na mwisho kuutabiri unabii tusioujua ili tuenende na mawimbi ya nyakati zetu tusiyoyajua.

Mkristo mwenzangu, niyasemayo siyo mageni mbele ya macho yako. Manabii hawa wa kubumba hawaoni shaka wala haya hata kidogo leo kusema Edgar ndiye “chaguo lile la Mungu” leo kwa watu wa Mungu. Je, kwa nini wanasema kama wasemavyo? Je, wanajua kile walicho na yale waliyoyalia kiapo kwa ajili ya taifa la Mungu? Kwa nini basi wanadanganyika kiasi hicho? Je, wanaifahamu karama ya Mungu ndani ya maisha na utume wao? Mtume Paulo anamwambia Timotheo hivi, Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu,” 2Tim 1:6. Kutokuchoka maana yake, usitafute urahisi wa jambo na kuutafsiri vinginevyo na karama uliyonayo kwa kuyaona mawimbi ya muda tu katika wakati wako. Kwa maana nyingine, palipo na giza tusema giza, na tufanye kadiri iwezekanapo kuuleta mwanga, na palipo mwanga tusema mwanga na uutetee mwanga huo ili udumu. Kwa nin basi katika hali hii twaingiwa na woga? Kwa  nini tunakufa gazi pasipo ganzi?Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7. Katika mazingira ya utata kama huu tufanye nini?

Wapendwa wana wa Mungu, katika mazingira na utata kama huo yatupasa kusimama katika kweli, hata  kama nikibaki mwenyewe. Yesu Kristo kwa kutambua ugumu huu anakuambia wewe na mimi leo kwamba, tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Yoh 8:32, 36. Mwana anatuweka huru, unapokuwa tayari kujiachia katika minyororo ya upumbavu kwa kuwa tayari kujifunza na kumsikiliza. Hii ndiyo habari njema ya wokovu, yaani, kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kuwa shuhuda ya neno hilo kwa maisha yako ya kila siku. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9. Je, hili lasema lolote juu ya maisha yako kama Mkristo leo?

Leo mimi kama mfuasi wa Kristo na muhudumu wake wa karibu, habari njema ya wokovu, yapaswa kuwa kipaua mbele changu. Na habari njema ya wokovu kwa ufupi kabisa ni kulishinda giza (dhambi) kwa kuukumbatia mwanga (utakatifu). Kwa habari hii njema ya wokovu, inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu,” 2Tim 1:10-11. Leo mimi kama mfuasi wa Kristo, na kwa upekee kama mhudumu wa karibu (Mkleri), bila kuijua habari njema, na kusoma alama za nyakati kadiri ya habari njema ile, ufuasi wangu na ukaribu wangu hautakuwa na mguso wowote kati ya kile nilicho na ushuhuda ule nipasao kuutoa. Nitabaki kuwa tukio kama utaratibu wa kawaida bila historia kama sehemu ya mang’amuzi. Ndugu yangu, unakuwa historia kama sehemu ya mang’amuzi unapoyachukulia yale yaliyotokea katika maisha yako, ukitazama kule unapokutamani kama hitimisho la kila kitu. Hapa tumaini lipo hata kama linachelewa au kucheleweshwa. Hapa ndipo mateso kama matukio katika maisha ya kila siku yanapata maana kama asemavyo Mtume Paulo, kwamba, Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile,” 2Tim 1:12. Hapa siku ‘ile’ ya maanisha ‘uzima ule wa milele’ tunao utamani.

Ndugu yangu, kutokuyaona maisha katika mtazamo huu wa umilele, ni tatizo kubwa sana leo, na hasa katika jamii yetu ya Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa tunaishi katika ulimwengu wa kufikirika na usiowezekana. Leo wengi tumeaminishwa uongo, na tumeupokea uongo huo kuwa ndiyo kweli. Hili ndilo analojaribu kulibadili Yesu katika akili za watu kwa nyakati zake zile na mazingira yake, na hasa kuhusa swala la kiyama. Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao,” Mk 12:18-19. Yesu Kristo haoni haya kusema lililo kweli na haki hata kama jambo hili limeaminika kuwa kweli ilhali kweli haipo ndani yake. Kristo anatutaka tutofautishe maisha tunayoishi leo na sasa, na maisha yale tutakayoishi mara baada ya kifo chetu.  Maisha ya ufufuko, yaani, maisha baada ya kifo, ni tofauti kabisa, kwa sababu tutakuwa na miili tofauti na hitaji tofauti. Miili tutakayokuwa nayo ni miili iliyotakatifuzwa,’ na isiyo shikiliwa au zuiliwa na ‘muda na nafasi.’ Ni miili iliyo huru kwa kila jambo na katika kweli na haki, na yote katika utukufu wa Mungu.

Na kwa namna hiyo Yesu anasema, watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni,” Mk 12:25. Tunaoa au kuolewa kwa sababu tupo chini ya shikamanizi la muda na nafasi. Ndugu yangu, katika egesho au kipimo muda na nafasi, hatuna chaguzi nyingine zaidi ya kile kilichopo katika kipimo hicho. Kumbe maisha ya ufufuko ni tofauti kabisa. Katika kweli hii Yesu anatutaka tujue hili, kwamba,  kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?” Mk 12:26. Huyu Mungu kwa lugha nyepesi ni Mungu aliye hai, na hai kwa kila kitu. Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana,” Mk 12:27. Tunapotea pale tunapomwona Mungu kama mfu kadiri ya ubinadamu wetu. Mungu wetu ni mwanzo na mwisho, Alfa na Omega, Ufu 22:13.

Tumsifu Yesu Kristo! 

Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile,” 2Tim 1:12


Tusali:-Ee Yesu, nijalie niwe kielelezo chako halisi popote pale nitakapokuwa, na iwe sehemu ya ushuhuda wangu. Amina

TAFAKARI: SHEREHE YA BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI

SHEREHE YA BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI
Somo: Sef 3:14-18a.
Zab: Isa 12:2-3, 4abc, 5-6
Injili: Lk 1:39-56
Nukuu:
Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15 

Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:17

“Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:41b-42

Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:46-49

TAFAKARI:Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu.” 

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anatambua ushiriki wa Mama Bikira Maria katika safari nzima ya wokovu wetu, na hivyo anaadhimisha siku hii, tendo lile ya Bikira Maria kwenda kumwamkia mpwa wake Elizabeti. Mama Bikira Maria naheshimiwa sana na kutukuzwa katika Kanisa letu Katoliki siyo kwa sababu ya uzuri wake, au upekee wake wa ajabu kama mwanamke, bali kwa unyenyekevu wake, hasa kwa kuwa tayari kuyapokea yote licha ya kutokujua nini hasa kitakachofuata au tokea katika maisha yake. Bikira Maria anaishinda hofu ile ya sintofahamu. Ukweli huu unajidhihirisha kwa maneno haya mazito ya Bikira Maria, “mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Maneno haya ya Mama yetu Bikira Maria, ni fundisho tosha ya kujiachia pasipo kujibakiza, hasa katika mazingira ya yale tusiyoelewa sawa sawa.

Leo tunaposherehekea siku ile Bikira Maria alipokwenda kumpasha habari Mpwa wake Elizabeti, itukumbushe kudumisha ujirani mwema. Ujirani mwema hudumishwa kwa kuwa na moyo safi, Lk 1:46-47. Moyo usio jilimbikizia maovu. Moyo uliyotayari kuona mazuri mara zote kwa watu wote. Moyo usipungukiwa kiti kwa nyakati zote na shida zote. Moyo uliyo tayari kutaambika kwa ajili ya wengine. Usafi wa moyo huu, ni tiketi ya kuuona uso wa Mungu. Moyo usio na hatia una nafasi kubwa sana kumwaona Mungu. Moyo huu una heri kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo,  Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu,” Mt 5:8. Mama yetu Bikira Maria pamoja na kuhesabiwa haki hiyo ya kuwa Mama wa Mungu, nafasi hiyo haikuwa sababu ya kujivunia, bali kujinyenyekesha katika udogo wa hali ya chini kabisa. Kujinyenyekesha kwake huku kuna kuwa chanzo cha mawasiliano ya kimungu kati ya fumbo lile lilikokuwa limejificha kati ya kile kilichokuwa tumboni mwake, yaani, Neno kufanyika Mwili na kukaa kwetu, na kile kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kuitaarisha njia ya Neno hili, yaani, Yohani Mbatizaji. Na mambo yalikuwa hivi, Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake,” Lk 1:41. Huu ni uthibitisha wa ubebaji wa Habari Njema aliyokuwa nayo Mama Bikira Maria. Je, wewe ni habari njema hapo ulipo? Hatuwezi kuwa habari njema kama tu wafuasi wa majungu. Wengi wetu tumebeba mimba za majungu na kwa namna hiyo hatuwezi kuwa habari njema hata kama tutajifungua.

Ndugu yangu, palipo habari njema, Roho Mtakatifu aliye umoja na tunda la upendo wa Mungu Baba na Mwana, hutuunganisha katika umoja wa kweli, na usio na unafiki. Na hivi ndivyo ilivyotokea kwa mpwa wake Bikira Maria, Elizabeti.  “Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:41b-42. Roho Mtakatifu ndiye anayezungumzu ndani ya Elizabeti. Ndugu yangu, hata pale ambapo hatuna cha kusema ila tumejiachia bila kujibakiza kwa Kristo Yesu, Roho Mtakatifu utusemea na kutushuhudia. Katika hili Yesu anasema, nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:18-20. Mawasiliano haya kati ya Mama Bikira na Mpwa wake Elizabeti ni mawasiliano yenye Umungu ndani yake.

Naye bila kujibakiza, Bikira Maria anayasema yaliyo moyoni mwake,  Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:46-49. Mama Bikira Maria kwa tendo hili anaona mpango mzima wa Mungu ndani yake. Pamoja na Mpango huo, Mama Bikira Maria hakuwa na sababu ya kujivuna na kujiinua zaidi ya kujinyenyekesha mbele za Mungu. Tendo hili linamtafakarisha Mama Bikira Maria kuyaona makuu ya Mungu kupitia kwake. Naye anasema, Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Akiwa mnyonge na mwenye kutostahili chochote zaidi ya kuwa mtumishi wa Bwana, Mama Bikira Maria anapata fursa ya kumshukuru Mungu na kulitukuza jina lake daima kwa kuutazama upya unyonge wa watu wake na taifa lake. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele,” Lk 1:54-55. Hakika Mama Bikira Maria ni kielelezo cha fadhila ya unyenyekevu. Hivyo kama kuna sababu ya kujisifu tujisifu kwa mambo ya udhaifu wetu kama asemavyo Mtume Paulo, 2Kor 11:30. Na penye udhaifu ndipo penye nguvu, 2Kor 12:10. Ni kwa unyenyekevu tu tunaweza kuona udhaifu wetu.

Wapendwa wana wa   Mungu, unyenyekevu huu kama ulivyo wa Mama yetu Bikira Marian dio unaoweza kutuondolea hukumu ya Mungu pale tunapomkosea Mungu na kuwa tayari kuanza upya Naye kwa njia ya toba ya kweli na majuto. Unyenyekevu wetu huujenga upya ukaribu wetu na Mungu na kwa namna hivyo Mungu yupo tayari kughairi hukumu yake kwetu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15. Mungu kamwe hafurahii kuangamia kwetu kama asemavyo Nabii Isaya, Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:7. Ndugu yangu, Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:17. Sifa na Utukufu kwa Mungu wetu ajuaye mwisho wa maisha yetu. Amini.

Tumsifu Yesu Kristo!

Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15


Tusali:- Ee Mama Bikira Maria, tujalie unyenyekevu wako ili nasi tufumbuliwe siri na mpango wa Mungu katika maisha yetu. Amina

domingo, 29 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Pet 1:2-7
Zab: 91:1-2, 14-15b, 15c-16
Injili: Mk 12:1-12
Nukuu:
kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo,” 2Pet 1:1b

 “Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii,” 2Pet 1:3 

 “Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu,” Mk 12:2 

Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6 

Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7 

Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8 

TAFAKARI:Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni.”

Wapendwa wana wa Mungu, ufunuo wa wazi wa Mungu katika historia ya wokovu wetu imekamilishwa kwa tendo lile la kumwilishwa, yaani, neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Tendo hili linakuwa mtikisiko mkubwa kwa watu wengi, na hasa wale ambao hawakuwa katika njia ya kweli na haki. Ni wazi kabisa tendo hili la kumwilishwa kwa neno linaubadilisha mtazamo mzima wa maisha, na tumaini jipya la wale wote Mungu aliowaridhia. Kwa kupitia Musa, watu walipata tumaini kwa kuishika torati. Ila kwa kupitia Kristo, neema na kweli likazaliwa tumaini jipya na mwanzo mpya. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Hivyo mtikisiko wa wazi unaonekana kwa wale wote waliojihesabia haki na kuhodhi mamlaka kama wao ndio miungu watu.

Injili ya leo inaeleza historia nzima ya wokovu wetu hadi, kilele chake kikiwa ni ufunuo wa wazi wa Mungu kwa watu wake, yaani Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu. Mfano wa wakulima katika shamba la mizabibu unatupa taswira halisi ya wale waliokuwa wapinzani wa mpango huo wa wokovu wa Mungu. Wapinzani hawa amboa walijihesabia haki na kujitwalia nafasi ya Mungu na  kuwa miungu watu, ndio waliowaangamiza wale wote waliolitangulia Neno, yaani, Bwana wetu Yesu Kristo. Kundi hili kabla ya Neno ndilo lililowachukua Mababa wa Imani, Manabii mbalimbali, na waamuzi. Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu,” Mk 12:2. Hata hivyo hawa wote waliuwawa.
Mungu hakuchoka, kukata tamaa, na wala kusitisha nia yake ya kumkomboa mwanadamu. Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6. Jambo la kushangaza mambo hayakuwa hivyo kutokana na ugumu wa mioyo ya watu, na hasa Wayahudi. Kwa kusukumwa na ubinafsi wao (ikia ni pamoja na mila na desturi zao) na kutetea maslahi yao kama miungu watu, Mwana huyu ya Mungu asiye na kosa wakamfanya kama walivyowafanya watangulizi wake. Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7. Lengo hapa ni kulinda maslahi yao, na kuendelea kudumu katika dhambi. Yesu Kristo anawaambia yote haya na sisi leo, kwa lengo la kubadili mwelekeo wa maisha na kuanza naye upya kwani kwake lipo tumaini la kweli na lililojaa neema.

Hata hivyo, kwa kuing’ang’ania dhambi na furaha zake, Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8. Na haya ndiyo mauti yaliyomfika mtu yule mwenye haki, ambaye ndiyo Kristo mwenyewe kwa kifo kile cha Msalaba. Na hili ndilo jiwe la Msingi ambalo kwalo kila ajengaye nyumba juu yake (Imani juu ya Mwana wa Mungu), nyumba hiyo itakuwa imara daima. Na hili ndilo itimisho ya andiko lile kwamba, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni,” Mk 12:10. Maneno haya ya Yesu kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee, Mk 11:27,  yanazua tafrani kubwa kwani yaliwachoma vizuri ndani ya mioyo yao. Kama ni ujumbe, ulifika na kupokelewa! Hivyo wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao,” Mk 12:12. Ndugu yangu, hii ni moja ya changamoto ya Imani yetu, hasa pale tunapopambana na giza kwa kuileta nuru ya kweli.

Kwa kuishi kweli ahadi zako za Ubatizo ni mwitikio wa wazi wa kupambana na lile lililo giza na gizani. Ni kuwa tayari kuyapokea na kuyapata yote aliyompata Kristo kwa sababu, Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea,” Yoh 1:9:11. Je, katika hali hii mimi na wewe tufanye nini?

Mpendwa katika Kristo, simulizi alilolitoa Yesu latukumbusha ni kwa namna gani mpango wa Mungu ulivyokuwa kuhusu wokovu wetu, na lina lengo la kuviendeleza vita hivi vya imani bila kuogoba. Nuru yapasa kuwa nuru ili giza lisiwepo. Hivyo mimi na wewe kwa kuwa nuru kuna mapaswa na sadaka yake. Basi pale tunapokuwa nuru kwa mapaswa na sadaka yake, isiwe sababu ya kuhuzunika wala kujiona tumesahauliwa na Mungu, bali tufurahi katika hali hiyo. Kwetu na iwe heri. Naye Yesu anasema hivi pale tutakapopatwa na hali hiyo, kwamba, “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Hapa tunahesabiwa haki na kuwa na dhawabu kubwa mbinguni.

Mitume, na hata wafuasi katika jumuiya ile ya kwanza ya Wakristo, hawakuacha kuwa nuru pale walipokuwa licha ya ugumu wa mazingira ya wakati ule. Mtume Petro haachi kujitambulisha katika Imani ya kweli ndani na katika Kristo kwa watu kama asemavyo,   kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo,” 2Pet 1:1b. Leo mimi kuwa Mkristo bila kielezo hai cha Kristo ndani yangu, ni sawa na kutokuishi nuru ile halisi ya Kristo ndani yangu. Kwa kutokufanya hivyo, Mtume Petro anasema, wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa,” 2Pet 1:2. Kristo hatoheshimika kabisa mbele za watu, na hasa kwa matendo ya kifisadi yanapofanywa na wale ambaye hujishuhudia mbele za watu kama Wakristo. Moja ya uwepo wa nuru halisi ndani ya maisha yetu ni kule kuwa watu wa haki, na watetezi wa haki kama Kristo Yesu alivyofanya na hata kuifia haki hiyo ili mimi na wewe leo tuwe huru. Huku ni kuishi tumaini la kweli ndani na katika Kristo pale ulipo na kadiri ya wito wako. Kwa kutokufanya hivyo ukijua kwa faidi binafsi ni kujiandalia hukumu. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii,” 2Pet 1:3. Je, Mungu hupendezwa haya yatokee kwako bila kusema lolote?

Wapendwa wana wa Mungu, dhamiri yako ndiyo mwalimu wako wa ndani. Dhamiri safi ni mwalimu wa kweli na haki ndani yako. Bila shaka mwalimu huyu ndani yako ni uwepo wa nguvu za Mungu ndani yako zenye lengo la kukufikisha pale Mungu alipo. Ni kwa maana hiyo kwamba, Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu; wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu,” 2Pet 1:4-5. Ndugu yangu, hukumu utakayoipata kwa kutokuitii sauti ya Mungu ndani yetu, yaani, ile dhamiri hai na njema ndani yetu, itakuwa nimeiandaa wenyewe kwa kujua. Hapa ndipo kwenye kulia na kusaga meno (Mt 8:12, 13:42, 50, 22:13, 24:51, 25:30, Mk 9:18, na Lk 13:28), maana yake, hutakuwa na jambo lolote la kujitetea. Na hivi ndivyo ilivyokuwa juu ya miji ile ya Sodoma na Gomora, kwamba,  akaihukumu.., akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya,” 2Pet 1:6.

Wapendwa wana wa Mungu, heshimu na kuitii dhamiri yako njema. Walizitii dhamiri zao na kusimama katika kweli na haki, Mungu aliwaepusha na aina zote za ufisadi na mwisho akawahesabia haki. Ni kwa namna hiyo, Mungu  akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu,” 2Pet 1:7. Basi tuenenda kama wana wa Nuru kwa kuwa na hofu ya Mungu ndani yetu. Amina.

Tumsifu Yesu Kristo! 

“Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu. Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:7b-8


Tusali:-Ee Yesu, uliye neema na kweli, tuwezesha mara zote kuishi katika neema hiyo na kweli hiyo kila siku ya maisha yetu. Amina

sábado, 28 de mayo de 2016

TAFAKARI: SHEREHE YA MWILI NA DAMU YA BWANA WETU YESU KRISTO

SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTO-C
Somo: Mwa 14:18-20
Zab: 110:1-4 (K) 4
Somo II: 1Kor 11:23-26
Injili: Lk 9:11-17
Nukuu:
Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana,” Mwa 14:18 

 “Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote,” Mwa 14:20 

naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu,” 1Kor 11:24 

Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu,” 1Kor 11:25

Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo,” 1Kor 11:26 

 “Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula,” Lk 9:13 

 “Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili,” Lk 9:17 

TAFAKARI: “Wapeni ninyi chakula.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hiki ndicho kiini na uwepo halisi wa Kristo katikati yetu. Kwa uwepo wa Mwili na Damu ya Yesu, mimi na wewe tulio wafuasi wake waaminifu tunaunganishwa na kufungamanishwa na Upendo huu wa ajabu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti,” Rum 8:1-2. Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ni chakula na Uzima wetu. Hii ndiyo Sakrameti Kuu ya Ekaristi Takatifu. Sherehe hii ya leo inaturudisha nyuma na kutafakari kwa undani siku ile ya Alhamisi Kuu ambayo ndiyo iliyokuwa siku rasmi kwa kusimikwa Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu.

Kwa maumbo haya ya Mkate na Divai, Mwili na Damu ya Yesu, Yesu Kristo ni uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake,  Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa ndani yetu. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.

Wapendwa katika Kristo, jibu la Yesu kwa wanafunzi wake, “Wapeni ninyi chakula, Yoh 9:13,” kwenye Injili ya leo pale wanafunzi wake walipomwendea ili awaage makutano nao wapate muda wa kujitafutia chakula, liliakisi kile kilicho tokea siku ile ya Alhamisi Kuu, yaani wajibu (Mkleri) na kiini cha Sakramenti ya Daraja Takatifu. Hivyo ili kuwe na mwendelezo wa chakula hicho-Ekaristi Takatifu, Yesu aliisimika rasmi Sakramenti ya Daraja Takatifu siku hiyo ya Alhamisi Kuu na kuwaonyesha kiini chake, yaani, kuwa watumishi na kutumika vilivyo kwa upendo wa kimungu, kwa tendo lile la kuwaosha miguu wanafunzi wake. Yesu kwa jibu lake hili anaonyesha utashi wake ikiwa na kukubali kwamba kwa hitaji hilo walilokuwa nalo wanastahili chakula. Pili, anawataka kwanza Mitume wake watoe kile walichokuwa nacho na kukishirikisha kwa upendo.

Leo Mama Kanisa anaposheherekea Sikukuu hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, tunakumbushwa pia wajibu na kiini cha Sakramenti ya Daraja Takatifu, vile vile bila kusahau ushiriki wetu katika ukuhani wa kawaida kwa kila Mbatizwa kwa Sakramenti ile ya Ubatizo (kupakwa mafuta Matakatifu ya Krisma, na kuunganishwa na taifa lake Mungu, kuendelea kuwa kiungo cha Kristo, kuhani, nabii na mfalme, hadi uzima wa milele Mbinguni). Kwa mantiki hiyo, Kanisa kama mwili wa Kristo uliojengwa na Wabatizwa wote, na Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu, linawajibu wa kuwalisha chakula waamini wake, wale wote wenye hofu ya Mungu, na wale ambao bado hawajamjua Kristo.

Jamii inayotuzunguka licha ya itikadi zao za kidini, siasa, utamaduni na desturi, wana njaa ya mwili na roho. Kama Kanisa linalosafiri-Kanisa la hija, lililosheni watakatifu na wadhambi, ni wakati wa kutafakari kwa makini zile heri nane kama zilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo 5:3-11, na kwa namna ya pekee mstari ule wa sita na tisa. “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:6,9. Jamii yetu ya leo ina njaa na kiu ya haki. Mtu katika ukamilifu wake ni mwili na roho. Mtu huyatamani yaliyo ya roho kama haya ya kimwili yapo sehemu yake na katika umaana wake. Hivyo, mtu na utu wake lazima uheshimiwe na kupewa stahili zake. Haki ya mtu kama tokeo la kuwajibika kwake lazima ilindwe na kutetewa kwa nguvu zote bila kupepesa macho. Ni kazi ya kila Mbatizwa kama Kanisa, na Kanisa kama Chombo na Sakramenti ya Wokovu, ‘kuwapa chakula’ katika maana ya kuamsha dhamiri zilizo lala, kuzijenga dhamiri zilizoharibiwa na kudumaa, na kuzifufua dhamiri zile zilizokwisha kufa, ile duniani hapa tunapoishi pale mahali salama kama sehemu pekee ya kujiandaa kwa maisha ya umilele.

Kila kukicha ulimwengu huu wa leo unapoteza usalama wake kwa sababu tu wapo watu wachache kwa ubinafsi wao (uroho wa madaraka) wanatumia vibaya uhuru na madaraka yao na kuzalisha machafuko. Katika eneo hili kila Mbatizwa anaalikwa kuulisha ulimwengu kuanzia pale alipo kwa kuwa mpatanishi. Kabla ya yote yakupasa kujipatanisha nafsi yako mwenyewe, wewe na jirani yako, wewe na mazingira yako, na wewe na Mungu. Upatanisho huu utuepusha na dhambi ya kijamii. Kwa kuishi na kufanya hivyo tunautendea haki ukuhani wetu wa kawaida, na unabii wetu. Nafasi uliyonayo leo kama Mkristo ni taa na nuru pale ulipo. Kristo ni kielelezo cha Nuru halisi kwetu licha ya kwamba walio wake, yaani, mimi na wewe kila siku tunamkataa. “Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua,” Yoh 1:10. Hivyo ndiyo maana ukuhani wa Kristo unafananishwa na ule wa Melkizedeki Mfalme wa Salemu. Historia yake haijulikani sana zaidi ya kile alichokifanya kama kuhani na Mfalme. Kumbe kwa muono huo mimi na wewe tunashirikishwa ukuhani wa Kristo bila kujali historia zetu wala makabila yetu. Sote tunaitwa kuhudumu na kuwa wahudumu ndani na katika Kristo. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana,” Mwa 14:18. Kwa nafasi yake kama kuhani anamlisha Abramu kwa kumbariki. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi,” Mwa 14:19. Na mwisho kwa uwepo wa Abramu anamsifu Mungu na kuwa mpatanishi kati ya Abram una maaduni zake kwa kuitafuta amani. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote,” Mwa 14:20.

Leo Kanisa linaposheherekea Sikukuu hii ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo, tunakumbushwa kuwa wakarimu. Yakupasa kuwa mkarimu ukitambua thamani ya kukombelewa kwako. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Kwa kutambua thamani hiyo, niwe mkarimu kuanzia pale nilipo ikiwa ni kwa wote wanaonizunguka. Niwe mkarimu na kujitoa katika Kanisa kwa vipaji vyangu na mali alizonijalia Mungu ili shughuli zake za kimisionari zisonge mbele na Kristo afikiwe kwa wate wote wenye njaa na kiu ya haki. Hivyo nikumbuke kuishi katika kiasi na kuwajali wengine.

Niepuke mara zote matumizi mabaya ya mali na kutapanya kile kilichozidi au baki baada ya kupata hitaji langu. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili,” Lk 9:17. Vikapu kumi na viwili, ni idadi ile ya jumla ya makabila yale kumi na mbili ya Wayahudi, yaani wana wa Yakobo. “Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili. Wana wa Lea ni Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Zabuloni. Wana wa Raheli, ni Yusufu na Benyamini. Wana wa Bilha, kijakazi wa Raheli, ni Dani na Naftali. Wana wa Zilpa, kijakazi wa Lea, ni Gadi na Asheri. Hawa ndio wana wa Yakobo aliozaliwa katika Padan-aramu,”  Mwa 35:22b-26. Kumbe tukiwa wakarimu na kushirikishana kwa upendo yale tuliyojaliwa kwa ukarimu na Mungu, hakuna atakayekosa.

Tujifunze kutoka mshumaa. Mshumaa upiga vita giza (njaa na kiu ya haki), na wakati huo huo kutoa bila kujibakiza (kuepuka ubinafsi, uroho wa madaraka, kujilimbikizia na kuwa sababu ya machafuko). Kumbe mimi na wewe haitoshi kulalamika tu bila kufanya chochote ili hali twaweza kubadili hali pale ulipo na kwa nafasi uliyo nayo. Kama si umeme uwe mshumaa, na kama si ushumaa ule kijinga cha moto. Hakuna sababu ya kupiga kelele chumbani kuna giza tororo ilhali umeushika mshumaa. Washa mshumaa huo, na ingia chumbani. Kuwa nuru na mwanga pale ulipo. “Wapeni ninyi chakula.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili,” Lk 9:17


Tusali:-Ee Yesu, nifundishe ukarimu. Amina