domingo, 31 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 4 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 4 YA MWAKA-C

Somo: 2Sam 15:13-14, 30, 16:5-13
Zab: 3:2-7
Injili: Mk 5:1-20
Nukuu:
Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza,” 2Sam 16:11 

Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo,” 2Sam 16:12

akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese,” Mk 5:7 

Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini,” Mk 5:13 
Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao,” Mk 5:17

lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu,” Mk 5:19 

Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu,” Mk 5:20

TAFAKARI:Kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu.”    

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna kati yetu asiye na jambo lolote la kumshukuru Mungu hata kama tumesongwa na dhiki ya kupindukia. Kushukuru kwa jambo lolote lile ni kuomba pia. Ni mara ngapi sala zetu zimekuwa na muono wa kushukuru? Mfalme Daudi anasongwa na upinzani mkubwa kutoka nje na ndani ya ufalme wake. Pamoja na hali hiyo, Mfalme Daudi hatoi nafasi ya kumlaumu Mungu. Kusamehewa  kifo kwa kosa la kuzina na mke wa Uria, hakukumwondolea upanga dhidi ya Ufalme wake. Bwana Mungu akasema, Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10.

Mtoto wake wa kumzaa, Absalomu anakuwa mwiba mkali katika ufalme wake. Mfalme Daudi anakosa ujasiri na kuingiwa hofu na amani kutoweka. Huyu ndiye aliyemua Goliathi kwa jiwe. Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa?” 2Sam 16:11a. Mfalme Daudi anatambua wazi matendo aliyomtendea Mungu na kujikwaa kwake. Hivyo kila kinachomtokea kina sababu na mkono wa Mungu ndani yake. Alipodhihakiwa njia na mtu asiyemjua alikotoka, Mfalme Daudi alijibu, Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo,” 2Sam 16:11b-12. Mfalme Daudi pamoja na kuujua ukweli huu, hakukata tamaa na wala hakumwasi Mungu.

Injili ya leo inaubeba ujumbe kama wa Mfalme Daudi ila kwa mtazamo mwingine. Hapa tunakutana na uponyaji wa mtu aliyeteswa na kundi kubwa la pepo. Hata walipoulizwa mpo wangapi haikuwa rahisi tutoa jibu la haraka. Badala yake walijibu, ‘Legioni, kwa kuwa walikuwa wengi.’ Uwepo wa Yesu ni vita dhidi ya uovu. Ni vita vya mwanga dhidi ya giza. Jina la Yesu linatisha. Jina hili ni tishio dhidi ya Shetani na mamlaka yake. Ni kwa sababu hiyo, mtu yule alipomwona Yesu, akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese,” Mk 5:7. Pepo wachafu wanatambua nguvu na mamlaka aliyokuwa nayo Yesu, na wanajua vita dhiki yake hawatashinda. Je, unaliamini jina hili Tukufu na Kuu kuliko Majina Yote?

Na hali ilivyozidi kuwa mbaya, pepo wale waliomba na kujisalimisha chini ya Mamlaka ya jina hili kuu, kwa kuwaingia nguruwe. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini,” Mk 5:13. Ukiangalia tendo hili alilofanya Yesu kiuchumi la kuwaruhusu wale pepo kuwaingia wale nguruwe waweza kutafsiri kwamba Yesu hakutenda haki kwa mfugaji wa wale nguruwe. Ndugu yangu, viumbe vyote ni mali ya Mungu, na Yeye Mungu anamamlaka yote juu ya viumbe vyake vyote. Na maandiko Matakatifu yanatuambia, Neno huyu alifanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:2. Hivyo Yesu alikuwa na mamlaka yote na uamuzi wake ulikowa sahihi.

Kwa upande mwingine, tendo hili la Yesu linathibitisha upekee na thamani ya mwanadamu kati ya viumbe vyote. Na sababu kubwa ni kwamba Mungu alipenda na kuchakua kumuumba mtu kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Kiumbe huyu, yaani mwanadamu imebeba chapa ya Mungu ndani yake. Binadamu anastahili heshima kubwa licha ya tofauti za kibinadamu tunazojiwekea, na zinazotokana na utofauti wa kimaisha, na kwa makusudi kabisa tunaruhusu zitugawe kimatabaka. Pamoja na upekee huu aliokuwa nao Mwanadamu, kamwe Mwanadamu huyu hawezi kumshurutisha Mungu atende kadiri atakavyo yeye. Kwani “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” 1Sam 2:6-8. Kumbe kila alitendalo Bwana lina sababu yake katika umilele wake.

Kama tendo la shukrani, mtu yule aliyewekwa huru na Yesu kutoka mamlaka ya shetani, anaomba kuandamana ya Yesu. Lakini Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu,” Mk 5:19. Ndugu yangu, unapotambua mkono wa Mungu katika maisha yako, anza hapo hapo kutoa ushuhuda huo na kulisifu jina la Bwana. Mtakatifu Fransisko wa Assis wakati fulani alisema, ‘hakuna sababu ya kwenda sehemu fulani na kuhubiri, ila tuhubiri kadiri tutembeavyo.’ Kwa upande mwingine, katazo hili ya Yesu kwa mtu huyu asiandamane naye linalenga kukoleza Imani ya kweli sehemu ile Mungu aliyokutendea makuu yake. Hivyo mtu yule akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu,” Mk 5:20. Ndugu yangu, wewe na mimi tunayo mengi ya kutoa shukrani kwa Mungu. Basi anza hapo ulipo.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti,” Zab 13:3


sábado, 30 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA MWAKA-C

JUMAPILI WIKI YA 4 YA MWAKA-C

Somo I: Yer 1:4-5, 17-19
Zab: 71:1-6, 15-17
Somo II: 1Kor 12:31-13:13
Injili: Lk 4:21-30
Nukuu:
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao,” 1Kor 13:1

Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi,” 1Kor 13:2

Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu,” 1Kor 13:3 

Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni,” 1Kor 13:4 

haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya,” 1Kor 13:5

haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,” 1Kor 13:6 

huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote,” 1Kor 13:7

Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,” 1Kor 13:8 

Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13

Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21

Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe,” Lk 4:23 

Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,” Lk 4:24 

Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo,” Lk 4:28

Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini,” Lk 4:29 

lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake,” Lk 4:30 

Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa,” Yer 1:5

Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii,” Yer 1:18

Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe,” Yer 1:19

TAFAKARI: Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 4 ya mwaka ‘C’ wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee Mama Kanisa anatutaka tuzame ndani zaidi katika fumbo hili la UPENDO. Uwepo wetu na yote yaliyopo katika ulimwengu huu ni tokeo la Upendo wa Mungu Baba. Mungu alivijua vitu vyote hata kabla ya kuumbwa kwayo, na ndivyo ilivyokuwa kwa mwanadamu. Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa,” Yer 1:5. Wito huu wa Nabii Yeremia unatukumbusha kwamba hakuna aliyeko duniani hapa kwa bahati mbaya. Kila mmoja wetu ni kusudi la Mungu, kwa sababu ya Mungu, na kwa ajili ya Mungu. Mungu aliviumba vitu vyote kwa sababu alipenda kuviumba na kuvifanya kama vilivyo kwa sifa na utukufu wake. Pamoja na uzuri huu, binadamu amependelewa zaidi kwa sababu ndiye aliyechukua chapa halisi ya Mungu. Mungu alichagua kumuumba mtu kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.

Hivyo asili ya Upendo ni Mungu, uwepo wa upendo ni Mungu, na Upendo ni Mungu. Upendo wa Mungu Baba kwetu ni Upendo wa Mwana pia kwetu. Kwa sababu,Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Huu wote ni upendo wa kweli wa Mungu Baba kwetu, na kupitia Mwana ambaye alifanyika mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Hivyo upendo huu asili yake ni Mungu mwenyewe kama asemavyo Yesu, Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Mungu ndiye aliyetupenda kwanza. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza,” 1Yoh 4:9-10, 19. Ni kwa namna hiyo tunajifunza haya kama sababu ya kuumbwa kwetu.

Tumeumbwa ili tumjue Mungu, tumpende Mungu, tumtumikie Mungu, na mwisho turudi kwake mbinguni. Hivyo ishi ya binadamu hapa duniani na ustawi wake wampasa kuustawisha upendo huo wa Mungu kwake mwenyewe, jirani, mazingira yanayomzunguka, na Mungu. Upendo na ambatio lake, yaani, ‘jukumu’ hili la msingi lisipoonekana kwa mwanadamu basi mwanadamu huyo kesha potea njia, na ishi yake haina makusudi ya kuumbwa kwake.

Yesu anaanza safari yake ya kukamilisha kile alichokijia kwa maneno haya, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Huu ndiyo mpango kazi wa Yesu ambao unasukumwa na UPENDO. Mpango kazi huenda pia na kauli mbiu ya kazi. Kauli mbiu ya Yesu juu ya wokovu wetu ndiyo hii, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Upendo na huruma ya Mungu huenda pamoja.

Upendo huu wa Mungu kupitia mwanaye Mpenzi Yesu Kristo unafungua mlango mpya wa huruma ya Mungu, yaani, ‘mwaka wa Bwana uliokubaliwa.’ Hivyo tuutumie vyema mwaka huu wa Kanisa wa huruma ya Mungu kwa kuchota baraka na neema za Mungu. Leo Yesu anatuambia, “maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21. Maandiko haya yametimia kwetu kwa sababu nguvu na uwezo vina yeye (Kristo) hata milele yote, Yud 1:25. Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile,” Yoh 5:19.

Ni wazi katika kutenda lililo la Mungu, yaani lenye kuongozwa na upendo wa kweli, tujiandae kupata upinzani. Yule mwovu shetani hafurahii yaliyo mazuri na mema yenye kuufunua Utukufu wa Mungu. Yesu Kristo mwenyewe alipata upinzani nyumbani mwake mwenyewe. Katika hili Yesu anasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,” Lk 4:24. Je, kama hatukubaliki nyumbani kwetu na watu wanaotufahamu iwe sababu ya kutokutenda mema? Jibu ni HAPANA! Tuendelee kutenda wema na upendo kwa wote, kwa sababu asili ya upendo ni Mungu, uwepo wa upendo ni Mungu, na Upendo ni Mungu.

Mtume Paulo anaeleza kwa undani upendo na mapaswa yake na yenye kutupeleka katika kusudi la uumbaji wetu. Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao,” 1Kor 13:1. Vipaji vyetu na karama zetu za pekee tulizopewa na Mungu, kama hazitakuwa kwa ajili ya wengine na furaha ya Mungu na jirani zetu, ni hasara kwetu. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi,” 1Kor 13:2. Wengine wamepewa unabii si kwa ajili yao binafsi au kujineemesha, bali umepewa unabii ili upeleke ujumbe huo wa Mungu kwa faida ya watu na wokovu wao na wewe mwenyewe.

Ndugu yangu, hata huo utajiri Mungu aliokupa si kwa ajili yako mwenyewe na kujiburudisha nafsi yako, bali kwa ajili ya kufaidiana na hasa kuwajali kwa njia ya pekee wale wahitaji wasio na chochote. Ni jambo la kusikitisha kuona jirani yako kila siku anaomba Mungu amkirimie angalau apate mlo mmoja kwa siku, wewe unayejua shida na dhiki ya jirani yako huyo ukiwa unasali na kuomba kila siku Mungu akupe maisha marefu ili uendelea kuvitumbua vinono katika utajiri wako. Ndugu yangu, swala hapa si tu kuona hitaji la jirani yako muhitaji, bali kutambua upendo wa Mungu na paswa lake kama Paulo Mtume anavyosema, Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu,” 1Kor 13:3. Ukweli ni kwamba unaweza kutoa bila kupenda, ila huwezi kupenda bila kutoa.

Maisha ya upendo wa kweli yana tabia zifuatazo kama anavyotufundisha Mtume Paulo. Sehemu ya kwanza ya tabia ya upendo ni hii, kwamba, Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni,” 1Kor 13:4. Kwa maneno mengine ‘upendo haujifaidishi wenyewe. Upendo wa kweli hutoka na kutafuta zaidi ya pale ulipo.’ Upendo huwa kwa ajili ya kingine zaidi ya kile kilicho katika ukamilifu wake. Sehemu ya pili ya tabia ya upendo ni kwamba, upendo haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya,” 1Kor 13:5. Kwa maneno mengine upendo ulenga katika ukamilifu bila kupoteza hata kile kilicho katika hali ya udhaifu. Sehemu ya tatu ya tabia ya upendo ni kwamba, upendo haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,” 1Kor 13:6. Upendo huu ulenga faida ya wote katika wote. Sote tu wana wa Mungu, wenye mahitaji yaliyo sawa licha ya tofauti zetu.

Sehemu ya nne ya tabia ya upendo ni kwamba, upendo huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote,” 1Kor 13:7. Mwenye upendo wa kweli hana sababu ya kuishi na mashaka pasipo sababu. Upendo huu utusaidia kukua mwili na roho. Upendo huu upo kwa ajili ya kurekebishana katika kukua na kuongezeka pasipo kuangamizana. Upendo huu unatoa fursa ya kuvumiliana katika kujengana na  kujuana tabia. Upendo huu hutoa fursa bila kipimo katika kusamehana. Sehemu ya tano ya tabia ya upendo ni kwamba, Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,” 1Kor 13:8. Upendo huu unatoa fursa ya mazungumzano hata pale ambapo hakuna uwezekano kinadharia wa mazungumzano hayo ambayo hayazungumziki. Kwenye tabia hii ya upendo hakuna lisilowezekana.

Tabia hizo tano za upendo hutuandaa kujibu maswali mawili la mwisho na ya pekee mbele ya Mungu katika kitu chake cha hukumu na haki. Pasipo shaka yoyote ile, ninashawishika kuona kwamba kila mmoja wetu kadiri ya wito na nafasi yake ataulizwa maswali haya na Mungu;
 Swali la kwanza: Je, ulifanya nini na Upendo wa Mwanangu Yesu Kristo aliyekupenda hadi akayatoa maisha yake kwa ajili yako?
Swali la pili: Je, umefanya nini na vipaji nilivyokupa?

Leo tuwapo hapa duniani tunaongozwa na mambo yote matatu, yaani, Imani kwa kile tusichokijua sawasawa ila kina uzima ndani yake, pili, Matumaini tukijua yote yatapita na uzuri wake na mwisho tutapata kile tunachokichuchumili yaani maisha ya umilele. Na tatu, twaishi ulimwenguni hapa kwa mapendo na hasa tukielekeza nguvu zetu katika tabia za upendo. Haya mawili, yaani Imani na Matumaini ukomo wake ni pale tutakapo ifikia Mbingu. Upendo na tabia zake zitadumu katika umilele wote kwa sababu UPENDO NI MUNGU. Hivyo, Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13.

Mzee Mapinduzi alikuwa mlinzi nyumbani kwa tajiri Mwana Mboka. Mzee Mapinduzi kila siku ufikapo muda wa kwenda lindoni kwa tajiri yake huchukua kindoo kidogo kwa ajili ya kubebea mabaki ya chakula na hasa mifupa ya nyama ambayo kwa kiasi kikubwa hubaki.

Mzee Mapinduzi alifanya hivi kwa zaidi ya miaka mitano. Siku moja Tajiri yake alimuuliza Mzee Mapinduzi, “hivi kwa sasa una mbwa wangani?” “Bosi idadi ya mbwa wangu ni ileile,” Mzee Mapinduzi alimjibu tajiri yake kwa hali ya uzuni. Muonekano ule wa Mzee Mapinduzi ulimfanya tajiri yake afikiri zaidi.

Kesho yake asubuhi na mapema Bwana Mboka kama ilivyo kawaida yake alidamka kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kukimbia. Ila siku ile alidhamiria kuondoka mguu kwa mguu na Mzee Mapinduzi kuwatazama mbwa wake. Walipo karibia nyumbani, mjukuu wa Mzee Mpinduzi alyejulikana kwa jina kama Tatu, alikuja mbio na kumpokea Babu yake kile kindoo cha mifupa na mabaki ya chakula.

Mtoto huyu alienda na kindoo kile moja kwa moja jikoni. Bwana Mboka alipotazama huku na kule hakuona dalili yoyote ya Mbwa. Hivyo alimuuliza Mzee Mapinduzi, “wale mbwa unaowaletea mifupa wapo  wapi?” Mzee Mapinduzi alimwita mke wake na wajukuu wake watano nje. “Hawa ndiyo mbwa wangu. Huyu ni mke wangu mpendwa Bibi Zaituna, na wajukuu wangu watano ambao tunawalea tangu wazazi wao wafariki kwa ugonjwa wa ukimwi.” Mzee Mapinduzi alimjibu tajiri yake huku machozi yakimtoka.

Bwana Mboka aliondoka taratibu kurudi nyumbani bila kusema neno. Siku ile ilikuwa nzito sana kwa Bwana Mboka. Jioni ilipofika, Mzee Mapinduzi alifika lindoni kama kawaida yake na kindoo chake. Bwana Mboka alimwita Mzee Mapinduzi na kumwambia, “hali niliyoiona leo asubuhi imenisikitisha sana. Mimi na familia yangu tumeamua haya yafuatayo: kukujengea nyumba nzuri ya kuishi, kuwasomesha wajuu zako, na kukutunza kama mzazi wetu wewe na familia yako.” Wote walikumbatiana kwa furaha na uchungu huku machozi yakiwatoka.

Tumsifu Yesu Kristo! 


Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu. Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake,” Zab 41:1-2

viernes, 29 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 4 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 3 YA MWAKA-C
30/1/2016
Somo: 2Sam 12:1-7a, 10-17
Zab: 59:12-17
Injili: Mk 4:35-41
Nukuu:
Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma,” 2Sam 12:5-6

Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo,” 2Sam 12:7 

Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10

Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:12 

Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?” Mk 4:38 

Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu,” Mk 4:29 

Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40

Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” Mk 4:41

TAFAKARI: “Wewe ndiye Mtu huyo.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, kunatofauti kubwa kuusema ukweli na kuuishi ukweli. Kuna tofauti kubwa pia ya kuhubiri haki na kutenda haki. Vile vile kunatofauti kubwa sana ya kusema kuhusu upendo na kuishi upendo. Kuyasema mambo kwa ufasaha ni taaluma ambayo mtu anaweza kuipa kwa kupitia njia na miongozo inayohusu jambo hilo. Kuishi jambo fulani ni kugeuzwa na jambo hili na kuwa sehemu ya jambo hilo. Kumbe kwa namna nyingine kama wasemavyo waswahili, ‘kuna kusoma na kuelimika.’ Hivi ni vitu viwili tofauti.

Nabii Nathani anatumwa na Mungu kwenda kwa Mfalme Daudi na kumwambia chukizo alilomfanyia. Nathani anamweleza Daudi uzito wa tatizo na dhambi aliyoifanya kwa jamii, kwa yeye mwenyewe na kwa Mungu. Kwa nafasi aliyokuwa nayo Daudi kama Mfalme ilimpasa awe mtetezi wa kweli, haki, Amani na Upendo. Ufalme wake kama ulivyo uliwakilishwa na taswira na fadhila hizo. Badala yake, Daudi anakuwa muhujumu wa hiyo kweli, haki, Amani, na Upendo. Huu ndio ule mfano wa mtu yule aliyekuwa na kondoo wake mmoja na aliyempenda kupita vitu vyote. Nathani hapa anamaanisha, mtu yule ni Uria, na kondoo wake ni mkewe Bath-sheba Daudi aliyezini naye, na matokeo yake kupelekea umauti wa Uria. Kama Kondoo, yaani wanawake, Daudi alikuwa nao wengi na ofisi yake kama Mfalme iliruhusu kuwa na wake hao wengi.

Mazungumzo ya Nabii Nathani na Mfalme Daudi kwa kupitia mfano wa Mtu na Kondoo wake aliyekuwa anampenda na hivyo kudhulumiwa, yanaamasisha sifa kuu na uwepo wa falme yoyote ile iliyo kwa ajili ya watu, yaani: ufalme wa haki, amani, kweli, na upendo. Hivyo Mfalme Daudi anaguswa na mfano ule na kumwambia Nabii Nathani, “Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma,” 2Sam 12:5-6. Mfalme Daudi anajiweka kitanzi mwenyewe kwa makosa yake. Ndugu yangu, kumbuka maneno ya Yesu, Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38. Ni kwa mizania hii, Nabii Nathani anamwambia Daudi bila kupepesa macho, Wewe ndiwe mtu huyo,” 2Sam 12:7. Hivyo kosa na adhabu inamstahili yeye mwenyewe.

Mungu anatoa adhabu kwa Mfalme Daudi kwa kosa lile ambayo ni chukizo kwake mwenyewe kama Mfalme na mtetezi wa haki za watu, chukizo na makwazo kwa jamii, na chukizo kwa Mungu aliye haki, kweli, amani, na pendo. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10. Kwa kutambua kosa lake na kulikiri, Mungu anathibitisha kuwa Yeye ni Upendo na Huruma na kumwondolea adhabu ya kifo Mfalme Daudi. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:12. Pamoja na hayo, kiumbe kile kama tokeo la uzinifu wa Daudi hakikuishi.

Wapendwa katika Kristo, wewe na mimi kwa njia moja au nyingine tumefanya kama Daudi na wakati mwingine zaidi hata ya Daudi. Hakuna njia nyingine ya kujikwamua katika hali hii zaidi ya kufanya toba ya kweli na majuto. Mungu aliye mwingi wa rehema na upendo yu tayari kutusamehe. Kwa maana Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli,” Zab 86:15. Amina 

Injili ya leo inatufundisha kwamba tukiamini nguvu na uwepo wa Mungu yote huwa salama. Maisha ni kama chombo cha kusafiri baharini, kuna nyakati husongwa na  dhoruba kali. Chombo chetu cha kusafiri “Mtumbwi”-pale tulipo, iwe maisha ya ndoa, au kitawa huanza kuzama kutokana na dhoruba kali-changamoto nyingi katika maisha. Hata hivyo, katika hali hii Bwana wetu Yesu Kristo si kwamba yupo mbali na dhoruba hizi. Katika sintofahau habarini, wanafunzi wake Yesu walianza kupiga mayowe kwa hofu ya kuzama maji. Yesu alikuwa nao, ila kalala. Wanafunzi wanamlalamikia Yesu wakiwa na tafsiri ya Yesu kutokujali kuagamia kwao. Yesu hana muda wa kujibizana nao zaidi ya kuokoa maisha kwanza. Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu,” Mk 4:29. Ndipo Yesu akawaambia, “Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40.

Mara nyingi tunapopatwa na matatizo na mahangaiko katika maisha tunakosa utulivu na kuhangaika hapa na pale, kuagua kwa mganga moja na mwingine, na kufanya matambiko kwa kila mzimu katika ukoo. Kitu cha kwanza ndugu yangu yakupasa kuutafuta utulivu wa ndani. Utulivu wa ndani tunaupata kwa Kristo mwenyewe kwa kuwa na Imani naye. Yesu anatuambia, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;  kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30. Je, yupo zaidi ya Yesu? Kwa akili yako tu bila Yesu hutoweza, kwa umashuhuri wako tu bila Yesu hutoweza, kwa utajiri wako tu bila Yesu hutoweza, na kwa nguvu ya madaraka yako tu bila Yesu hutoweza pia. Basi na tuwe na hofu ya Mungu ndani yetu hata kama hatujamjua Yesu. Tuongozwe na dhamiri njema katika utu wema.

Tumsifu Yesu Kristo!


Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao,” Zab 86:5

jueves, 28 de enero de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 3 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 3 YA MWAKA-C
Somo: 2Sam 11:1-4a, 5-10a, 13-17
Zab: 51:3-6a, 6bcd-7, 10-11
Injili: Mk 4:26-34
Nukuu:
Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho,” 2Sam 11:2

Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa,” 2Sam 11:3-4

Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito,” 2Sam 11:5 

Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi,” 2Sam 11:6

Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake,” 2Sam 11:9

Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe,” 2Sam 11:15 

Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa,” 2Sam 11:17 

Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi,” Mk 4:26

Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32

TAFAKARI: “Madhara ya kuficha na kutokukiri kosa ni kujiangamiza zaidi katika uovu.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna kati yetu asiyekuwa na mapungufu yake. Mapungufu yako yanathibitisha ubinadamu wako. Kuyatambua mapungufu yako ni hatua muhimu sana kuelekea ukamilifu ambao ndio wito wa kila mmoja wetu. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Jambo la kushangaza ni kwamba kati yetu wapo ambo hawapendi na hawayakubali mapungufu yao na kuchukua hatua kuelekea ukamilifu. Badala yake huvaa vinyago ambavyo huwaharibu kabisa na kupoteza sura yao halisi. Wengi kati yetu tunaisha maisha ya kuigiza ilhali kwa uhakika tunasutwa na nafsi zetu.

Kuvutwa na kuwashwa kwa tamaa hasa za mwili ni jambo la kawaida kwa binadamu yeyote. Tumeumbwa na hali hiyo ndani ya miili yetu. Hata hivyo tatizo lipo hapa; pale ambapo tunapozifurahia hisia hizo na kukubali kuendeshwa nazo. Ni katika hali hii tunazungumzia matendo ya mwili, ikimaanisha nafsi kuegemea mwili na siyo roho. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,  ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Hakika kwa matendo haya hakuna mbingu!

Mfalme Daudi katika tembeatembea yake jioni katika hekalu lake anakutana na changamoto ndani ya nafsi yake. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho,” 2Sam 11:2. Ndugu yangu, macho huweza kupendezwa na kitu chochote kile, ila sio kila kitu kipendezacho macho yetu cha faa katika makuzi ya roho na mwili hasa pale tunapojifurahisha nacho kwa kuwashwa tamaa za mwili pasipo kujizuia. Si vibaya kuona uzuri na kuvutwa nao katika maana ya kuusifu uzuri wa uumbaji wa Mungu. Mfalme Daudi hakuishia kuona tu na kumsifu Mungu kwa uumbaji wake, bali alifanyia kazi tazamo lile. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa,” 2Sam 11:3-4.

Kosa la kwanza la Daudi ni hili; hata baada ya kupata taarifa kwamba mwanamke yule alikuwa Bath-sheba, binti Eliamu, mke wa Uria-ambaye ni mmoja wa askari wake, hakuweza kuishinda tamaa yake. Bila shaka Daudi kama mfalme alikuwa na fursa ya kuwa na wanawake wote ambao hawakuwa wameolewa. Mamlaka yake na uwezo wake uliruhusu uwezekano huo. Hata hivyo anatimiza hamu na tamaa ya mwili wake kwa mke wa mjakazi wake Uria. Kila tendo ufanyalo katika maisha yako ndugu yangu linatokeo lake, liwe zuri au baya. Na hakuna kilicho siri chini ya jua hata kama utakuwa mwenyewe au wawili katika jambo hilo. Mtu wa pili ukiwa mwenyewe ni Mungu. Na mtu wa tatu mkiwa wawili ni Mungu pia. Nafasi ya Mungu ni kama kivuli unachotemba nacho, au mnachotembea nacho. Ndivyo ilivyokuwa kwa Daudi. Matokea ya tendo lile la uzinifu la Daudi, ilikuwa ni mimba. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito,” 2Sam 11:5. Tokeo hili la uzinifu linakuwa shitusho la kile alichokifanya. Mfalme Daudi hakuona uovu wake hadi katika tokeo hili la mimba.

Salama ya Mfalme Daudi hadi hatua hii ilikuwa kukiri kosa lake na kuanza upya katika upya na Mungu ambaye ndiye shahidi asiyefichwa chochote. Badala yake, Daudi anautazama ufalme wake, na nafasi yake, hivyo anaficha kosa lake kwa kufanya kosa lingine ambalo ni kubwa zaidi. Daudi anatoka kwenye uzinifu na kuelekea umauti. Hivi ndivyo tufanyavyo pale tunapotaka kula “keki na kuishikilia wakati huo huo.”  Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi,” 2Sam 11:6. Lengo la kuitwa Uria nyumbani na Daudi ni kutaka kudanganya kuhusu mimba ile. Alijua Uria akilala na mke wake ni rahisi kuhalalisha kosa lake. Je, haya yana tofauti na yatendekayo katika familia zetu? Anayemjua baba wa mtoto ni mama. Hivyo akina baba wengi katika familia zetu leo wamekuwa wakiuziwa mbuzi kwenye gunia. Kwa kweli inasikitisha sana!

Uria akijua vigezo na masharti ya kazi yake hasa nyakati za vita, haikuwa busara kulala na mke wake. Uria ni mtiifu kwa viapo vya kazi yake kama askari. Haikuruhusiwa askari kulala na mke wake nyakati za vita. Hivyo, “Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake,” 2Sam 11:9. Mfalme alifanya mbinu zote hata kumlewesha ili Uria ajichanganye na kulala na mke wake ila Uria alikuwa dhabiti katika viapo vyake kama askari.

Baada ya zoezi kugonga ukuta, Mfalme anabuni mbinu nyingine. Daudi anamrudisha Uria vitani na kutoa maelekezo kwa waraka kwa Yoabu kiongozi wa vita na askari wa vita, akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe,” 2Sam 11:15. Hapa tunaona tamaa ya Mfalme Daudi inazaa mauti. Tuelewe wazi kwamba kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti,” Yok 1:14-15. Kweli Uria asiyejua hili wala lile anawekwa mstari wa mbele na kupoteza maisha yake. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa,” 2Sam 11:17. Kwa tendo hili Daudi anapata amani ya muda mfupi tu. Daudi anaendelea kuteswa na dhamiri yake mbaya. Mfalme Daudi kuanzia sana anaishi katika hatia.

Wapendwa katika Kristo, hakuna shaka kabisa kati yetu wapo ambao maisha yao wanaongozwa na hatia. Watu hawa hutumia muda wa maisha yao yote wakiepuka lawama na kuficha aibu. Watu wanaoongozwa na hatia wanaonewa sana na kumbukumbu. Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya usoni.Wanajiadhibu bila kujua kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda dhambi, hatia yake ilimtenga na Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani," Mwa 4:12. Hali hii inawaeleza jinsi watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga katika maisha bila lengo.

Ndugu yangu, sisi ni matokeo ya muda wetu uliopita lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo. Kusudi la Mungu halifungwi na muda wako uliopita. Ona! Alimbadilisha muuaji Musa na kuwa kiongozi mzuri; akambadilisha Gidioni aliyekuwa mwoga akawa shujaa na hodari; anaweza kufanya mambo ya ajabu na maisha yako yaliyobaki. Tazama pia maisha ya Mt. Augustino wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake.

Mungu ni mtaalam wa kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha kubwa wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na Mungu amefuta mashtaka yao."

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, toba ya kweli kwa dhambi zako ndiyo njia pekee ya kuishi katika amani ya kweli. Bila kufanya toba ya kweli mbingu ni ndoto kuifikia. Yesu leo anatupa aina mbili za mfano wa Ufalme wa Mungu. Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi,” Mk 4:26. Maana yake, anayezikuza mbegu hizo na kuwa kile kilichokusudiwa na Mungu mwenyewe. Na katika makuzi haya yaani maisha yako kila siku ni wakati wa wewe kuwa kile Mungu alichokusudia uwe. Hivyo ni wazi Mungu anapenda tuwe wanadamu kama alivyotuumba kwa sura na mfano wake. Tunapojaribu kuwa kitu kingine ni chukizo kwa Mungu na hapo tunakuwa wabaya kuliko hata shetani.

 Mfano wa pili wa Ufalme wa Mungu ni huu; Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32. Hapa tunakumbushwa kwamba hakuna kisicho na umaana mbele ya Mungu katika mwonekano wake, iwe ukubwa au udogo. Vyote vinaudhihirisha Utukufu na Uzuri wa Mungu, na kwayo kwa kuwa kile kilicho ufikia ukamilifu wake ambao ndio kusudio la kuumbwa kwake. Hivyo ndugu yangu jipokee ulivyo na yakamilishe yaliyo ndani yako kadiri ya mpango wa Mungu katika ukamilifu wake.

Tumsifu Yesu Kristo!


Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako,” Zab 119